Ndoa Ya Mut'ah
SWALI:
Assalam alaykum, baaya ya kukutakieni salaam na waislam wote kwa jumla, napenda kwanza kukupongezeni waanzilishi wa Hii website njema kabisa. Allah akuzidishieni uwezo na elimu, msichoke na muendelee katika juhudi hizi kwa ajili ya Allah SWT.
Ama dhumun hasa ni kutaka kuuliza masuali mengi ambayo yamekuwa yakinikera katika nafsi yangu siku nyingi, haswa nikiwa nakutana na waislam wenzangu kujadili mambo haya ambayo kutokana na waislam wengi kwa wakti huu tumekuwa na elmu finyu ya dini yetu, ningependa niwekwe sawa na kuridhishwa na majibu yenu sahihi na mema.
Kwa leo ningependa kuuliza:
Vipi kuhusu ndoa ya Mutwa na nini haswa maana yake hii neno Mutwa, na jee ni kweli Mtume SAW aliiruhusu na kuikataza baadae, na kuna hikma gani katika kuiruhusu na kuikataza? Nimepata kusikia kuwa baadhi ya Sahaba kama Binu Abbas alikuja kuiruhusu baadae tena na akaikataza, jee kwanini alifanya hivi? Jee kwa sasa inaweza kutumika katika mambo ya Dharura? Haswa kwa wale waliopo safarini kama America, Canada na Europe na wamewaacha wake zao Afrika kwa siku nyingi sasa, jee wanaweza kuoa hii ndoa ya Mutwa ili wajiepushe na mitihani ya kidunia?
JIBU:
Mut’ah ni neno ambalo lina majina mengine kama al-Mawqit (yaani muda) na Ndoa ya al-Munqatwi‘ (yaani kukatika).
Hii ina maana ya ndoa inayofungwa baina ya mwanamume na mwanamke kwa muda wa siku moja au wiki au mwezi. Imeitwa jina hilo kwa sababu mwanamume anapata faida na kustarehe kwa muda uliowekwa (Sayyid Saabiq, Fiqhus Sunnah, Mj. 2, uk. 38).
Maana yake ya kilugha ni kustarehe, lakini kishari’ah ni ndoa inayofungwa kwa muda maalumu kwa ujira unaojulikana (Abu Ilyaas Chisti Sabiri, Shiaism: Myth or Reality, uk. 121). Na Abuu Bakr al-Jazairiy amesema hayo hayo katika kitabu chake Minhaajul Muslim ukurasa wa 561.
Lakini Khomeini aliyekuwa kiongozi wa Kishia ametoa tafsiri ifuatayo: “Mut’ah maana yake ni makubaliano ya kimatamshi baina ya mwanamume na mwanamke (awe bikira au aliyeachwa au mjane) ambaye hana mume, kuishi kama mume na mke kwa muda uliokubaliwa kwa kiwango maalumu cha pesa kinacholipwa huyo mwanamke baada ya kuisha muda wa Mut’ah. Qaadhi wala mwakilishi au yeyote kuwa shahidi hakuhitajiki. Makubaliano haya hupangwa kibinafsi na kisiri baina ya watu wawili. Mwanamume halazimiki kisheria kutoa himaya, chakula na mavazi kwa mwanamke. Kitu muhimu anachokitoa ni kumpa huyo mwanamke kiwango kile cha pesa walichokubaliana. Baada ya kupewa hizo pesa mafungamano yao tayari huisha. Muda wa kubakia pamoja ndani ya Mut’ah kunaweza kuwa mchana mmoja na usiku wake au hata saa moja au masaa mawili.” [Tahrirul Wasiylah, uk. 292].
In shaa Allaah vipengele ambazo tumevipigia msitari tutavirudia hapo mbele.
Ifahamike ya kwamba halali na haramu katika Uislamu ni kazi ya Allaah (سبحانه و تعالي) peke yake. Allaah (سبحانه و تعالي) anasema:
اتَّخَذُواْ أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ ﴿31﴾
“Wanawafanya Wanachuoni wao na watawa wao kuwa ni waabudiwa badala ya Allaah. [9: 31].
