Vunja Jungu: Wamemfanya Allaah Ni Wa Ramadhwaan Tu!
Vunja Jungu: Wamemfanya Allaah Ni Wa Ramadhwaan Tu!
Abuu 'Abdillaah
BismiLlaahi waswalaatu wassalaamu ‘alaa RasuwliLLaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa ba’ad,
Ndugu Waislam,
Tunaukaribia mwezi Mtukufu wa Ramadhwaan. Mwezi wenye fadhila tele zisizohesabika idadi yake. Mwezi ambao ndani yake utakapofunga kwa Iymaan ya dhati na kuitakidi kuwa kuna malipo, basi utaghufuriwa madhambi yako yaliyotangulia. Mwezi ambao haufananishwi na miezi mingine kwa mavuno na ujira, du’aa ya mwenye Swawm haikataliwi, anapofunga Muislam huwa na furaha mbili; furaha wakati anapofungua na furaha wakati anapokutana na Mola wake. Mwezi ambao Swawm itamuombea shufaa mja siku ya Qiyaamah, itakaposema siku hiyo kumuambia Allaah, “Ee Rabb, nimemzuia chakula chake, na matamanio yake ya kimwili mchana kutwa, basi niache nimwombee Shafa'ah.”
Mwezi ambao ni hifadhi na kinga nzito kabisa ya mja kutokana na moto, na harufu ya mdomo wa aliyefunga (japo atakuwa anapiga mswaki) itakuwa ni bora kuliko harufu ya misk mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Atakayefunga siku moja katika mwezi huo akitaka radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ikiwa hiyo itakuwa ndio siku ya mwisho ya maisha yake, basi ataingia Peponi. Kuna mlango wa Jannah maalum kwa wale wafungao uitwao Ar-Rayyaan, ambao wataingia wao tu, na watakapoingia mlango huo utafungwa na hatoingia yeyote mwengine. Huo ndio mwezi ambao ni nguzo ya Uislam, ndani yake kunapatikana usiku mtukufu ambao ni bora kuliko miezi elfu moja, katika mwezi huo milango ya Jannah huwa wazi, milango ya moto hufungwa na mashetani hufungwa minyororo. Mwezi utakapofunga wote, Swawm yake ni sawa na kufunga miezi kumi. Na katika kila wakati wa kufutari, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huchagua watu wa kuwaweka huru na moto.*
Ndugu Muislam, baada ya kujua fadhila zote hizo za mwezi huu Mtukufu, badala ya watu kujiandaa kwa mambo mema ya kheri kama kuanza kujizoesha na Swawm za Sunnah kama zile za Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe n.k., au kutoa Swadaqah kwa maskini ili nao wapate maandalizi mazuri ya mwezi huo wenye baraka, au kujiandaa kwa kufanya mengi ya kheri ambayo yametanawai, kinyume chake kumekuwa kuna wengi wenye majina ya Kiislam ambao huukaribisha mwezi huu Mtukufu kwa kila aina ya maasi kwa jina la ‘Vunja Jungu’ kama ijulikanavyo katika maeneo mengi Tanzania, au ‘Mfungo’ kama inavyojulikana katika maeneo ya Sawaahil (pwani) ya Kenya.
Jambo hilo licha ya kuwa halipo katika Dini yetu hii tukufu na safi, bali ni jambo ambalo haliwezi kufanywa na Muislam mwenye Iymaan na khofu ya Mola wake na ndio maana tukawaita hao wayafanyao hayo kuwa ni Waislam jina.
Katika masiku ya mwisho ya Shaabaan, na haswa zaidi siku ile ya mwisho, watu hao hukusanyana na kufanya sherehe (party) kwa kusikiliza nyimbo na kucheza muziki na kunywa vinywaji vya haramu. Pombe siku hiyo kwa wale walevi ndio inanywewa kama kisasi, wengine ndio siku ya uzinzi kwa kuwa Ramadhwaan wanaogopa kuyafanya hayo, wale wavuta sigara ambao kidogo wanachelea kuvuta katika mwezi wa Ramadhwaan nao paketi zitavutwa kwa mfululizo, wala unga hali kadhalika na mengi mengineyo machafu huwa ndio siku yake rasmi hiyo. Bila kuwasahau wenye kwenda mapkniki na kutumbua.
