010 - Yuwnus

 

 

يُونُس

 

010-Yuwnus

 

 

010-Yuwnus: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ﴿١﴾

1. Alif Laam Raa.[1] Hizi[2] ni Aayaat za Kitabu chenye hikmah.

 

 

 

أَكَانَ لِلنَّاسِ عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِّنْهُمْ أَنْ أَنذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا أَنَّ لَهُمْ قَدَمَ صِدْقٍ عِندَ رَبِّهِمْ ۗ قَالَ الْكَافِرُونَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ مُّبِينٌ﴿٢﴾

2. Je, imekuwa ni ajabu kwa watu kwamba Tumemfunulia Wahy mtu miongoni mwao kwamba: Waonye watu na wabashirie wale walioamini kwamba watapata cheo kitukufu mbele ya Rabb wao. Makafiri wakasema: Hakika huyu bila shaka ni mchawi bayana.

 

 

 

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۖ مَا مِن شَفِيعٍ إِلَّا مِن بَعْدِ إِذْنِهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ﴿٣﴾

3. Hakika Rabb wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu[3] ya ‘Arsh. Anaendesha mambo yote. Hakuna mwombezi yeyote ila baada ya Idhini Yake. Huyu Ndiye Allaah Rabb Wenu, basi mwabuduni. Je, hamkumbuki?

 

 

 

إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا ۖ وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا ۚ إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ ۚ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ﴿٤﴾

4. Kwake ni marejeo yenu nyote. Ni Ahadi ya Allaah ya kweli. Hakika Yeye Anaanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha ili Awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. Na wale waliokufuru watapata kinywaji cha maji ya kuchemka mno, na adhabu iumizayo kwa sababu ya kukufuru kwao.  

 

 

 

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ ۚ مَا خَلَقَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴿٥﴾

5. Yeye Ndiye Aliyejaalia jua kuwa ni mwanga na mwezi kuwa ni nuru, na Akaukadiria[4] vituo ili mjue idadi ya miaka na hesabu. Allaah Hakuumba hivyo ila kwa haki. Anafasili waziwazi Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) kwa watu wanaojua.

 

 

 

إِنَّ فِي اخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَّقُونَ﴿٦﴾

6. Hakika katika kukhitilafiana usiku na mchana na Alivyoviumba Allaah katika mbingu na ardhi, bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Dalili za wazi) kwa watu walio na taqwa.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ﴿٧﴾

7. Hakika wale wasiotaraji kukutana Nasi, na wakaridhika na uhai wa dunia na wakakinaika nayo, na wale ambao wanaghafilika na Aayaat Zetu (za kiulimwengu na kisharia).

 

 

 

أولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمُ النَّارُ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٨﴾

8. Hao makazi yao ni moto, kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ ۖتَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ﴿٩﴾

9. Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Rabb wao Atawaongoza kwa sababu ya imaan zao. Itapita chini yao mito katika Jannaat zilojaa neema.

 

 

 

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ ۚ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿١٠﴾

10. Wito wao humo ni: Subhaanak (Utakasifu ni Wako) ee Allaah! Na maamkizi yao humo ni Salaamun! Na wito wao wa mwisho ni AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Rabb wa walimwengu.

 

 

 

وَلَوْ يُعَجِّلُ اللَّـهُ لِلنَّاسِ الشَّرَّ اسْتِعْجَالَهُم بِالْخَيْرِ لَقُضِيَ إِلَيْهِمْ أَجَلُهُمْ ۖ فَنَذَرُ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ﴿١١﴾

11. Na lau Allaah Angeliwaharakizia watu shari kama wanavyojihimizia kheri, bila shaka wangehukumiwa muda wao (wa kuangamizwa). Basi Tunawaacha wale wasiotarajia kukutana Nasi katika upindukaji mipaka ya kuasi kwao, wakitangatanga kwa upofu.

 

 

 

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ الضُّرُّ دَعَانَا لِجَنبِهِ أَوْ قَاعِدًا أَوْ قَائِمًا فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُ ضُرَّهُ مَرَّ كَأَن لَّمْ يَدْعُنَا إِلَىٰ ضُرٍّ مَّسَّهُ ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْمُسْرِفِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿١٢﴾

12. Na inapomgusa binaadamu dhara hutuomba anapolala ubavu, au anapokaa au anaposimama wima. Tunapomuondolea dhara, hupita kama kwamba hakutuomba dhara iliyomgusa.[5] Hivyo ndivyo walivyopambiwa wapindukao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

 

وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا الْقُرُونَ مِن قَبْلِكُمْ لَمَّا ظَلَمُوا ۙ وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ وَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْقَوْمَ الْمُجْرِمِينَ﴿١٣﴾

13. Na kwa yakini Tuliangamiza karne nyingi kabla yenu walipodhulumu na wakawajia Rusuli wao kwa hoja bayana, na hawakuwa wa kuamini. Hivyo ndivyo Tunavyowalipa watu wahalifu.

 

 

 

ثُمَّ جَعَلْنَاكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ مِن بَعْدِهِمْ لِنَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ﴿١٤﴾

14. Kisha Tukakufanyeni warithi waandamizi katika ardhi baada yao, ili Tutazame vipi mtatenda.

 

 

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ ۙ قَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا ائْتِ بِقُرْآنٍ غَيْرِ هَـٰذَا أَوْ بَدِّلْهُ ۚ قُلْ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أُبَدِّلَهُ مِن تِلْقَاءِ نَفْسِي ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ ۖ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ﴿١٥﴾

15. Na wanaposomewa Aayaat Zetu bayana, wale wasiotaraji kukutana Nasi husema: Lete Qur-aan isiyokuwa hii au ibadilishe. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hainipasii mimi kuibadilisha kwa khiyari ya nafsi yangu. Mimi sifuati ila tu yale niliyofunuliwa Wahy. Hakika mimi nakhofu nikimuasi Rabb wangu, adhabu ya Siku iliyo kuu kabisa.

 

 

 

قُل لَّوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا تَلَوْتُهُ عَلَيْكُمْ وَلَا أَدْرَاكُم بِهِ ۖ فَقَدْ لَبِثْتُ فِيكُمْ عُمُرًا مِّن قَبْلِهِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ﴿١٦﴾

16. Sema: Kama Angetaka Allaah nisingelikusomeeni (hii Qur-aan) na wala Asingelikujulisheni nayo. Kwani nimekwishaishi nanyi umri wote kabla yake.  Je, basi hamtii akilini?

 

 

 

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِآيَاتِهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْمُجْرِمُونَ﴿١٧﴾

17. Basi nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemtungia Allaah uongo au akazikadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili) Zake? Hakika wahalifu hawatofaulu.

 

 

 

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ۚ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿١٨﴾

18.  Na wanaabudu pasi na Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na wanasema: Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah. Sema: Je, mnamjulisha Allaah yale Asiyoyajua katika mbingu na ardhini? Utakasifu ni Wake na Ametukuka kwa ‘Uluwa na yale yote wanayomshirikisha.

 

 

 

وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلَّا أُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُوا ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ فِيمَا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ﴿١٩﴾

19. Na watu hawakuwa ila ni ummah mmoja kisha wakakhitilafiana. Na kama si neno lililotangulia kutoka kwa Rabb wako, bila shaka ingehukumiwa baina yao katika yale wanayokhitilafiana.   

