Kutoa Sadaka Na Pesa Za Kusaidiwa Na Serikali Na Zile Za Chumo La Haraam

 

SWALI:


asalam alaikum warahma tullahi wabarakatum, mie ni kijana ambae naishi ktk nchi za ulaya nina suala langu hili, ktk nchi za ulaya uchumi wao mwingi ni ktk biashara ya ulevi, na kodi yaani tax sasa kwa yule ambae anafanya kazi kuuza magazeti au kuyasambaza magazeti majumbani na wakati ndani ya magazeti hayo yana matangazo ya ulevi au anasa zisizokubaliwa, jee mshahara wake wa halali? na pia  kwa yule ambae anafanya kazi kwenye madaladala yaani dreva  na anawapakia walevi au ulevi au mambo yasio husika ndani ya mabasi hayoau ndani ya basi hilo kuna matangazo ya ulevi au anasa mbovu jee mshaharawake ni halali na anaweza kutoa zaka? Na pia kwa wale ambao hawana kazi, serikali ya nchi hio inawasaidia kuwapapesa za mahitaji yao jee pesa hizo zinafaa kutoa sadaka? Wakati uchumi wao ni ktk kodi (tax) na biashara ya vinywaji vya haramu ili waweze kuwasaidia wananchi wao kuwatoza tax kubwa wananchi wenye kazi na kuboresha vinyaji vya haramu kwa wingi ili waweze kuwasaidia wananchi wao jee inafaa pesa hizo kutoa sadaka? Inshallah nategemea mtanijibu kwa ufasaha kwa nguvu zake Allah (s .w)Bottom of Form.

 


 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Yapo majarida na magazeti ambayo yanatoa na kusambaza habari za kawaida kwa yanayojiri katika ulimwengu na habari za kibiashara na nyenginezo. Katika magazeti kama hayo ikiwa miongoni mwa matangazo ni ya ulevi, kamari na kadhalika lakini asili yake ni habari ambayo ni halali, kazi kama hiyo inafaa. Ikiwa gazeti au jarida au vipeperushi ni haswa kwa shughuli ambazo ni haramu kama kutangaza ulezi, kamari, au kuonyesha picha za watu walio uchi basi kazi kama hiyo itakuwa ni haramu.

Ikiwa kazi ya daladala asli yake ni kubeba abiria wa kawaida kabisa siyo haswa kwa walevi kazi kama hiyo itakuwa ni sahihi lakini ikiwa ni unaweka daladala au taksi katika mlango wa balaa au sehemu nyengine za maasiya nawe ni kuwabeba hao tu, basi shughuli kama hiyo itakuwa haramu. Sasa ikiwa ni dereva wa basi la kiwanda cha pombe na kukawa pia na matangazo kama hayo ya ulevi ndani yake, hayo mawili yote yatakuwa ni haramu. Lakini ikiwa unapeleka basi la abiria, hivyo kukiwa na matangazo ya ulevi kazi yako inakuwa sawa na pato lako pia ni sahihi.

Lakini inafaa kwa mfanya kazi ambaye ni Muislamu awafanyie Da‘wah wakuu wa kampuni ili hata hayo matangazo yaondoshwe. Ikiwa pato lako ni halali ukawa na akiba iliyofikia nisaab (kiwango cha chini) na kikapitiwa na mwaka inabidi utoe Zakah.

Kawaida serikali huchukua kodi kutoka sehemu tofauti pamoja na sehemu ambazo biashara ni haramu. Sehemu hii ya kodi ni ndogo ambayo serikali hupata kutoka kwa raia lakini sehemu kubwa inatoka kwa watu au biashara ambazo ni halali. Kwa hivyo usaidizi huo ni halali kuchukua na ikiwa ni halali basi kutoa sadaka pia inafaa.

Na hapa tunatoa nasaha kwa ndugu zetu Waislamu wasiwe ni wenye kutegemea kupatiwa misaada kutoka kwa serikali au kwa watu wengine bali wafanye juhudi katika kufanya kazi na kupata pato la kutoa jasho. Hilo ndilo jambo busara zaidi kwa vijana wetu kwa kufuata ruwaza njema kutoka kwa Mitume (a.s.) ambao walikuwa hawali isipokuwa kwa wanachokitolea jasho. Mtume (s.a.w.w) alikuwa anachunga wanyama wa watu wa Makkah na kupata hela ndogo na pia alikuwa mfanyi biashara. Manabii wengine kama Nabii Nuh (a.s.) alikuwa ni seremala, Nabii Idris (a.s.) mshonaji, Nabii Dawuud (a.s.) mfuaji vyuma, na kadhalika.

Na Mtume (s.a.w.w) amesema: “Allah hakutuma Mtume isipokuwa alikuwa ni mchungaji wanyama”.

Hii ni kuonyesha walikuwa wakifanya kazi na kupata kwa jasho lao na si kuwa tegemezi kama Waislam wengi leo hii!

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share