Watu hao kwa kufanya hivyo, wanamkebehi na wamemfanya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa ni Muabudiwa wa Ramadhwaan! Ama miezi kumi na moja iliyobaki, haabudiwi wala haogopwi wala hafuatwi amri Zake na za Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Wengine ndio wanaukaribisha kwa kufanya manunuzi (shopping) ya mikeka ya kuswalia – maana miezi yote iliyopita, kwao Swalaah haikuwa ni fardhi kwao, kanzu hununuliwa kwa wingi, Misikiti huanza kushehena hadi inakuwa kero badala ya furaha kwa wale wenye kudumisha Swalaah za Jama’aah kwa miezi yote ya mwaka kwani hata nafasi za mbele walizozoea kuzipata huwa ni adimu au hata kukosa kabisa kwa hao wavamizi wa Ramadhwaan. Vilevile kina dada waliokuwa hawajui hata kuvaa Hijaab, basi utawaona wanaanza kununua leso za kujitanda, kanga zimeongezeka biashara, wanaojitahidi zaidi baibui nazo zimekuwa ni pato kwa wauzaji. Nyumba mbalimbali utaanza kusikia Qur-aan zikisomwa kwenye maredio, kofia na kanzu zimeanza kushamiri kwenye miili ya wengine. Hayo yote ni dhana ya wayafanyayo kuwa ni ‘heshima’ na ‘taadhima’ kwa mwezi huu. Ila walichoghafilika ndugu zetu hao, ni kuwa mafuhumu hiyo, ni mafuhumu inayoonyesha kuwa katika miezi iliyobaki, hakuna kinachowapasa wao kufanya hayo, hivyo, kumfanya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa Kuwepo Kwake na Uwezo Wake, Nguvu Zake na Amri Zake hazina uzito wowote ila Ramadhwaan tu. Nayo ni mafuhumu potofu na dhana iliyo ovu.
Ni wajibu wa jamii linapoonekana jambo lolote ovu, kulizuia, kulikemea au kulikasirikia na kulisusia endapo tutakuwa tupo katika udhaifu wa kutumia njia mbili za awali. Na hii ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 71]
Vile vile Hadiyth kutoka kwa Nabiy wetu mpenzi (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu basi akiondoe (akibadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Iymaan)) [Muslim]
Uongofu Ni Ule Wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Na Upotofu Ni Kuzusha Na Kutenda Maasi:
Muislamu inampasa afuate mafunzo yaliyo sahihi na kujiepusha na yasiyo sahihi kwani kufuata uzushi ni kumpotosha mtu na hatari yake ni kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kila khutbah yake:
Akisema katika Khutbah za Ijumaa,
((Amma Ba'ad, hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu cha Allaah, na uongofu ulio bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu)) [Muslim] na katika riwaayah nyingine ((na kila upotofu ni katika moto))
Na pia alieleza katika Hadiyth nyingine:
((Atakayezusha katika mambo yasiyokuwa (katika Dini) yetu basi itarudishwa [haitopokelewa])) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Uzushi huu wa Vunja Jungu ambao ni mchafu na ovu, ni jambo linalopaswa kukemewa na Waislam wote wa hali zote; Mashaykh, Maimaam, Maustaadh, walinganiaji na watu wa kawaida. Katika kila mnasaba na kila khutbah kukemewe hayo hadi jamii ifahamu ubaya wake na madhara yake na mwisho mbaya ambao unaoweza kumfika mtendaji wa tendo hilo.
Kila mwenye kuvunja jungu angepaswa ajiulize wakati anapofikiria kufanya uovu wake, kuwa kufanya hivyo ni kufuata mafundisho ya nani? Ikiwa hayo hayapo katika Dini, achilia mbali kumuudhi Muumba. Ajiulize pia, ana uhakika gani wa kuwa ataishi hadi kuikuta hiyo Ramadhwaan? Je, akichukuliwa katikati ya tendo lake ovu kama hilo anafikiria khatima yake ni nini? Kuna uhakika gani wa kuufika huo mwezi na kuumaliza na hata kughufuriwa madhambi hayo aliyoyatenda? Nani anayemiliki uhai mikononi mwake? Wangapi wenye siha wameondoka na siha zao? Wangapi vijana wameondoka na ubarubaru wao? Je, hawajiulizi yote hayo?
Na hao ndugu zetu wanapofikiwa na mawaidha haya, au wakapata kujua ubaya wa wayafanyayo, basi wasiwe wenye ukaidi wa kuyafuata na kuyafanyia kazi. Wasiwe kama watu wa zamani walivyokuwa wakipelekewa Manabii kuwatoa katika kiza cha kuabudu masanamu na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuwaingiza katika mwanga ya uongofu ulio na hoja za wazi, ikawa kila wakipewa mawaidha, wao hutaka kubakia katika ujinga na ukaidi wao kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٤﴾
Na haiwafikii Aayah yoyote ile katika Aayaat za Rabb wao isipokuwa huwa ni wenye kuipuuza. [Al-An’aam: 4]
Na Ndiyo maana pia wameambiwa katika Qur-aan baada yao na sisi pia kuwa tuende tukaone hizo athari za kuangamizwa kwao ili iwe funzo kwetu:
قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ ثُمَّ انظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿١١﴾
Sema: “Nendeni katika ardhi, kisha mtazame vipi ilikuwa hatima ya wenye kukadhibisha.” [Al-An’aam: 11]
Athari zao hizi nyingi zimejulikana kwetu kutokana na mafunzo haya ya Qur-aan lakini ni nani mwenye kutaka kutafakari na kujitoa katika upotofu na kupata uongofu? Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa hao wasiotaka kupata uongofu ni vipofu wa moyo:
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾
Je, basi hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo za kutia akilini au masikio ya kusikilizia; kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani. [Al-Hajj: 46]
Naam ndugu Waislamu, mwenye kupofoka macho anaweza kuwa na iymaan ya Dini, kwani wangapi waliokuwa vipofu lakini wamepata hidaaya? Wangapi wameweza kuhifadhi Qur-aan na hata kuwa ni ‘Ulamaa wakubwa wa Ummah na mifano ni mingi. Lakini wangapi waliokuwa na macho kamili lakini wakawa ni vipofu wa nyoyo; wakiwa wametawaliwa na upotofu na ufisadi?
