103 - Al-'Aswr
الْعَصْر
103-Al-‘Aswr
103-Al-‘Aswr: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
وَالْعَصْرِ ﴿١﴾
1. Naapa kwa Al-‘Aswr (zama).[1]
إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢﴾
2. Hakika binaadam bila shaka yumo katika khasara.
إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾
3. Isipokuwa wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana haki, na wakausiana subira.[2]
[1] Allaah Anaapia Kwa Al-‘Aswr:
Allaah Anaapia kwa Al-‘Aswr ambayo ni usiku na mchana ambamo ndani yake matendo ya waja yanatendwa. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[2] Khasara Kwa Binaadam Isipokuwa Mambo Manne:
Suwrah imetoa mukhtasari wa binaadam kutokuwa katika khasara isipokuwa kwa mambo manne:
(i) Imaan: Kuamini Aliyotuamrisha Allaah tuyaamini. Na imaan haiwezi kukamilika bila ya kuwa na ilimu, kwani ilimu ni tawi la imaan, haitiimi bila kwayo.
(ii) Amali njema: Inajumuisha amali zote za kheri, za dhahiri na za siri, zinazohusiana na haki za Allaah na haki za Waja wake, ni sawa ikiwa ni amali za faradhi au zinazopendekezwa (na za khiari).
(iii) Kuusiana ya haki: Ambayo ni imaan na matendo mema, yaani, kuusiana kwayo, kuhimizana na kushajiishana kuyafanya.
(iv) Kuusiana kuvuta subira. Katika utiifu wa Allaah, kutokutenda maasi, na kukubali Qadar za Allaah zinazoumiza.
Kwa mambo mawili ya kwanza, mtu anajikamilisha mwenyewe. Na kwa mawili ya mwisho, mtu anawasaidia wengine kuwakamilisha. Na kwa kuyakamilisha mambo haya manne, mtu atakuwa salama kutokana na khasara na atapata mafanikio makubwa. [Tafsiyr As-Sa’diy]