‘Adiy bin Haatim (رضي الله عنه) ambaye alikuwa Mnasara kabla ya kusilimu alimwambia Mtume صلي الله عليه وآله وسلم)) wao hawawaabudu hao wanavyuoni na watawa wao. Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alimjibu:
“Je, wao si wanahalalisha iliyoharamishwa na Allaah (سبحانه وتعالي) na kuharamisha aliyohalalisha Allaah (سبحانه و تعالي) nanyi mukawafuata?” Akasema: “Ndio”. Akasema: “Huko ndiko kuwaabudu”.
Kuna vitu wakati wa Utume wa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) vilikuwa halali kisha vikaharamishwa, mfano ni ndoa ya Mut’ah na pombe. [Tazama Qur-aan, 5: 90-91].
Na kuna vingine vilikuwa havifai kufanywa kisha vikahalalishwa, mfano mzuri ni kuzuru makaburi. Waislamu walipohamia Madiynah, Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) aliwakataza kuzuru makaburi na baadae akawaambia wazuru kwani itawakumbusha wao Aakhirah. [Muslim].
Na chochote anachoharamishiwa mwanaadamu na Allaah (سبحانه و تعالي) basi huwa kina madhara makubwa sana kwake.
Jambo ambalo limewekwa katika masikio ya watu ni kuwa ndoa hii ya Mut’ah ilikatazwa na Amiyr Al-Muuminiyn ‘Umar (رضي الله عنه) lakini ilikuwa halali wakati wa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم). Hebu tuangalie kulitokea nini wakati huo.
Yahyaa amenihadithia kutoka kwa Maalik, naye kutoka kwa Bin Shihaab, naye kutoka kwa Urwa bin Az-Zubayr kwamba Khawlah bint Hakim alikuja kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab na kusema: “Rabi‘ah bin Umayyah amefanya ndoa ya Mut’ah na mwanamke na sasa ana mimba yake”. ‘Umar bin Al-Khattwaab alitoka nje na huku amekasirikia akilikokota joho lake, akasema, “Ndoa hii ya Mut’ah, kama mimi ningewakumbusha kutoka mwanzo, basi nitaamuru watu kutiwa adhabu ya kupigwa mawe na kuiondosha kabisa!” [Al-Muwattwaa). Katika sharh yake Imaam Muhammad anasema: “Hakika Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) amewakataza Mut’ah na ‘Umar (رضي الله عنه) aliposema; ningewaadhibu hadd ya shariy’ah ni kwa sababu ya utawala wake, kwani yeye alikuwa na haki ya kuzuia kila ovu na hamu kwa nguvu ya utawala”.
Tunaona kuwa hapa ‘Umar (رضي الله عنه) alichukua lile jukumu la kuondoa Munkar kwa mkono wake akiwa ni mtawala wa Dola. Na kwa kuwa ummah huu haukubaliani katika upotofu hakuna aliyesimama kumkosoa ikiwa alikosea katika jambo hilo kama ambavyo baadhi ya nyakati nyengine alivyokuwa akikosolewa na kurekebishwa na watu mbali mbali pale alipokuwa akikosea.
Ndoa hii ilikuwa ipo hata kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (صلي الله عليه وآله وسلم) na alipopatia wahyi jambo hili liliendelea kwa muda lakini baadae likaharamishwa kabisa. Hebu tutazame baadhi ya Hadiyth ya kuonyesha hayo:
Imepokewa kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alisema:
“Yeyote anayetoa kama mahari kwa mke wake kipimo cha mikono miwili ya unga au tende amejihalalishia mke huyo kwake”. Abuu Daawuwd anasema: “Hadityh hii imepokewa na ‘Abdur-Rahmaan bin Mahdi, kutoka kwa Swaalih bin Ruumaan, kutoka kwa Abuu Az-Zubayr naye kutoka kwa Jaabir kama kauli yake (haikufika kwa Mtume)”.