 

 

 

وَيَقُولُونَ لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۖ فَقُلْ إِنَّمَا الْغَيْبُ لِلَّـهِ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ﴿٢٠﴾

20. Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa Aayah (Ishara, Dalili) yoyote (ya kihisia) kutoka kwa Rabb wake? Basi sema: Hakika ya ghaibu ni ya Allaah Pekee. Basi ngojeeni, hakika na mimi niko pamoja nanyi katika wanaongojea. 

 

 

 

 

وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً مِّن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُمْ إِذَا لَهُم مَّكْرٌ فِي آيَاتِنَا ۚ قُلِ اللَّـهُ أَسْرَعُ مَكْرًا ۚ إِنَّ رُسُلَنَا يَكْتُبُونَ مَا تَمْكُرُونَ﴿٢١﴾

21. Na Tunapowaonjesha watu rehma baada ya dhara iliyowagusa, tahamaki wanafanya hila kuzichafua Aayaat (na Ishara, Dalili) Zetu. Sema: Allaah Ni Mwepesi zaidi wa Kutibua hila. Hakika Wajumbe Wetu wanaandika hila mnazopanga.

 

 

 

هُوَ الَّذِي يُسَيِّرُكُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا كُنتُمْ فِي الْفُلْكِ وَجَرَيْنَ بِهِم بِرِيحٍ طَيِّبَةٍ وَفَرِحُوا بِهَا جَاءَتْهَا رِيحٌ عَاصِفٌ وَجَاءَهُمُ الْمَوْجُ مِن كُلِّ مَكَانٍ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ أُحِيطَ بِهِمْ ۙ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ لَئِنْ أَنجَيْتَنَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ﴿٢٢﴾

22. Yeye Ndiye Anayekuendesheni katika bara na bahari. Mpaka mnapokuwa katika majahazi na yakawa yanakwenda nao kwa upepo wa kheri, mzuri, na wao wakafurahia, mara ukawajia upepo wa dhoruba, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakayakinisha kwamba wameshazungukwa. Hapo humwomba Allaah wakimtakasia Yeye Dini[6] (wakisema): Ukituokoa katika haya, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.  

 

 

 

فَلَمَّا أَنجَاهُمْ إِذَا هُمْ يَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۗ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا بَغْيُكُمْ عَلَىٰ أَنفُسِكُم ۖ مَّتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُكُمْ فَنُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٢٣﴾

23. Lakini Anapowaokoa, tahamaki wao wanafanya tena uovu wa maasi na dhulma katika ardhi bila ya haki. Enyi watu! Hakika baghi[7] yenu (uovu wenu) utawarudia wenyewe. Ni starehe ya uhai wa dunia. Kisha Kwetu marejeo yenu, na Tutakujulisheni mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

إِنَّمَا مَثَلُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ مِمَّا يَأْكُلُ النَّاسُ وَالْأَنْعَامُ حَتَّىٰ إِذَا أَخَذَتِ الْأَرْضُ زُخْرُفَهَا وَازَّيَّنَتْ وَظَنَّ أَهْلُهَا أَنَّهُمْ قَادِرُونَ عَلَيْهَا أَتَاهَا أَمْرُنَا لَيْلًا أَوْ نَهَارًا فَجَعَلْنَاهَا حَصِيدًا كَأَن لَّمْ تَغْنَ بِالْأَمْسِ ۚ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿٢٤﴾

24. Hakika mfano wa uhai wa dunia ni kama maji Tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika nayo mimea ya ardhi katika wanayoila watu na wanyama. Mpaka ardhi inapokamilisha uzuri wake na ikapambika, na wakayakinisha watu wake kwamba wanao uwezo juu yake (kuivuna), tahamaki Amri Yetu ikaijia usiku au mchana, Tukaifanya kama iliyofyekwa kama kwamba haikusitawi jana. Hivyo ndivyo Tunavyofasili waziwazi Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) kwa watu wanaotafakari.

 

 

 

وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَىٰ دَارِ السَّلَامِ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٢٥﴾

25. Na Allaah Anaitia katika Daar As-Salaam (Nyumba ya amani) na Anamwongoza Amtakaye kuelekea njia iliyonyooka.

 

 

 

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ وَلَا يَرْهَقُ وُجُوهَهُمْ قَتَرٌ وَلَا ذِلَّةٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿٢٦﴾

26. Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (huko Jannah) jazaa nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah).[8] Na vumbi halitowafunika nyuso zao wala madhila. Hao ni watu wa Jannah, humo wao watadumu.

 

 

 

وَالَّذِينَ كَسَبُوا السَّيِّئَاتِ جَزَاءُ سَيِّئَةٍ بِمِثْلِهَا وَتَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ مَّا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِنْ عَاصِمٍ ۖ كَأَنَّمَا أُغْشِيَتْ وُجُوهُهُمْ قِطَعًا مِّنَ اللَّيْلِ مُظْلِمًا ۚ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿٢٧﴾

27. Na wale waliochuma maovu, jazaa ya uovu ni mfano wake vile vile, na madhila yatawafunika. Hawatopata atakayewaepusha na (Adhabu ya) Allaah. (Zitakuwa) nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wenye giza kubwa. Hao ni watu wa motoni, humo wao watadumu.

 

 

وَيَوْمَ نَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ نَقُولُ لِلَّذِينَ أَشْرَكُوا مَكَانَكُمْ أَنتُمْ وَشُرَكَاؤُكُمْ ۚ فَزَيَّلْنَا بَيْنَهُمْ ۖ وَقَالَ شُرَكَاؤُهُم مَّا كُنتُمْ إِيَّانَا تَعْبُدُونَ﴿٢٨﴾

28. Na Siku Tutakayowakusanya wote, kisha Tutawaambia wale walioshirikisha: Bakieni mahali penu nyinyi na washirika wenu. Kisha Tutawatenganisha baina yao. Na washirika wao watasema: Hamkuwa mkituabudu sisi.

 

 

 

فَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ إِن كُنَّا عَنْ عِبَادَتِكُمْ لَغَافِلِينَ﴿٢٩﴾

29. Basi Allaah Anatosheleza kuwa Mwenye Kushuhudia yote baina yetu na baina yenu kwamba sisi tulikuwa hatuna khabari na ibaada zenu. 

 

 

 

هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَّا أَسْلَفَتْ ۚ وَرُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۖ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ﴿٣٠﴾

30. Huko (Qiyaamah) kila nafsi itatiwa mtihanini[9]  kwa yote iliyoyatanguliza. Na watarudishwa kwa Allaah, Mawlaa[10] wao wa haki. Na yatawapotea yale yote waliyokuwa wakiyatunga (ya uongo).

 

 

 

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾

31. Sema: Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Au nani anayemiliki kusikia na kuona?   Na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye hai? Na nani anayeendesha mambo (yote)?  Watasema: Ni Allaah. Basi sema: Je, basi hamuwi na taqwa?[11]

 

 

 

فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ﴿٣٢﴾

32. Basi Huyo Ndiye Allaah, Rabb wenu wa haki. Na kuna nini baada ya haki ila upotofu? Basi vipi mnageuzwa?

 

 

 

كَذَٰلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ فَسَقُوا أَنَّهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٣٣﴾

33. Hivyo ndivyo Neno la Rabb wako lilivyothibiti juu ya wale waliofanya ufasiki kwamba hawatoamini.

 

 

 

 

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ۚ قُلِ اللَّـهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ﴿٣٤﴾

34. Sema: Je, yuko kati ya washirika wenu anayeanzisha uumbaji kisha anaurudisha? Sema: Allaah Anaanzisha uumbaji kisha Anaurudisha. Basi vipi mnaghilibiwa?  