Kuacha Maovu Ni Kufanya Jihaad Ya Nafsi Ambayo Ni Jihaad Bora Kabisa
Aliulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaaba, "Je, Hijrah gani iliyo bora?" Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: ((Ni kuhama yale Anayochukia Rabb wako Mtukufu)) [Swahiyh Al-Albaaniy kutoka kwa An-Nasaaiy]
Hivyo mwenye kuacha maovu kama haya ya uzushi wa Vunja Jungu bila shaka atakuwa amepata daraja ya kufanya Jihaad.
Na thawabu hizo ambazo usawa wake pia ni wa Hijrah pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kuzipata mtu atakapokuwa katika twaa'a wakati wa fitnah, nao ni kama wakati wetu huu uliojaa fitnah (mitihani, misukusuko, Uislam kukabiliwa na Uadui ndani na nje n.k.) kila aina, khaswa kwa zama hizi ni mkorogo ulio katika Dini wa yale yaliyo sahihi na yaliyo ya uzushi (Bid’ah). Kwa hiyo, anapojikita mtu katika msimamo thabiti na kujiepusha na fitnah hizo, bila shaka atakuwa amepata fadhila hizo za Hijrah iliyokusudiwa:
Kutoka kwa Ma'qil bin Yasaar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kufanya ‘ibaadah wakati wa fitnah, ni sawa na kufanya Hijrah kwangu)) [Muslim]
Basi na tujiepusha na yote Aliyokataza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuzidisha ‘ibaadah kwa wingi khaswa katika miezi mitukufu na mwezi kama huu wa Sha’baan ambao una fadhila na pia ni ni mwezi ambao tunategema kughufuriwa madhambi yetu. Kwa nini tujiongezee madhambi baada ya kughufuriwa? Tumekosa hata chembe cha shukurani kwa Mola Muumba!
Nyakati hizi ndugu Waislamu tuzitumie katika ‘ibaadah ili tujichumie mema mengi, kwani ni nyakati ambazo kwa neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zinatumiminikia kila kukicha, angalau tuzingatie na kushukuru kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا ﴿٦٢﴾
Naye Ndiye Aliyejaalia usiku na mchana ufuatane kwa atakaye kukumbuka au atakaye kushukuru. [Al-Furqaan: 62]
Ndugu Waislam, kama wanataka kuvunja jungu kama waitavyo hao wavunjaji, basi kwanini wasifanye kama Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa kila ukikaribia kuingia kwa mwezi wa Ramadhwaan wakizidisha kusoma Qur-aan na wale wenye uwezo kimali wakitoa mali kuwapa maskini ili kuwapa nguvu kujiandaa na mwezi wa Ramadhwaan.
Ni muhimu kwa Waislamu kufanya maandalizi ya Ramadhwaan kwa kujielimisha juu ya namna ya kuukabili mwezi mtukufu hasa kuelewa maana na makusudio ya funga, namna ya kufunga kwa kuzingatia masharti, mambo yanayobatilisha Swawm, pamoja na Sunnah zilizokokotezwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha namna iliyo bora ya kukaribisha Swawm ya Ramadhwaan, hivyo tunapaswa kufunga Sunnah za Jumatatu na Al-Khamiys pamoja na kuisoma Qur-aan kwa wingi kama alivyotuagiza.
Vilevile Ramadhwaan inapoingia Waislam wanatakiwa wajiepushe kabisa na mambo yote ya laghwi (upuuzi) ambayo hupoteza Swawm kama vile kuangalia mpira, sinema za kipuuzi, misalsalaati, kucheza bao, karata, usoro, dhumna, drafti, keramu n.k. Laghwi ni jambo lolote la kipuuzi ambalo hupoteza muda na kumsahaulisha mja kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Katika zama hizi, Sunnah zimetengwa mbali na bid’ah ndizo zenye kufuatwa na kuwa ndio mwendo wa Waislamu wengi, kwa sababu ya ujinga wa kuigiza tu watu bila ya dalili, na kutopenda kujifunza mafunzo mema yaliyo sahihi ya Kiislamu. Mafunzo ambayo yamekamilika na kumfaa kila bin Aadam popote na wakati wowote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينا
((Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.)) [Al-Maaidah: 3]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuthibitishe mioyo yetu katika Iymaan, na Atuongeze kwenye hidaaya, na Atughufurie madhambi yetu makubwa na madogo. Aamiyn
Marejeo ni kutoka katika Hadiyth Sahihi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika vitabu vifuatavyo:
- Swahiyhul-Bukhaariy
- Swahiyhu Muslim
- Musnad Ahmad
- Swahiyhut-Targhiyb
- Sunnan An-Nasaaiy
- Al-Bayhaqiy
- Silsilatus-Swahiyhah
- Swahiyhul-Jaami’i
- Fat-hul-Baariy