Pia imepokewa kwa Abu ‘Aaswim kutoka kwa Swaalih bin Rumaan, kutoka kwa Abuz Zubayr, ambaye ameipokea kutoka kwa Jaabir ambaye amesema: “Katika uhai wa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) tulikuwa tunafanya Mut’ah kwa kutoa kipimo cha mikono ya unga” [Abuu Daawuwd].
Hapa Jaabir (رضي الله عنه) anaelezea lililokuwa likitendeka wakati huo wa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) kuhusu ndoa hii. Na Hadiyth nyingine ni ifuatayo:
Imepokewa kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) kwamba Abu Nadrah amehadithia kwamba: “Nilipokuwa safari pamoja na Jaabir, mtu mmoja alikuja na kusema: ‘Kuna tofauti ya rai baina ya Bin ‘Abbaas na Bin Zubayr (رضي الله عنه) kuhusu Mut’ah mbili (faida, Tamattu’ katika Hajj na Ndoa ya Mut’ah ya wanawake)’, hapo Jaabir alisema: ‘Tumekuwa tukifanya hivyo katika uhai wa Mtume wa Allaah (سبحانه و تعالي) (صلي الله عليه وآله وسلم) na baadae ‘Umar (رضي الله عنه) akatukataza tusifanye hivyo, na hatukufanya hivyo tena.” [Muslim].
Lakini zipo Hadiyth ambazo zipo wazi kabisa katika kuharamishwa huko kwa ndoa hiyo. Baadhi yao ni hizi hapa chini:
1. Imepokewa kwa Swabrah bin Ma'bad al-Juhaniy (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) aliruhusu ndoa ya Mut’ah kwetu sisi. Hivyo mimi na mtu mwengine tuliondoka na kumuona mwanamke wa Banu ‘Aamir, ambaye alikuwa na ngamia wa kike mdogo mwenye shingo ndefu. Tulijipeleka kwake (ili tuweze kuingia katika Mut’ah), naye akasema: “Mutanipatia nini kama mahari?” Nikasema: “Joho langu”. Na mwenzangu naye akasema: “Joho langu”. Joho la mwenzangu lilikuwa zuri na bora kuliko langu, lakini mimi nilikuwa mdogo. Sasa alipoangalia joho la mwenzangu alilipenda, na aliponiangalia mimi akaniona napendeza zaidi kwake. Hivyo alisema: “Sawa, wewe na joho lako zanitosha mimi”. Nikabakia kwake kwa masiku matatu. Na baadaye Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alisema: “Yeyote mwenye mwanamke kama aina hiyo ambaye kwamba wamepatana kuingia katika ndoa ya Mut’ah, amuache aende zake (asimalize mapatano yake na yeye)” [Muslim].
2. Imepokewa kwa Salamah bin Al-Akwa’ (رضي الله عنه) kwamba Mtume wa Allaah (سبحانه و تعالي) (صلي الله عليه وآله وسلم) aliwaruhusu watu kufunga ndoa ya Mut’ah kwa siku tatu katika ule mwaka wa Awtas na baada ya hapo akaiharamisha kabisa.” [Muslim].
3. Yahyaa amenihadithia mimi kutoka kwa Maalik, naye kutoka kwa Bin Shihaab kutoka kwa ‘Abdullaah na Hasan, watoto wa Muhammad bin ‘Aliy bin Abi Twaalib kutoka kwa baba yao (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) aliharamisha ndoa ya Mut’ah na wanawake na nyama ya punda wa mjini siku ya Khaybar. [Muwattwaa ya Imam Maalik].
4. Imepokewa kwa Saburah bin Ma‘bad al-Juhaniy (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) aliharamisha Mut’ah na wanawake (Abu Daawuud).
5. Imepokewa kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alikataza ndoa ya Mut’ah siku ya Khaybar na kula nyama ya punda (wa mjini).” [Al-Bukhaariy na Muslim].
6. Ja‘far bin Muhammad (Asw-Swaadiq) [Huyu kwa Mashia ni Imaam wao wa 6] alipoulizwa kuhusu Mut’ah alisema: “Hiyo ni zinaa katika kiini chake.” [Al-Bayhaqiy].