 

 

 

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ ۚ قُلِ اللَّـهُ يَهْدِي لِلْحَقِّ ۗ أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لَّا يَهِدِّي إِلَّا أَن يُهْدَىٰ ۖ فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ﴿٣٥﴾

35. Sema: Je, yuko kati ya washirika wenu anayeongoza kwenye haki? Sema: Allaah Anaongoza kwenye haki. Je, basi anayeongoza kwenye haki anastahiki zaidi kufuatwa au yule asiyeongoza isipokuwa tu yeye aongozwe?  Basi mna nini? Vipi mnahukumu?

 

 

 

وَمَا يَتَّبِعُ أَكْثَرُهُمْ إِلَّا ظَنًّا ۚ إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ﴿٣٦﴾

36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Hakika dhana haifai kitu chochote mbele ya haki. Hakika Allaah Ni Mjuzi kwa yale yote wayatendayo.

 

 

وَمَا كَانَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ أَن يُفْتَرَىٰ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ﴿٣٧﴾

37. Na haiwezekani hii Qur-aan kuwa imetungwa bila kuwa imetoka kwa Allaah, lakini inasadikisha yale yaliyokuja kabla yake na ni tafsili ya Vitabu (vilivyoitangulia).[12] Haina shaka ndani yake, imetoka kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّثْلِهِ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٣٨﴾

38. Je, wanasema (Qur-aan) ameitunga (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)?  Sema: Hebu basi leteni Suwrah ya mfano wake,[13] na waiteni mnaoweza pasi na Allaah mkiwa ni wakweli.

 

 

 

بَلْ كَذَّبُوا بِمَا لَمْ يُحِيطُوا بِعِلْمِهِ وَلَمَّا يَأْتِهِمْ تَأْوِيلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ﴿٣٩﴾

39. Bali wamekadhibisha yale wasiyoyaelewa vyema ilimu yake, na wala uhakika wake halisi haujawafikia. Hivyo ndivyo walivyokadhibisha wale wa kabla yao. Basi tazama vipi ilikuwa hatima ya madhalimu.

 

 

 

وَمِنْهُم مَّن يُؤْمِنُ بِهِ وَمِنْهُم مَّن لَّا يُؤْمِنُ بِهِ ۚ وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِالْمُفْسِدِينَ﴿٤٠﴾

40. Na miongoni mwao wako wanaoiamini, na miongoni mwao wako wasioiamini. Na Rabb wako Anawajua zaidi mafisadi.

 

 

 

وَإِن كَذَّبُوكَ فَقُل لِّي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ ۖ أَنتُم بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٤١﴾

41. Na wakikukadhibisha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi sema: Mimi nina amali zangu, nanyi mna amali zenu. Nyinyi hamna dhima na yale niyatendayo, na wala mimi sina dhima na yale myatendayo.

 

 

 

وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ ۚ أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ وَلَوْ كَانُوا لَا يَعْقِلُونَ﴿٤٢﴾

42. Na miongoni mwao wako wanaokusikiliza. Je, kwani wewe unasikilizisha viziwi japokuwa hawatii akilini?

 

 

 

وَمِنْهُم مَّن يَنظُرُ إِلَيْكَ ۚ أَفَأَنتَ تَهْدِي الْعُمْيَ وَلَوْ كَانُوا لَا يُبْصِرُونَ﴿٤٣﴾

43. Na miongoni mwao wako wanaokutazama. Je, kwani wewe unaongoza (wahidike) vipofu japokuwa hawaoni?

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ﴿٤٤﴾

44. Hakika Allaah Hadhulumu watu chochote, lakini watu wenyewe ni wenye kudhulumu nafsi zao.

 

 

 

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ كَأَن لَّمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّنَ النَّهَارِ يَتَعَارَفُونَ بَيْنَهُمْ ۚ قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّـهِ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ﴿٤٥﴾

45. Na Siku Atakayowakusanya (wataona) kama kwamba hawakuishi isipokuwa saa moja ya mchana, watatambuana. Kwa yakini wamekhasirika wale waliokadhibisha kukutana na Allaah, na hawakuwa wenye kuhidika.

 

 

 

وَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ اللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ﴿٤٦﴾

46. Na kama Tutakuonyesha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) baadhi ya yale Tunayowaahidi (ya adhabu) au Tukikufisha, basi Kwetu ni marejeo yao, kisha Allaah Ni Mwenye Kushuhudia yote juu ya yale wanayoyatenda.

 

 

 

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ ۖ فَإِذَا جَاءَ رَسُولُهُمْ قُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿٤٧﴾

47. Na kila ummah una Rasuli. Basi anapokuja Rasuli wao inahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatodhulumiwa.

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٤٨﴾

48. Na wanasema: Lini (itafika) hiyo ahadi[14] mkiwa ni wakweli?

 

 

 

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ ۚ إِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَلَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً ۖ وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ﴿٤٩﴾

49. Sema: Siimilikii nafsi yangu dhara wala manufaa isipokuwa Aliyotaka Allaah. Kila ummah una muda maalumu. Utakapofika muda wao, basi hawatoweza kuakhirisha saa moja wala hawatoweza kutanguliza.

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُهُ بَيَاتًا أَوْ نَهَارًا مَّاذَا يَسْتَعْجِلُ مِنْهُ الْمُجْرِمُونَ﴿٥٠﴾

50. Sema: Mnaonaje ikikufikieni Adhabu Yake usiku au mchana, sehemu ipi wanaihimiza wahalifu?

 

 

 

أَثُمَّ إِذَا مَا وَقَعَ آمَنتُم بِهِ ۚ آلْآنَ وَقَدْ كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ﴿٥١﴾

51. Kisha tena itakapotokea ndio mtaiamini? Je, sasa tena? Na ilhali mlikuwa mnaihimiza?

 

 

 

ثُمَّ قِيلَ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا بِمَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ﴿٥٢﴾

52. Kisha wataambiwa wale waliodhulumu: Onjeni adhabu ya kudumu milele. Kwani je, mtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?

 

 

 

وَيَسْتَنبِئُونَكَ أَحَقٌّ هُوَ ۖ قُلْ إِي وَرَبِّي إِنَّهُ لَحَقٌّ ۖ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ﴿٥٣﴾

53. Na wanakuuliza: Je, hiyo (adhabu na Qiyaamah) ni kweli?  Sema: Ndio! Naapa kwa Rabb wangu! Hakika hiyo bila shaka ni kweli! Nanyi si wenye kuweza kushinda (kuikwepa).

 

 

 

وَلَوْ أَنَّ لِكُلِّ نَفْسٍ ظَلَمَتْ مَا فِي الْأَرْضِ لَافْتَدَتْ بِهِ ۗ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ ۖ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ ۚ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿٥٤﴾

54. Na kama ingelikuwa kila nafsi iliyodhulumu, inamiliki yote yaliyomo katika ardhi, bila shaka ingeliyatolea fidia kwayo. Na wataficha (au watafichua) majuto watakapoona adhabu. Na itahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatodhulumiwa. 

 

 

 

أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴿٥٥﴾

55. Tanabahi! Hakika ni vya Allaah vilivyomo katika mbingu na ardhi. Tanabahi! Hakika Ahadi ya Allaah ni kweli, lakini wengi wao hawajui.

