06-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) - 1

 

2. ‘Umar Bin Al-Khattwaab  (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Aliyebashiriwa Pepo

 

 

Jina lake lilikuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab bin Nufayl bin ‘Abdil-‘Uzza Qurayshiy Al-’Adawiy. Lakabu yake ilikuwa Abu Hafsw. Alikuwa na udugu na Mtume kwa kizazi chake cha nane.

Mama yake alikuwa Hantamah bint Haashim bin Al-Mughirah bin ‘Abdillaah bin ‘Umar bin Makhzuum na alikuwa binamu wa Abu Jahal.

 

 

Kuzaliwa Na Malezi Yake

 

 

Alizaliwa miaka mitatu baada ya mwaka wa ndovu, na alikuwa miongoni mwa Maquraysh wema. Alikuwa balozi wa Maquraysh. Kila ulipotokea ugomvi kati ya Maquraysh na makabila mengine, walikuwa wakimtuma ‘Umar kama Mjumbe (balozi) wao. Aidha walikuwa wakimtuma katika mikutano ya majigambo iliyokuwa ikifanyika katika zama za jahiliya.

         

‘Umar alipobaleghe, baba yake alimfunza kuchunga ngamia. Hii ilionekana amali nzuri lakini inayochosha. Al-Khattwaab alimfundisha mwanae kuvumilia ugumu uliotokana na kazi hiyo. Kila ‘Umar alipochoka na kutaka kupumzika, baba yake alimhimiza na kumtaka avumilie matatizo, na hivyo akamfunza kuwa mvumilivu. Sehemu ‘Umar aliyochungia wanyama wake iliitwa Daghnan.

         

Baada ya kuteuliwa kuwa Khalifah, mara moja alipita malishoni, na alisema. “Allaah Aliyetukuka, Inashangaza mabadiliko ya majaaliwa! Nilikuwa nikiwalisha wanyama wangu hapa, katika malisho haya huku nimevaa shati la sufu. Nilipochoka, baba akinipiga. Sasa mimi ni mtawala, na hapana aliye juu yangu isipokuwa Allaah.”

         

Katika ujana wake, alifanya shughuli zilizofanywa na Waarabu wa daraja la juu. Alishughulikia nasaba (kizazi), mieleka, kuendea khutbah rasmi na ubingwa wa kupanda farasi. Baadaye alikuwa bingwa na kutambua nasaba na mpiga mieleka asingeshindika. Alikuwa akishindana mieleka katika uwanja wa ‘Ukaaz.

         

Wakati huo huo alijifunza kusoma na kuandika, na alikuwa mmoja wa watu kumi na saba wa kabila la Quraysh walioweza kusoma na kuandika.

 

 

Umbile  Lake

 

‘Umar alikuwa na rangi nzuri ya uso, kipara, ndevu nyingi na alikuwa mrefu. Watu wanasema alipokuwa akitembea utadhani alipanda mnyama. Ndevu zake zilikuwa ndefu na mvi kwenye ncha zake.

 

 

Kurejea Kwenye Uislamu

 

Siku moja ‘Umar alichukua panga lake na kutoka nje. Alikutana na mtu wa Banu Zuhrah na kumwuliza: Unakwenda wapi ewe ‘Umar?”

Alijibu:

“Nakwenda kumuua Muhammad.”

Yule mtu akamuuliza:

“Unajihakikishiaje usalama kwa Banu Haashim na Banu Zuhrah utakapomuua?”

‘Umar alimwambia yule mtu:

“Nikuambie jambo litakalokufadhaisha Ewe ‘Umar! Dada yako na shemeji yako wamerejea katika Uislamu na wameitelekeza dini unayoiamini.”

‘Umar alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dada yake na akamkuta mwanaume Muhajirina. Jina lake Khabbaab. Khabbaab aliposikia sauti ya ‘Umar, alijificha ndani ya nyumba.

“‘Umar aliingia na kumkuta dada yake na mumewe, na alisema:

“Nimesikia nini ndani ya nyumba hii?” Walikuwa wakisoma Surah Twa-haa (Sura Na. 20 ya Qur-aan Tukufu). Walijibu.

“Hapana, tulikuwa tunazungumza tu.”