7. Ibn Maajah amenukuu Hadiyth ya kwamba Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alisema: “Enyi watu! Nilikuwa nimewaruhusu nyinyi kufanya Mut’ah lakini sasa Allaah (سبحانه و تعالي) ameiharamisha mpaka Siku ya Qiyaamah”.
8. Imepokewa kwa Saburah al-Juhaniy ambaye alikuwa katika vita vya kufungua Makkah pamoja na Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم). Mtume wa Allaah (سبحانه و تعالي) (صلي الله عليه وآله وسلم) aliwaruhusu kufanya Mut’ah na wanawake. Akasema: “Hakutoka katika mji huo isipokuwa aliharamisha ndoa hiyo Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم)” [Muslim].
9. Imaam Ash-Shafi‘iy amesema: “Sijui kitu ambacho kilihalalishwa na Allaah (سبحانه و تعالي), kisha Akakiharamisha, kisha Akakihalalisha kisha Akakiharamisha isipokuwa Mut’ah”.
Hizi Hadiyth zipo wazi kuhusu jambo hilo la kuharamishwa kwa ndoa hii ya Mut’ah.
Katika Hadiyth iliyo juu ya Jaabir (رضي الله عنه) inatuonyesha kuwa yeye alikuwa na rai kuwa hata baada ya kufariki Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) bado ndoa aina hii ilikuwa inafaa. Jambo hili si ajabu kwani si kila Swahaba zilimfikia Hadiyth zote na ndipo ‘Umar alivyowakumbusha wote wakatoka katika msimamo huo. Mfano mzuri wa kulifahamisha hilo ni pale alipoaga dunia Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alikuja Faatwimah (رضي الله عنها) kwa Khalifah Abuu Bakr (رضي الله عنه) kutaka mirathi yao ya shamba, lakini Abuu Bakr (رضي الله عنه) aliwaambia kuwa amemsikia Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) akisema kwamba: “Sisi kongamano la Mitume haturithiwi na tunachoacha ni sadaka”. Hapo Faatwimah bint Rasuul na mumewe waliridhika na hawakuwa ni wenye kudai tena shamba hilo.
Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنه) alikuwa na msimamo huo huo lakini baadae aliubadilisha kwa maneno. Isome Hadiyth ifuatayo kuhusu jambo hilo:
Imepokewa kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنه) kwamba: “Ndoa ya Mut’ah ilikuwa ikifanyika tu siku za mwanzo za Uislamu. Mtu alikuwa akielewana na mwanamke anayemtaka na hivyo baada ya makubaliano alikuwa akimuoa kwa muda ambao aliona atakaa hapo, na mwanamke alikuwa akimchungia vitu vyake na kumpikia. Lakini Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنه) anasema pindi aya ifuatayo ilipoteremka:
إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿6﴾…
“…Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.” [23: 6],
hivyo kujamiiana na yeyote mwingine ikawa haramu.” [At–Tirmidhiy].
Ndoa hii ifahamike ya kwamba ina fadhila kubwa katika Dini ya Rawaafidh (Mashia) peke yake. Hebu tazama wanavyomsingizia Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) katika jambo hili la Mut’ah:
Mullah Baqir Majlisi anasema,
Bwana Salmaan al-Faarisi, Miqdaad bin Aswad na ‘Ammar bin Yaasir (رضي الله عنهم) wamesema kuwa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtu ambaye atafanya Mut’ah mara moja ataingia Peponi. Wakati mwanamume anaanza kufikiri kufanya Mut’ah basi Malaika mmoja huteremka kumlinda mpaka atakapofanya ndoa hiyo…” [Bihaarul Anwaar].
Katika Hadiyth nyingine wanasema kuwa Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) alisema:
“Mwenye kufanya Mut’ah mara moja atafika daraja ya Imaam Husayn, mara mbili daraja ya Imaam Hasan, mara tatu daraja ya Imaam ‘Aliy na mara nne daraja ya Mtume mwenyewe.” [Mullah Fat-hullah Kashani, Tafsiyr Minhajus Swaadiqiyn, Mj. 1, uk. 356].
