024 - An-Nuwr
النُّور
024-An-Nuwr
024-An-Nuwr: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
سُورَةٌ أَنزَلْنَاهَا وَفَرَضْنَاهَا وَأَنزَلْنَا فِيهَا آيَاٍ بَيِّنَاتٍ لَّعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١﴾
1. Suwrah Tumeiteremsha, na Tukaifaradhisha (hukmu zake), na Tukateremsha humo Aayaat bayana ili mpate kukumbuka.
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾
2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamme mpigeni kila mmoja katika wawili hao mijeledi mia. Na wala isiwashikeni huruma kwa ajili yao katika Hukmu ya Allaah mkiwa nyinyi mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na washuhudie adhabu yao kundi la Waumini.
الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ ۚ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾
3. Mwanamme mzinifu hafungi nikaah isipokuwa na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina, na mwanamke mzinifu haolewi isipokuwa na mwanamme mzinifu au mshirikina. Na imeharamishwa hivyo kwa Waumini.[1]
وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٤﴾
4. Na wale wanaowasingizia wanawake watwaharifu[2] kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni mijeledi themanini. Na wala msipokee ushahidi wao abadani. Na hao ndio mafasiki.
إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥﴾
5. Isipokuwa wale waliotubu baada ya hayo na wakanyoosha sawa matendo yao, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.
وَالَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوَاجَهُمْ وَلَمْ يَكُن لَّهُمْ شُهَدَاءُ إِلَّا أَنفُسُهُمْ فَشَهَادَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٦﴾
6. Na wale wanaowasingizia wake zao na hawana mashahidi isipokuwa nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa ni kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Allaah kwamba yeye ni miongoni mwa wakweli.[3]
وَالْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَتَ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كَانَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٧﴾
7. Na (kiapo) cha tano kwamba Laana ya Allaah iwe juu yake, akiwa ni miongoni mwa waongo.
وَيَدْرَأُ عَنْهَا الْعَذَابَ أَن تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٨﴾
8. Na itamwondokea (mke) adhabu atakapotoa ushahidi mara nne kwa kiapo cha Allaah kwamba yeye (mumewe) ni miongoni mwa waongo.
وَالْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ اللَّـهِ عَلَيْهَا إِن كَانَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٩﴾
9. Na (kiapo) cha tano kwamba Ghadhabu ya Allaah iwe juu yake akiwa (mumewe) ni miongoni mwa wakweli.
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ حَكِيمٌ ﴿١٠﴾
10. Na lau kama si Fadhila ya Allaah juu yenu na Rehma Yake, na kwamba Allaah Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Hikmah wa yote (basi Angeliwaadhibuni bila kukawia).
إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾
11. Hakika wale walioleta singizio la kashfa (kumzulia Mama wa Waumini ‘Aaishah رضي الله عنها), ni kundi miongoni mwenu. Msilichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata yale aliyochuma katika dhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kuu.[4]
لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾
12. Kwa nini mlipoisikia (tetesi la kashfa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?
لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾
13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na kwa vile hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾
14. Na lau si Fadhila ya Allaah juu yenu na Rehma Yake duniani na Aakhirah, ingekuguseni adhabu kuu kwa yale mliyojishughulisha nayo kuyaropoka.
إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾
15. Mlipolipokea (tetesi la kashfa) kwa ndimi zenu, na mkasema kwa midomo yenu, yale ambayo hamkuwa na ilimu nayo. Na mnalidhania ni jambo jepesi, ilhali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno.
وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾
16. Na kwa nini mlipolisikia (tetesi la kashfa) msiseme: Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! (Utakasifu ni Wako). Huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!
يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾
17. Allaah Anakuwaidhini msirudie abadani mfano wa haya, mkiwa ni Waumini wa kweli.
وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٨﴾
18. Na Allaah Anakubainishieni Aayaat (Hukumu za Sharia, Mawaidha). Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.
إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾
19. Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini, watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui.
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾
20. Na lau si Fadhila ya Allaah juu yenu na Rehma Yake, na kwamba Allaah Ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu (basi Angeliwaadhibuni bila kukawia).
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ وَمَن يَتَّبِعْ خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ فَإِنَّهُ يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۚ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَىٰ مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُزَكِّي مَن يَشَاءُ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢١﴾
21. Enyi walioamini! Msifuate nyayo za shaytwaan. Na yeyote atakayefuata nyayo za shaytwaan, basi hakika yeye anaamrisha machafu na munkari.[5] Na lau si Fadhila ya Allaah juu yenu na Rehma Yake, basi asingelitakasika miongoni mwenu hata mmoja abadani, lakini Allaah Anamtakasa Amtakaye. Na Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.
وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾
22. Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika Njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[6]
إِنَّ الَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ الْغَافِلَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ لُعِنُوا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾
23. Hakika wale wanaowasingizia machafu wanawake watwaharifu, walio mbali na hayo, Waumini, wamelaaniwa duniani na Aakhirah na watapata adhabu kuu.[7]
يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾
24. Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.[8]
يَوْمَئِذٍ يُوَفِّيهِمُ اللَّـهُ دِينَهُمُ الْحَقَّ وَيَعْلَمُونَ أَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ الْمُبِينُ ﴿٢٥﴾
25. Siku hiyo Allaah Atawalipa kikamilifu malipo yao ya haki, na watajua kwamba Allaah Ndiye wa Haki, Mwenye Kubainisha.
الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ ۖ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ ۚ أُولَـٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ ۖ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٢٦﴾
26. Kauli ovu inaendana na watu waovu, na watu waovu wanaendana na kauli ovu. Na kauli njema inaendana na watu wema, na watu wema wanaendana na kauli njema.[9] Hao wametakaswa na tuhuma za wanayoyasema, watapata Maghfirah na riziki karimu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾
27. Enyi walioamini! Msiingie nyumba zisizokuwa nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee Salaam (‘alaykum) wenyewe. Hivyo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.
فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ ۖ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ۖ هُوَ أَزْكَىٰ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٢٨﴾
28. Na msipokuta humo yeyote, basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rejeeni! Basi rejeeni. Huo ni utakaso zaidi kwenu. Na Allaah Ni Mjuzi wa myatendayo.
لَّيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ مَسْكُونَةٍ فِيهَا مَتَاعٌ لَّكُمْ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا تَكْتُمُونَ ﴿٢٩﴾
29. Hakuna kosa kuingia majumba yasiyokaliwa ambako humo mna manufaa yenu. Na Allaah Anajua yale yote mnayoyadhihirisha na yale yote mnayoyaficha.
قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾
30. Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale wayatendayo.
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾
31. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao[10] isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume[11], au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao (vikuku na kadhaalika). Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu.
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٣٢﴾
32. Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha katika Fadhila Zake. Na Allaah Ni Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote.
وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّىٰ يُغْنِيَهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَالَّذِينَ يَبْتَغُونَ الْكِتَابَ مِمَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ فَكَاتِبُوهُمْ إِنْ عَلِمْتُمْ فِيهِمْ خَيْرًا ۖوَآتُوهُم مِّن مَّالِ اللَّـهِ الَّذِي آتَاكُمْ ۚ وَلَا تُكْرِهُوا فَتَيَاتِكُمْ عَلَى الْبِغَاءِ إِنْ أَرَدْنَ تَحَصُّنًا لِّتَبْتَغُوا عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَمَن يُكْرِههُّنَّ فَإِنَّ اللَّـهَ مِن بَعْدِ إِكْرَاهِهِنَّ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٣﴾
33. Na wajizuie (yaliyoharamishwa) wale ambao hawapati uwezo wa ndoa mpaka Allaah Awatajirishe kwa Fadhila Zake. Na wale wanaotaka kuandikiwa kuachiwa huru katika wale ambao imemiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkijua wema kwao. Na wapeni katika Mali ya Allaah Aliyokupeni. Na wala msiwalazimishe vijakazi wenu kufanya ukahaba kama wakitaka kujisitiri, ili mtafute mafao ya uhai wa dunia. Na yeyote yule atakayewalazimisha, basi hakika Allaah, baada ya kulazimishwa kwao huko, ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[12]
وَلَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَمَثَلًا مِّنَ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُمْ وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٣٤﴾
34. Na kwa yakini Tumekuteremshieni Aayaat zinazobainisha wazi, na mifano kutoka kwa wale waliopita kabla yenu, na mawaidha kwa wenye taqwa.
اللَّـهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ ۖ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ ۖ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ ۚ نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ ۗ يَهْدِي اللَّـهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣٥﴾
35. Allaah Ni Nuru ya mbingu na ardhi. Mfano wa Nuru Yake ni kama shubaka, ndani yake mna taa yenye mwanga mkali. Taa hiyo yenye mwanga mkali iko katika (tungi la) gilasi. Gilasi hiyo ni kama kwamba nyota inayong’aa na kumeremeta, inawashwa kutokana na mti wa baraka wa zaytuni, hauko Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung’aa japokuwa moto haujayagusa, Nuru juu ya Nuru. Allaah Anamwongoza kwa Nuru Yake Amtakaye. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu. Na Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi.[13]
فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّـهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ﴿٣٦﴾
36. Katika nyumba ambazo Allaah Ameidhinisha litukuzwe na litajwe humo Jina Lake, wanamsabihi humo asubuhi na jioni.
رِجَالٌ لَّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ ۙ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ ﴿٣٧﴾
37. Wanaume ambao haiwashughulishi tijara wala uuzaji na kumdhukuru Allaah na kusimamisha Swalaah, na kutoa Zakaah wanakhofu Siku zitakapopinduka humo nyoyo na macho.