“Nina wasiwasi ya kuwa mmeacha dini yenu.” Mume wa dada yake (shemeji) alimwambia.”

“Je, Ungeweza kugundua ukweli kama dini ingelikuwa tofauti na yako?”

‘Umar alimpiga sana, dada yake alifika na kumsukuma ‘Umar ili asiendelee kumpiga mumewe. ‘Umar alimpiga sana dada yake mpaka akatoka damu usoni.

Dada yake ‘Umar alimwambia kaka yake kwa hasira:

“Huoni ya kuwa ukweli upo katika dini nyingine minghairi ya dini yako? Nakiri ya kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah, na ninakiri ya kwamba Muhammad ni Mjumbe na mtumwa Wake.”

 

‘Umar alisema:

“Nipe ulichonacho ili niweze kukisoma.” ‘Umar alikuwa anajua kusoma na kuandika. Dada yake alimwambia: “Wewe si twahara, na hutakiwi kukigusa, mpaka utakapotwharika. Wale waliotakaswa ndio wanaogusa Qur-aan. Nenda kaoge au katawadhe (Wudhuu).

Kwa hiyo alikwenda kupata Wudhuu, na kisha alianza kusoma mpaka alipofikia:

“Hakika Mimi ndiye Allaah. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na usimamishe Swalah kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.” (20: 14)[1]. [usahihi wa kisa hiki una mashaka, maelezo zaidi chini]

 

Kutokana na hayo ‘Umar alitambua ukweli. Alisisitiza kutangaza ukweli japokuwa Waislamu walikuwa dhaifu katika zama zile.

Ibn ’Umar alisema: ‘Umar aliporejea kwenye Uislamu (na kutangaza habari zile) aliuliza: “Nani aliyekuwa mbora wa kuwalingania watu?” Watu walijibu: “Jamiyl bin Ma’mar Al-Jumahi.”

 

Ibn ‘Umar  alisema:

“Kwa hiyo baba yangu alitoka nikamfuata. Nilikuwa mkubwa nakuelewa yaliyokuwa yakisemwa. ‘Umar alikutana na Jamiyl na kumwambia: “Lazima uwe na uwezo wa kupata habari za kusilimu kwangu.”

 

Jamiyl hakuchelewa. Alichukua joho lake na kutoka nje. “‘Umar na mimi tulimfuata ambapo Jamiyl alisimama katika mlango wa Al-Ka’bah na kupiga ukelele.

 

“Enyi Maquraysh! ‘Umar ameasi (ameacha dini ya mababu zake).”

‘Umar  alimwambia:

“Umesema uongo, lakini nimesilimu.” Baadhi ya Maquraysh walimshambulia ‘‘Umar  na walipigana naye mpaka akaanguka.

 

 

Al-Faaruuq

           

Mjumbe wa Allaah aliwapa majina maalum baadhi ya Maswahaba ili kuelezea baadhi ya mwenendo wao. Mathalan, AsaduLlaah (Simba wa Allaah) kwa Hamzah , SayfuLlaah (Upanga wa Allaah) kwa Khaalid bin Waliyd na Al-Faaruuq (mpambanuzi wa yaliyo sahihi na batili) kwa ‘Umar.

           

‘Umar  anasimulia kisa kinachohusu kupewa jina la Al-Faaruuq;

“Hamzah alirejea kwenye Uislamu siku tatu kabla yangu. Kisha, Allaah Aliufungua moyo wangu katika Uislamu. Baada ya kutamka shahada. Nilimwambia Mjumbe wa Allaah. “Hatuko kwenye ukweli ima tunaishi ama tunakufa?” Mjumbe wa Allaah alisema: “Ndiyo bila shaka, mko katika ukweli ima mko hai au mmekufa. “

‘Umar alisema: “Kwa nini tunajificha kama ndiyo hivyo? Kwa yule aliyekutuma na ukweli, lazima tutoke nje. Kwa hiyo tulitoka nje katika safu mbili. Hamzah aliiongoza moja na mimi niliongoza ya pili mpaka tukaingia Msikitini.”

‘Umar  aliendelea kusema.

“Maquraysh waliniangalia na wakamwangalia Hamzah, utusi utusi ulikuwa mbele yao. Mjumbe wa Allaah alinipa jina la Al-Faaruuq kuanzia pale.”