Swali la kujiuliza ni kuwa je, akifanya zaidi ya mara nne atakuwa daraja ya nani?
Je, Hukmu Ya Mut’ah Katika Shariy’ah Ni Ipi?
Waislam wote kwa Ijmaa wanakubaliana kuwa ndoa hii ya Mut’ah ni haramu. Na lau itafanyika basi ndoa itakuwa batili, kwa dalili zifuatazo:
1. Hii ndoa haifungamani wala haina uhusiano na kanuni zinazofahamika za ndoa kama ilivyoelezwa katika Qur-aan kwa nikaah, talaka, eda na mirathi. Hivyo itakuwa batili kama ndoa nyinginezo zilizo batili kama shighaar na muhallil.
2. Hadiyth zilizo wazi kabisa zimekuja kuharamisha.
3. ‘Umar (رضي الله عنه) aliharamisha akiwa juu ya Minbar na wakakubali Maswahaba (رضي الله عنه), nao si watu wa kukubali makosa.
4. Al-Khattwaabiy anasema: “Uharamu wa Mut’ah ni kwa Ijmaa isipokuwa baadhi ya Raaafidhah (Mashia) na katika hili wanakwenda kinyume na ‘Aliy (رضي الله عنه) ambao wanamchulia kuwa Imaam wao.”
5. Lengo kubwa la Mut’ah ni kukidhi uchu pekee wala haina kusudio la kuzaana wala kuhifadhi watoto ambayo ndio malengo makuu ya ndoa. Kwa hivyo katika lengo inafanana na zinaa. Kisha jambo linamdhuru mwanamke anapochukuliwa kama bidhaa na kama inavyowadhuru watoto ambao watakuwa wanahamishwa kutoka nyumba moja hadi nyengine na huenda wasijue baba zao halisi.
6. Kulingana na Khomeini aliyekuwa mtawala wa Iran na Mashia wote ulimwenguni, ni kuwa ndoa hii ina masharti yafuatayo: Qaadhi wala mwakilishi au yeyote kuwa shahidi hakuhitajiki. Makubaliano haya hupangwa kibinafsi na kisiri baina ya watu wawili. Mwanamume halazimiki kisheria kutoa himaya, chakula na mavazi kwa mwanamke.
Masharti haya yote yanavunja zile nguzo zilizowekwa na shari’ah ili ndoa ya Kiislamu iwe sawa. Mfano ni:
a) Kuwepo na walii, kwani Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna ndoa pasi na walii” (Asw-habus Sunan).
b) Mashahidi wawili waadilifu, kwa kauli ya Allaah (سبحانه و تعالي):
وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ... ﴿2﴾
“Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilfu miongoni mwenu” [65: 2] na Mtume (صلي الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna ndoa pasi na walii na mashahidi wawili waadilifu.” [Al-Bayhaqiy na Ad-Daaraqutniy]. Haya masharti yanakwenda kinyume kabisa.
c) Hii si nguzo bali ni jukumu la mwanamume kumpatia mke malazi, chakula, mavazi, matibabu na mengineyo, lakini kwa Khomeini na Mashia ni kuwa yote hayo hapatiwi isipokuwa ujira tu.
Katika Sehemu Ya Pili Ya Swali, Kuwa Je, Tunaweza Kufanya Ndoa Hii Kwa Dharura Kwa Wale Ambao Wapo Safarini?
Jawabu ya hili ni: “Maswahaba wengi sana wana rai kuwa baada ya kukamilika shariy’ah ya Kiislamu, ndoa ya Mut’ah imeharamishwa kabisa. Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنه) ana rai tofauti ya hiyo kwa dharura. Kuna mtu alimuuliza (yaani Ibn ’Abbaas) kuhusu kuoa wanawake kwa muda na akaruhusu. Mtumishi wake akauliza: ‘Je, hii si mtu akiwa tu katika hali ngumu, wakati ambapo wasichana ni kidogo na mfano wake?’ Akajibu: ‘Ndio’ [Al-Bukhaariy).
