Uwahaabi: Ufafanuzi Na Majibu Juu Ya Majungu Dhidi Ya Shaykh Muhammad 'Abdil-Wahhaab
Uwahaabi:
Ufafanuzi Na Majibu Juu Ya Majungu Dhidi Ya
Shaykh Muhammad ‘Abdil-Wahhaab
Yaliyomo:
Kufahamika vibaya kwa Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab
Margoliouth
Goldziher
Arberry
Encyclopaedia Britannica
Ameer Ali
Kumbu kumbu za Humphrey
Arnold
Utangulizi
Alhamdulilah Rabil ‘alamina, Wa swalaatu wa salaam ‘alaa Muhammad, na jamaa zake pamoja na Swahaba zake.
Harakati za kuanza kuhuisha Uislaam zilizoanzishwa na Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (1115 H - 1206 H/ 1703 M – 1792 M) zilikuwa na mwelekeo wa kufikia mahali zikubalike na zichukue mwelekeo mzuri katika Bara la Arabia na baadaye kufanikiwa. Harakati hizi zilipandikiza mbegu zenye kuangalia kupatikana kwa uongozi wenye busara. Uongozi huo ulikuwa umekula kiapo cha kusimamisha dola ya Sharia kwa ukamilifu kwa kutumia Kitabu na Sunnah katika harakati zake zote. Harakati hizi zilipata heshima na ushindi kutoka kwa Allaah na hivyo imebakia kuwa ni nguvu ambayo ina uwezo wa kutosha kwa kipindi cha karne mbili sasa tangu harakati hizo zianze licha ya kuwa na mapambano makubwa na mazito hapa na pale kutoka upande wa siasa na upande wa kidini.
Hata hivyo harakati hizi zilivuka mipaka ya Bara la Arabia na kuleta matunda mazuri katika nchi nyingine kadhaa nje kupitia mikono ya wanachuoni ambao walio wachaji Allaah na wakweli katika matendo yao ambao walikuwa wamechukua na kuiga mambo ya harakati za Muhammad ‘Abdul-Wahhaab. Harakati hizi zilikuwa zina baraka, kama mti mzuri ulivyo, mizizi yake huwa imekita chini na kushamiri na matawi yake kutandazike katika anga.
Lakini kama kawaida ya shughuli nyingi za kuleta marekebisho katika jamii, harakati hizi nazo zilipambana na kivumbi cha mishale iliyoelekezwa kwake ikuvurumishwa kuelekea kwa mwanzilishi wake na hata kupinga imani na itikadi yote nzima ya mafunzo yake. Kwa kuanzia, harakati hizi zilipewa jina la kudharaulisha, “Uwahabi” jina ambalo halikukubalika kwa mwanzilishaji wake, ingawa hivi sasa watu wanalikubali na kulitumia bila uzito.
Mbaya zaidi serikali katika eneo hilo ilitupiwa kashfa nyingi katika lugha nzito ambazo kiwazi wazi zilionesha jinsi gani uadui dhidi ya harakati hizi zilivyokuwa na kuonesha kiwango kikubwa cha uadui waliokuwa nao wapinzani wa harakati hizi. Makala mengi yaliandikwa ili kuwavuta wale watu ambao walikuwa wana mazoeya ya kufanya mambo ya uzushi katika dini na ushirikina, lakini makundi ya kutosha ya watu ambao walikuwa ni wanachuoni wa dini ya Kiislamu kutoka nchi mbali mbali za Kiislamu walisimama na kupambanua ukweli wa jambo zima kwa hoja nzito kwa kusema kuwa harakati hizo zilikuwa zimesimamia misingi ya haki na wapinzani walikuwa wanajaribu kuleta vitu visivyokuwa na msingi katika Uislaam.
Hoja za wasomi hawa zilifanya hoja dhidi ya harakati za Muhammad ‘Abdul-Wahhaab kuonekana wepesi wake. Kwa kuwa makala nyingi juu ya mada hii zimo katika Kiarabu makala haya yameandikiwa katika lugha ya Kingereza - na pia kufasiriwa Kiswahili (kwenye karatasi ya asili imeandika kiurdu, sisi tumeona tuandike kiswahili) ili kupanua wigo wa wasomaji wa habari hizi kwa lengo la kutetea msimamo wa Shaykh ‘Abdul-Wahhaab na wanachuoni wote ambao walisimama nyuma yake wakimuunga mkono na kumtetea katika sehemu mbali mbali za dunia.
Kwa kuwa makala hii ni fupi hatuna fursa ya kuandika kwa urefu vitu vingi wala haitowezekana kuandika mambo yote na kuyatolea hoja hapa In Shaa Allaah, msomaji ataridhika na hicho kidogo kitakachopatikana na tunaomba dua zetu hicho kidogo kiwe na faida kwa wasomaji.
Hakika Allaah Ndiye Anayewaongoa kuelekea njia iliyo sahihi…
Margoliouth
Tunaanza makala yetu kwa kujadili maandishi kutoka kitabu kiitwacho Encyclopaedia of Religion and Ethics (Munjidi wa mambo ya Dini na Maadili)[1] Hiki kinasemekana kuwa ni kitabu kikongwe sana ambacho kinajadili mambo ya dini na kitabu cha rejea katika dini kikiwa kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
William Margoliouth, ambaye alikuwa ni mwandishi wa Sura ya “Wahhaabism” – Uwahabi, anasema kuwa Mawahabi wanatofautiana na Ahlus Sunnah wal Jama’ah katika maeneo kumi:
- Wao wanaamini kuwa Allaah Ana sifa za maumbile ya kimwili kama ana Uso na Mikono.
- Kutumia akili hakuna nafasi katika mambo ya dini ambayo yana ufumbuzi wake moja kwa moja kutokana na Hadiyth.
- Wanakataa Ijma’aa
- Wanakataa Qiyaas
- Imaam wa madhehebu mbali mbali hawana mamlaka juu ya dini na wale wanaowafuata imaam hao, wao si Waislamu.
- Waislamu ambao wanakataa kuwafuata na kujiunga na Mawahabi nao si Waislamu.
- Hakuna Shufaa’ kutoka kwa Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au mtu yeyote mchaji.
- Kuzuru makaburi kumetazwa
- Kuapa kwa kutumia jina lisilokuwa la Allaah kumekatazwa.
- Kuchukua ahadi kwa yeyote asiyekuwa Allaah ni haraam na kuchinja katika makaburi kwa ajili au kwa jina la watakatifu ni haraam.
Mwandishi huyu anasema kuwa ana wasiwasi juu ya ukweli wa ibara namba tano (5) kuwa ni kitu kinachowahusu Wahabi maana wao ni wafuasi wa Imaam Ahmad bin Hanbal, yeye akiwa miongoni mwa Imaam wanne (maarufu wa Kiislamu). Margoliouth anamaliza makala yake kwa kusema kuwa Imam Ahmad (alifariki 1831) alianzisha U-Wahabi nchini India baada ya Hija yake ya mwaka 1824. Kilicho cha ajabu ni kuwa msomi kama huyu W. Morgoliouth, aliweza kunukuu vitu vingi sana vilivyo dhidi ya ‘Abdul-Wahhaab, na hana chochote cha kumtetea isipokuwa ibara namba tano iliyotajwa hapo juu.
Hivyo wacha tujaribu kurekebisha hilo na tutatia marekebisho yetu iwapo italazimika.