لِيَجْزِيَهُمُ اللَّـهُ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٨﴾
38. Ili Allaah Awalipe mazuri zaidi kutokana na yale waliyoyatenda, na Awazidishie katika Fadhila Zake. Na Allaah Humruzuku Amtakaye bila ya hesabu.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا وَوَجَدَ اللَّـهَ عِندَهُ فَوَفَّاهُ حِسَابَهُ ۗ وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٣٩﴾
39. Na wale waliokufuru, amali zao ni kama sarabi jangwani. Mwenye kiu hudhania kuwa ni maji. Hata anapoyafikia hayakuti kitu chochote, na anamkuta Allaah mbele Yake, Naye Amlipe kikamilifu hesabu yake. Na Allaah Ni Mwepesi wa Kuhesabu.[14]
أَوْ كَظُلُمَاتٍ فِي بَحْرٍ لُّجِّيٍّ يَغْشَاهُ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ سَحَابٌ ۚ ظُلُمَاتٌ بَعْضُهَا فَوْقَ بَعْضٍ إِذَا أَخْرَجَ يَدَهُ لَمْ يَكَدْ يَرَاهَا ۗ وَمَن لَّمْ يَجْعَلِ اللَّـهُ لَهُ نُورًا فَمَا لَهُ مِن نُّورٍ ﴿٤٠﴾
40. Au ni kama viza katika bahari ya kina kirefu, imefunikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake kuna mawingu. (Tabaka za) Viza juu yake viza. Anapoutoa mkono wake, anakaribia asiuone. Na ambaye Allaah Hakumjaalia Nuru, basi hawi na Nuru.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ ۖ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٤١﴾
41. Je, huoni kwamba wanamsabihi Allaah walioko mbinguni na ardhini[15], na (pia) ndege wakiwa wamekunjua mbawa zao. Kila mmoja (Allaah) Amekwishajua Swalaah yake na tasbihi yake. Na Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayafanyao.
وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿٤٢﴾
42. Na Ni wa Allaah Pekee ufalme wa mbingu na ardhi. Na kwa Allaah Pekee ndio mahali pa kuishia.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُزْجِي سَحَابًا ثُمَّ يُؤَلِّفُ بَيْنَهُ ثُمَّ يَجْعَلُهُ رُكَامًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلَالِهِ وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مِن جِبَالٍ فِيهَا مِن بَرَدٍ فَيُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ وَيَصْرِفُهُ عَن مَّن يَشَاءُ ۖ يَكَادُ سَنَا بَرْقِهِ يَذْهَبُ بِالْأَبْصَارِ ﴿٤٣﴾
43. Je, huoni kwamba Allaah Anasukuma mawingu, kisha Anayaambatisha baina yake, kisha Anayafanya matabaka ya mirundi? Basi utaona matone ya mvua yanatoka katikati yake. Na Anateremsha kutoka mbinguni katika milima ya mawingu mvua ya mawe, Akamsibu nayo Amtakaye, na Akamuepushia Amtakaye. Hukaribia mwako wa umeme wake kupofua macho.
يُقَلِّبُ اللَّـهُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّأُولِي الْأَبْصَارِ ﴿٤٤﴾
44. Allaah Hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo kuna zingatio kwa wenye kuona kwa umaizi.
وَاللَّـهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِّن مَّاءٍ ۖ فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ ۚ يَخْلُقُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤٥﴾
45. Na Allaah Ameumba kila kiumbe kinachotembea kutokana na maji. Basi miongoni mwao wako wanaotembea juu ya matumbo yao, na miongoni mwao wanaotembea kwa miguu miwili, na miongoni mwao wanaotembea juu ya minne. Allaah Anaumba Atakavyo. Hakika Allaah juu ya kila kitu Ni Muweza.[16]
لَّقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ ۚ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤٦﴾
46. Kwa yakini Tumeteremsha Aayaat bainifu, na Allaah Anamwongoza Amtakaye kuelekea Njia Iliyonyooka.
وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na (wanafiki) wanasema: Tumemwamini Allaah na Rasuli, na Tumetii. Kisha hugeuka kundi miongoni mwao baada ya hayo. Na wala hao si wenye kuamini.
وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahukumu baina yao, mara hapo kundi miongoni mwao wanakengeuka.
وَإِن يَكُن لَّهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ ﴿٤٩﴾
49. Na inapokuwa haki ni yao, wanamjia (Rasuli) wakitii.
أَفِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَن يَحِيفَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ ۚ بَلْ أُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٥٠﴾
50. Je, mna maradhi katika nyoyo zao[17], au wametia shaka, au wanakhofu kwamba Allaah na Rasuli Wake watawadhulumu katika kuwahukumu? Bali hao ndio madhalimu.
إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾
51. Hakika kauli ya Waumini (wa kweli) wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahukumu baina yao ni kusema: Tumesikia na Tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّـهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٥٢﴾
52. Na yeyote yule atakayemtii Allaah na Rasuli Wake, na akamkhofu Allaah na akamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِنْ أَمَرْتَهُمْ لَيَخْرُجُنَّ ۖ قُل لَّا تُقْسِمُوا ۖ طَاعَةٌ مَّعْرُوفَةٌ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na wakaapa kwa Allaah, viapo vyao thabiti vya nguvu, kwamba: Ukiwaamrisha, bila shaka watatoka. Sema: Msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo.
قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾
54. Sema: Mtiini Allaah na mtiini Rasuli. Mkigeukilia mbali, basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa tu, nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na mkimtii mtaongoka, na hapana juu ya Rasuli isipokuwa ubalighisho bayana.
وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾
55. Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya warithi katika ardhi kama Alivyowafanya warithi wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao, wawe wananiabudu Mimi wasinishirikishe na chochote. Na na yeyote atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki.[18]
وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾
56. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Rasuli ili mpate kurehemewa.
لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ ۖ وَلَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٥٧﴾
57. Usidhanie kabisa wale waliokufuru kuwa ni wenye kushinda katika ardhi, na makazi yao ni moto. Na ubaya ulioje kwa hakika wa mahali pa kuishia!
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ ۚ مِّن قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُم مِّنَ الظَّهِيرَةِ وَمِن بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاءِ ۚ ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَّكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلَا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ ۚ طَوَّافُونَ عَلَيْكُم بَعْضُكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٨﴾
58. Enyi walioamini! Wakuombeni idhini wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume, na wale wasiofikia umri wa kubaleghe miongoni mwenu mara tatu: kabla ya Swalaah ya Alfajiri na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri (kulala) na baada ya Swalaah ya ‘Ishaa. Nyakati tatu za faragha kwenu. Hakuna ubaya kwenu na wala kwao baada ya nyakati hizo, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Allaah Anakubainishieni Aayaat na (Ishara, Hukmu za Sharia, Dalili). Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.[19]
وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٩﴾
59. Na watoto miongoni mwenu watakapofikia baleghe, basi waombe idhini (wakati wote) kama walivyoomba idhini wale wa kabla yao. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat na (Ishara, Hukmu za Sharia, Dalili) Zake. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.
وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ ۖ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٦٠﴾
60. Na wanawake wazee waliokatika hedhi ambao hawataraji kuolewa, hakuna ubaya juu yao kupunguza baadhi ya nguo zao bila ya kudhihirisha mapambo yao. Na kama wakijiwekea staha kujisitiri ni kheri kwao. Na Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.
لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ ۚ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا ۚ فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾
61. Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa, na wala nyinyi wenyewe kama mtakula majumbani mwenu, au majumbani mwa baba zenu, au majumbani mwa mama zenu, au majumbani mwa kaka zenu, au majumbani mwa dada zenu, au majumbani mwa ‘ammi zenu, au majumbani mwa shangazi zenu, au majumbani mwa wajomba zenu, au majumbani mwa makhalati zenu au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Hakuna ubaya kama mkila pamoja au mbali mbali. Mtakapoingia majumbani toleaneni Salaam (‘alaykum) maamkizi kutoka kwa Allaah, yenye Baraka, mazuri. Hivyo ndivyo Anavyokubainishieni Allaah Aayaat na (Ishara, Hukmu za Sharia, Dalili) ili mpate kutia akilini.[20]
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَإِذَا كَانُوا مَعَهُ عَلَىٰ أَمْرٍ جَامِعٍ لَّمْ يَذْهَبُوا حَتَّىٰ يَسْتَأْذِنُوهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۚ فَإِذَا اسْتَأْذَنُوكَ لِبَعْضِ شَأْنِهِمْ فَأْذَن لِّمَن شِئْتَ مِنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمُ اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٢﴾
62. Hakika Waumini wa kweli ni wale waliomwamini Allaah na Rasuli Wake. Na wanapokuwa pamoja naye (Rasuli) katika jambo la umoja hawaondoki mpaka wamuombe idhini. Hakika wale wanaokuomba idhini, hao ni wale wanaomwamini (kweli) Allaah na Rasuli Wake. Basi wanapokuomba idhini (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili ya baadhi ya shughuli zao, basi mpe idhini umtakaye miongoni mwao, na waombee Maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.
لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا ۚ قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا ۚ فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾
63. Msifanye wito wa Rasuli baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Kwa yakini Allaah Anawajua miongoni mwenu wale wanaoondoka kwa kunyemelea. Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.
أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ قَدْ يَعْلَمُ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ وَيَوْمَ يُرْجَعُونَ إِلَيْهِ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا ۗ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٦٤﴾
64. Tanabahi! Hakika ni vya Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na ardhi. Kwa yakini (Allaah) Anajua mliyo nayo. Na Siku watakayorejeshwa Kwake, Atawajulisha yale yote waliyoyatenda. Na Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi.
[1] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/ Hukmu Ya Zinaa Na
Bonyeza kiungo kifuatacho:
[2] Kuwasingizia Machafu Wanawake Watwaharifu Ni Miongoni Mwa Mambo Saba Yanayoangamiza:
Rejea Aayah (23) ya Suwrah hii An-Nuwr.
[3] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/Hukmu Ya Zinaa Na Kuweko Mashahidi Na
Bonyeza kiungo kifuatacho:
[4] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/Kutakaswa Kwa Mama Wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) Kutokana Na Singizio La Kashfa Na Radd Kwa Wanaoendelea Kumzulia
Bonyeza kiungo kifuatacho ambako kuna uthibitisho wa Hadiyth inayoelezea tukio hilo kwa maelezo marefu na bayana kabisa. Na Aayah zinazofuatia An-Nuwr (24:23-26) pia zinahusiana na tukio hili.
