Wenye Kuishi Nchi Za Masaa Mengi Na Katika North Na South Pole Vipi Wafunge Swiyaam Zao?

SWALI 1:

Kuhusu muda wa kufunga kaskazini ya dunia - wanatheolojia na wanazuoni wa Kiislamu wanashindwa kutoa majibu ya uhakikaKwa sisi tunaofunga na tunaishi nchi za Kaskazini (Norway, Sweden, Denmark, Finland, Iceland, visiwa vya Faeroe, Greenland) tuko kwenye majira ya Kiangazi na huku majira haya mchana ni mrefu na usiku ni mfupi!

Kuraani Tukufu inasema : Baada ya kuyakinisha jua limetua, waliofunga ni lazima juu yao kufuturu (tafsiri ya Sheikh Said Mussa kwenye kitabu chake cha Kiswahili: Saumu na shuruti zake, uk.16). Hii ina maana tunatakiwa kufunga mpaka tutapoona jua limezama! Kipindi hiki huku, kwa hapa Oslo nilipo jua linazama kwenye saa 3 na nusu hadi nne za usiku saa za ulaya ya kati (Saa 4 na nusu hadi tano za usiku za Afrika Mashariki).

Kwa wale wanaoishi kaskazini ya Norway, ndio usiseme. Jua linazama kwenye saa 5 hadi 6 za usiku za ulaya ya kati (CET = Central European Time) au saa 6 hadi 7 za usiku za Afrika Mashariki (EAT = East African Time).  Mwisho wa kula daku huku, ni kwenye saa 9 na dakika 25 za alfajiri au saa 10 na dakika 25 za alfajiri za Afrika Mashariki. Huku Kaskazi ya dunia tumeanza kufunga kwa masaa 18 badala ya masaa 13 ya Makka (kuchwa na kucha kwa jua): Ni masaa mengi.

 

Kadri siku zinavyoenda, jua taratibu linawahi kuzama na linachelewa kutoka. Lakini mpaka mwezi wa Ramadhani ukiisha, bado mchana utakuwa mrefu ukilinganisha na usiku.

Waislamu tunaofunga huku tumekuwa tunajiuliza maswali kadhaa wa kadhaa juu ya nyakati za majira ya Kiangazi yalivyo huku kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, ukilinganisha na nchi Afrika, Asia, Mashariki ya Kati, Marekani ya Kusini na  Kaskazini. Wanatheolojia na wanazuoni wa Kiislam huku wameshindwa kutoa majibu ya ufasaha juu ya majira ya Kiangazi huku (mchana mrefu usiku mfupi) na muda wa kufunga na kula daku. Wanahitilafiana sana.

Imam Senaid Kobilica, Sheikh Mkuu wa Baraza la Waislam Norway (IRN = Islam Råd Norge) amesema juzi kuwa; wataitisha kikao cha Mashehe na Maimam baada ya Ramadhani kwisha ili kujadili utata uliojitokeza wa suala hili. Imam Kobilica anakubaliana na Imam Basim Ghozlan wa msikiti wa Rabita hapa Oslo kuwa watu wanaweza kufuata masaaa 13,5 ya kufunga ya Makka. Wakati Imam Syed Nehmat Shah wa msikiti wa Central Jamaat-e Ahl-e Sunnat na Imam Hafiz Mehboob ur Rehman wa Islamic Cultural Centre hapa Oslo wanasema kuwa lazima waumini wa Kiislam wafuate masaa yaliyoandikwa kwenye Kuraani Tukufu; Kucha na kuchwa kwa jua!

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwakani utaangukia Julai. Na huku hizi nchi za Kaskazini Julai ni katikati ya Kiangazi! Jua linapotea kama saa moja sana sana masaa mawili. Je, itakuwaje kwa wale watakaojaliwa kuufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani?

Manaake itabidi wafunge kama masaa 23 hivi. Kwa wale waishio kuvuka nyuzi za Actic wao itabidi wasifunge, kwani jua huwa halizami kabisa!!!

