Zingatio 3: Ramadhwaan Mgeni Bora
Zingatio 3: Ramadhwaan Mgeni Bora
Naaswir Haamid
Kwa hakika tumejiwa na mgeni bora kuliko wote. Hayupo kwa muda mrefu na siku chache tu atatuacha. Huyu si mwengine bali ni mwezi mtukufu wa Ramadhwaan. Kama tutakavyoanza kwa hisabu ya Ramadhwaan ya kwanza ndivyo tutakavyofika hadi Ramadhwaan ya 29 au 30 In Shaa Allaah.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea kuhusu fadhila za mwezi huu: "Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Jannah hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri]" [Imepokewa na Imaam Ahmad]
Lengo la ujio wa Ramadhwaan si jengine ila kuwatoa Waislamu kwenye fikra za shaytwaan kwenda katika uchaji Allaah. Huu ni mwezi wa kuomba tawbah, kuifikiria Aakhirah zaidi kuliko dunia. Ni mwezi wa kufikiriana baina ya Waislamu kwa kila mwenye kuhitajia msaada ukiwa wa hali au mali.
Huu si mwezi wa kununua mikeka ukitaraji futari huku jirani yako amelala njaa siku tatu. Si mwezi wa kwenda kutafuta hijabu ukitaraji kuigeuza tambara baada ya Ramadhwaan. Wala si mwezi wa kwenda kutafuta karata na kuvingarisha vibaraza vya keram. Hao ni wachache wa akili wanaochukulia mwezi huu kuwa ni mzigo na adhabu kwao. Na bila ya kuwasahau wanaojali kujilimibikizia mali kwa kupandisha bei ya bidhaa za masoko.
Wenye akili huutumia mwezi huu kwa kufuta dhambi, kuongeza mema, kuzidisha kisimamo cha usiku, kuhudhuria darsa, kuhama vitanda kwa kuomba maghfira usiku, kukithiri i’tikafu na mengineyo mazuri. Na wapo pia wanaopata angalau juzuu moja kwa siku kila baada ya alfajiri na kupata uchangamfu mzuri wa mwili bila ya kurudia tena kitandani.
Unadhifu wa matendo ya Ramadhwaan ni kuitimiza amri ya Swawm bila ya kutafuta hoja. Kwani Waumini wa kweli husema:
سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ
Tumesikia na tumetii” [Al-Baqarah: 285]
Itakuwa ni hasara kubwa kumaliza Ramadhwaan tukiwa bado tumo kwenye usajili wa watu wa Motoni. Allaah Atukinge na adhabu hiyo!