Baadaye, Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنه) alipoona ya kwamba watu wamekuwa walegevu na wamebobea katika kufanya ndoa aina hizo bila ya haja yoyote, alibadilisha hukumu aliyotoa awali pamoja na rai yake kuhusu hilo” (Ibn Qayyim al-Jawziyah, Zaad Al-Ma‘ad, Mj. 4, uk. 7].
Rawaafidh (Mashia) wamefasiri baadhi ya Aayah kinyume kimakusudi ili kuhalalisha ndoa hiyo ya Mut’ah. Mojawapo ya Aayah hiyo ni:
…وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاء ذَلِكُمْ أَن تَبْتَغُواْ بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً وَلاَ جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا تَرَاضَيْتُم بِهِ مِن بَعْدِ الْفَرِيضَةِ إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿24﴾
“Na imehalalishwa kwa ajili yenu min ghairi ya hawa na watafuteni pamoja na mali yenu katika hali ya wenye kufanya nikaha si wenye kufanya zinaa. Na basi kwa ile faida mliochukuwa ninyi na wanawake hao mmefanya (MUT’AH), basi wapeni mahari yao yaliyo faradhi.” [4: 24].
Hii ni tafsir ya kutoka Anwaarul Bayaan ya Haji Naji Ghulamali Haji Esmail kutoka lugha ya Kigujarati unaweza kutaazama hiyo katika kijitabu cha Ali Muhammad Haji Aladina Noorani, Njama ya Kuhalalisha Zina (Fedheha kwa Wanawake), uk. 17.
Na katika gazeti la The Muslim, Jan/Feb. 1991, No. 13 la Raafidh (Mshia) Faruq lililokuwa likichapishwa Nairobi linatoa tafsiri ya aya hiyo kwa kusema: “And lawful for you are all (women) beside those mentioned so that you may seek by means of your wealth taking them into marriage and not committing fornication and this with whom you concluded Mut’ah (Famastamta‘tum) give them their dowries”.
Sasa tazama tafsiri nyinginezo kuhusu Aayah hii:
Prohibiting the Mut`ah of Marriage (Tafsir Ibn Kathiyr)
Also (forbidden are) women already married, except those (captives and slaves) whom your right hands possess. Thus has Allâh ordained for you. All others are lawful, provided you seek (them in marriage) with Mahr (bridal money given by the husband to his wife at the time of marriage) from your property, desiring chastity, not committing illegal sexual intercourse, so with those of whom you have enjoyed sexual relations, give them their Mahr as prescribed; but if after a Mahr is prescribed, you agree mutually (to give more), there is no sin on you. Surely, Allâh is Ever AllKnowing, AllWise. (The Meaning of The Noble Quran In the English Language A Summarized Version of At-Tabari, Al-Qurtubi and Ibn Kathir with comments from Sahih Al-Bukhari By
Dr. Muhammad Taqi-ud-Din Al-Hilali & Dr. Muhammad Muhsin Khan)
“And [also prohibited to you are all] married women except those your right hands possess. [This is] the decree of Allāh upon you. And lawful to you are [all others] beyond these, [provided] that you seek them [in marriage] with [gifts from] your property, desiring chastity, not unlawful sexual intercourse. So for whatever you enjoy [of marriage] from them, give them their due compensation as an obligation. And there is no blame upon you for what you mutually agree to beyond the obligation. Indeed, Allāh is ever Knowing and Wise.” (Translation of the Meaning of the Quran by Saheeh International)
“…Basi wale munaowaoa miongoni mwao wapeni mahari yao...” (Abdallaah Saleh Farsi).
“… Ambao mumestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari …” (Al-Amin bin Aly Mazrui, Tafsiri ya Qur’ani tukufu).