1- Imani ya Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab juu ya sifa za Allaah ni sawa na imani ya watu wa Salaf, Waislamu waliotangulia. Wao walisema kuwa Allaah anazo sifa zote ambazo Yeye Mwenyewe kazitaja na kuzitangaza kuwa ni Zake. Hilo linahusu hali yake ya kusema kuwa nafsi yake ina Uso, Mikono na Jicho na sifa za matendo kama vile kupenda, kuchukia na Kuwepo kwake katika 'Arsh na kushuka Kwake. Wale watu wa Salaf wanakubali majina hayo na sifa hizo bila (takyiyf wala ta’atwiyl) kuuliza namna gani matendo yanafanyika wala bila kubadilisha au kukanusha matendo hayo na sifa hizo wala bila kufanya tashbiyh yaani kufananisha matendo hayo kwa kawaida ya matendo ya binaadamu. Na msingi wao kuamini hivyo ni kauli ya Allaah,
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11].
Kama vile sifa za Allaah hazilingani wala kufanana na zifa za binaadamu, hali kadhalika Hali Yake Subhaanahu wa Ta’ala haifanani na kiumbe chochote wala mtu yeyote.
2- Hoja kwamba wafuasi wa ‘Abdul-Wahhaab hawatambui wala hakubali ijtihaad hii ni hoja ya kuwazulia moja kwa moja. Tunachosema ni kuwa ‘aqli’ haiwezi kutumika bila kutegemezwa kwenye Wahy (ambayo ni Qur-aan na Sunnah). Tukichukua kiasi cha jicho na mwanga, tunafahamu wazi kabisa kuwa jicho linahitaji mwanga ili liweze kufanya kazi.
Mwanga huu unaweza ni mwanga wa kawaida kutoka kwenye jua, mwezi, nyota au mwanga wa kutengenezwa na binaadamu. Kwa hali hiyo, akili za mwanaadamu inapata mwanga na kuweza kufanya kazi zake vizuri katika mipaka ya ufunuo na uwezo wa Allaah ambao unafanya akili iwe na mwelekeo sahihi na kuwa yenye kuaminika katika maoni yake. Akili ya mwanaadamu ikikosa kujiegemeza kwa Wahy wa Allaah itaelekea kwengine kusiko kuwa ndiko na kuingia gizani na kupotea katika mwelekeo.
Akili za binaadamu zinatofautiana sana na zimo katika mafungu mafungu; hoja za mwanafalsafa zitakuwa tofauti na hoja za mwana hesabu.
3- Imeelezwa kuwa 'Mawahabi' wanakataa Ijmaa'. Hili nalo si sahihi. Imaam Ahmad bin Hanbal, alikuwa anaamini kuwa Ijmaa' ya kweli ni ile ya Swahaba. Kipindi cha Swahaba kinajulikana vizuri vipi kilianza na vipi kilifikia ukomo wake. Swahaba walishuhudia Wahy ukiteremka na waliukubali ujumbe kutoka kwa Nabiy (Swala Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wao wakiwa ndio watu wa kwanza. Imaam Muhammad Abu Zahrah alisema kuna Ijmaa' aina mbili: “Ijmaa' katika suala zima la faradhi ya matendo jambo ambalo linakubaliwa na wote. Na Ijmaa' katika upande wa pili wa Sharia'h, kama vile kuwapiga vita watu walioritadi. Rai zinatofautiana kwa aina ya pili ya Ijmaa' zimenasibishwa kwa Imam Ibn Hanbal. Baadhi ya wanachuoni wamesema kadhaa kutoka kwake kama:
“Yeyote anayedai kuwa kuna Ijmaa' ni muongo”
Imam Ibn al Qayyim alisema, “Mtu yeyote atakayedai kuwepo Ijmaa' ni muongo, na (Imam Hanbal) hakupendelea kuweka mbele Ijmaa' wakati kulikuwa na Hadiyth sahihi.”
Na ‘Abdullaah, mtoto wa Imaam Ahmad alisema: “Nilimsikia baba yangu akisema, “Mtu akidai Ijmaa', ni muongo. Ni kama vile mfano wa kadhia ya tofauti kati ya watu ilijitokeza, lakini hakujua kuhusu hilo. Atakachoweza kusema ni, ‘hatukujua ni nani aliyekataa”.
Maneno haya yanaonesha kwamba Imaam Ahmad alikuwa hakatai kuwa Ijmaa' ilkuwepo na ikitumika, lakini hakuna hilo kutokea baada ya Maswahaba kupata.[2]
4- Inadaiwa pia kuwa Imaam Ahmad hakukataa misingi ya kuwepo Ijmaa'. Hili si kweli kwa sababu Shaykh alikuwa na msimamo kama ilivyo msimamo wa Madh-hab ya Hanbaliy. Imaam Abu Zahra anasema, ‘Imepokelewa kutoka kwa Ahmad kuwa hakuna mtu anaweza kujivua na hali ya Qiyaas kama vile ilivyokuwa ikitumiwa na Swahaba”.
Mara baada ya Imaam Hanbal kuweka msimamo huu wa Ijmaa', wafuasi wa madh-hab ya Hanbal wanaufuata bila shaka. Qiyaas kilitumika kila mara palipotokea jambo jipya ambalo hawakuwa na uwezo wa kufanya marejeo kwenye Hadiyth au hawakupata athari ya Maswahaba au maneno yao .[3]
5- Madai kuwa viongozi wa madhehebu nyingine hawana nafasi ya kutoa maoni au uongozi kwa 'Mawahabi' na wafuasi wao si Waislamu; pia
6- Na kauli ya “Yeyote asiyekubali kujiunga na harakati za 'Uwahabi' ni kafiri” tunasema hivi:
Kauli zote mbili ni za uongo wa kutunga. Shaykh ‘Abdullaah, mtoto wa Shaykh Muhammad Ibn 'Abdil-Wahhaab, aliandika risala baada ya kuingia Makkah akiwa ni mshindi wa madh-hab wakiwa wameongozana na Mwana wa Mfalme, Sa’uwd bin ‘Abdil-‘Aziz siku ya Jumamosi, Tarehe 8 Muharram, 1218 akiwa amesema haya yafuatayo:
“Madhehebu yetu kwa misingi yote ni madhehebu ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah. Njia zetu zote ni njia za Salaf, (wakongwe) wachaji Allaah wa Mwanzo katika Uislaam. Sisi tuko katika msimamo aliokuwa nao Ahmad bin Hanbal, lakini hatumkatai yeyote anayefuata moja ya madhehebu manne za imaam…”
Na pia anaendelea kusema:
“…Watu wote wanaotuzulia uongo ili wafiche ukweli na kuwapa watu hali ya uongo; wanawafanya watu waamini kuwa tunateremsha hadhi ya Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema kuwa sisi tunafundisha kuwa hakutakuwa na shafa'ah (yaani Nabiy atawaombea watu wake na watu wa ummah nyingine na kuwa si rukhsa kuzuru kaburi lake; pia hatutegemei kauli za 'Ulamaa wa madhehebu; na kuwa tunawaona kuwa watu wote ni makafiri kwa sababu hawajajiunga na harakati za Muhammad ‘Abdul-Wahhaab na tunawakaza watu wasitoe Salaam kwa Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia hatutambui haki za Ahlul Bayt, kwa madai yote haya jibu letu ni:
“Subhaana-Allaah! Huu hakika ni uongo mkubwa.”