024-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nuwr Aayah 11-22: إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ
Aayah hii ya (11) hadi (22), ni Aayah zinazomtakasa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutokana na singizio la kashfa juu yake. Singizio ambalo lilisababisha rabsha, huzuni na dhiki katika nyumba ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na jamii nzima katika mji wa Madiynah. Tetesi la singizio hilo lilimuumiza mno Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na ahli wake na liliwatia dhiki, huzuni na ukosaji wa utulivu. Ikawa ni kipindi kigumu mno kuvumilia mpaka zilipoteremka Aayah hizi kumtakasa ‘Aaishah Mama wa Waumini (رضي الله عنها).
Na hii ni radd kwa wanaojinasibisha na Uislamu kuendelea kumzulia mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumtusi hadharani pamoja na Swahaba wengineo wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Aayah hizi ni ushahidi, hoja, burhani na dalili za waziwazi kabisa. Aayah ambazo zimesomwa tokea hapo zilipoteremka, na zinasomwa hadi leo, na zitaendelea kusomwa hadi Siku ya Qiyaamah.
[5] Shaytwaan Anachochea Na Kuamuru Machafu Na Ni Adui Bayana:
Rejea Suwrah Ibraahiym (14:22) kwenye rejea nyenginezo za kutahadharishwa na shaytwaan. Rejea pia Al-Israa (17:64).
[6] Wenye Fadhila: Amekusudiwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq:
Aayah hii iliteremka kwa ajili ya Abubakar Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه), wakati alipoapa kuwa hatomsaidia Mistwah Bin Uthaathah kwa lolote lile, baada ya kuongea maneno mabaya ya kumtuhumu ‘Aaishah (رضي الله عنها). Baada ya Allaah kuteremsha Aayah za kumtakasa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها), na nafsi zenye imaan zikatulia na kupata ahueni, na Allaah (سبحانه وتعالى) Akapokea tawbah za wote walioyazungumza hayo katika Waumini, na wakasimamishiwa hadd waliosimamishiwa, ndio Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Fadhila Zake Akamuingiza upole na huruma Abubakar (رضي الله عنه) kwa ndugu yake, ambae ni Mistwah Bin Uthaathah, kwani yeye ni mtoto wa Mama mdogo wa Abubakar (رضي الله عنه), na alikuwa maskini asiyekuwa na mali isipokuwa ile anayopewa na Abubakar (رضي الله عنه). Na alikuwa ni katika wale waliohajiri katika njia ya Allaah. Hakika aliharakisha kufanya tawbah ambayo Allaah Aliikubalia kutokana na kosa hilo.
Abubakar (رضي الله عنه) alikuwa ni maarufu kwa kutenda wema, mwenye fadhila kubwa, na mwenye kujitolea katika kuwasaidia ndugu na wasiokuwa ndugu. Baada ya kuteremka Aayah hii mpaka Kauli Yake Allaah:
أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾
“Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.”
Yaani: Hakika malipo ni kwa mujibu wa matendo, kama utakavyoweza kumsamehe aliyekukosea, ndio na Sisi Tutakusamehe wewe, na kama utakavyoachilia mbali mabaya uliyofanyiwa na Sisi pia Tutaachilia mbali mabaya yako. Baada ya kuyasikia maneno hayo, Abubakar (رضي الله عنه) akasema: “Bali tunahitajia (msamaha). Naapa kwa Allaah! Hakika sisi tunapenda ee Rabb wetu Utughufurie.” Kisha akarejea kumfanyia Mistwahi yale yote aliyokuwa akimfanyia yakiwemo kumpatia matumizi, na akasema: “Naapa kwa Allaah! Sitoacha kumsaidia tena!” Haya maneno yanakuwa kama majibu ya alichokisema awali: “Naapa kwa Allaah sitomsaidia kwa lolote lile,” Kwa sababu hii, ndio maana Abubakar (رضي الله عنه) amekuwa ni mkweli msadikishaji. Allaah Amridhie yeye pamoja na bint yake. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
[7] Kuwasingizia Machafu Wanawake Watwaharifu Ni Miongoni Mwa Mambo Saba Yanayoangamiza:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟ قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!” Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, sihri (uchawi), kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
[8] Viungo Vya Mwili Vitashuhudia Matendo Ya Binaadamu:
Rejea Yaasiyn (36:65), Fusw-swilat: (41:20-22), Al-Israa (17:13-14).
[9] Kauli Ovu Zinaendana Na Watu Waovu Kauli Njema Zinaendana Na Watu Wema:
Yaani: Kila mtu muovu katika wanaume na wanawake, ni lazima maneno yake na matendo yake yawe sawa na uovu wake ulivyo. Ni hulka inayoendana naye, inayonasibiana naye na inayofanana naye. Na kila mtu mwema katika wanaume na wanawake, ni lazima maneno yake na matendo yake yawe sawa na wema wake ulivyo. Ni hulka inayoendana naye, inayonasibiana naye na inayofanana naye.
Maneno haya ni jumuishi yaliyofunga duara, hayatoi mpenyo wa kutoka chochote ndani yake. Na kati ya vipengele muhimu zaidi vilivyo ndani ya maneno haya ni kwamba Manabii hasa wale Ulul-‘azmi (waliofungamana na ahadi ya nguvu), wakiongozwa na bwana wao Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ndiye mbora wa wema katika viumbe, hanasibiani nao isipokuwa kila mwanamke aliye mwema. Hivyo basi, kumzushia uongo ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa jambo hili, ni kumtia dosari Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na ndio makusudio ya uzushi huu waliyoyakusudia wanafiki. Na vile tu bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) amekuwa mke wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), inajulikana moja kwa moja kuwa hawezi kuwa isipokuwa ni mwanamke mwema aliyetakasika na kuwa mbali kabisa na jambo hili baya.