 

 

 

هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٥٦﴾

56. Yeye Ndiye Anayehuisha na Anayefisha, na Kwake mtarejeshwa.

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾

57. Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rehma kwa Waumini.[15]

 

 

 

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾

58. Sema: Kwa Fadhila za Allaah na kwa Rehma Yake basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.[16]

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ لَكُم مِّن رِّزْقٍ فَجَعَلْتُم مِّنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّـهُ أَذِنَ لَكُمْ ۖ أَمْ عَلَى اللَّـهِ تَفْتَرُونَ﴿٥٩﴾

59. Sema: Mnaonaje zile riziki Alizokuteremshieni Allaah, kisha mkazifanya katika hizo ni haramu na halali. Sema: Je, Allaah Amekupeni idhini au mnamtungia (uongo) Allaah?

 

 

 

وَمَا ظَنُّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَشْكُرُونَ﴿٦٠﴾

60. Na nini dhana ya wale wanaomtungia Allaah uongo Siku ya Qiyaamah? Hakika Allaah bila shaka Ana Fadhila (nyingi) juu ya watu, lakini wengi wao hawashukuru.

 

 

 

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦١﴾

61. Na hushughuliki katika jambo lolote, wala husomi humo katika Qur-aan, wala hamtendi amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Rabb wako hata cha uzito wa chembe (kama atomu) katika ardhi, wala mbinguni, wala kidogo kuliko hicho, wala kikubwa zaidi ya hicho, isipokuwa kimo katika Kitabu bainifu.[17]

 

 

 

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴿٦٢﴾

62. Tanabahi! Hakika Vipenzi wa Allaah hawana khofu na wala hawatohuzunika.[18]

 

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ﴿٦٣﴾

63. Ambao wameamini na wakawa wana taqwa.

 

 

 

لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۚ لَا تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٦٤﴾

64. Watapata bishara katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Hakuna mabadiliko katika Maneno ya Allaah. Huko ndiko kufuzu kukubwa mno.

 

 

 

وَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا ۚ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٦٥﴾

65. Na wala maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika taadhima zote ni za Allaah Pekee. Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ ۗ وَمَا يَتَّبِعُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ شُرَكَاءَ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ﴿٦٦﴾

66. Tanabahi kwamba ni wa Allaah wote waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na hawafuati wale wanawaomba pasi na Allaah kuwa ni washirika (Wake). Hawafuati isipokuwa dhana, nao hawana isipokuwa wanabuni uongo.

 

 

 

هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ﴿٦٧﴾

67. Yeye Ndiye Aliyekufanyieni usiku ili mpate utulivu humo, na mchana kwa ajili ya kuonea. Hakika katika hayo zipo Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) kwa watu wanaosikia (wakazingatia).

 

 

 

قَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ الْغَنِيُّ ۖ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ إِنْ عِندَكُم مِّن سُلْطَانٍ بِهَـٰذَا ۚ أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴿٦٨﴾

68. Wanasema: Allaah Amejifanyia mwana![19] Subhaanah! (Utakasifu ni Wake) Yeye Ni Mkwasi. Ni Vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Hamna nyinyi dalili kwa hayo. Je, mnasema juu ya Allaah msiyoyajua?

 

 

 

قُلْ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ﴿٦٩﴾

69. Sema: Hakika wale wanaomtungia uongo Allaah hawatofaulu.

 

 

 

مَتَاعٌ فِي الدُّنْيَا ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ نُذِيقُهُمُ الْعَذَابَ الشَّدِيدَ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ﴿٧٠﴾

70. Starehe ya muda katika dunia, kisha Kwetu ndio marejeo yao, kisha Tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya ukafiri wao.

 

 

 

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ نُوحٍ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِن كَانَ كَبُرَ عَلَيْكُم مَّقَامِي وَتَذْكِيرِي بِآيَاتِ اللَّـهِ فَعَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْتُ فَأَجْمِعُوا أَمْرَكُمْ وَشُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُنْ أَمْرُكُمْ عَلَيْكُمْ غُمَّةً ثُمَّ اقْضُوا إِلَيَّ وَلَا تُنظِرُونِ﴿٧١﴾

71. Na wasomee khabari ya Nuwh, alipoiambia kaumu yake: Enyi kaumu yangu! Ikiwa kukaa kwangu na kukumbusha kwangu Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) za Allaah kumekuwa ni mashaka juu yenu, basi kwa Allaah natawakali. Hivyo pangeni jambo lenu na washirika wenu (mnidhuru), kisha jambo lenu lisifichike kwenu, kisha nihukumuni (kwa adhabu) wala msinipe muhula.

 

 

 

فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَمَا سَأَلْتُكُم مِّنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٧٢﴾

72. Lakini mkikengeuka, basi sijakuombeni ujira wowote. Sitaki ujira isipokuwa kwa Allaah na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu.

 

 

 

فَكَذَّبُوهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ فِي الْفُلْكِ وَجَعَلْنَاهُمْ خَلَائِفَ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۖ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنذَرِينَ﴿٧٣﴾

73. Lakini walimkadhibisha. Tukamuokoa (Nuwh) pamoja na waliokuwa naye katika jahazi, na Tukawafanya wao ndio waliobakia (warithi)[20] na Tukawagharikisha wale waliokadhibisha Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) Zetu. Basi tazama vipi ilikuwa khatima ya walioonywa.

 

 

 

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِ رُسُلًا إِلَىٰ قَوْمِهِمْ فَجَاءُوهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا بِهِ مِن قَبْلُ ۚ كَذَٰلِكَ نَطْبَعُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْمُعْتَدِينَ﴿٧٤﴾

74. Kisha Tukapeleka baada yake Rusuli kwa kaumu zao, wakawajia kwa hoja bayana, lakini hawakuwa wenye kuyaamini yale waliyoyakadhibisha zamani.  Hivyo ndivyo Tunavyopiga chapa juu ya nyoyo za wenye kutaadi.

 

 

 

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَىٰ وَهَارُونَ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ بِآيَاتِنَا فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ﴿٧٥﴾

75. Kisha baada ya hao, Tukamtuma Muwsaa na Haaruwn kwa Firawni na wakuu wake kwa Aayaat (Miujiza, Ishara) Zetu, wakatakabari na wakawa watu wahalifu.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِندِنَا قَالُوا إِنَّ هَـٰذَا لَسِحْرٌ مُّبِينٌ﴿٧٦﴾

76. Ilipowajia haki kutoka Kwetu, walisema: Hii bila shaka ni sihiri bayana.

 

 

 

قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ ۖ أَسِحْرٌ هَـٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ﴿٧٧﴾

77. Muwsaa akasema: Je, mnasema (ni sihiri bayana) haki ilipokujeni? Hii ni sihiri hii? Na wachawi hawafaulu.

 

 

 

قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَلْفِتَنَا عَمَّا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا وَتَكُونَ لَكُمَا الْكِبْرِيَاءُ فِي الْأَرْضِ وَمَا نَحْنُ لَكُمَا بِمُؤْمِنِينَ﴿٧٨﴾

78. Wakasema: Je, umetujia ili utugeuze tuyaache yale tuliyowakuta nayo baba zetu, na ili muwe nyinyi wawili na ukubwa na uadhama katika nchi? Na sisi hatutawaamini nyinyi.

