Az-Zubayr Bin Awwaam (رضي الله عنه)

 

Az-Zubayr Bin  Awwaam (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Muhammad Faraj Saalim As-Saiy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Mwanafunzi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Anapotajwa Twalhah, lazima atafuatilia kutajwa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu), na pia anapotajwa Az-Zubayr lazima atafuatilia Twalhah (Radhwiya Allaahu 'anhu). Na mara nyingi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kuzungumza nao kisha anasema:
"Twalhah na Az-Zubayr majirani zangu Peponi".

 

Wote wawili wanahusiana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Twalhah (Radhwiya Allaahu 'anhu) uhusiano wake na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unakutana kwa Murrah bin Ka'ab, kwani jina lake ni;

Twalhah bin 'UbaydiLLaah bin 'Amru bin Ka'ab bin Sa'ad Bin Tayim bin Murra bin Ka'ab.

 

 

Ama Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu) anakutana na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Qusay bin Kilaab, kwani jina lake ni;
Az-Zubayr bin Awwaam bin Khuwaylid bin Asad bin 'Abdul-Uzza bin Qusay bom Kilaab.
Na jina la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni Muhammad bin 'AbdiLLaah bin 'Abdil-Muttwalib bin Haashim bin 'Abdul-Manaaf Bin Qusay bin Kilaab  bin Murrah bin Ka'ab bin Luayy.

 

Mama  yake Az-Zubayr, ni Bi Swafiyyah bint 'Abdul-Muttwallib bin Haashim bin 'Abdul-Manaaf, yeye ni shangazi yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia dada yake Hamza (Radhwiya Allaahu 'anhu) (Bwana wa Mashuhadaa).

 

 

Watu hawa, Twalhah na Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhum) walishabihiana sana katika umbile lao na katika tabia zao, na wote walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini ya Kiislaam.
Az-Zubair (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa na umri wa miaka kumi na tano tu wakati alipojiunga na wenzake katika Uislaam na katika kuupiga vita ushirikina, na alikuwa mmoja katika watu sita waliochaguliwa na 'Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) achaguliwe mmoja wao kuwa Khalifah baada ya kufa kwake.

 

Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu) pia anajulikana kuwa ni mtu wa mwanzo kuunyanyua upanga wake juu kwa ajili ya kuupigania Uislaam.

Katika siku za mwanzo wakati Waislaam walipokuwa bado dhaifu na wachache sana wakijificha ndani ya nyumba ya Al-Arqam na kujifunza Qur-aan na mafundisho mengine ya dini, habari zilienea kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameuliwa. Aliposikia habari hizo, Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu) juu ya udogo wake wa umri wake, aliinuka akaunoa upanga wake kisha akaunyanyua juu huku akipita katika mitaa ya mji wa Makkah ili kuhakikisha juu ya ukweli wa habari hizo na huku akiwaahidi Maquraish kuwa ikiwa habari hizo ni kweli, basi atawakata vichwa vyao mmoja baada ya mwengine mpaka awamalize au wammalize.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana naye akiwa nje ya mji wa Makkah, na baada ya kuijuwa sababu ya Az-Zubayr kuwa katika hali ile, alifurahi sana na akamuombe du'aah yeye pamoja na upanga wake.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema juu yake;

"Hakika kila Rasuli ana mwanafunzi wake mtiifu, na mwanafunzi wangu mtiifu ni Az-Zubayr bin Awwaam".
Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu) si mtoto wa shangazi yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tu, bali yeye pia ni mume wa Asmaa bint Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu)

Share