 

 

Kuhama  Kwake  (Kuhajiri)

 

 

Mateso ya makafiri yalipozidi sana, na njia za kuwatesa Waislamu zilipokuwa hazivumiliki baada ya kifo cha Abu Twaalib, ‘ami yake Mtume, Waislamu waliruhusiwa kuhajiri huku wakiacha nyuma mali zao Makkah na wakitarajia malipo na furaha ya mbele Siku ya Qiyaamah.

           

Kutokana na kuwaogopa makafiri, Waislamu walikuwa wakihama kwa siri. ‘Umar ndiye aliyekuwa mtu pekee ambaye hakumwogopa yoyote, na alihama bila kificho.

           

Ali bin Abi Twaalib  alisema:

“Sikumfahamu mtu aliyehama kwa dhahiri isipokuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab. Alipokuwa tayari kuhama, alichomoa upanga wake, akachukua upinde mabegani mwake na akachukua mishale mkononi mwake. Alikwenda Al-Ka’bah ambapo alitufu na wakuu wa Kiquraysh walikuwepo. Kisha alikwenda Maqaam Ibraahiym, aliswali rakaa mbili kwa unyenyekevu mkubwa, na alisema:

“Nyuso hizi zitafedheheshwa. Yeyote anayetaka mama yake afikwe na msiba, basi anifuate nyuma ya milima ile.

‘Aliy  alisema:

“Watu wote dhaifu walimfuata, na aliwafundisha yale ambayo yangewasaidia, na wakaelekea Madinah.”

 

 

Kulingana  na  Qur-aan  Takatifu

 

 

Qur-aan Takatifu iliteremshwa na kufanana na fikra (utashi) wa ndani na ‘Umar , zaidi ya mara moja: Anas bin Maalik  alisimulia ya kuwa ‘Umar alisema:

“Allaah alijibu maombi (du’aa) yangu kuhusu mambo matatu: Maqaam Ibraahiym, Hijaab kwa mwanamke wa Kiislamu, na kuhusu mateka wa Vita vya Badr.”

 

Katika siku ya Badr, Allaah Aliwapa ushindi Waislamu dhidi ya makafiri, ambapo makafiri sabini waliuawa, na wengine sabini walichukuliwa mateka. Mtume alishauriana na Abu Bakr, ‘Umar na ‘Aliy juu ya mateka hao.

Abu Bakr alisema:

“Hao ni binamu zetu, ndugu zetu na jamaa zetu. Nashauri uchukue fidia kutoka kwao ili tujiimarishe zaidi ya hayo Allaah Aliyetukuka anaweza kuwaongoza na wakatuunga mkono.”.

Mtume alisema:

“Unaonaje? Ewe kijana wa Al-Khattwaab!”

‘Umar alisema:

“WaLlaah, naona kinyume cha anavyoona Abu Bakr. Nakuomba unipe fulani bin fulani (jamaa wa ‘Umar) ili nimkate shingo yake, ‘Aqiyl (kaka yake ‘Aliy) mpe ‘Aliy amkate shingo yake, na mpe Hamzah kaka yake (fulani bin fulani) amkate shingo yake. Allaah Anajua kuwa hatukuwa na huruma na makafiri. Na hao niliowataja ndio viongozi  na watukufu wao.”

 

Mjumbe wa Allaah alimili kwa rai ya Abu Bakr na akachukua fidia kutoka kwa mateka. Allaah Mtukufu Aliteremsha Aayah ifuatayo kuthibitisha rai ya ‘Umar.

“Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Allaah anataka Akhera. Na Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (8: 67)[2]

 

‘Umar bin Al-Khattwaab alisema:

“Ewe Mjumbe wa Allaah! Utaifanya Maqaam Ibraahiym kuwa sehemu ya Swalah.”

Allaah Mtukufu aliteremsha Aayah ifuatayo:

“Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Ka’abah) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia. Na tuliagana na Ibraahiym na Ismaa’iyl: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu.”(2: 125).