Hivyo basi yeyote yule anayenasibisha fikra hizi kwetu anakuwa anatunasibisha sisi na fikra za uongo.[4]
7- Madai kwamba Shaykh Ibnul ‘Abdil-Wahhaab hakuwa anaamini kuwepo kwa shafaa'h ya Nabiy (swala Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala wachaji Allaah hawatopata fursa ya kufanya shafa'ah. Jibu letu ni kuwa, mwandishi wa makala hii alikuwa bila wasiwasi wowote haelewi tofauti zilizopo katika ya shafa'ah mbili; Shafa'ah ya kwanza ni shirki (ambayo ni yeye mwenyewe anafanya kuomba anafanya shafa'ah). Ya pili ni shafa'ah ambayo inakubalika kwa sababu hawezi kuifanya bila idhini wala ridhaa ya Allaah na hiyo ni Siku ya Qiyaamah, jambo ambalo Shaykh alikuwa analisema na kulitangaza, kwamba Nabiy atafanya hivyo kwa sababu ameteuliwa na Allaah na shafa'ah hiyo kwa heshima yake.[5] Na hao wapinzani wa Shaykh kama wanadhani kuwa Shaykh alikuwa anakataza wasyilah kupitia Rusuli na wachaji Allaah, jibu letu ni kuwa watu wengi hawakuwa wanafahamu misimamo ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab na Imaam Hanbal juu ya kadhia hii na mwisho wake ni kutoa tuhuma za uongo usiokuwa na ukweli. Shaykh Ibn Taymiyyah amesema kuwa kufanya tawasul kupitia kumwamini Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa kumpenda Nabiy na kwa kumfuata maamrisho yake kwa kuiga matendo yake na kauli zake na kumtii yeye ni kitu ambacho kinakubalika na vikundi vyote viwili vya Waislamu Lakini tawasul kupitia Nabiy ni vizuri ijulikane kuwa ni jambo nyeti na utata na upinzani ukizuka basi jambo hili lirejeshwe kwa Allaah na Nabiy Wake.[6]
8- Na Madai kuwa 'Mawahabi' wanakataza kuzuru makaburi kwa kusema kuwa hilo ni haram, jambo hili litajadiliwa hapo baadaye. Wakati maoni ya Goldziher yatakapokuwa yanajadiliwa.
9- Na kauli kuwa 'Mawahabi' wanasema kuwa ni haraam kuapa kwa kitu kisichokuwa Allaah, hiyo ni kauli ya kweli na hilo limethibitishwa na Hadiyth sahihi. ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema kuwa Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wasallam) amesema: “Mtu yeyote atakayeapa kwa jina lilisokuwa Allaah basi atakuwa amefanya tendo la shirki” Hadiyth hii imepokelewa na [At-Tirmidhiy] ambaye aliipa daraja ya kuwa ni hasan. Hadiyth hii pia ilipewa daraja ya sahihi na [Al-Haakim].
Pia Ibn Mas’uwd alisema, “Ni bora kwangu kuapa kwa Jina la Allaah wakati naongopa kuliko kuapa kwa asiyekuwa Allaah kwa jambo la kweli.[7]
10- Inaaminika pia kuwa Ibn ‘Abdil-Wahhaab alisema kuwa viapo kwa majina ya wale ambao si Allaah ni haraam, na nyama zilizochinjwa makaburini kwa majini ya wachaji ni haraam. Hayo ni sahihi kabisa, kwa sababu hayo ni kutokana na mafunzo halisi ya Uislaam, na kila Muislamu anapaswa kuamini hivyo. Shaykh kaweka Mlango maalumu kwa jina la: “Ni Haraam kuchinja mnyama katika eneo ambalo huchinjwa wanyama kama kafara kwa vitu vingine visivyokuwa Allaah.” Mlango mwingine unasema, “Kuapa kwa jina la asiyekuwa Allaah ni Shirk.” Milango yote inatoa hoja za kutoka ndani ya Qur-aan na Hadiyth juu ya usahihi wa kauli hiyo ya Imaam.
Goldziher
Na sasa tunakuja kwenye maandishi ya Mjerumani ambaye alikuwa ni Mustashriq[8] Ignaz Goldziher katika maandishi ya “Muslim Studies”? Masomo juu ya Uislaam. Muslim Studies ilipatikana katika mijalada miwili (two volumes) katika lugha ya Kijerumani mwaka 1889 na kutafsiriwa katika Kiingereza mwaka 1967. Mwandishi huyu aliandika mlango mmoja mrefu wenye kurasa 96 ambao aliuita “Kuwatukuza Mawalii katika Uislaam”. Alizungumza kwa kirefu sana juu ya miujiza ya mawalii kwa Waislamu wakiwa hai au wakiwa ni maiti. Pia katoa mifano mingi sana ya kutukuza makaburi kutoka mandiko ya Kiislamu na tabia za Waislamu kwa ujumla. Lengo lake ni kuonesha kuwa hakuna tofauti ya Uislaam na Ukristo katika kuwatukuza mawalii. Akirejea aayah za Qur-aan na Hadiyth zinazopinga hali hiyo anasema:
Baada ya haya yote hakuna haja ya kueleza kwa kirefu kuwa ndani ya Uislaam katika asili yake kulikuwa hakuna nafasi ya kuwatukuza mawalii kama ilivyokuja kutokea na kuendelea hapo baaadaye. Qur-aan inakataza kuwatukuza mawalii katika kauli isemayo kuwa:
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ
Wamewafanya Wanazuoni Marabai wao wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah, [At-Tawbah: 31]
Kisha anamnukuu Karl Hase juu ya ukuzaji wa mawalii kwa kusema:
Hii ilikuwa ni njia ya kujaza pengo kati ya dini zinazoamini Allaah Mmoja na dini za miungu wengi[9]
Baada ya mwandishi huyu kuwa ameingiza mifano mingi ndani ya maandishi yake juu ya kutukuza mawalii kama ilivyo kawaida ya Waislamu wa kawaida na jinsi wanavyoyazuru makaburi kwa ajili ya kuomba ili kuondokana na haja zao, pia ametoa mfano wa wasomi wa Kiislamu ambao walipinga mfumo huo wa Shirk. Anamnukuu Imaam Ibn Taymiyyah katika kadhia ya tawasul na kuondoka kwenda kwenye maziara ambayo si Misikiti mitatu. Anasema:
Hii inaonesha kuwa 'Uwahabi' ulikuwepo hata hapo kale na pia 'Uwahabi' ulionesha hali halisi ya Uislaam. Kutokana na mwangalio huo ni vizuri kwa Waislamu wajaribu kuangalia hali ilikuwaje hapo kabla ya 'Uwahabi', utamaduni ulikuwaje na vipi dini ya Allaah Mmoja ilivyokuwa inapambana na ushirikina wa miungu wengi, vitu ambavyo viliingia kutoka mababu zao au viliingizwa kutoka nje kabisa ya maeneo ya Kiislamu. Yaani hali ya upagani ilijipenyeza vipi katika Uislaam. Kuna haja ya kutaja kitu kimoja ambacho kilitokea karibu karne sita au saba hivi kabla ya 'Uwahab'i haujaibuka hapo mwaka 1711. Hili ni tukio liliopata kuzuka katika Msikiti wa Mu’ayyad, huko Cairo. Siku moja jioni ya mwezi wa Ramadhwan. Kulikuwa kunaelezwa habari za Bwana Birgewi. Basi alisimama kijana mmoja ambaye alikuwa anajulikana kwa jina la Rumi na kwa nguvu kabisa akasema kwa hamasa zote dhidi ya tabia ya kuwatukuza mawalii na kuzuru makaburi ya mawalii na akasema kuwa Uislaam wa namna hiyo ni ushirikina. Alisema, Hivi nani alipata kuona hayo maandiko ya watu waliopita kabla yetu? Hakuna. Hata Nabiy Mwenyewe. Haya yote makaburi ya mawalii lazima yaharibiwe, wale wanaobusu majeneza ni makafiri, makazi ya mawalii na nyumba nyingine za namna hiyo lazima zivunjwe na hao madaruweshi lazima wasome badala ya kuwa wanacheza ngoma” Ilitolewa fatwa baadaye ya kupinga kauli yake huyo kijana na baadaye kijana huyo alitoweka kabisa mjini Cairo katika mazingira yasiyojulikana. Hao 'Ulamaa, hawajaacha kupamba makaburi ya mawalii wao na kusema kuwa wale wanaoyapinga hayo ni wapuuzi.”[10]
Lengo la mwandishi hapa ni kuonesha kuwa 'Uwahabi' una msimamo kama jinsi asili ya ya Uislaam ilivyo kuwa wanakataa hali ya kuzuru makaburi ya mawalii na pia wanakataza hali ya kuomba kutoka kwa maiti kwa sababu dini ya Uislaam haijapata kuruhusu jambo hilo. Kwa kuangalia kidogo kitabu cha Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab “Kadhia za siku kabla ya Uislaam” inatosha kuonesha kuwa Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), alipinga tabia za kijahiliyyah yaani za mila kabla ya Uislaam kuja. Kitabu hiki kina mambo kadhaa kama vile Sura zifuatazo:
- Kufanya makaburi ya watu wa kale kama mahali pa ibada
- Kuchukua makapi ya vitu vilivyokuwa vya Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuvifanya Msikiti au sehemu ya Msikiti.