 

 

 

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ائْتُونِي بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ﴿٧٩﴾

79. Na Firawni akasema: Nileteeni kila mchawi mjuzi.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ﴿٨٠﴾

80. Walipokuja wachawi, Muwsaa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa.

 

 

 

فَلَمَّا أَلْقَوْا قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئْتُم بِهِ السِّحْرُ ۖ إِنَّ اللَّـهَ سَيُبْطِلُهُ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُصْلِحُ عَمَلَ الْمُفْسِدِينَ﴿٨١﴾

81. Basi walipotupa, Muwsaa alisema: Mliyokuja nayo ni sihiri.  Hakika Allaah Atayabatilisha. Hakika Allaah Hatengenezi amali za mafisadi.

 

 

 

وَيُحِقُّ اللَّـهُ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ﴿٨٢﴾

82. Na Allaah Atathibitisha haki kwa Maneno Yake japokuwa watakirihika wahalifu.

 

 

 

فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِّن قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِّن فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَن يَفْتِنَهُمْ ۚ وَإِنَّ فِرْعَوْنَ لَعَالٍ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الْمُسْرِفِينَ﴿٨٣﴾

83. Basi hawakumwamini Muwsaa isipokuwa vijana katika kaumu yake kwa sababu ya kumkhofu Firawni na wakuu wao wasiwatese. Na hakika Firawni ni jeuri katika ardhi, na hakika yeye bila shaka ni miongoni mwa wapindukao mipaka.

 

 

 

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ﴿٨٤﴾

84. Na Muwsaa akasema: Enyi kaumu yangu! Ikiwa mmemwamini Allaah, basi Kwake mtawakali, mkiwa ni Waislamu.

 

 

 

فَقَالُوا عَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ﴿٨٥﴾

85. Wakasema: Tumetawakali kwa Allaah. Ee Rabb wetu! Usitujaalie kuwa ni mtihani kwa watu madhalimu.

 

 

 

وَنَجِّنَا بِرَحْمَتِكَ مِنَ الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ﴿٨٦﴾

86. Na Tuokoe kwa Rehma Yako na watu makafiri.

 

 

 

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ وَأَخِيهِ أَن تَبَوَّآ لِقَوْمِكُمَا بِمِصْرَ بُيُوتًا وَاجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ قِبْلَةً وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ﴿٨٧﴾

87. Na Tukamfunulia Wahy Muwsaa na kaka yake kwamba: Watengenezeeni watu wenu katika mji nyumba, na zifanyeni nyumba zenu sehemu za ibaada na simamisheni Swalaah. Na wabashirie Waumini.

 

 

 

وَقَالَ مُوسَىٰ رَبَّنَا إِنَّكَ آتَيْتَ فِرْعَوْنَ وَمَلَأَهُ زِينَةً وَأَمْوَالًا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا رَبَّنَا لِيُضِلُّوا عَن سَبِيلِكَ ۖ رَبَّنَا اطْمِسْ عَلَىٰ أَمْوَالِهِمْ وَاشْدُدْ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُوا حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ﴿٨٨﴾

88. Na Muwsaa akasema: Ee Rabb Wetu! Hakika Wewe Umempa Firawni na wakuu wake mapambo na mali katika uhai wa dunia. Ee Rabb wetu, ili wapoteze (watu) Njia Yako. Rabb wetu! Ziangamize mali zao na fanya nyoyo zao ziwe ngumu kwani hawatoamini mpaka waone adhabu iumizayo.

 

 

 

قَالَ قَدْ أُجِيبَت دَّعْوَتُكُمَا فَاسْتَقِيمَا وَلَا تَتَّبِعَانِّ سَبِيلَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨٩﴾

89. (Allaah) Akasema: Imekwishaitikiwa duaa yenu nyinyi wawili, basi lingamaneni sawasawa na wala msifuate njia ya wale ambao hawajui.

 

 

 

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٩٠﴾

90. Tukawavukisha wana wa Israaiyl bahari. Basi Firawni akawafuata na jeshi lake kwa baghi[21] (dhulma) na uonevu mpaka ilipomfikia (Firawni) gharka akasema: Nimeamini kwamba hapana mwabudiwa wa haki, isipokuwa Yule waliyemwamini wana wa Israaiyl, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.

 

 

 

آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ﴿٩١﴾

91. Sasa (ndio unaamini) na ihali umeasi kabla, na ulikuwa miongoni mwa mafisadi!?

 

 

 

فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً ۚ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ﴿٩٢﴾

92. Basi leo Tunakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako ili uwe Aayah (Ishara, Zingatio, Dalili) kwa watakaokuja nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu.  

 

 

 

وَلَقَدْ بَوَّأْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مُبَوَّأَ صِدْقٍ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ فَمَا اخْتَلَفُوا حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْعِلْمُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ﴿٩٣﴾

93. Na kwa yakini Tuliwapa makazi wana wa Israaiyl; makazi mazuri, na Tukawaruzuku katika vizuri, na hawakukhitilafiana mpaka ilipowajia ilimu. Hakika Rabb wako Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah katika yale yote waliyokuwa wakikhitilafiana.

 

 

 

فَإِن كُنتَ فِي شَكٍّ مِّمَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ فَاسْأَلِ الَّذِينَ يَقْرَءُونَ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكَ ۚ لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ﴿٩٤﴾

94. Na ukiwa una shaka (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika yale Tuliyokuteremshia, basi waulize wale wanaosoma Kitabu kabla yako. Kwa yakini imekujia haki kutoka kwa Rabb wako, basi usijekuwa miongoni mwa wanaoshuku.[22]   

 

 

وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَتَكُونَ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٩٥﴾

95. Wala usijekuwa miongoni mwa wale waliokadhibisha Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) za Allaah ukawa miongoni mwa waliokhasirika.    

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ حَقَّتْ عَلَيْهِمْ كَلِمَتُ رَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٩٦﴾

96. Hakika wale ambao Neno la (ghadhabu la) Rabb wako limethibiti juu yao, hawataamini.

 

 

 

وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ﴿٩٧﴾

97. Japokuwa itawajia kila Aayah (Ishara, Dalili, Mawaidha) mpaka waone adhabu iumizayo.

 

 

 

فَلَوْلَا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَىٰ حِينٍ﴿٩٨﴾

98. Basi kwa nini usiweko mji mmoja ukaamini na imaan yake ikawafaa - (haukutokea) isipokuwa kaumu ya Yuwnus. Walipoamini, Tuliwaondoshea adhabu ya hizaya duniani, na Tukawasterehesha mpaka muda maalumu.[23]

 

 

 

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَآمَنَ مَن فِي الْأَرْضِ كُلُّهُمْ جَمِيعًا ۚ أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ﴿٩٩﴾

99. Na kama Angetaka Rabb wako, basi wangeliamini wote pamoja walioko katika ardhi. Je, basi wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) utashurutisha watu mpaka wawe Waumini?

 

 

 

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تُؤْمِنَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَجْعَلُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ﴿١٠٠﴾

100. Na haiwezekani nafsi yoyote ikaamini isipokuwa kwa Idhini ya Allaah. Naye Hujaalia adhabu (na upotofu) kwa wale wasiotia akilini.

 

 

 

قُلِ انظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ﴿١٠١﴾

101. Sema: Tazameni yaliyoko mbinguni na ardhini. Lakini Aayaat (Ishara, Dalili) zote na maonyo (ya Rusuli) hayawafai kitu watu wasioamini.

 

 

 

فَهَلْ يَنتَظِرُونَ إِلَّا مِثْلَ أَيَّامِ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِهِمْ ۚ قُلْ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ﴿١٠٢﴾

102. Je, wanangojea jingine (la maangamizi) isipokuwa mfano wa siku za wale waliopita kabla yao? Sema: Basi ngojeeni, hakika mimi ni pamoja nanyi miongoni mwa wanaongojea.