 

‘Umar bin Al-Khattwaab alisema:

“Pia nilisema: ‘Ewe Mjumbe wa Allaah! Watu wazuri na wabaya wamekuzuru! Utawaamrisha akina mama na Waumini wajisitiri (wavae Hijaab)! Kwa hayo Aayah Takatifu ya Al-Hijaab iliteremshwa.”[3]

 

Ilisimuliwa ya kuwa Qur-aan Takatifu ililingana (ilisadifu) na rai ya ‘Umar katika hali 21. Hii ni dalili ya wazi aliyoruzukiwa ‘Umar na Allaah. Mjumbe wa Allaah alisema:

“Bila shaka Allaah ameandika ukweli katika ulimi na moyo wa ‘Umar.”

Ibn ‘Umar alisema:

“Hapana jambo lililowafika watu nao pamoja na ‘Umar wakalizungumzia isipokuwa Qur-aan iliteremshwa kulingana na aliyoyasema ‘Umar.

 

 

Kuchaguliwa Kuwa Khalifa

 

 

Abu Bakr alipohisi ya kuwa kifo kilikuwa kikimjongelea, alishauriana na Maswahaba kuhusu atakayechukuwa uongozi baada yake. Aliwajua maswahaba wote na alimjua aliyefaa zaidi. Alijua ya kuwa ‘Umar alikuwa mkweli wa dhati, na alimjua ya kuwa anaheshimika, hivyo alimpendekeza kuwa Khalifa, lakini halikuwa jukumu lake kuamua. Kwa hiyo aliwaita Maswahaba kutaka ushauri. Aliwaambia:

“Ninakufa, kwa hiyo lazima tumchague Khalifa anayefaa.”

Maswahaba wakamwambia:

“Uamuzi ni wako.”

Abu Bakr  akaanza kushauriana na Maswahaba juu ya ‘Umar

‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf alisema:

“Yeye ni bora kuliko umdhaniavyo.”

 ‘Uthmaan alisema:

“Najua ya kuwa anachokificha ni bora kuliko anachokidhihirisha na hapana kati yetu aliye bora kuliko yeye.”

‘Aliy alisema:

“‘Umar ni kama ulivyomuelezea.” Usayd bn Hudayr alisema:

“Allaah Amuongeze awe mwema baada yako, kwani anachokificha ni bora kuliko anachodhirisha. Hapana anayeweza kumzidi katika suala hili.”

Mmoja wao alimwambia Abu Bakr:

Utamjibu nini Mola iwapo atakuuliza: Ulimteua vipi na ilhali ulimjua kuwa ni mkali?”

Abu Bakr alimjibu:

“Ningesema: Ee Allaah, Nimemteua mbora kuliko wote.” Kisha alimwamuru ‘Uthmaan aandike Agizo la kumteua ‘Umar kuwa Khalifa.

 

 

Mwenye Nguvu Na Muaminifu

             

Du’aa ya kwanza aliyoomba ‘Umar baada ya kuchaguliwa ni msaada na ulinzi kutoka kwa Allaah:

“Ee Allaah! Mimi ni mkali, naomba unifanye mpole. Mimi ni dhaifu hivyo nipe nguvu. Na mimi ni bakhili, nifanye mkarimu”.

         

Kwa kuwa alijua umuhimu wa Baytul Maal (hazina ya serikali) kwa mtawala kuidhibiti, alisema:

“Ee Allaah! Nimekuwa kama mlezi wa yatima. Nikiwa tajiri wa wastani. Sitochukua mshahara. Na ikiwa vinginevyo. Nitachukua kiasi cha kukidhi haja.”

         

Wakati fulani ‘Umar aliugua, alitakiwa kutumia asali kama dawa, na ilikuwepo chupa kubwa iliyojaa asali katika hazina ya dola (Baytul Maal). ‘Umar  alipanda juu ya mimbari na alisema:

“Mkiniruhusu nichukue nitafanya hivyo. Vinginevyo ni haramu kwangu.” (Walimruhusu).

‘Umar alikuwa mwangalifu katika utunzaji wa mali ya ummah kwa kuweka kumbukumbu sahihi.