- Kuwasha taa na mishuma kwenye makaburi
- Kuweka siku maalumu ya kuzuru makaburi
- Kutoa kafara au kuchinja wanyama karibu ya makaburi
- Kuchukua baraka kutoka kwa watu ambao wanadhaniwa kuwa walikuwa watukufu au mawalii.
Katika kitabu hiki anaonesha katika sura tulizozitaja hapo juu kuwa kwa kutumia Hadiyth kuwa watu wa Jahilliyah (kabla ya Uislaam) waliyachukua mambo hayo kutoka kwa Ahlul Kitaab; Mayahudi na Wakristo Uislaam ulikuja kuyavunjilia mbali mambo hayo, lakini yakawa yamerejeshwa tena miongoni mwa Waislamu na hivyo kulikuwa kuna haja ya kuusafisha Uislaam tena kwa kuyaondoa hayo ambayo alikuja Nabiy akayaondoa.
Hapa hebu tunukuu kauli ya wazi kabisa ya Mfalme ‘Abdul-Aziz bin 'Abdir-Rahman Aal Su'uwd katika mzozo uliotokea India mwaka 1924, ambapo aliulizwa nini hukumu ya kujengea upya makaburi. Aliwajibu hivi:
Sisi tunajishughulisha na kutengenza sehemu takatifu na kuziweka katika hali ya heshima na nzuri. Ama kuzijenga tena upya tutafanya hivyo kufuatana na shari'ah ya Kiislamu inavyoruhusu. Ni wajibu wetu kutimiza amri za Shari'ah katika sehemu takatifu kama zilivyoelezwa na wazee wetu waliotangulia katika (ummah huu) na kama wanavyoainisha maimaam wanne. Niko tayari kuzijenga hizo sehemu takatifu hata kwa dhahabu na fedha iwapo 'Ulamaa watasema kuwa kufanya hivyo ni wajibu wangu.[11]
Hata hivyo Goldziher ananasibisha jiwe jeusi katika Ka’abah kuwa ni mabaki ya ushirikina uliokuwepo kabla ya Uislamu. Hilo tunalipinga na kulikataa na tutatumia maneno ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allahu ‘anhu) ambaye alisema wakati analibusu: “Najua kuwa wewe ni jiwe tu ambalo halitii faida wala halileti hasara. Laiti nisingelikuwa nimemwona RasuluLlaahi anakubusu nisingelikubusu.[12]
Hali kadhalika kauli za Goldziher juu ya bid’ah siyo sahihi:
“Msimamo mkali na mutwatwarifina upo kwa 'Mawahabi' kwa kutaka kufuata Sunnah, hata katika mambo madogo madogo wao wanakuwa na msimamo mkali hasa kama vitu kama vile bid’ah. Uwahabi wa kisasa unafuata mfumo wa kale katika kuviita vitu kuwa ni bid’ah, si vile tu ambavyo vinapingana na Sunnah bali hata vitu ambavyo haviangukii katika mkondo huo wao wanaviita bid’ah tu. Ni wazi kuwa uhafidhina umekuwa ukipinga kila kitu kipya, wanakataza kutumia kahawa na tumbaku pamoja na kuchapisha kwa mashine yote hiyo chini ya msimamo mmoja tu. Hata hivyo Waislamu wa leo wanatofautiana katika kutumia kisu na uma (wakati wa kula)[13]
Inapaswa ifahamike kuwa inajulikana kuwa kitu kuwa ni bid’ah haitegemei hali ya watu walivyo; wakiwa wana furaha au wamechukizwa, sivyo, bali kuna msingi yake iliyo wazi kabisa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Yeyote anayezusha jambo katika jambo (dini) letu hili, jambo ambalo hali uhusiano na hili (Uislamu) basi litatupiliwa mbali” [14]
Hali kadhalika alisema vile vile, “Yeyote atakayefanya jambo si katika mambo yetu (Uislamu) basi litakataliwa”[15]
Hadiyth za Bid’ah:
Hivyo suala zima la bid’ah linahusiana na mambo ambayo yasiyokuwa ya kidini. Jambo hili linatawaliwa na masharti kadhaa ambayo yanafanya kitu kuitwa kuwa ni bid’ah ni jambo gumu kinyume na vile yule mjerumani anavyotaka kuonesha watu hali ilivyo na kuyanasibisha mambo hayo yote kwa 'Uwahabi'.
Arberry
Dini za Mashariki ya Kati
Kwa ujumla maoni juu ya Arberry jinsi mamlaka ya Saudia ilivyoanza na maelezo yake juu ya harakati za Muhammad ‘Abdul-Wahhaab yanakubalika. Lakini maelezo yake ya mwisho juu ya Uwahabi kuna haja ya kujadiliwa
Anasema:
"Mawahabi wanaweza kuendelea katika hali ya kujirekebisha kwa muda gani bila kupoteza hali yao halisi ya asili. Hilo linategemea mambo vitu vingi hasa juu ya uzuri na uwezo wa uongozi na hali ya kiujumla ya mawahabi. Kuazima fikra kutoka mashariki na magharibi na kuziingiza katika mfumo wao kutaendelea na iwapo wao watakuwa imara na kubakia na fikra zao basi hawawezi kulegalega na wataweka hali yao katika mfumo wa asili na hapo ndipo watakapokuwa na uwezo wa kuendeleza dola yao kama ambavyo ilivyo asisiwa na wazee wao katika imani ambayo waliijenga.”[16]
Arberry pia anajadili kama Sayyid Ahmad Ash-Shahiid (1786-1831) aliathiriwa na 'Uwahabi' alipokwenda kufanya Hija huko Makkah. Arberry anasema kuwa wazo hilo alianza kulipata kwa mara ya kwanza kutoka kwa W.W. Hunter katika kitabu cha “Indian Mussulmans” na wazo hilo lilipingwa na Sayyid ‘Abdul-Baariy katika kitabu chake "Siasa za Sayyid Ahmad Barelwi" na pia lilipingwa na Sayyid Mahmud Hussayn ndani ya kitabu cha “History of the Freedom Movements”.
