019-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Dhulma Irudishwe Duniani Kabla Ya Malipo Ya Aakhirah

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 19

 

Dhulma Irudishwe Duniani Kabla Ya Malipo Ya Aakhirah

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ:  ((مَنْ كَانَتْ عِنْدَهُ مَظْلَمَةٌ مِنْ أَخِيهِ مِنْ عِرْضِهِ أَوْ  مِنْ شَيْءٍ  فَلْيَتَحَلَّلْهُ مِنْهُ الْيَوْمَ قَبْلَ أَنْ لاَ يَكُونُ دِينَارٌ وَلاَ دِرْهَمٌ ، إِنْ كَانَ لَهُ عَمَلٌ صَالِحٌ أُخِذَ مِنْهُ بِقَدْرِ مَظْلَمَتِهِ. وَإِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِ صَاحِبِهِ فَحُمِل عَلَيْهِ))  رواه البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Aliyekuwa na kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana ‘amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe)). [Al-Bukhaariy.]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Tahadharisho la kumtendea mtu dhulma, kwani dhulma ni viza (giza) Siku ya Qiyaamah.

 

Hadiyth: ((Ogopeni dhuluma, kwani dhuluma ni viza Siku ya Qiyaamah)) [Muslim]

 

Na dhalimu ana adhabu kali Aakhirah. Rejea: Al-‘Araaf (7: 41), Maryam (19: 72),  Ghaafir (40: 52).

 

 

2. Allaah Ameharamisha dhulma na kutahadharisha kama ilivyo katika Hadiyth Al-Qudsiy:

 

عن أبي ذَرٍّ الْغِفاريِّ رضي الله عنه، عن النبيِّ صلى الله عليه وسلم فيما يَرْويهِ عن رَبِّهِ عَزَّ وجَلَّ أَنَّهُ قال:  (( يا عِبادي إنِّي حَرَّمْتُ الظُلْمَ على نَفْسِي وَ جعَلْتُهُ بَيْنَكُمْ مُحَرَّماً فلا تَظَالَمُوا))  رَوَاهُ مُسْلِمٌ     

Imepokelewa kutoka kwa Abu Dharr Al-Ghifaariyy (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  akisimulia yale aliyopokea kutoka kwa  Rabb wake (Aliyetukuka na Jalaali):  ((Enyi waja Wangu, Nimeikataza nafsi Yangu dhulma na Nimeiharamisha kwenu (hiyo dhulma), kwa hivyo msidhulumiane…[Muslim]

 

 

 

3. Kuwekeana heshima ni katika mambo makuu yanayohimizwa katika Uislamu.

 

 

4. Kutahadhari kuchuma ya haramu kwa kudhulumu watu kula mali zao bila ya haki. Rejea: An-Nisaa (4: 29, 161).

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

 وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِّنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٨٨﴾

Na wala msiliane mali zenu kwa ubatilifu na mkazipeleka (rushwa) kwa mahakimu ili mle sehemu katika mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua. [Al-Baqarah (2: 188).]

 

 

5. Dhulma inaharibu ‘amali njema, kwani tajiri anayedhulumu atakuwa masikini Siku ya Qiyaamah, na masikini aliyedhulumiwa atakuwa tajiri Siku ya Qiyaamah. Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ؟))‏ قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لاَ دِرْهَمَ لَهُ وَلاَ مَتَاعَ .‏ فَقَالَ: ((إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاَةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ))  مسلم‏

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Je, Mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swiyaam, na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni))].  [Muslim]

 

 

6. Kuharakiza kulipa dhulma duniani wakati fursa bado ipo kabla ya kufikia mauti.

 

 

7-Hatari ya kumdhulumu mtu kwa sababu du’aa ya mwenye kudhulumiwa inatakabaliwa moja kwa moja:  Hadiyth:

عنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا) أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) بَعَثَ مُعَاذًا إِلَى الْيَمَنِ فَقَالَ:  ((اتَّقِ دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ فَإِنَّهَا لَيْسَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ اللَّهِ حِجَابٌ))

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas  (رضي الله عنهما)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alimpeleka Mu’aadh Yemen akasema: ((Iogope du’aa ya aliyedhulumiwa, kwani haina pazia baina yake na baina ya Allaah.)) [Al-Bukhaariy (2448), Swahiyh At-Tirmidhiy (2014), Swahiyh Al-Jaami’ (1037)]

 

Na pia Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنه):

   اتَّقوا دعوةَ المظلومِ، فإنها تَصعدُ إلى السماءِ كأنها شرارةٌ

((Ogopeni du’aa ya aliyedhulumiwa kwani inapanda mbinguni kama cheche za moto.)) [Al-Haakim katika Al-Mustadrak ameisahihisha Al-Albaaniy; Swahiyh Al-Jaami’ (118), Swahiyh At-Targhiyb (2228)]

 

8. Anayedhulumiwa ana Ahadi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Atamnusuru na kumlipizia dhulma aliyotendewa kwa dalili Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ثَلاَثَةٌ لاَ تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ، الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ، وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ يَرْفَعُهَا اللَّهُ دُونَ الْغَمَامِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَتُفْتَحُ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاء، وَيَقُولُ بِعِزَّتِي لأَنْصُرَنَّكِ وَلَوْ بَعْدَ حِينٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)  ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: (([Watu] Watatu hazirudishwi du'aa zao; Imaam muadilifu, mwenye Swawm mpaka afuturu, na du'aa ya aliyedhulumiwa, Anainyanyua Allaah bila ya mawingu Siku ya Qiyaamah na inafunguliwa milango ya mbingu na Anasema: “Kwa Utukufu Wangu, Nitakunusuru japo baada ya muda”.)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (2526) Ibn Maajah, Ahmad]

 

 

 

9. Anayedhulumiwa avute subira kwa kutegemea kulipwa Aakhirah, thawabu za ‘amali njema kutoka kwa   aliyemdhulumu na pia madhambi yake kubebeshwa huyo mtu aliyemdhulumu.

 

 

10. Kwa jinsi dhulma ilivyokuwa inachukiwa na Allaah (سبحانه وتعالى), Ameiharamisha hata kuwatendea watu mafasiki wenye dhambi n ahata makafiri:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((دَعْوَةُ الْمَظْلُومِ مُسْتَجَابَةٌ وَإِنْ كَانَ فَاجِرًا فَفُجُورُهُ عَلَى نَفْسِهِ))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah Radhwiya ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Du’aa ya aliyedhulumiwa (dhidi ya aliyemdhulumu) ni yenye kuitikiwa japo akiwa ni mtendaji dhambi kwani dhambi zake ni dhidi ya nafsi yake.)) [Ahmad, Swahiyh At-Targhiyb (2229), Swahiyh Al-Jaami’ (3382)]

 

عَنْ أنس رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: اتَّقُوا دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ وَإِنْ كَانَ كَافِرًا فَإِنَّهُ لَيْسَ دُونَهَا حِجَابٌ

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (رضي الله عنه)  kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Ogopeni du’aa ya aliyedhulumiwa hata akiwa ni kafiri, kwani haina baina yake kizuizi.)) [Ameisahihisha Al-Albaaniyn katika Swahiyh At-Targhiyb (2231)

 

Share