Muda Wa Kumnyonyesha Mtoto Na Je Kuna Malipo Kama Hukumnyonyesha?
Muda Wa Kumnyonyesha Mtoto Na Je Kuna Malipo Kama Hukumnyonyesha?
SWALI
Asalaam alaykum.
Mimi nauliza ni muda gani wa kumyonyesha mtoto halafu kama haukutimia imetokea bahati mbaya unaweza kumlipa yule mtoto?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Muda wa kunyonyesha ni miaka miwili na hakuna fidia ya kumlipa mtoto ikiwa hutomnyonyesha mtoto wako. Mas-ala yote haya yamekusanyika dalili zake katika kauli ifuatayo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ ۚ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ ۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ۗ وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُوا أَوْلَادَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّا آتَيْتُم بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢٣٣﴾
Na wazazi wa kike wanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha. Na ni juu ya mzazi wa kiume kuwapatia chakula chao na nguo kwa mujibu wa ada. Hailazimishwi nafsi ila kwa iliwezalo. Asidhuriwe mzazi wa kike kwa ajili ya mwanawe, na wala mzazi wa kiume kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi (wa baba) mfano wa hivyo. Watakapotaka kumwachisha kunyonya kwa maridhiano baina yao wawili na mashauriano basi hapana dhambi juu ya wawili hao. Na mtakapotaka kutafuta wa kuwayonyesha watoto wenu, basi si dhambi kwenu ikiwa mtalipa mlichoahidi kwa mujibu wa shariy’ah. Na mcheni Allaah na jueni kwamba hakika Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuona. [Al-Baqarah: 233]
Lakini, mama anafaa atambue kuwa kumnyonyesha mtoto ni jambo lenye kumpatia faida nyingi mtoto pamoja na mama yake, kwani ni jambo la kiasili Alilojaaliya Allaah ('Azza wa Jalla) na kwa Rahmah Yake kubwa na Hikmah Yake na bila shaka faida zake hakuna asiyezikubali, kwani hata madaktari wametambua faida nyingi baada ya utafiti. Baadhi ya hizo faida tunazitaja hapa:
Faida Kwa Mtoto Mwenyewe:
1-Mtoto analindika na maradhi mengi ya kila aina.
2-Imepatikana asilimia ndogo ya vifo vya watoto wanaonyonyeshwa vifuani.
3-Asilimia kubwa imeonekana kuwa watoto wanaonyonyeshwa huwa ni wenye akili kubwa (mahodari) na wenye utulivu zaidi.
4-Maziwa ya mama ni chakula kamili anachokihitaji mtoto katika miezi yake ya mwanzo.
5-Maziwa ya mama yako tayari wakati wowote na yako katika hali ya joto linalomfaa mtoto.
6-Huenda maziwa ya kutengenezwa yakamfanyia mtoto mzio (allergy), ama maziwa ya kifuani hayana matatizo kama hayo.
7-Hupata hamu ya kupenda kula zaidi (appetite).
Faida Kwa Mzazi:
1-Mama atapata himaya kutokana na maradhi ya saratani (cancer).
2-Fuko la uzazi hurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kunyonyesha.
3-Mwili wa mama hupunguka uzito uliomzidi.
4-Ni njia ya kupunguza masarifu ya hela kwa kununua badala yake maziwa ya sinai (ya kutengenezwa) na pia kuepukana na malipo ya hospitali kutokana na utafiti ulioonekana kwamba asilimia kubwa ya watoto wasionyonyeshwa hupata maradhi mara kwa mara.
5-Kujipunguzia kazi za kutengeneza maziwa ya sinai (ya kutengenezwa) na kupata faida ya wakati zaidi, kwani ya kifuani yako tayari hayahitaji wakati wa kutengeneza, mbali pia kujiepusha na kazi za kukosha chupa na vifaa vya maziwa ya sinai.
6-Wakati wowote, mahali popote yako tayari hana haja mama ya kubeba chupa za maziwa anapotoka nje au anapokuwa safarini.
Faida Baina Ya Mama Na Mtoto:
1-Mtoto na mama wote kupata utulivu na kutulia nafsi.
2-Huathiri mapenzi baina yao yakawa makubwa zaidi.
3-Mama huridhika kuwa ameitumia Rahma na neema ya Allaah (Subhaana wa Ta'aalaa) na hutosheka kuwa ametimiza wajibu wake kwa mwanawe kwani wengi wanaoacha kunyonyesha huja kujuta baadaye.
Baada ya kutambua faida hizo hatudhani kama mama yeyote atapenda kuacha kumnyonyesha mtoto wake, kwani hii ni Rahmah na neema mojawapo kubwa kutoka kwa Allaah ('Azza wa Jalla) Aliyemjaalia mja Wake, kwa hivyo kwa nini mama asiitumie neema hii?
Na Allaah Anajua zaidi