Wengi Si Hoja: Idadi Kubwa Ya Wafuasi Haimanishi Kuwa Jambo Walifanyalo Ni La Haki

 

Wengi Si Hoja[1]

Idadi Kubwa Ya Wafuasi Haimanishi Kuwa Jambo Walifanyalo Ni La Haki 

 

 Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

BismiLLaah Al-HamduliLLaah was Swalaatu was Salaamu 'alaa RasuwliLlaah
 

Amma ba'd.

 

 

Wengi Si Hoja

 

Kutokana na tabia za watu wa zama za Jaahiliyyah (zama za ujinga kabla ya Uislamu) ni kwamba walikuwa wakiangalia kundi lenye wafuasi wengi kuwa ni ushahidi wa jambo walifanyalo kuwa ni la sawa na kundi lenye wafuasi kidogo wakisema hawa wako kwenye batili. Ilikuwa kiakili zao ni kwamba jambo lifanywalo na wafuasi wengi ni la haki na jambo lifanywalo na wafuasi wachache ni la batili machoni mwao hivi ndivo walivyokuwa wakipima ukweli na uongo.

 

 

Kama hivi ndio kipimo cha kubainishia ukweli na makosa, basi ni makosa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

 وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

116. Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo. [Al-An’aam: 116]

 

 

Na Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

    قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٧﴾

Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Allaah (Pekee), lakini watu wengi hawajui. [Al-A’raaf: 187]

 

 

Na Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِم مِّنْ عَهْدٍ ۖ وَإِن وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ ﴿١٠٢﴾

Na Hatukuwakuta wengi wao kuwa ni (wakweli) wa ahadi. Bali kwa yakini Tumewakuta wengi wao ni mafasiki. [Al-A’raaf: 102]

 

Kwa hivyo, kipimo si idadi ya watu wengi au kidogo kuwa jambo la kishariy’ah ya Dini linakuwa ni sawa au makosa. Bali kishariy’ah ya Dini tunaangalia ukweli na haki iko wapi hata kama yuko mmoja pekee yake ndiye atakuwa kwenye haki na atapaswa kuungwa mkono na watu wote. Na ikiwa idadi kubwa ya watu wako upande wa makosa na batili, ni waajib kuwapinga na watu wasilazimishwe kukubali makosa na upotofu wa watu kama hao. Mazingatio yanapaswa yawekwe kwenye ukweli wenyewe kimakinifu. Na kwa ajili hio ndio ‘Ulamaa wamesema: “Haki haitambuliki kwa njia za watu bali watu wanatambulikana kwa haki yenyewe’’.

 

Hivyo, yule aliyesimama katika haki, anapaswa kufuatwa na kuungwa mkono.

 

Kwenye visa Alivyotueleza Allaah ('Azza wa Jalla)  kuhusu Umati zilotangulia, Anatueleza yakuwa kila mara haki ina wafuasi kidogo kama Anavyosema:

 

  وَمَنْ آمَنَ ۚ وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ﴿٤٠﴾

 Na hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache. [Huwd: 40]

 

 

Na kwenye Hadiyth ambayo inayohusiana na umati zilizopita  aliyofikishiwa Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema aliona Nabii aliyekuwa na wafusasi kidogo pamoja naye, na Nabii mwengine alokuwa na wafuasi wawili au mmoja wakifuatana naye. Na Nabii mwengine ambaye alikuwa hana mfuasi hata mmoja. [Al-Bukhaariy]

 

Kwa hivyo ki-Dini hatuamui jambo kulingana na wingi wa wafuasi au udogo wao, bali tunatakikana tupime ukweli uko wapi na makosa yako wapi. Kwa hivyo, hata kama ukweli una wafuasi wachache inatakikana watu wote waufuate kwani huko ndio kujiokoa na upotevu.

 

Makosa ama upotevu hautetewi na kuungwa mkono kwa ajili tu una wafuasi wengi. Hivi ndivyo inatupasa Waislamu kutumia kipimo hiki katika kuhukumu mambo.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Uislamu ulianza ugeni na utarudi kuwa mgeni kama ulivyokuja.” [Muslim].

 

Haya yatatokea wakati uovu, fitnah, na upotevu utakapozidi. Hakutabakia mtu kwenye ukweli ila wale watakaokubali kuonekana kama wageni kwa watu wao na makabila yao (kwa ajili ya Dini yao). Wataonekana kama watu wa maajabu na wageni kwa watu wao.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa Unabiy wakati ulimwengu umefunikwa na kutomwamini Allaah na upotevu. Na alipolingania watu, ni watu wachache sana walimwamini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakawa naye. Ni hadi baadaye kabisa ndio wakazidi kuwa wafuasi wengi. Kabila la ki-Quraysh bila kutaja Bara Arabu zima lilikuwa kwenye upotevu. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa peke katika kulingania watu. Kwa hiyo walomfuata walikuwa wachache sana katika kulinganisha na idadi ya ulimwengu mzima.

 

Hivyo, hatuangalii kundi lipi lenye wafuasi wengi. Tunaangalia ni kundi lipi lenye kufuata haki.

 

Na kuufanikisha ukweli. Naam, ikiwa idadi kubwa ya watu wameshikamana na haki, basi hayo ni mambo mazuri kabisa. Lakini, mfumo wa Allaah ('Azza wa Jalla)  unaonyesha kuwa watu wengi wanashikamana na batili na upotofu.

 

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utatilia hima.   [Yuwsuf: 103]

 

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

116. Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo. [Al-An’aam: 116]

 

 

Marejeo:

Sharh Masaail Al-Jaahiliyyah (Uk. 60-62) cha Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.

 

 

[1]  Kwenye (sharh) kusherehesha maneno ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema: “Kutokana na kanuni zao kubwa, walikuwa wakivutika na wengi wanaofanya mambo hayo, wakiona kuwa wengi ndio wako sawa na hivyo jambo maadam lafanywa na wengi, basi ndio sahihi. Kadhalika walikuwa wakihukumu jambo kuwa ni batili au ni jambo la ajabu, kwa sababu tu lafuatwa na wachache. Hivyo basi, Allaah ('Azza wa Jalla)  Akawashushia muongozo kinyume na hivyo walivyokuwa wakiamini na kuhukumu mambo. Na haya yamebainishwa sehemu nyingi ndani ya Qur-aan.”

 

Share