Watu mpaka tumefikia kusema kuwa: Wakati dini ya Kislamu inaanza watu waliokuwa wanaishi enzi hizo hawakujua kama kuna nchi huku kaskazini zilizo na majira ambayo ni tofauti na yale yaliyoko huko kulikoanzia Uislam na matokeo yake ndo utata huu tulionao kama kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu. Wangejua kuwa huku wakati wa majira ya theluji kukoje na wakati wa majira kiangazi kukoje, labda utata huu usingekuwepo.

 

SWALI 2:

Assalam alykum,

je itakuwaje pindi Ramadhani itakapoangukia wakati wa winter ambapo kuna maeneo mengine mchana waweza kuwa hata mpaka saa moja tu kati ya masaa 24? na hili haliko mbali sana kutokea, labda katika miaka 7 mpaka 8 ijayo hili lawezekana! ufumbuzi ukipatikana itakuwa ni suluhisho pia katika Ramadhani zijazo takriban miaka miwili ijayo ambapo itakuwa peak ya summer na huenda mchana ukawa zaidi ya masaa ishirini je watu wa huku ughaibuni watafunga masaa yote hayo?

Hii ni challenge kidogo, hivyo maulamaa tunaomba ftwa zenu juu ya hili, nimetoa kesi zote mbili ili majibu yasiwe bias, kwani it is evident that Ramadhan inafikia katika miezi yote ya mwaka mzima wa kizungu (Gregorian)
Nawaombea kwa Allah (SW) awaongoze wale wote watakaoshiriki kulitafutia ufumbuzi suala hili bila kuvuka mipaka na wakati huo huo kuuelimisha Umma wa kiislam hasa wale wanaotoka katika maeneo ya Tropiki kwenda Ughaibuni ambapo majira ya mwaka ni tofauti kabisa!!

Wabillah Tawfiq,

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Mtu yeyote anayeishi katika nchi ambayo usiku unaweza kutofautishwa na mchana kutokana na kupambazuka Alfajiri na kuzama jua (Maghrib), lakini masiku yakawa marefu sana katika majira ya joto na (wakati mwingine) yakawa mafupi sana katika majira ya baridi, ni wajibu kufunga na kutekeleza Swalah tano kila siku katika wakati unaojulikana katika Shari'ah.

Allaah Anasema:

“Leo Nimekukamiliishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na nimekupendeleeni Uislamuuwe ndiyo Dini.” [Al-Maaidah 5: 3]

 

Na vilevile Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuamrisha funga na kutueleza fadhila na malengo yake:

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [Mumefaradhishiwa] Swawm, kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.” [Al-Baqarah 2: 183]

 

Na Allaah Anafafanua wakati ambapo Swawm inapaswa kuanza na kumalizika:

 “Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku [jua linapozama Maghrib].” [Al-Baqarah 2: 187]

Hivyo, kwa ndugu wanaoishi katika nchi hizo ambao wanawajibika (kufunga) wajitenge na chakula na vinywaji na kila kitu ambacho kinabatilisha Swawm kwa kila mchana wa Ramadhaan, kuanzia wakati wa asubuhi mpaka jioni katika Miji yao, maadamu tu usiku unaweza kutofautishwa na mchana, na maadam mchana na usiku kwa pamoja unakusanya masaa ishirini na nne. Inajuzu kwao kula, kunywa, kufanya Jimai, n.k. wakati wa usiku tu, hata kama ni utakuwa mfupi. Shari'ah ya Uislamu ni ya ulimwengu mzima na inawahusu watu wote na inatumika kwa watu wote na nchi zote.  Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Basi sasa changanyikeni nao na takeni Aliyokuandikieni Allaah. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku [jua linapozama, Maghrib]. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa I’tikafu Msikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah, basi msiikaribie. Namna hivi Allaah Anabainisha Ishara Zake kwa watu ili wapate kumcha.” [Al-Baqarah 2: 187] 

Yeyote yule ambaye atashindwa kukamilisha Swawm yake kwa sababu siku ni ndefu, au ambaye anajua kutokana na uzoefu au ushauri wa kutoka kwa daktari mwaminifu, au anahisi kuna uwezekano kuwa Swawm itasababisha kifo chake au itamfanya awe mgonjwa sana, au itafanya ugonjwa alionao (ikiwa ni mgonjwa) kuwa mbaya zaidi au kuzuia kupona kwake, anaweza kuvunja Swawm yake na kulipa siku ambazo zilimpita katika mwezi ambao anaweza kufanya hivyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine.” [Al-Baqarah 2: 185] 