 

 

 

ثُمَّ نُنَجِّي رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ حَقًّا عَلَيْنَا نُنجِ الْمُؤْمِنِينَ﴿١٠٣﴾

103. Kisha Tunawaokoa Rusuli Wetu na wale walioamini. Hivyo ndivyo haki Kwetu kuwaokoa Waumini.

 

 

 

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي شَكٍّ مِّن دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّـهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ﴿١٠٤﴾

104. Sema (Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Enyi watu! Ikiwa mna shaka na Dini yangu, basi mimi siabudu ambavyo mnaviabudu badala ya Allaah, lakini namwabudu Allaah Ambaye Anakufisheni. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waumini.

 

 

 

 

وَأَنْ أَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴿١٠٥﴾

105.  Na elekeza uso wako kwa Dini (ya Allaah), usimili kwengine na wala usijekuwa miongoni mwa washirikina.

 

 

 

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾

106. Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

 

 

 

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾

107. Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha Fadhila Zake. Humfikishia (Fadhila Yake) Amtakaye katika Waja Wake. Naye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُمُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ وَمَا أَنَا عَلَيْكُم بِوَكِيلٍ﴿١٠٨﴾

108. Sema: Enyi watu!  Kwa yakini imekujieni haki kutoka kwa Rabb wenu. Basi atakayehidika, hakika anahidika kwa faida ya nafsi yake. Na atakayepotoka, hakika anapotoka kwa hasara ya nafsi yake. Nami si mdhamini wenu.

 

 

 

وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَاصْبِرْ حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ﴿١٠٩﴾

109. Na fuata (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) yale uliyofunuliwa Wahy, na subiri mpaka Allaah Ahukumu. Naye Ni Mbora wa wanaohukumu.

 

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2]  Sababu Ya Kutarjumi “Hizi” Badala Ya “Hizo” Kulingana Na Neno تِلْكَ:  

 

Rejea Al-Baqarah (2:2). Na Suwrat Yuwsuf (12:1), Ar-Ra’ad (13:1), Al-Hijr (15:1), An-Naml (27:1), na Luqmaan (31:2), Suwrah zote zimeanzia kama hivyo.

 

[3] Istawaa اسْتَوَى

 

Yuko juu kwa namna inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake Yeye Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-A'raaf (7:54) kwenye maelezo bayana ya maana yake, yenye kutofautiana na maana ya katika Suwrah Al-Baqarah (2:29) na Suwrat Fusswilat (41:11).

 

[4] Takdiri (Qudura, Uwezo, Ukadiriaji) Wa Allaah (عزّ وجلّ) Katika Uumbaji Na Uendeshaji Wa Ulimwengu:

 

Aayah inayofuatia pia inahusiana uumbaji wa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Yaasiyn (36:38) kwenye maelezo yenye faida tele.

 

[5] Hali Ya Binaadam Asiyekuwa Muumini Anapopatwa Dhara:

 

Rejea pia Huwd (11:10-11), Al-Israa (17:83), Ar-Ruwm (30:33), Az-Zumar (39:49), Fusw-Swilat (41:49) (41:51).  

 

Muumini hapaswi kuwa katika hali hiyo ilivyotajwa katika Aayah tukufu kwamba awe mwenye kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kumwabudu na kumnyenyekea na kumuomba duaa tele wakati anapopatwa dhara. Na pindi anapoondoshewa dhara hizo, basi humsahau Allaah (سبحانه وتعالى)! Ametufunza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth ifuatayo:

 

عن ابنِ عباسٍ رضي الله عنهما، قَالَ: كنت خلف النَّبيّ صلى الله عليه وسلم يومًا، فَقَالَ:  يَا غُلامُ، إنِّي أعلّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَألْتَ فَاسأَلِ الله، وإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ باللهِ. وَاعْلَمْ: أنَّ الأُمَّةَ لَوْ اجْتَمَعَتْ عَلَى أنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبهُ اللهُ لَكَ، وَإِن اجتَمَعُوا عَلَى أنْ يَضُرُّوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأَقْلاَمُ وَجَفَّتِ الصُّحفُ . رواه الترمذي، وَقالَ:  حديث حسن صحيح

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  [juu ya mnyama]. Akaniambia: “Ee kijana! Mimi nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi. Mhifadhi Allaah utamkuta yupo mbele yako. Unapoomba, muombe Allaah. Unapotaka msaada, mtake Allaah. Fahamu kuwa, lau ummah (wote) utajikusanya ili wakunufaishe kwa jambo, basi hawataweza kukunufaisha ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah. Na wakijumuika ili wakudhuru kwa jambo, hawataweza kukudhuru ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah. Kalamu zimeshasimama na karatasi zimeshakauka.” [At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

وفي رواية غيرِ الترمذي:  احْفَظِ الله تَجِدْهُ أَمَامَكَ، تَعرَّفْ إِلَى اللهِ في الرَّخَاءِ يَعْرِفكَ في الشِّدَّةِ، وَاعْلَمْ: أنَّ مَا أَخْطَأكَ لَمْ يَكُنْ لِيُصِيبكَ، وَمَا أصَابَكَ لَمْ يَكُنْ لِيُخْطِئَكَ، وَاعْلَمْ: أنَّ النَّصْرَ مَعَ الصَّبْرِ، وَأَنَّ الفَرَجَ مَعَ الكَرْبِ، وَأَنَّ مَعَ العُسْرِ يُسْرًا

 

Riwaayah nyingine isiyokuwa ya At-Tirmidhiy imesema:

 

“Mhifadhi Allaah utamkuta Yupo mbele yako. Mjue Allaah katika raha Naye Atakujua katika shida. Ujue kuwa, lililokukosa halikuwa ni lenye kukupata, na lililokusibu halikuwa ni lenye kukukosa. Ujue kuwa nusura ipo pamoja na subira, faraja ipo pamoja na dhiki, na kwenye uzito kuna wepesi.”

 

Basi Muumini anapaswa kumshukuru Rabb wake katika hali yoyote ile. Na hilo ni jambo la jaabu kwa Muumini wa kweli kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

وعن أبي يحيى صهيب بن سنانٍ رضي الله عنه، قَالَ: قَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم:  عَجَبًا لأمْرِ المُؤمنِ إنَّ أمْرَهُ كُلَّهُ لَهُ خيرٌ ولَيسَ ذلِكَ لأَحَدٍ إلا للمُؤْمِن: إنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكانَ خَيرًا لَهُ، وإنْ أصَابَتْهُ ضرَاءُ صَبَرَ فَكانَ خَيْرًا لَهُ رواه مسلم

Amesimulia Abuu Yahyaa Swuhayb (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya hali ya Muumini kuwa mambo yake yote ni kheri. Na haiwi hivyo (sifa hiyo) kwa yeyote ila kwa Muumini. Anapofikwa na furaha hushukuru na huwa kheri kwake, na anapofikwa na matatizo husubiri na huwa ni kheri kwake .”[Muslim]

 

[6]  Shirki Za Washirikina Wa Zama Hizi Ni Kubwa Zaidi Kuliko Za Washirikina Wa Awali:

 

Rejea pia Al-Israa (17:67), Al-‘Ankabuwt (29:65), na Luqmaan (31:32) ambako Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja hali kama hiyo ya washirikina. Washirikina wa zamani walikuwa wakimshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika hali za raha. Lakini wanapokumbwa na shida kama hiyo ya bahari kuchafuka, wakapatwa na hofu kubwa ya kuangamia na kughariki, hapo walikuwa hawaombi miungu au washirika wao, bali walimuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee na kuelekea Kwake.