Arberry anajumuisha kwamba harakati za Ahlul-Hadiyth nazo zilituhumiwa kuwa na hali ya 'Uwahabi' ndani yake katika kipindi cha mwisho wa karne ya 19. Kauli yetu kwa maoni haya ni kuwa hali mpya ya dola ya Saudia ilianza mwanzoni mwa karne ya 20 wakati ambapo uongozi wake ulianza harakati na juhudi za kutaka kuunganisha maeneo yote ya nchi za Khaliji ya Arabia na wakafanikiwa kwa baraka za Allaah.
Mamlaka ya Saudia ilifanikiwa kuweka uhusiano wa karibu na majirani zake na ukweli ni kwamba wakati huo nchi zilizokuwa ni marafiki kwa Saudi zilikuwa ni nyingi kuliko zile ambazo zilikuwa na uhusiano wa mbali, maadui na wapinzani wake.
Pia ni ukweli kuwa katika historia ya Mamlaka kulikuwa na mashiko makubwa juu ya ‘Aqiydah ya Tawhiyd na walikuwa wanapinga kila hali ya kufanya Shirk na ushirikina na hali hiyo bado ipo na inaonekana wazi wazi na inaendelea kama ilivyoanza wakati walipoasisi harakati hizo za Shaykh miaka 200 iliyopita. Siri ya mafanikio hayo ni ile hali ya kupambana na shirk na ushirikina pia na Tawfiyq ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Maoni ya Arberry kwamba Sayyid Ahmad Shahiyd aliathiriwa na uwahabi alipokwenda Hija pia yametajwa na Morgoliuth. Mwandishi maarufu, Mas’ud Alam An-Nadawi alisema haya juu ya hilo:
“Na hali kadhalika hali ya kutiwa nguvu upya harakati za Uislamu na Imamiy ambazo zilianza India zilikuwa zinafanana na harakati za Najd kiasi ambacho hata wale waliokuwa wanaunga mkono harakati hizo walidhania kuwa harakati hizo zilikuwa ni kitu kimoja.”
Hali ya kufanana kwa harakati hizo si kitu cha ajabu kwa sababu asili ya harakati hizo ni Qur-aan na Sunnah. Lakini harakati hizo zina mifumo ambayo imetofautiana na namna ya ulinganiaji na jinsi ya kuendesha shughuli japo kuwa wanakubaliana katika mambo ya msingi. Harakati za kuhuisha Jihaad ambazo zilianzishwa na Sayyid Ahmed Shahid (alifariki 1246) hazikuwa zimeathiriwa na harakati za Najd.[17] Hali kadhalika Ahlul Hadiyth wa India nao waliitwa kuwa ni 'Mawahabi' kwa sababu nao harakati zao zilikuwa kupinga Shirk na kupambana na mambo ya uzushi (bid’ah) na ushirikina miongoni mwa Waislamu.
Munjid/ Encylopaedia Britannica
Munjid wa Birtannica: Harakati za 'Uwahabi' chini ya Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab, zinaelezwa kama alivyokuwa anadai mwandishi wa makala hiyo hivi:
“Baada ya kukamilisha masomo yake rasmi katika mji mtakatifu wa Madiynah, huko Arabia, ‘Abdul-Wahhaab aliishi nje ya nchi kwa miaka mingi. Alifundisha kwa miaka minne huko Basra, Baghdad huko Iraq ambako alimuoa mwanamke aliyekuwa na uwezo wa mali. Alipofariki yule mama alirithi mali hiyo. Mwaka 1736 alianza kufundisha Iran vitu vilivyokuwa vinahusiana na Usufi.”[18]
Makala hiyo imemalizia kwa kuzungumza vitu vinavyomzungumzia vizuri tu Shaykh ‘Abdul-Wahhaab na wafuasi wake walikuwa wakijiita kuwa ni "Muwahiduwn" Jina la 'Uwahabi' lilikuwa ni jina ambalo liilitengenezwa na wapinzani wao.
Uzushi kuhusu safari za Shaykh zimenukuliwa kutoka kwa Morgoliouth. Huyu bwana katika makala yake katika Munjid wa Encyclopaedia of Islam alizua kuwa Shaykh alioa mwanamke mwenye mali huko Baghdad ambaye alimrithi baadaye mali elfu mbili.
Kisha alisafiri kuelekea Kurdistan, Hamadan, Qum na Isfahan. Waandishi wengine kama Palgrave, Zwemmer na Brigges katika maandiko yake, “Brief History of Wahhabis” nao pia wamedai kuwa Shaykh alisafiri mbele zaidi ya Baghdad na Damascuss. Lakini madai haya yote ni uongo kwa sababu hakuna ushahidi wa Shaykh kuwa alisafiri mbele zaidi ya Basrah kwenda Baghdad, Syria na Misri.[19]
Ameer Ali
Ameer Ali: 'The Spirit of Islam'
Mwandishi wa kitabu hiki alikuwa katika Halmashauri ya Mahakama ya Serikali ya Mfalme wa Uingereza Nchini India mapema mwa karne ya 20 (ambapo India ilikuwa chini ya Uingereza kama koloni), na anasema:
“Huko Najd, chini ya utawala wa Mawahabi ambao waliitwa kuwa ni Mawahiduna wa Kiislamu, watu wasiotaka kubadilika walichapwa viboko msikitini. Na leo chini ya utawala wa Ibn Saud, wafuasi wake ambao wanajiita kuwa ni Ikhwan au ndugu katika imani wanafuata njia zile zile za kuendesha dini na ibada zake. Swalah kwa jamaa ikiwa ni jambo la lazima na hali inapelekea kuwepo Imam kuwa nalo ni lazima.[20]
Akijadili juu ya Azariqa ambao ni kikundi miongoni mwa Khawaarij, Ameer Ali anasema,
“…Miongoni mwa watu hawa Azariqa ni watu ambao wana msimamo mkali wa kipekee yao peke yao tu. Wanaona kuwa kila asiyefuata mwelekeo wao wa dini ni kafiri, na anapaswa kusilimishwa kwa nguvu au auwawe. Hakuna huruma kwa makafiri au mushriki (na hao wakiwa pamoja na Waislamu wasiokuwa wao, Wakristo na Mayahudi) Kwao wao kila dhambi ina daraja moja: kuua, uzinzi ulevi, kuvuta yote hayo ni makosa yaliyolaaniwa dhidi ya dini. Wakati Waislamu wengine wakiwemo Shia na Sunni wanasema kuwa kila mtoto anazaliwa katika fitrah na anabakia hivyo mpaka aharibiwe na elimu atakayopata, Azariqa wanasema kuwa mtoto wa kafiri ni kafiri. Wakristo wa Othodoksi wanasema kuwa mtoto kama hajabatizwa bado hajawa miongoni mwa Wakristo: Hawa Ma-Khawariji nao kama wakristo nao wanasema kuwa kila mtoto ambaye hajasema Shahada bado hajaingia katika uongofu. Hawa Ma-Azariqa walimalizwa na Hajjaaj bin Yusuf, lakini hali hiyo ilijitokeza tena ilijitokeza karne tisa baadaye chini ya Uwahabi.”[21]
Kisha anasema tena,
Mawahabi wamelezwa katika sura nzuri na Bwana Pelgrave ambaye alitembelea nchi za Arabia ya Kati, lakini ukweli ni kwamba hawa ni kizazi cha Azariqa ambao baada ya kuzidiwa nguvu na Hajjaaj ibn Yusuf walikimbia katika sehemu za Arabia ya Kati. Msimamo wa ‘Abdul-Wahhaab unafanana kabisa na msimamo mkali wa wafuasi wa Nafi bin Azraq. Kama hao watangulizi wao, Mawahabi wanawaona Waislamu wasiokuwa wao kuwa ni makafiri na halali kwa kuwapiga vita na kuwatia utumwani. Mwangalio wao wa kidini na jinsi wanavyoendesha dola si sahihi kwa sababu wanapingana na hali ya maendeleo na usongaji mbele.[22]
Sisi tunasema hivi kwa hayo:
i-Miongoni mwa madhehebu tofauti za Kiislamu hakuna msimamo tofauti juu ya ulazima wa Swalah. Bali kuna tofauti ndogo ndogo ambazo ni kuwa je Swalah hiyo iswaliwe Msikitini au la. Wengine wanasema kuwa ni lazima iwapo atakuwa Muislamu huyo anaishi karibu na Msikiti ambapo anaweza kusikia adhana. Ni katika siku za hivi karibuni tu ndipo imeonekana kuwa jambo hili, limelegezewa mwangalio. Al-Ikhwaan waliweka msimamo mkali kwa yule atakayekwenda kinyume na hilo ambao ni wavivu kuhudhuria jamaa Msikitini na hilo ilikuwa ni kujaribu kuzuia hali iliyoanza kujitokeza ya watu kulegeza hali ya kuswali katika Jamaa'ah lau kama Msikiti uliokuwa karibu. Hali hiyo ilikuwa haihitajii adhabu na msimamo mkali, kwa mfano leo huko Saudia, watu wanajaa Misikitini japo kuwa hakuna kiboko.