 

“Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri  iwezavyo.” [Al-Baqarah 2: 286] 

 

“Hapendi Allaah kukutieni katika taabu.” [Al-Maaidah 5: 06] 

 

Ama yale maeneo ambayo jua halizami (hakuna machweo) kwa miezi sita ya mwaka, na halichomozi (hakuna macheo) kwa kipindi kingine kama hicho, hukumu ya Swawm ya watu hao ni kama hukumu ya Swalah zao. Kama tutakavyobainisha kwa dalili mbalimbali za Ahaadiyth. Wanachotakiwa kufanya watu wa nchi hizo ni kukadiria mchana na usiku kulingana na nchi ya/za jirani ambayo Waislamu hufunga kwa kufuata nyakati zao za kawaida za Alfajiri na Maghrib; nchi ambazo nyakati zao za Swalah zinajulikana, na ambazo usiku wao na mchana wao unawafikiana na kutekeleza Swalah zao na Swawm zao bila tabu wala taklifa zozote.

 

Kadhaalika, kwa kauli za Wanachuoni wengine, wao huruhusika kufuata nyakati za Makkah, lakini wawe tokea mwanzo wamefuata Swawm yao kulingana na nchi jirani. Na Swawm yao itakuwa sahihi.

 

Na hakuna Mwanachuoni yeyote aliyepinga uwajibu wa kufunga Swawm kwa wenye kuishi nchi hizo. Japo mas-alah haya hayajajadiliwa huko nyuma na Wanachuoni wa kale, lakini kuna makubaliano (Ijmaa’) ya uwajibu wa kufunga maadam mwezi wa Ramadhaan umewafikia.

 

Hata hivyo, pamoja na kuwa suala hili halijazungumzwa na Wanachuoni wa huko nyuma, ila Wanachuoni wa karibuni wamekijadili na tutaonyesha misimamo miwili iliyo maarufu katika qadhiyah hii.

 

Msimamo wa kwanza ni wa Wanachuoni wa Al-Azhar Misr

 

Wanachuoni wa Al-Azhar Misr wenye mamlaka ya kutoa Fatwa, wanaeleza kuwa Waislamu wa nchi kama Norway na nyingine kama hiyo, ambazo wapo katika nyakati ambazo mchana ni mrefu sana na usiku ni mfupi sana, basi wanatakiwa wafunge kwa kufuata Makkah au Madiynah. Kadhaalika, wameeleza kuwa Waislamu hao wa nchi hizo, wanaweza kufuata nchi za jirani ambazo mchana wake ni wa kawaida.

 

Msimamo wa pili ni Wanachuoni wa Saudia ambalo ni jopo la Kamati ya Utoaji Fatwa na Utafiti wa Kielimu, na ukiungwa mkono na Mufti wa zamani wa Misr, kama ifutavyo:

Yeyote anayeishi katika nchi ambayo jua halizami wakati wa majira ya joto na halichomozi wakati wa majira ya baridi, au ambaye anaishi katika nchi ambayo mchana unaendelea kwa miezi sita na usiku unaendelea kwa miezi sita, kwa mfano, anatakiwa kuswali Swalah tano kila kipindi cha masaa ishirini na nne. Kwa hali kama hii, wanapaswa kukadiria wakati wao kwa kuangalia nchi ya jirani ambayo nyakati zake za Swalah tano za kila siku zinaweza kutofautishwa na mtu, kwa sababu iliwahi kuthibiti katika Hadiyth ya Israa na Mi'raaj kuwa Allaah Alikuwa kafaradhisha juu ya Ummah wake Swalah hamsini kila mchana na usiku, kisha Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea kumuomba Mola wake apunguze mpaka [Allaah] Akasema, “Ee Muhammad, Swalah tano kila mchana na usiku, na kwa kila Swalah malipo yake yatakuwa kumi, hivyo zitakuwa Swalah hamsini...”