 

Ama washirikina wa zama hizi, hawa shirki zao hazina tofauti katika hali zao za raha au za shida. Kuna wanaowaomba wafu katika makaburi daima dawamu, ni sawa iwe katika hali ya raha au ya dhiki. Pia utakuta hata maskini au fakiri akipatwa na mtihani akawa katika dhiki kubwa, anamwendea mganga, au mtabiri, au hata mchawi ili amwondolee hali yake hiyo wakati mganga mwenyewe hawezi kujiondoshea matatizo aliyonayo. Hivyo watu hawa, shirki zao ni za kudumu nyakati zote.  Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab (رحمه الله) amesema: “Washirikina wa zama zetu ni waovu zaidi katika shirki zao kuliko washirikina wa zamani kwa sababu, wa zamani walimshirikisha Allaah katika raha, lakini walitakasa (ibaada zao) wakati wa shida. Ama washirikina wa sasa, shirki zao ni za kuendelea daima wakiwa katika raha au katika shida. [Kanuni Ya Nne -Al-Qawaaid Al-Arba’]

 

[7] Maana Ya Baghi Katika Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

 

[8] Waumini Watamuona Allaah  (عزّ وجلّ)  Katika Jannah (Pepo):

 

Kumuona Allaah (عزّ وجلّ) Peponi ni katika ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah Wal Jamaa’ah ambayo baadhi ya makundi potofu hawaiamini ilhali dalili zake zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Rejea Suwrah Al-Qiyaamah (75:22-23). Na katika Sunnah ni Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ صُهَيْبٍ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فِي قَوْلِه‏:‏ ‏ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَى وَزِيَادَةٌ  قَالَ ‏"‏ إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ نَادَى مُنَادٍ إِنَّ لَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ مَوْعِدًا يُرِيدُ أَنْ يُنْجِزَكُمُوهُ قَالُوا أَلَمْ تُبَيِّضْ وُجُوهَنَا وَتُنَجِّنَا مِنَ النَّارِ وَتُدْخِلْنَا الْجَنَّةَ قَالَ فَيُكْشَفُ الْحِجَابُ ‏.‏ قَالَ فَوَاللَّهِ مَا أَعْطَاهُمُ اللَّهُ شَيْئًا أَحَبَّ إِلَيْهِمْ مِنَ النَّظَرِ إِلَيْهِ ‏

Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ

Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (huko Jannah) jazaa nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah).” [Yuwnus (10:26)]

 

“Watakapoingia Watu wa Jannah katika Jannah, wataitwa: Enyi Watu wa Jannah! Hakika nyinyi mna ahadi (kwa Allaah) na Anataka Kuitimiza. Watauliza: (Ni ahadi ipi hiyo?) Kwani Hukuzing’arisha nyuso zetu, na Hukutuokoa na moto, na Hukutuingiza Jannah?” Akasema: “Litaondoshwa pazia. (Na watamtazama Allaah) Akasema: Basi Wa-Allaahi, Hakuwahi Allaah kuwapa jambo walilolipenda zaidi kuliko hilo (kumuona Allaah).” [At-Tirmidhiy, Na riwaayah nyenginezo kama hiyo zimepokelewa na Imaam Muslim, Ibn Maajah]

 

[9] Kila Nafsi Itatiwa Mtihanini:

 

Kila nafsi itatahiniwa kwa kuhesabiwa amali alizotenda mtu duniani; ikiwa ni za kheri alipwe kheri, na ikiwa ni uovu alipwe maovu.  Amali hizo ambazo zimerekodiwa katika Sahifa ya kila mtu, hakuna hata chembe ya atomu itakayokosekana kurekodiwa ndani yake. Rejea Az-Zalzalah (99:6-8), Fus-swilat (41:20-22), Yaasiyn (36:12) (36:65),  An-Nuwr (24:24), Al-Israa (17:13-14), Al-Infitwaar (82:10-12), Qaaf (50:18), Ghaafir (40:16-17), na Al-Anbiyaa (21:47).

 

[10] Mawlaa "مَوْلَى":  Rejea Faharasa Ya Majina Mazuri Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Na Sifa Zake.

 

[11] Washirikina Waliamini Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah Lakini Walikanusha Tawhiyd Al-Uluwhiyyah:

 

Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab (رحمه الله) ametaja katika Al-Qawaaid Al-Arba’ kwamba Aayah hii na nyenginezo; Rejea Al-‘Ankabuwt (29:61) kwenye faida ziyada. Rejea pia (29:63), Luqmaan (31:25), Az-Zumar (39:38), na Az-Zukhruf (43:9) (43:87), ni dalili kuwa washirikina waliamini Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah (Kumpwekesha Allaah katika Uola Wake) kwamba Yeye ni Rabb Aliyewaumba, na Aliyeumba mbingu na ardhi, na Anayewaruzuku, na Anayewaendeshea mambo yao yote. Lakini ushirikina wao umekuja katika kutokumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) katika Tawhiyd ya Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah katika ibaada) walipowaabudu masanamu kwa kuwaelekezea ibaada zao.

 

[12] Qur-aan Inashuhudia Na Inadhibiti Vitabu Vya Nyuma Kutoka Mbinguni:

 

Rejea Al-Maaidah (5:48).

  

[13] Changamoto Kwa Makafiri Walete Mfano Wa Qur-aan Lakini Kamwe Hakuna Awezaye!:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anatoa changamoto kama hii na Anatoa changamoto na vitisho kwa kiumbe yoyote yule kati ya majini na wanaadam kwamba ikiwa hawamwamini, basi walete mfano wa Qur-aan, lakini hakuna awezaye! Rejea Al-Israa (17:88), Al-Baqarah (2:23-24), Huwd (11:13-14), na At-Twuwr (52:33-34). Watu walijaribu, lakini walishindwa! Mmoja wao ni Musaylamah Al-kadh-dhaab (mrongo) aliyedai kuwa amepewa Unabii baada ya Nabiy Muhammad  (صلى الله عليه وآله وسلم). Rejea Al-An’aam (6:93) kwenye Hadiyth inayowataja waongo hao. 

 

[14] Ada Ya Makafiri Kuuliza Lini Adhabu Itawafikia Au Lini Qiyaamah Kitatokea:

 

Aayah hii hadi Aayah (10:54), Allaah (سبحانه وتعالى) Anawahakikishia makafiri kwamba Atawateremshia adhabu na Atakisimamisha Qiyaamah, na hapo watataka kuamini, lakini imaan zao hazitawafaa lolote, na majuto yatakuwa ni yao kwa kutokuamini!       Rejea: Al-Hajj (22:47), Al-Anbiyaa (21:38-40), An-Naml (27:71-72), Saba-a (34:29-30), Yaasiyn (36:48-54), na Al-Mulk (67:25-28).

 

[15] Qur-aan Ni Shifaa (Poza, Tiba), Mawaidha, Mwongozo Na Rehma:

 

Rejea Al-Israa (17:82) na Fusw-Swilat (41:44) kwenye uchambuzi na faida kadhaa.