ii-Risala ya Shaykh HamAad bin NaasWir bin ‘Uthmaan Ma’mari An-Najdiy (alifariki 1225 H) inatoa ruhusa ya kuwapiga vita wale ambao hawaswali kwa sababu ya uvivu. Anatoa taarifa ya Ijmaa' isipokuwa aliyekuwa na msimamo huo ni Imaam Adhw-Dhwaahiriy. Na huu ndio msimamo wa madhehebu ya watu wa Hanbal. Na watu wa Najd wana msimamo kuwa yeyote aachaye Swalah kwa makusudi ni kafiri.[23]
iii-Kauli ya Ameer Ali ya kuwa Mawahabi na Khawaarij wanafanana si kauli ngeni. Zayn Dahlaan alikuwa na msimamo huo na alichukua Hadiyth ambazo wanazozitumia Khawaarij kama hoja zao na kuzitumia kuwafananisha na wanaowaita 'Wahabi' katika kitabu chake kiitwacho “Ad-Durrar As-Sunniyah' na “Al Futuwhaat Al-Islaamiyyah.”[24]
Kauli ya Ameer Ali inayoelezea juu ya kufanana kati ya 'Mawahabi' na Khawaarij, sana sana wa Azariqa, inaonyesha ujinga mkubwa juu ya kufahamu itikadi ya Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab, ambayo ni uhuishaji wa mafundisho sahihi ya Salaf. Hebu tuangalie ukweli wa madh-hab ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.
a) Khawaarij wanatangaza kwamba mtu yeyote atakayetenda madhambi makubwa ni kafiri. Shaykh anaona kuwa mtu kuwa kafiri ni kutoka na ijimaa' ikiwa na dalili dhahiri inayothibitisha kuwa mtu ni kafiri. Shaykh aitakidi kuwa mtu ni kafiri kama hamna dalili yenye kuthibitisha hilo. Kwa mfano kauli yake kuhusu wanofanya madhambi makubwa kwa mfano; ulevi wa pombe.
Kama watu hawa watazidi kung'ang'ania vitu ambavyo ni haraam na kuvigeuza kuwa ni halali, watakuwa na nembo ya ukafiri. Ikiwa wataamini kwamba ni haraam na wakatenda ya haraam basi wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko. Watangu wema (Salaf) hawakumuona na kumuhesabu mtu kuwa ni kafiri kwa mtu kuyachukuwa ya haramu na kufanya ni ya halali yake, hadi ukweli utakapobainika kuhusu watu hawa. Lakini ikiwa wataendelea na dalili hizi zikapatikana yafaa watu hawa kuitwa ni makafiri.[25]
b) Khawaarij wanaona kuwa ni halali kuwapiga waasi. Kuhusu hili Shaykh anasema "Ama kuhusu mambo ya vita na kupigana, hatupigani na mtu yeyote isipokuwa ni kulinda heshima na maisha yetu. Watu hawa wametuvamia katika ardhi zetu, hatuna uchaguzi wowote. Tunaweza kupigana nao kwa lile waliotufanyia sisi. Qur-aan inatuelezea kuwa:
فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ ۚ
Basi anayekushambulieni nanyi mshambulieni kwa kadiri ya alivyokushambulieni. [Al-Baqarah: 194]
kwa maana hiyo tunaweza kupigana na wale wenye kuitukana Dini ya Nabiy wetu Muhammad (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), baada ya kuikubali.[26]
iii) Makhawaarij walijulikana kama wapingaji wa viongozi wa Kiislamu. Waliimuua ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), mmoja katika Makhalifa waongofu. Katika imani ya Salafi ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab. Mwandishi anasema "Anaamini wajibu wa kuwatii maimaam ikiwa maimaam hao ni wachaji Allaah au waasi, muda wa kwamba hawawataki watu wasimuabudu Allaah. Ikiwa mtu amekuwa Khalifa, au ameupata ukhalifa huo kwa kutumia nguvu, basi ni wajibu kumtii, ama kumfanyia uasi mtu huyo ni haraam[27]
iv) Moja katika sifa za kipekee za Azariqa ni imani waliyonayo kuwa watoto wa makafiri nao ni makafiri. Ili kujua itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jamaa'ah na wafuasi wa Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab, tunatoa hapa fatwa ya Mwanachuoni wa zama hizi, 'Allaamah Shaykh ‘Abdul-'Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu) kuwa amesema:
"Kulingana na maelezo ya Wanachuoni, Mtu ambaye Da'wah haikumfikia, kwa sababu mojawapo; labda alikuwa mbali na Uislaam na Waislam (hakupata kujua Uislaam wala kuusikia), au kwa sababu alipofikia baleghe alishaharibikiwa na akili yake, au watoto wa makafiri ambao nao wangali bado ni watoto, watu wote hawa watawekwa kwenye mtihani siku ya hukumu. Watakaopita mtihani huo wataingia Jannah. Ama ambao watafeli mtihani huo basi makazi yao yatakuwa motoni. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuhifadhi na siku hiyo na Atuhifadhi na moto wa Jahannam.
Kwa kuwepo kwa Hadiyth nyingi sahihi kuhusiana na suala hili, rai sahihi ni kuwa watoto wa makafiri ambao walikufa kabla ya kufikia baleghe ni kuwa wataingizwa Jannah.[28]
v) Ameer Ali anakubali na kukiri 'Mawahabi' wanapinga kumshabihisha Allaah.
Anaelezea kutoridhishwa na utawala wao, lakini haelezi vile vile sababu iliyompelekea hivyo. Mamlaka ya Saudi Arabia imesimamia kuwepo kwa utawala wa Shari'ah na kusimama Dini ya Allaah. Katika jumla ya neema za utawala huu ni: kuwepo kwa utulivu, amani, katika sehemu zote za utawala wao. Nchi imepiga hatua kubwa katika maendeleo na teknolojia kwa haraka kabisa. Lau Ameer Ali angeendelea kuishi hadi sasa hivi angeshuhudia upotofu wa utabiri wake aliokuwa nao.