Tafsiri zote za Kiarabu kama ile ya Ibn Kathiyr, Ash-Shawkaaniy, n.k. simesema hivyo hivyo isipokuwa ya Atw-Twabariy ambayo imesema kuwa hii inamaanisha Mut’ah lakini kisha ikaharamishwa hata hivyo inaonyesha uharamu wake.
Tazama katika tafsiri zote hizi zinatueleza kuwa Famastamta‘tum ni kupata faida au kustarehe, sasa hii Mut’ah iko wapi! Hii ni ima kutoielewa lugha ya Qur-aan au kufanya kusudi kuwapoteza watu katika Njia ya Allaah (سبحانه و تعالي) ya kweli.
Mwisho tunamalizia na visa viwili ambavyo vimetokea Kenya kuhusu masuala haya ambayo yanatuonyesha ya kwamba hawa wanaotaka wengine wafanye Mut’ah hawataki wasichana wao watendewe hivyo.
Sheikh Khwaja, mwanzilishi wa Ma’ahad al-Banaat (Girls Institute) katika mji wa Nairobi alikuwa anafuatwa sana na bolozi wa Iran Kenya na mkurugenzi wa Iranian Cultural Centre baada ya mapinduzi ya Khomeini Iran ili aingie katika Uraafidhah (Ushia). Alikataa kwa muda mrefu lakini hawakumwachilia, na waliendelea kumfuata kila wakati. Mwishowe aliwaambia (kwa lengo la kutaka wamwache wasimfuate tena) ya kuwa yeye yupo tayari kufanya hivyo lau atapewa binti ya Khomeini afanye naye Mut’ah. Huo ndio ukawa mwisho wa kufuatwa na mahusiano yao yakakatika!! Sasa kwa nini lakini iwe hivyo, wakimbie na kukasirika wakati jambo hilo kwao ni halali??
Mfano wa pili ni wa mtu anayejulikana kuwa ni mhubiri wao maarufu Afrika Mashariki ambaye ameandika vitabu kadhaa vya Kishia, Kenya. Katika mji wa Mombasa. Alikuwa kila wakati katika mabaraza akizungumzia kuhusu umuhimu wa ndoa hii ya Mut’ah. Siku moja kulikuwa na kijana tajiri ambaye aliona kuwa mambo yamezidi sana kuhusu hilo. Alipokuja huyo mhubiri wao siku hiyo na kuanzia kuzungumzia kuhusu ndoa hiyo, yule kijana akamwambia: “Wewe unanijua kuwa mimi ni muweza kifedha. Na kwa sababu ya umuhimu wa ndoa hii mimi nataka unipatie binti yako tufunge ndoa ya Mut’ah kwa pesa zozote unazotaka”. Muhubiri huyo wa Kirafidha alikuwa mkali na kuanza kutusi na kuanzia siku hiyo hakupita tena katika baraza hiyo.
Ikiwa watu hawa ambao ndio waliotakiwa wawe mfano mzuri kwa wafuasi wao na wanaadamu wanashindwa kutekeleza jambo ambalo kwao lina umuhimu mkubwa na fadhila za hali ya juu, itakuwaje kwa watu wa kawaida. Amesema Allaah (سبحانه و تعالي) Aliyetukuka:
أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنسَوْنَ أَنفُسَكُمْ وَأَنتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ أَفَلاَ تَعْقِلُونَ ﴿44﴾
“Je, mnaamrisha watu watende mema na mnajisahu nafsi zenu na hali ya kuwa nyinyi mnasoma Kitabu; je hamtii akilini?” [2: 44].
Na amesema Aliyetukuka kutuelezea atakayopata mwenye kufanya hivyo:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ ﴿2﴾
“Enyi walioamini! Kwanini mnasema yale msiyoyafanya?
كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ ﴿3﴾
Ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya?” [61: 2–3].
Allaah (سبحانه و تعالي) Atulinde na kusema tusiyoyatenda na Atuepushe na madhalimu wanaotaka kuwapoteza wengine na wenye kutumia dini kama chombo cha kujinufaishia wao na matamanio ya nafsi zao.
Wabillahi At-Tawfiyq.
Wa Allaahu A’alam