 

[16] Fadhila Za Allaah Na Rehma Yake:

 

Fadhila ya Allaah ni Qur-aan ambayo ni neema kubwa kabisa. Rehma Yake ni Dini ya haki, mwongozo na imaan, kumwabudu Allaah kwa mapenzi, na kumtambua (kwa Majina na Sifa Zake). Basi hayo wayafurahie, kwa sababu hayo ni kheri (na bora) kuliko wanayoyakusanya katika mapambo, mafao na anasa za dunia. [Imaam As-Sa’diy]

 

[17] Hakuna Kinachofichika Kwa Allaah (سبحانه وتعالى); Kiwe Cha Dhahiri Wala Cha Siri, Kikubwa Wala Kidogo Vipi:

 

Rejea Al-An’aam (6:59) kwenye faida na maelezo bayana. Na rejea pia Ghaafir (40:19) kwenye maelezo na rejea mbalimbali. Na pia Luqmaan (31:16).

 

[18] Awliyaa (Vipenzi) Wa Allaah (عزّ وجلّ):

 

Aayah tukufu imetaja sifa mbili kwa Muislamu zinazomfanya kuwa yeye ni Kipenzi cha Allaah. Sifa hizo ni imaan na taqwa. Na zote mbili zinapatikana moyoni.  Rejea Al-Baqarah (2:2) kupata maana ya taqwa. Na Vipenzi wa Allaah (عزّ وجلّ) ni kuanzia Manabii Wake wote, Swahaba (رضي الله عنهم), Shuhadaa, na Swalihina wote wengineo ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaridhia. Hadiyth nyingi zimetaja Waumini wenye kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى). Hadiyth hizo zinataja amali zao watendazo, sifa zao na fadhila zao. Miongoni mwazo ni:

 

1-Wenye Kutenda Amali Zaidi Ya Alizofaridhisha Allaah (سبحانه وتعالى):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  إِنَّ اللَّهَ قَال:َ مَنْ عَادَى لِي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِي بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ،  وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ، فَإِذَا أَحْبَبْتُهُ كُنْتُ سَمْعَهُ الَّذِي يَسْمَعُ بِهِ، وَبَصَرَهُ الَّذِي يُبْصِرُ بِهِ، وَيَدَهُ الَّتِي يَبْطِشُ بِهَا، وَرِجْلَهُ الَّتِي يَمْشِي بِهَا، وَإِنْ سَأَلَنِي لَأُعْطِيَنَّهُ، وَلَئِنْ اسْتَعَاذَنِي لَأُعِيذَنَّهُ   البخاري

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema: Atakayemfanyia uadui Kipenzi Changu, basi Ninatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hanikaribii na kitu chochote Ninachokipenda zaidi kama amali Nilizomfaridhishia. Na haachi Mja Wangu kuwa anajikurubisha Kwangu kwa amali za Sunnah mpaka Napata Kumpenda. Ninapompenda, basi Mimi Huwa masikio yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayonyoshea, na miguu yake anayotembelea nayo. Na kama ataniomba, kwa hakika Nitampa, na kama ataniomba kinga, kwa hakika Nitamlinda.” [Al-Bukhaariy]

 

Pia,

 

2-Wenye Kushikamana Na Qur-aan Kwa Kuisoma, Kuihifadhi, Na Kufuata Maamrisho Yake:

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ لِلَّهِ أَهْلِينَ مِنْ النَّاسِ)) قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ مَنْ هُمْ قَالَ: ((هُمْ أَهْلُ الْقُرْآنِ أَهْلُ اللَّهِ وَخَاصَّتُهُ)) أحمد و إبن ماجه

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Anao watu wake maalum kati ya wanaadam.” Wakamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah ni nani hao? Akasema: “Hao ni watu wa Qur-aan (wenye kuifanyia kazi), hao ndio Watu wa Allaah na Wateule Wake.” [Ahmad, Ibn Maajah]

 

[19] Kumsingizia Allaah Kuwa Ana Mwana:

 

Rejea Al-Maaidah (5:17), (72-76), (116-118), Maryam (19:88), na At-Tawbah (9:30-31).

 

[20] Nuwh Na Kizazi Kilobakia, Naye Ni Rasuli Wa Kwanza Ardhini, Na Ni Baba Wa Wanaadam Baada Ya Aadam: Rejea Asw-Swaffaat (37:77).

 

[21] Maana Ya Baghi Katika Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

 

[22] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Hakuwa Na Shaka Kamwe Wala Hakukadhibisha Aayaat Za Allaah (سبحانه وتعالى):  

 

Aayah Hii Na Ifuatayo Yuwnus (10:94-95), Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) hakutilia shaka lolote Aliloteremshiwa na Allaah (سبحانه وتعالى), bali yeye alikuwa ni mwenye yaqini kabisa. Hili linathibitishwa kwa Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):  

 

 آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ  

“Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia).” [Al-Baqarah (2:285)]

 

Qataadah, Ibn ‘Abbaas, Sa’iyd bin Jubayr, Hasan Al-Baswiry wamesema kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakutia shaka wala hakuuliza lolote (katika Wahy). [Tafsiyr Ibn Kathiyr] 

 

Kauli Yake hiyo Allaah (سبحانه وتعالى) kumwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

فَإِن كُنتَ فِي شَكٍّ

 

“Ukiwa una shaka…”

 

Ni katika njia Anazozitumia Allaah (سبحانه وتعالى) kuelekeza maswali kama hayo kwa makafiri kama vile Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):  

قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ﴿٨١﴾

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Kama ingelikuwa Ar-Rahmaan Ana mwana (kama mnavyodai), basi mimi ningekuwa wa mwanzo katika waja (Wake).” [Az-Zukhfur (43:81)]

 

Ufafanuzi wa:

فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ

“Basi mimi ningekuwa wa mwanzo katika waja (Wake):

 

Ina maana: Ningekuwa wa mwanzo wa wanaokanusha madai yenu, na wa mwanzo kuamini kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Hana mwana. Kwa sababu inajulikana wazi kuwa washirikina wa Makkah walimzulia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa Malaika ni watoto Wake wa kike. Na Mayahudi wakamzulia kuwa ‘Uzayr ni mwana wa Allaah. Na Manaswara wakamzulia kuwa Nabiy ‘Iysaa ni mwana wa Allaah. Basi ndio maana hapa Allaah (سبحانه وتعالى) Anamwambia Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم): “Sema…..” lakini swali hilo hakika ni kuligeuza kwa Manaswara. Na kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anathibitisha kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ﴿٩٤﴾

“Kwa yakini imekujia haki kutoka kwa Rabb wako, basi usijekuwa miongoni mwa wanaoshuku.” [Yuwnus (10:94)]

 

Na Aayah hizi mbili na nyenginezo kama hizi makafiri huzichukulia hoja kutaka kuipotosha Qur-aan na kutaka kuitia upogo Risala ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametilia shaka Wahy alioteremshiwa, na kwamba alikadhibisha Aayah Za Allaah (سبحانه وتعالى) na madai yao mengineyo. Lakini uhakika ni kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anazielekezea kwa makafiri. ‘Ulamaa wameelezea mengi na kufafanua kwa upana Aayah kama hizi.

 

[23] Kaumu Ya Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) Hawakuteremshiwa Adhabu:

 

Imaan haikuwafaa watu wa mji wowote walioamini walipoishuhudia adhabu isipokuwa watu wa mji wa Yuwnus mwana wa Mattaa. Kwani wao walipohakikisha kwamba adhabu ni yenye kuwashukia, walirejea kwa Allaah kwa kutubia kidhati, na ulipofunuka ukweli wa tawbah yao, Allaah Aliwaondolea adhabu ya hizaya baada ya kuwa karibu na wao, na Akawaacha ulimwenguni wakisterehe mpaka muda wao wa kuishi kukoma. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

 

Share