         

Abu Bakr alisimulia ya kuwa aliingia kwa ‘Umar wakati wa kukusanya Zakaah siku ya jua kali, alimkuta ‘Uthmaan amekaa chini ya kivuli. Ali na ‘Umar  walikuwa wamesimama juani wakirekodi rangi na umri wa ngamia wa Zakaah. ‘Aliy alipomwambia ‘Uthmaan “Hajasikia msemo wa binti wa Shu’ayb akimweleza baba yake’;

“Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.” (28: 26)?”

‘Aliy alimnyooshea kidole ‘Umar  alimwambia:

“Huyu ana nguvu na mwaminifu.”

 

‘Umar alipotaka kuwadhibu watu kwa jambo lolote, alianza na ‘ailah yake. Aliwakusanya na kuwambia:

“Watu wamewaangalia kama ndege wanaowinda wanavyowaangalia wanyama. WaLlaahi, iwapo nitamsikia mmoja wenu anafanya ninalotaka kulikataza, nitampa adhabu maradufu.”

 

Alikuwa akifuatilia hali za raia wake. Twalhah alimwona akiingia katika nyumba usiku wa kiza, na kisha akaingia nyumba nyingine. Asubuhi aliingia ndani ya nyumba na kumkuta ajuza kipofu asiyejiweza. Alimuuliza: “Una habari gani juu ya mtu anayekuzuru kila mara?” Alijibu: “Huwa ananitembelea kila mara kukidhi mahitaji yangu na kuniondolea machungu.”

         

Aliwahudumia raia zake wa Dola ya Kiislamu kutokana na kumcha Allaahna alikuwa akisema:

“Kwa jina la Yule aliye mtuma Muhammadkwa ukweli, iwapo ngamia aliibiwa katika Euphrates, nachelea Allaahasije akaitaka familia ya Al-Khattwaab kuwajibika kwa sababu hiyo.”

 

 

Mwasisi (Mtangulizi)

         

‘Umar alikuwa mwasisi wa mambo mengi:-

·         Alikuwa wa mwanzo kuitwa “Kiongozi wa Waumini” (Amiyrul–Muuminiyn) aliwambia: “Nyie ni waumini, na mimi ni Kiongozi.”

·         Kwa mara ya mwanzo, watu walimwita, “Khalifa wa Khalifa wa Mjumbe wa Allaah

·         ‘Umar alikuwa na mwanzo kufanya mwaka wa mwandamo kuwa kalenda rasmi ya Waislamu.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuanzisha mfumo wa wizara za serikali ambapo mishahara na kumbukumbu za wafanyakazi wa dola na askari zilianzishwa. Pia alianzisha mfumo wa kuweka kumbukumbu za taarifa alizotuma kwa Magavana na wakuu wa nchi.

·         ‘Umar alikuwa na mwanzo kuunda jeshi la polisi ili kulinda usalama.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuamuru sala ya Taraweeh kwa jamaa Msikitini.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuwatia adabu watu waliokosea. Fimbo yake ilikuwa inatisha kuliko mapanga.

 

 

[1] Kisa hiki cha kurejea katika Uislamu kwa ‘Umar hakijachukuliwa kama Hadiyth Sahihi. Ilikusanywa na Al-Bayhaqiy katika Ad-Dalaail 3/219) na Ibn Sa’d klatika Al-Twabaqaat (23.267) na Al-Haakim katika Al-Mustadrak (4/95) kwa kupitia Is-haaq bin Yuusuf Al-Azraq, alisema:”Al-Qasim bin ‘Uthmaan alitusimulia kwa mamlaka ya Anas bin Maalik.”

Isnad hizi ni dhaifu. Udhaifu wake unatokana na Al-Qaasim bin ‘Uthmaan Al-Basr. Ad-Daaraqutniy anasema katika Sunan yake: “Hadiyth hii ni dhaifu.” Al-Haafidh anasema katika Al-Lisaan (4/542) kuwa Imam Al-Bukhaariy alisema. “Anayo Hadiyth ambayo haikuungwa mkono na wote” Adh-Dhwahaak anasema katika Miyzaan Al-l’tidaal (3/375) katika kitabu wasifu wake: “Alimsimulia Is-haaq Al-Azraq Hadiyth, na kisa cha kusilimu kwa ‘Umar kinaonekana kuwa dhaifu.

 

[2] Tafsir Ibn Kathiyr.

[3] Ar–Riyadh An-Nadim 2/287.

 

 

Share