Kwa nini asiwe hivyo? Kwani kuna asiyemjua?! Mkweli katika wanawake, mbora wao, mwenye ilimu zaidi kuliko wao, na mwema wao. Isitoshe, ni kipenzi cha Rasuli wa Rabb wa walimwengu ambaye haujateremshwa Wahyi kwake akiwa kitandani mwa mke kati ya wakeze, isipokuwa pale alipokuwa kitandani mwa ‘Aaishah tu, si kwa mke mwingine yeyote.
Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaweka wazi jambo hilo, kwa namna inayomfunga kabisa mdomo mwenye lengo la kuchafua, wala kuacha nafasi yoyote kwa shaka na shubha ndipo Anasema (سبحانه وتعالى):
أُولَـٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ ۖ
“Hao wametakaswa na tuhuma za wanayoyasema.”
Hao wanaoashiriwa hapa ni ‘Aaishah (رضي الله عنها) pamoja na wanawake wengine ambao wako mbali na kufanya uchafu.
لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٢٦﴾
“Watapata Maghfirah na riziki karimu.”
Ni maghfirah yanayozamisha madhambi, na rizki watayoipata Peponi itokayo kwa Rabb Mkarimu. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[10] Hijaab Na Ahkaam Zake
[11] Iliowamiliki Mikono Yao Ya Kulia: Rejea An-Nisaa (4:3).
[13] Allaah Ni Nuru Ya Mbingu Na Ardhi:
اللَّهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ
“Allaah Ni Nuru ya mbingu na ardhi.”
Ni Nuru ya kihisia (inayoonekana) na Nuru ya kidhahania (isiyoonekana), na hilo ni kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Dhati Yake Ni ni Nuru, na Stara Yake ni Nuru.
Kupitia Nuru hiyo, ndio ‘Arsh ikapata Nuru, Kursiy ikapata Nuru, jua, mwezi, na Jannah (Pepo) pia. Vile vile, Nuru ya kidhahania inarudi kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kwa maana kwamba, Kitabu Chake ni Nuru, Sharia Zake ni Nuru, imaan na maarifa katika nyoyo za Manabii na Waja Wake Waumini pia Nuru. Kama si Nuru ya Allaah, basi giza juu ya giza lingepandana na kubebana, kwa sababu hii ndio utakuta kila panapokosekana Nuru panakuwa na giza.
مَثَلُ نُورِهِ
“Mfano wa Nuru Yake.”
Ambayo Huwaongoza kwayo watu kuifuata, ni Nuru ya imaan na Qur-aan katika nyoyo za Waumini.
كَمِشْكَاةٍ
“Ni kama shubaka.”
Tundu liliopo ukutani (kwa ajili ya kuwekea taa).
فِيهَا مِصْبَاحٌ
“Ndani yake mna taa yenye mwanga mkali.”
Kwa sababu hilo tundu huwa linakusanya mwanga usisambae.
الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ الزُّجَاجَةُ
“Taa hiyo yenye mwanga mkali iko katika (tungi la) gilasi.”
Kutokana na usafi wake na kupendeza kwake.
كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ
“Gilasi hiyo ni kama kwamba nyota inayong’aa na kumeremeta.”
Inaangaza kama lulu
يُوقَدُ مِنْ شَجَرَةٍ مُبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ
“Inawashwa kutokana na mti wa baraka wa zaytuni.”
Inawashwa taa hiyo, kutokana na mafuta ya zaytuni ambayo Nuru yake inaangaza sana.
لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ
“Hauko Mashariki wala Magharibi.”
Haiangazi Mashariki tu, kiasi kwamba jioni hakufikiwi na Nuru, na wala si Magharibi tu kwamba asubuhi hakufikiwi na Nuru. Na yasipo kuwepo mambo haya mawili basi inakuwa kati na kati katika ardhi, kama zaytuni za Sham, zinapatwa na jua asubuhi na jioni, zinakuwa nzuri, na mafuta yake yanakuwa masafi zaidi, ndio Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ ۚ
“Yanakaribia mafuta yake kung’aa japokuwa moto haujayagusa.”
Kutokana na usafi wake, yakiguswa na moto yanawaka sana.
نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ ۗ
“Nuru juu ya Nuru.”
Nuru ya moto na nuru ya mafuta. Na picha ya mfano huu ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Ameupiga na Akautumia kuelezea hali ya Muumini ambaye Nuru ya Allaah (سبحانه وتعالى) iko ndani ya moyo wake ni kwamba umbile asilia aliloumbiwa nalo mwanaadam ni sawasawa na mafuta safi, kwani umbile lake liko safi na limeandalika (kupokea) mafundisho ya kumuabudu Allaah (سبحانه وتعالى), na kufanya kila kilicho halali, ikifika (kwenye moyo) ilimu na imaan, basi Nuru hiyo itawaka kwenye moyo wake. Ni sawa na moto uliopo kwenye utambi wa hiyo taa, naye akiwa na moyo msafi usiokuwa na makusudio mabaya, wala ufahamu mbaya kuhusu Allaah (سبحانه وتعالى), basi ikiwa imaan itaingia ndani ya moyo huo, utanunurisha mwanga wa ajabu, kwa kuwa hauna takataka za aina yoyote. Hii inakuwa sawa na taa yenye mng’ao wa lulu. Kwa hali hii, itamkusanyikia Muumini huyu Nuru ya fitwrah (maumbile ya asili), Nuru ya imaan, Nuru ya ilimu, na Nuru ya maarifa. Kwa hiyo ni Nuru juu ya Nuru.
