Kufuturu Wakati Wekundu Bado Haujamalizika Inajuzu?

SWALI

ASALAM ALAYKUM,

kwanza kabisa napenda kuwashukuru kwa elimu kubwa munayotupa na inshallah allah (s.w.t) ndiye atakaye walipa malipo mema kabisa.

Suali langu ni hili;

mimi naishi (london)sasa wakati wa sala huku huwa ninatizama ktk calendar maalum za kiislamu au ktk tv za huku ambazo za kiislamu hutoa adhana kila wakati wa sala.lakini kinachonishangaza mie na wenzangu wengu tu wakati wa sala ya magharib huadhiniwa adhana wakati ukitizama nje yaani juu ktk mawingu utaona bado kuna wekundu haujaondoka wote na ukikaa kama dakika tano hivi mpaka saba ndio utaona unaondoka wote suali langu ni jee inafaa kula tunaposikia adhana tuu au tusubiri mpaka wekundu umalizike? Tunaomba jawabu kutoka kwenu wenye elimu kwani hapa tunashaka kubwa na jambo hili na hizi ramadhani zetu. Jazakawallahulkeheir.namuomba allah akupeni uwezo wa kutujibu haraka ili tupate ukweli.

Kwa kuongeza hii huona wakati hali ya hewa ya siku ile inapokuwa kuna jua na ikiwa kuna wingu au mvua basi huwa hatuuwoni huu wekundu.samahani kwa maelezo marefu.

 


 

 

 JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaana wa Ta'aala)   Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn.

Pili tunatoa tena shukurani kwako kwa kutuma Swali lako hili ukiwa umeweka maudhui yake iliyo wazi kabisa, jambo ambalo hutufanyia wepesi sisi kuweza kulipata swali tunapotaka kulijibu haraka. Tunaomba ndugu zetu wengine wote watimize utaratibu huu muhimu.

Kwa hakika hili ni suala ambalo huwachanganya Waislamu lakini tukifahamu vilivyo Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutakuwa na tatizo lolote.

Kwanza ni muhimu sana tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana tuwe ni wenye kufanya haraka kufungua mwadhini (kufuturu/kufutari) na kufanya haraka kuswali Swalah ya Magharibi. Kufanya haraka huku hakuna maana ya kuwa tuanze kula kabla ya wakati wake. Imepokewa na Sa‘d ibn Sahl (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watu watabakia katika kheri (na njia nyoofu) maadamu watafanya haraka kufuturu” (al-Bukhaariy, Muslim, Maalik, na at-Tirmidhiy).

Sasa huku kufanya haraka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kufuturu/kufutari ni kupi? Imepokewa na Abu Ibraahiym ‘Abdillaahi bin Abi Awfaa (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: Tulikuwa safarini pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amefunga. Jua lilipokuchwa aliwaambia baadhi ya watu: “Ewe fulani, shuka ututengezee uji wa shayiri”. Akasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Lau utaingia usiku?” Akasema: “Shuka ututengezee uji wa shayiri”. Akasema: “Hakika bado ni mchana”. Akasema: “Shuka ututengezee uji wa shayiri”. Akasema: “Akashuka na kuwatengenezea uji wa shayiri, naye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanywa”. Kisha akasema: “Munapouona usiku umetokea kutoka huku, basi amefuturu aliyefunga”. Akaashiria kwa mkono wake upande wa mashariki (al-Bukhaariy, Muslim, na Abu Daawuud). Hii inaashiria jua linapokuchwa hata ikiwa wekundu wake bado unaonekana, wakati wa Magharibi unaweza kuwa umeingia. Akatosheleza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa maadam kushakuwa giza upande wa mashariki ambako jua ndilo latokea basi hata kama upande wa Magharibi bado giza halijatanda, Maghrib inakuwa ishaingia tayari. Na ikiwa upande wa Magharibi kutakuwa ni giza na jua jekundu lishapotea, hiyo haitokuwa tena ni maghribi bali itakuwa ni 'Ishaa. Na hii hadiyth haipingani na Aayah ya Suratul Baqarah: 187 isemayo: {{...Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku...}}, bali inaifasiri na kuifafanua kwa uwazi na upana. Na maana timizeni Swawm hadi usiku, makusudio ya usiku hapo kwa mujibu wa wafasiri wote ni Magharibi, na Magharibi imefafanuliwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni pale muda wa Swalah ya Maghrib inapoingia pamoja na kuwepo wekundu wa jua. Kinyume na walivyofahamu vibaya Aayah hiyo baadhi ya watu kama Mashia ambao wanangojea hadi liingie giza kabisa! Wanajikalifu kwa uchache wa ufahamu na kujikuta wakifutari wakati wa 'Ishaa mara nyingi.

Katika hili haifai mtu kutia wasiwasi kwani tayari wanazuoni na wataalamu wa Kiislamu wamefanya juhudi ya siku nyingi kuangalia kuchomoza na kuchwa kwa jua mpaka wakaja na nyakati hizo katika jadwali za miji tofauti. Ikiwa adhana inaadhiniwa wakati huo basi ni juu yako kufungua. Ikiwa una tashwishi yoyote basi ni juu yako uende katika Msikiti au Markaz iliyo karibu nawe ili uulizie jambo hilo. Lakini ni jambo ambalo halina utata kabisa.

Na haifai katika siku za Ramadhaan kufanya kama wengi miongoni mwa Waislamu wanavyofanya kuongeza dakika tano au mfano wake kwa kisingizio kuwa hilo ni kuhakikisha. Kabla ya Ramadhaan huwa watu wanafuata jadwali nyengine na wakati wa Ramadhaan kuongeza dakika hizo.

Wakati wa Magharibi unakuwa mfupi, hivyo unapochelewa kufungua huenda ukachelewa kuswali Magharibi. Hilo litakupelekea wewe kutoka katika kufuata maagizo ya Mtume (Swalla Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Hali ya hewa ikibadilika na wekundu huo wa jua ukawa hauonekani kama ulivyosema, basi utafuata muda uliopangwa kutokana na kujulikana hizo nyakati.

Na Allah Anajua zaidi

 

 


Share