Kumbukumbu za Humphrey
Kitabu hiki (kitabu cha 30 kinachoelezea kumbukumbu za Humphrey) kilifasiriwa katika lugha ya kiurdu huko India, mchapishaji alidai kuwa Humphrey alikuwa ni jasusi wa Kiingereza, ambaye kazi yake kubwa ilikuwa kufanya ujasusi dhidi ya dola ya Ottoman na ukhalifa wake katika karne ya 18. Bwana huyu alijificha katika kitambulisho cha Uislaam na alijifunza lugha ya Kiarabu kisha alisafiri hadi Basra alipokutana na Shaykh, Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab. Walipokutana wakazoeana na wakawa marafiki wakubwa. Mchapishaji anadai kuwa kumbukumbu hizi zilibaki mafichoni hadi zilipokuwa katika mikono ya wajerumani wakati wa vita vya pili vya dunia, na ndipo alipozipata na kuzichapisha kama ni njia za kuponda na kuukashifu utawala wa Kiingereza. Kumbukumbu hizi zilitarjumiwa katika lugha za Kifaransa, Kiarabu na Kiurdu. Msomaji wa kitabu hiki bila shaka ataona na kubainikiwa kuwa hivi ni visa na riwaya ya kufikirika tu, lengo si jambo lingine zaidi ya kumkashifu Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab. Ushahidi wetu katika kuonesha kuwa kitabu hiki ni mkorogo tu ni kutokana na sababu mbili zifuatazo: kwanza kabisa ni ushahidi wa Kihistoria kutokana na yaliyomo katika kumbukumbu hizo, na pili ni jitihada zetu za kutafuta bila mafanikio kazi ya asili ya kitabu hiki (maandiko ya asili kutoka katika lugha ya Kiingereza).
1-Tuanze na msafara wa maktaba ya Kiingereza kitengo cha vitabu adimu, kitengo hiki kina vitabu vilivyochapishwa kabla ya mwaka 1975. Kuna vifunguzi (entries) 72 chini ya jina Humphrey, lakini hakuna hata kimoja kinachohusiana na maudhui yetu hii. Tuliona kifunguzi kimoja chini ya kumbukumbu za Humphrey (iliyochapwa mwaka 1734), lakini kumbukumbu hizi pamoja na kuwa zimeandikwa hivyo hazikuwa za Humphrey huyo anayetajwa bali ni zilikuwa ni kumbukumbu za Duke wa Gloucester ambaye alikuwa amehifadhi kumbukumbu zake na familia tawala ya wakati wake. Mwandishi wa kitabu kilichobuniwa anaonesha kichwa cha habari katika moja ya kurasa zake inayoitwa, 'Ukoloni unaotakiwa' na 'Jasusi la Kiingereza katika nchi za Kiislamu' hatukuona kabisa kitabu hiki katika maktaba ile maarufu ya vitabu adimu, hata katika tafiti yetu ya kutafuta chini ya neno 'Jasusi' hatukupata chochote. Ugunduzi wa kompyuta umesaidia sana kupata upenyo wa kujua na kupata vitabu vilivyoadimika, hata hivyo tumejitahidi lakini hatukupata hata kwa kutumia njia hiyo; kwa jitihada hizo zilizotangulia tunahitimisha kuwa hakukuwepo na kitabu kama hicho, hata hivyo tulichonacho ni tarjama iliyotengenezwa na maadui wa Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab.
2-Humphrey anadai kuwa alisafiri hadi Istanbul katika mwaka 1710 akiwa na umri wa miaka 20. Alirejea London na akasafiri tena kwenda Basrah katika mwaka 1712 baada ya safari ndefu majini iliyodumu kwa muda wa miezi sita. Madai haya hayaingii akilini, safari ya majini kutoka London hadi nchi za Gulf haikuwa ndefu kiasi hicho. Alidai kuwa alikutana na Shaykh At-Taee, mmoja katika Ma-Shaykh wa Basrah. Kadhalika alidai kukutana na fundi seremala mwenye asili ya Ki-Iran ambae akiitwa ‘Abdul-Riza na ambae alianza kufanya nae kazi. Huko ndipo alipokutana na kijana aliyekuwa akizungumza Kituruki, Kifursi na Kiarabu na aliyekuwa akivaa joho la ki-uanafunzi aliyekuwa akijulikana kwa jina la Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.[29] Madai haya yalikuwa ni ya uongo kabisa. Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab alizaliwa mwaka 1703, alibaleghe akiwa na umri wa miaka 12 na ndipo baba yake akamwozesha. Baada ya kusafiri kwenda Hijaaz kwa ajili ya Hija, alirejea Najd na akakaa na baba yake ili asome kwake. Hakuwahi kusafiri kwenda kutafuta elimu ila ulipofikia mwaka wa 1722 aliposafiri kuelekea Makkah, kisha Madiynah na Basrah. Hakuna uwezekano wowote wa Shaykh na kisa cha kufikirika cha Humphrey kukutana Basrah kwani tarehe hazilingani. Wanachuoni wote waliofanya utafiti wa maisha ya Shaykh wanapinga madai haya ya Shaykh kusafiri kuelekea Uturuki na Iran. [30]
3-Kitabu kinadai kuwa Shaykh alionesha hamu ya kusafiri kwenda Istanbul, lakini alishauriwa na Humphrey kuwa asiende kwa kuogopa kuwa huenda akauawa na watawala wa dola ya Ottoman. Lakini alimshauri Shaykh badala ya kwenda Istanbul basi aende Isfahaan na Shaykh akafuata ushauri wake huo na akaenda Isfahaan. Huu nao ni uongo mwingine. Sayyid ‘Abdul-Haliym Al-Jundiy amenukuu kuwa, 'Al-Imam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab 'Kiongozi aliyehuisha njia ya Salafi' nilizungumzia suala hili na kumuuliza Shaykh Ibn Baaz, ambae alikataa kuwa Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab kusafiri kuelekea Kurdistan na Iran. Shaykh Ibn Baaz aliniambia kuwa habari hii alipata kutoka kwa Ma-Shaykh zake, akiwamo wajukuu wa Shaykh Ibn ‘Abdil-Wahhaab na haswa zaidi Shaykh wake mwenyewe, Muhammad bin Ibraahiym.[31]
4-Humphrey anadai kuwa Shaykh alianza Da'wah yake katika mwaka 1143 Hijriyyah. Huu ndio wakati pekee alipotumia tarehe ya Hijriyyah katika kitabu chake. Hii inathibitisha udhaifu wake wa hakika za kihistoria, kwani Shaykh alirejea Huraymilah miaka mitatu kabla ya kifo cha baba yake katika mwaka wa 1153, na ndipo alipoanza Da'wah yake baada ya kifo cha baba yake.