Na baada ya kuwa hii ni Nuru ya Allaah (سبحانه وتعالى), sio kila mmoja anafaa kuipata ndio Allaah Anasema:
يَهْدِي اللَّـهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاءُ
“Anamwongoza kwa Nuru Yake Amtakaye.”
Ni katika wale ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Anafahamu utakasifu wao, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atazidisha kuwatakasa, na kuwakuza kiimani.
وَيَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ
“Na Allaah Anapiga mifano kwa watu.”
Ili wapate kufahamu na kutambua huruma ya Allaah kwao, na Ihsaan Yake kwao, na ili haki iwe wazi wapate kuiacha baatwil. Hakika mifano huwa inakaribisha maana hasa kutokana na vitu vinavyoonekana na kuhisika, ndio waja wataelewa kwa uwazi zaidi.
وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
“Na Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi.”
Ilimu ya Allaah (سبحانه وتعالى) imeenea katika vitu vyote, ili mtambue kwamba Aliyepiga mifano hiyo, ni Yule Anayetambua uhakika wa mambo na uchambuzi wake, na kwamba mifano hiyo ni maslahi kwa waja, hivyo basi, la kukushughulisheni ni kulizingatia hilo, si kulipuuza, kwani Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Anajua na ninyi hamjui. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[14] Waliokufuru Amali Zao Ni Kama Sarabi Jangwani:
Mifano miwili hii Allaah (سبحانه وتعالى) Ameipigia kwenye matendo ya makafiri kwamba ni baatwil yatakwenda bure na atakuja kujuta yule aliyeyatenda, ndio Akasema: Waliomkufuru Rabb wao na kuwakadhibisha Manabii Wake, amali zao ni kama sarabi jangwani. Mwenye kiu hudhania kuwa ni maji.
Mtu mwenye kiu kikali anadanganyika tofauti na mtu mwingine kutokana na kuhitajia maji kutokana na kiu, na hii ndio kudhania kuliko baatwil, atapakusudia ili azime kiu alicho nacho, lakini akifika anajuta sana, na hapo kiu kinazidi, kwa sababu ya kukatika matarajio yake. Hayo ndio matendo ya makafiri ambayo ni sawa sawa na sarabi. Mtu mjinga asiyejua mambo anahisi kuwa ni matendo yenye manufaa. Ule muonekano wake unamdanganya kutokana na matamanio ya nafsi yake, anahisi kuwa ni matendo yenye manufaa, na yeye anayahitajia hayo, bali analazimika kuyahitaji kama anavyohitaji maji mtu mwenye kiu, mpaka siku akiyafikia matendo yake siku ya Qiyaamah atayakuta yamepotea, na hatokuta chochote kile, na hali kuwa hayajaondoka, na hayamsaidii kwa lolote, bali anamkuta Allaah (سبحانه وتعالى) mbele Yake, Naye Amlipe kikamilifu hesabu yake. Yaani: Hakitofichika Kwake kitu chochote kile kidogo, kikubwa, kingi na kichache. Na Allaah Ni Mwepesi wa Kuhesabu. Yaani: Na wala watu majaahili wasidhanie lina uzito hilo, ni lazima litokee, na Allaah (سبحانه وتعالى) Amepiga mfano wa sarabi jangwani, pasipo na miti wala mimea. Na huu ni mfano wa nyoyo zao; hakuna kheri humo wala wema, ikawa sababu ya matendo yao kuwa safi, bali ni kwa sababu ya kizuizi kilichopo ambacho ni ukafiri. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[15] Kila Kitu Kinamsabbih Allaah (عزّ وجلّ):
Rejea Al-Hashr (57:1) kwenye rejea zinazotaja viumbe na vitu Alivyoviumba Allaah kuwa vinamsabbih Yeye Allaah (عزّ وجلّ).
[16] Baadhi Ya Aina Ya Viumbe Alivyoumba Allaah (سبحانه وتعالى):
Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amekiumba kila kitambaacho ardhini kutokana na maji, kwani maji ndio asili ya kuumbwa kwake. Na miongoni mwa vitambaavyo. Kuna anayetembea kwa matumbo yake kama vile nyoka na mfano wake, na katika hao kuna anayetembea kwa miguu miwli kama binaadam, na miongoni mwao kuna anayetembea kwa miguu minne kama wanyama na mfano wake. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anaumba Anachotaka, na Yeye ni Muweza wa kila kitu. [Tafsiyr Al-Muyassar]
[17] Nyoyo Zenye Maradhi:
Rejea Suwrah Muhammad (47:20) kwenye maelezo na rejea mbalimbali kuhusu nyoyo zenye maradhi.
