Kulea Watoto Wa Mume Kwa Mke Mwingine

 





 

SWALI:

Assalaamu alaykum, wa Ramadhan Kareem!

Nasikitika kua nyumba nyingi, wanawake hawalei watoto wa mume kwa ndoa nyengine vile wanavyo walea watoto wao. Ikiwezekana, tafadhali tupe hukmu ya watu kama hawa.Jazakumullah kher!

 

 



JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allaah Mtukufu, Swalah na salamu zimfikie kipenzi chetu, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wetu wema na waliowafuata kwa kheri mpaka Siku ya Kiyama.

Hili ni tatizo ambalo lipo katika nyumba zetu na huwa linaletwa zaidi na malezi mabaya ya vijana. Hili ni duara ambalo halina mwanzo na hivyo halina mwisho. Watoto wanainukia katika nyumba za mama wa kambo au baba wa kambo wakawa wanateswa na kusumbuliwa na hata kudhulumiwa. Hivyo wao wanapooa au kuolewa na mume au mke ana watoto wake nao huwa kama wanalipiza kisasi kwa hilo.

Kwa sababu hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihimiza sana mume achague mke ambaye ameshika Dini na mke naye achague mume aliyeshika Dini na mwenye maadili mema. Ikiwa hatutafanya hivyo basi kutakua na fitna na ufisadi mkubwa katika ardhi.

Tatizo hilo linapotokea inatakiwa watu watumie njia za kutatua na kuwarudisha katika utii kwa Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mume na mke wanatakiwa mwanzo wakae watizame shida hiyo na kuangalia njia muafaka ambazo zitaleta ufanisi baina ya wazazi na watoto. Ikiwa tatizo limeendelea inabidi wawakilishi wa familia hizo mbili wakutane na baadae pia Mashekhe washirikishwe katika kutatua migongano hiyo. Na kwa kutumia njia hizo basi Insha’Allaah ufumbuzi utapatikana ambao utaleta ufanisi.

Tujue kuwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wamekataza dhulma katika njia zote. Na mwenye kudhulumu atakuwa katika kiza cha Siku ya Kiyama na adhabu ambayo atapatiwa na Allaah. Tunawanasihi watu ambao katika mabega yao wana jukumu la ulezi wa watoto wawe ni wa kwao au wa wazazi wengine wasiwe ni wenye kuwadhulumu kwa njia yoyote ile. Watekeleze jukumu lao la ulezi kwa njia bora zaidi na Allaah Atawabariki hapa duniani na kesho Akhera pia.

Na  Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share