5-Kadhalika kuna ushahidi mwingine kuwa Humphrey alikuwa mbali na elimu ya Historia. Humphrey alisafiri kuelekea Istanbul katika mwaka 1710, akitoa sababu zenye kuweza kuonekana kuwa ni za kweli (ingawaje hazikuwa ni za kweli) kuwa Uingereza inakusudia kuyapa umuhimu mkubwa makoloni yake. Empire ya Uingereza ilikuwa ni pana sana na ilikuwa inapigiwa mfano kuwa jua lilikuwa halizami katika utawala wake. Pamoja na kuwa visiwa vya Uingereza kuwa ni vidogo lakini utawala wake uliotapakaa India, China na mashariki ya kati ulikuwa ni mpana na ilihitajika uongozi makini kutawala. Wizara ya makoloni iliamua kuwa na majasusi ili kukusanya habari kutoka katika nchi tofauti tofauti na ndipo hapo Humphrey alipohusishwa.[32] Kihistoria matukio haya si sahihi kuyanasibisha katika matukio ya mwanzoni mwa karne ya 18. Wakati huo India haikuwa koloni; kampuni ya East India ilianza safari zake za biashara katika karne ya 17 lakini hata hivyo haikuwa na nguvu za kisiasa hadi mwaka 1757 Bengal ilipotekwa. Biashara zilianza kupanuka pale pindi uongozi wa kampuni ulipohamishiwa moja kwa moja ukawa chini ya Uingereza katika mwaka 1898. Kwa hivyo basi, hakukuwa na koloni la India kabla ya mwaka 1710. Kadhalika Uingereza wakati huo haikuwa na koloni China; Hong Kong iliangukia katika utawala wa Uingereza katika suluhu ya mwaka 1898. Inathibitika kabisa kuwa mbunifu wa 'Kumbukumbu hizi za Humphrey katika kubuni kwake hakuzingatia hakika za kihistoria. Alitengeneza kisa chake hichi mwishoni mwa karne ya 19 wakati wa kilele cha utawala wa Muingereza duniani, pindi ilipokuwa kweli kuwa jua halizami katika utawala wake. Kufanya kwake hivyo amejinasibisha kuwa yeye ni mwandishi wa vitabu vya riwaya vya kubuni na si mwandishi anayeandika hakika za kihistoria za mtu.
6-Mwandishi ananasibisha matendo na maneno mengi kwa Shaykh ambazo zinapingana na imani yake, mafundisho yake na tabia za Kiislamu alizokuwa nazo Shaykh. Hakuna haja ya kujadili kashfa hizi zisizokuwa za msingi. Kwani tumeshathibitisha uongo wa kitabu hiki.
7-Ili kuyapa umuhimu kumbukumbu zile, mwandishi anatoa visa vya serikali ya Uingereza ya kuzuia umoja miongoni mwa Waislamu; lengo ni kuonesha tofauti za kiitikadi na kidini miongoni mwao, kadhalika na watu kuwa mbali na kujifunza lugha ya Kiarabu ambayo ni lugha ya Qur-aan na badili yake wakuze lugha zao za kitaifa na kujenga shule za mishenari ili kudhoofisha nafasi ya Waislamu kisiasa na kiuchumi.
Nimejaribu kuthibisha uongo wa kitabu hiki kihistoria na kwa uongo wa mwandishi mwenyewe, kwani naamini kuwa hakuna aliyeandika hapo kabla. Ukweli ni kuwa kitabu hiki (Kumbukumbu Za Humphrey) hakistahiki kusomwa ukiachilia mbali hata kukifanyia utafiti wa kina. Lakini kwa ajili ya kutekeleza majukumu na Amana niliyokuwa nayo nilipendelea nitoe mwanga kuhusiana nayo ili kubainisha uongo uliokuwepo ndani yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hujua nia za watu.
Arnold
Tumalizie waraka wetu huu kwa maelezo ya Prof. Arnold kuhusu harakati za 'Wahabi' katika 'Kueneza Uislaam':
"Kwa wakati huu kuna vipengele viwili ambavyo vinashughulika na harakati za kueneza Uislaam ulimwenguni na haswa katika ulimwengu wa Kiislamu. Cha kwanza ni jitihada za kuhuisha Uislaam katika maisha ya watu na jitihada hizi zinarejea tokea wakati wa Tajdidi za Wahabi mwishoni mwa karne ya 18; pamoja na kuwa harakati hizi zimeishia katika kusimamisha utawala wa kisiasa tu katika mipaka ya Najd[33], hata hivyo harakati nyingine zinaendelea Afrika, India na Malaysia hata kwa wakati huu tulionao, harakati hizi zimezaa harakati zingine ambazo zina nguvu katika ulimwengu wa Kiislamu. Katika kurasa zilizotangulia tumeona kuwa ni jinsi gani harakati hizi zilivyoathiri kuenea kwa mwamko huu; kilele cha hamasa kimepatikana na maisha mapya yanapatikana katika taasisi za Kiislamu, kwa hakika hii imesaidia kuhamasisha elimu ya itikadi na masomo yake na kuanzisha taasisi zake, yote haya yamesaidia kuamsha mwamko wa Kiislamu.”[34]
[1] Encyclopaedia of Religion and Ethics: Ed. By James Hasting (Edinburg) 12: 660-661
[2] M. Abu Zahrah: Taariykh Al-Madhaahib Al-Islaamiyyah, uk. 532.
[3] M. Abu Zahrah: Taariykh Al-Madhaahib Al-Islaamiyyah.
[4] ‘Abdullaah bin 'Abdir-Rahmaan bin Swaalih Al-Bassaam: 'Ulamaa Najd Khilaal Sitah Quruwn 1:51
[5] Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab: Kitaabut Tawhiyd, Baabu Ash-Shafaa'ah.
[6] Ibn Tayymiyyah: Majmuw' Al-Fataawaa: 264.
[7] Kitaabut-Tawhiyd: Baabu Qawli Allaahi Ta’aalaa:
فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا
Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye
[8] Msitashiriki 'Mustashriq' ni mtu wa ki-Magharibi ambaye anasoma habari za watu wa Mashariki, ikiwemo Uislamu na ulimwengu wa Kiislamu.
[9] Ignaz Goldziher: Muslim Studies, uk. 259.
[10] Rejea iliyotangulia, uk. 334-335.
[11] Salaahudin Yusuf: Qabari Parasti, uk. 193.
[12] Swahiyh Muslim
[13] Goldziher 34.
[14] Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, Ibn Maajah. Hadiyth iliyopokelewa na Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha).
[15] Musnad Ahmad, Swahiyh Muslim, kama ilivyopokewa na Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allahu 'anha).
[16] A.J. Arberry: Religion in the Middle East, uk. 281-282.
[17] Mas’ud An-Nadawi: Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab, uk. 199.
[18] The New Encyclopaedia Britannica 10: 510-511.
[19] An Nadawi uk. 40 Hamishi na 4.
[20] Ameer Ali: The Spirit of Islam, uk. 125-126.
[21] Ameer Ali: The Spirit of Islam, uk. 356.
[22] Ameer Ali: The Spirit of Islam, uk. 357.
[23] An-Nadawi: uk. 215.
[24] Ahmad Bin Hajar Al-Butami: Shaykh Muhammad ‘Abdul Wahab Uk 50
[25] Dr. Swaalih bin 'Abdillaah Al-'Abuwd: 'Aqiydat Ash-Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab As-Salafiyyah 1: 348.
[26] Rejea iliyotangulia, 1:348.
[27] Rejea iliyotangulia, 1:465.
[28] Shaykh ‘Abdul-'Aziyz bin Baaz: Majmuu' Al-Fataawa 8: 98.
[29] Rejea iliyotangulia, uk. 35.
[30] Dr. S. A Al-Abuud, 1:188.
[31] Rejea iliyotangulia, 1: 186.
[32] Humphrey, uk. 6.
[33] Tufahamu kuwa kitabu hiki kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1896 kisha kilichapishwa tena mwaka 1913. hata hivyo, huzungumzia nyakati zile kabla ya kuchapishwa kitabu
.