Rejea pia Al-Hajj (22:46) kwenye maelezo kuhusu maana ya moyo uliopofuka.
Rejea pia Ash-Shu’araa (26:88-89) kwenye ufafanuzi na maelezo kuhusu moyo uliosalimika.
[18] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/Ahadi Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Waumini Watiifu, Wenye Kutenda Mema Wasiomshirikisha Na Chochote
Bonyeza kiungo kifuatacho:
Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaahidi walioamini miongoni mwenu na wakafanya matendo mema kwamba, Atawarithisha ardhi ya washirikina na atawafanya ni wasimamizi wa hiyo ardhi, kama Alivyofanya kwa waliokuja kabla yao kati ya wale waliomuamini Allaah na Rusuli Wake. Na Aifanye Dini yao ambayo Ameridhika nayo na Akawachagulia, nayo ni Uislamu, ni Dini yenye ushindi na uthabiti, na Azigeuze hali zao kwa kuwaondolea kicho na kuwaletea amani, iwapo watamwabudu Allaah Peke Yake, na watasimama imara kwa kumtii, na wasimshirikishe na kitu chochote. Na Mwenye kukanusha baada ya hilo la kupewa usimamizi, amani, uthabiti na utawala kamili, na akakanusha Neema za Allaah, basi hao ndio waliotoka nje ya utiifu kwa Allaah. [Tafsiyr Al-Muyassar]
[19] Baadhi Ya Adabu Za Sitara Katika Familia:
Enyi ambao mlimuamini Allaah na Rasuli Wake, na mkazifanyia kazi sheria Zake! Waamrisheni watumwa wenu, wajakazi wenu na watoto waungwana ambao umri wao haujafikia wa kubaleghe, waombe ruhusa wakitaka kuingia (vyumbani) kwenu katika nyakati za mapumziko yenu na kuvua nguo zenu; Kabla ya Swalaah ya Alfajiri, kwa kuwa huo ni wakati wa kuvua nguo za kulalia na kuvaa nguo za baada ya kuamka, na wakati wa kuvua nguo kwa mapumziko ya kipindi cha mchana wakati wa jua kali, na baada ya Swalaah ya ‘Ishaa, kwa kuwa huo ni wakati wa kulala. Nyakati tatu hizi ni za kujifunua na kujiacha wazi na kunapungua kujisitiri. Lakini katika nyakati sizokuwa hizo, si makosa wakiingia bila ya idhini, kwa kuwa wao wanahitaji kuingia kwenu, wao ni wa kuingia na kutoka mara kwa mara kwa kutumika, na kwa kuwa dasturi iliyozoeleka ni kuwa nyinyi mnatembeleana nyakati hizi kwa kutimiza haja zenu zenye maslahi kwenu. Na kama Alivyowafafanulia Allaah (سبحانه وتعالى) hukumu za kutaka ruhusa (ya kuingia majumbani), Anawafafanulia Aayaat Zake, Hukumu Zake, Hoja Zake na Sharia za Dini Yake. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anayajua sana yanayowafaa viumbe Wake, Yeye ni Mwingi wa hekima katika Upelekeshaji Wake mambo yao. [Tafsiyr Al-Muyassar]
[20] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah/ Baadhi Ya Adabu Za Kula Na Za Kuingia Katika Nyumba:
Bonyeza kiungo kifuatacho:
Hawana dhambi watu wenye nyudhuru miongoni mwa vipofu, viguru na wagonjwa, kuyaacha mambo ya lazima ambayo hawawezi kuyatekeleza, kama kupigana Jihaad na mfano wake katika vitu ambavyo vinahitajia kwa kipofu aweze kuona, na kiguru awe mzima (aweze kutembea na kukimbia), na mgonjwa awe na afya nzuri. Na nyinyi, enyi Waumini, hamuna makosa kula kwenye majumba ambayo ndani yake kuna wake zenu na watoto wenu. Na hapa yanaingia majumba ya watoto, au majumba ya baba zenu, au mama zenu, au ndugu zenu wa kiume, au dada zenu, au ami zenu, au mashangazi zenu, au wajomba zenu, au mama zenu wadogo, au kwenye nyumba ambazo mliwakilishwa kuzisimamia wakati wenyewe hawapo kwa ruhusa yao, au kwenye nyumba za marafiki. Hakuna makosa yoyote kwenu kula mkiwa pamoja au mbalimbali. Na muingiapo kwenye nyumba zinazokaliwa au zisizokaliwa, amkianeni nyinyi kwa nyinyi kwa maamkizi ya Kiislamu, nayo ni:
السَّلامُ عَلَيْكُم ورَحْمَةُ اللهِ وَبَرَكاتُهُ
au
السلام علينا وعلى عباد الله الصالحين
Maamkizi haya Allaah (سبحانه وتعالى) Ameyaweka, nayo yana baraka, yanakuza kusafiana niya na kupendana, ni mazuri yanayopendeza kwa mwenye kuyasikia. Na kwa mfano wa ufafanuzi huu anawafafanulia Allaah alama za Dini Yake na Aayaat Zake, ili mzifahamu na mzitumie. [Tafsiyr Al-Muyassar]