Zingatio: Wakati Ni Huu

Naaswir Hikmaany

 

Ubora wa mambo ni kujihisabu ya kwamba huna chochote ndani ya kapu lako la thawabu. Hali hiyo itakupatia hima ya kuchuma kheri zaidi na zaidi. Ramadhwaan ni wakati wa kuchuma machumo mema ili kupata salama mbele ya Mola Mtukufu. Hakuna ajuaye ya kwamba ataishi kuimaliza Ramadhwaan, wala anayeweza kunena ya kuwa ataishuhudia Ramadhwaan ya mwaka ujayo.

 

Ramadhwaan ni wakati wa kudhihirisha utiifu mbele ya Muumba, kwani lengo kuu la kuletwa kwetu ni kumuabudu Yeye tu bila ya mshirika:

 

{{Na sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu mimi.}} [Suratudh-Dhaariyat: 56].

Umefika wakati wa kudhihirisha khofu kwa Mola wetu Mtukufu. Haitokuwa na maana iwapo Ramadhwaan itamalizika hali ya kuwa nafsi haijazuilika kutenda maovu. Sio wakati wa kukaa kucheza bao, karata na mengineyo. Huu ni wakati kwa kila mtu kuirudi nafsi yake kwa mabaya aliyoyafanya.

Kutoka kwa  Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalah tano, na Ijumaa mpaka Ijumaa, na Ramadhaan mpaka Ramadhaan, zitamfidia baina yake madamu atakua ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa)) [Imepokewa na Muslim]

Huu ni wakati wa kuurekebisha ulimi kuwa ni wenye kusema kweli, kuacha fitna na kuacha kusengenya katika maisha yote yaliyobaki:

 

{{Na wale ambao ni wenye kujitenga na upuuzi}} [Suratul-Muuminuun: 3]

 

Funga ya kweli kweli ni ile ambayo ulimi pamoja na viungo vyote vinafunga na kuacha maasi kama linavyoachwa tumbo bila ya chakula. Na maovu ya kusengenya ni makubwa kwani Allaah Anasema:

 

{{Je anapenda mmoja wenu kula nyama ya ndugu yake akiwa maiti, mkamchukia?! Na mcheni Allaah hakika Allaah ni mwingi wa kusamehe na mwenye kurehemu.}} [Suratul-Hujuraat: 12]

 

Katu mwenye kufunga hatakiwi kupoteza wakati wake hata kidogo kwa mambo ya michezo. Huu ni wakati wa kutembelea wagonjwa ili kujionea tofauti ya uzima na ugonjwa. Ni wakati wa kulisha masikini ili kulichana chana pazia baina ya tajiri na masikini. Ramadhwaan ni wakati wa kuwa na uchu wa kukimbilia mema na pamoja na kuwa na wivu wa wakati wako namna sawa unavyoona wivu kwa ahli yako. Bila ya kusahau kusoma mno Qur-aan, kuswali kwa wingi, kukaa I’tikaaf pamoja na kuhudhuria darsa tofauti.

 

Basi tusikae tukawa na hiari katika amri za Mola wetu. Kwani Analotuamrisha Allaah lina kheri kwetu. Hekima za Swaum Anazijua zaidi Yeye Mtunga Shariy'ah kwani hatukupewa katika elimu ila kichache mno:

 

{{Hamkupewa katika elimu isipokuwa kidogo.}} [Suratu-Bani Israil: 85]

 

Bila ya kusahau kwamba fadhila za kufunga Ramadhwaan zitalipwa kikamilifu na Mola Siku ya Qiyaamah:

 

{{Bila shaka ahadi ya Allaah ni haki; basi yasikudanganyeni maisha ya (hii) dunia, wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Iblisi) katika (mambo ya) Allaah.}} [Suratu-Luqmaan: 33]

Share