Na imethibitiki katika Hadiyth ya Twalhah bin 'UbaydiLlaah (Radhiya Allaahu' anhu) kuwa kasema: Mtu kutoka Najd na nywele ambazo hazikuchanwa alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na tukasikia sauti yake ya juu lakini hatukuweza kuelewa kasema nini, mpaka alipofika karibu na ndio tukajua kuwa alikuwa anauliza kuhusu Uislamu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “(Unapaswa kuswali) Swalah tano kila siku mchana na usiku.” Yule mtu akauliza, “Je, ninatakiwa kufanya kitu kingine?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Hapana, isipokuwa tu kama utapenda kwa hiari yako Swalah (yaani za naafilah)...” 

Na imethibitiki katika Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ’anhu) kuwa kasema: Tulikatazwa kumuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu jambo lolote, hivyo sisi tulikuwa tukipenda kufanya hivyo, hadi mtu mmoja mwenye ufahamu mzuri kutoka miongoni mwa watu wa jangwani akaja na kumuuliza: “Ee Muhammad, mjumbe wako ametujia kwetu na kusema kwamba unadai kuwa Allaah kakutuma. ”Akajibu, “Kasema kweli.” ...mtu huyo (jangwnai) akasema, “Na (huyo) mjumbe wenu anadai kwamba tunatakiwa kuswali Swalah tano kwa kila siku na mchana.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ”Kasema kweli.” Mtu huyo akasema, ”Naapa kwa yule aliyekutuma, Allaah kakuamrisha juu yako hilo?” Akasema”Ndiyo...”

 

Imethibitika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Maswahaba wake wake kuhusu Dajjaal. Akaulizwa ni muda gani atakuwa juu ya ardhi, akasema, “Siku arobaini, siku moja itakuwa kama mwaka, siku moja itakuwa kama mwezi, siku itakuwa kama wiki na zinazobaki itakuwa kama siku zenu.” Kukasemwa, “Ee Mtume wa Allaah, siku ambayo itakuwa ni kama mwaka, je, swalah ya siku moja itatutosheleza juu yetu [kwa hiyo siku moja]?” Akasema, ”Hapana, mtu atazikadiria.”

 

Hivyo basi, siku ambayo itakuwa kama mwaka haitochukuliwa kama siku moja ambayo Swalah tano zitatosheleza, kinyume chake ni wajibu juu yetu kuswali Swalah tano katika kipindi cha masaa ishirini na nne. Akawaamuru kutekeleza Swalah katika vipindi vyake kama siku ya mara kwa mara. 

Kwa hiyo, Waislamu katika Nchi hizo waliouliza swali, wanaweza kukadiria wakati wa Swalah katika nchi hizo, kwa kuegemea nyakati ambazo zinatumiwa na nchi za jirani nazo ambazo kunawezwa kutofautishwa mchana na usiku na ambapo nyakati za Swalah tano za kila siku huwa zinajulikana kulingana na ishara ilivyoelezwa katika shari'ah, ndani ya kipindi cha masaa ishirini na nne.

 

Vile vile wanawajibikia kufunga Ramadhaan. Wanaweza kuweka muda kwa ajili ya Swawm zao na kuamua mwanzo na mwisho wa Ramadhaan na wakati wa kuanza kufunga na kufungua (kufuturu) kila siku kwa kufuata nyakati za asubuhi (macheo) na jioni (machweo, Maghrib) za nchi ambayo ipo karibu ambayo (nchi hiyo) kunawezwa kutofautishwa usiku na mchana. Kipindi kwa jumla lazima kijumuishe masaa ishirini na nne, kwa sababu ya Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Dajjaal alivyotajwa hapo juu, ambapo aliwaambia Maswahaba wake jinsi watavyoamua wakati wa kila siku wa Swalah tano. Hakuna tofauti katika suala hili kati ya funga (Swawm) na Swalah. 

Na Allaah Anajua Zaidi. Swalah za salaam zimuendee Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

[Al-Lajnah al-Daa'imah lil-Buhuuth al-'Ilmiyyah wa'l-Iftaa. 6/130-136]

 

Mufti wa zamani wa Misr, Hasanayn Makhluuf, yeye anaeleza kuwa, Waislamu walioko nchi ambazo mtu anafunga taqriban masaa ishirini, hakuna tofauti yao na wengine katika kufunga Ramadhaan ila tu pindi mtu atakapokuwa ana udhuru au maradhi au kufunga kwa masaa yote hayo kutamletea madhara ya kiafya, kifo au kuathirika kupona maradhi yake ya nyuma endapo atafunga kwa muda mrefu na hilo ni baada ya kushauriwa na daktari mwaminifu juu ya hilo. Na yeyote yule ambaye atashindwa kufunga katika nyakati hizo za masaa marefu kutokana na sababu hizo, basi atatakiwa alipe masiku atakayoacha.

[Fataawa Shaykh Makhluuf 1/272, Majallah Al-Buhuuth Al-Islamiyyah, Toleo 25, uk, 32]

 

Na rai hii ya msimamo wa pili, ndio inayokubaliana zaidi na dalili za Qur-aan na Hadiyth ambazo zimeonyesha wazi kuwa funga imewajibishwa kwa kila atakayeona au kusikia taarifa za mwezi na vilevile kwa kupambanuka usiku na mchana (wakati wa kuanza Swawm na wa kumaliza kwake). Dalili hizo ni hizi tunazirudia:

 

”Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine.” [Al-Baqarah: 185]

Anasema Imaam Ibn Kathiyr:  ”Na hii amri iko wazi kwa wale watakaoshuhudia mwezi kufunga ukiondosha si wasafiri na si wagonjwa.” [1/381]

 

Vilevile Aayah ifuatayo:

”...Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa I'tikaaf Msikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah, basi msiikaribie. Namna hivi Allaah anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.” [Al-Baqarah: 187]

 

Waliolezwa katika Aayah hii ni wale wenye kuweza kutofautisha baina ya usiku na mchana, weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku.

 

Kadhaalika, Aayah hiyo haijafunga au kuweka mipaka suala la Swawm kwa watu fulani tu, bali limewakusudia Waislamu wote ambao wanapaswa kufunga bila kujali maeneo yao na masaa yao ya kufunga. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Ukiwa usiku umetokeza kutokea huku, na mchana umeishia huku, na jua litakapozama, basi Swawm itakuwa imemalizika” [Al-Bukhaariy 2/240 na Muslim 3/132, kutoka kwa Ibn `Umar]

 

Kwa kuhitimisha jibu hili, ni kuwa, Muislamu popote alipo ikiwa ni Norway, Sweden,  au nchi zingine za Scandinavia na popote pengine, anapaswa afunge maadam kunabainika mchana na usiku japokuwa mchana ni mrefu zaidi. Tunafahamu kuwa Waislamu wengine walioko nchi mbalimbali za Ulaya kama Uingereza n.k. Ramadhaan hii ya msimu wa joto wameanza kufunga kwa masaa 18 na hakuna malalamiko yoyote na wengi wanaona ni kawaida hivi sasa. Na hali ya joto la Ulaya si kama la nchi za Kiarabu na za Sahara kwa ujumla ambapo pamoja na kuwa wanafunga masaa yasiyozidi 13 lakini joto lake ni kali kupita kiasi na ufungaji ni mgumu usioelezeka, lakini washazoea na washakubali amri hiyo na kuridhia. Kwa hiyo mtu anaweza kufunga masaa mengi yakawa mepesi kuliko yule anayefunga masaa machache na yakawa mazito zaidi.

 

Isitoshe, Uislamu hausemi mtu huyo huyo ambaye anaishi nchi hizo, kulipa masaa ya Swawm za zile nyakati alizofunga masaa machache wakati wa majira ya baridi. Hivyo, ukifika wakati wa majira ya kufunga masaa machache, Uislamu unamruhusu maadam atafunga kwa kuonekana Alfajiri na kuzama jua. Na kama hauonekani mchana na usiku, basi atafuata nchi ya jirani ambayo wanaona mchana na usiku na kujua nyakati za kuanza kufunga Alfajiri na kufungua jua likizama, hata kukiwa kufunga huko kutakuwa kwa masaa machache.

 

Hivyo, ifahamike, Uislamu ni Dini ya huruma na wepesi na endapo kuna ambaye atashindwa kufunga kwa wingi wa masaa kwa kuathirika siha yake na kupatwa na madhara, basi anaruhusiwa na Shari’ah kufungua au kutokufunga na akalipa wakati mwengine utakaokuwa hauna madhara naye.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share