11-Wewe Pekee Tunakuabudu: Nyakati, Mahali Na Hali Za Kutakabaliwa Du'aa

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

11 - Nyakati, Mahali Na Hali Za Kutakabaliwa Du'aa

 

 

 

Neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) juu ya waja Wake kujaalia miezi bora kuliko miezi mingine, masiku bora kuliko mengineyo, masaa bora kuliko mengineyo, mahali bora kuliko pengineko. Vile vile kujaalia hali kadhaa kuwa ni hali zenye kutakabaliwa du’aa. Kwa hiyo Muislamu ajitahidi kuomba katika nyakati au hali zifuatazo:

 

 

1. Du’aa Wakati Wa Kuamka Usiku:

 

Unapoamka usiku, jambo la kwanza kufanya ni kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuomba utakacho:

 

عَنْ عُبَادَةُ بْنُ الصَّامِتِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَنْ تَعَارَّ مِنْ اللَّيْلِ فَقَالَ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ وَلاَ حَوْلَ ولاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ، ثُمَّ قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي، أَوْ دَعَا اسْتُجِيبَ لَهُ، فَإِنْ عَزَمَ فَتَوَضَّأَ ثُمَّ صَلَّى قُبِلَتْ صَلَاتُهُ))

Kutoka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeamka usiku akasema: Laa ilaaha illa-Allaah  Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku wa-Lahul-Hamdu wa-Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr, wa Subhaana-Allaah wal-HamduliLLaah walaa ilaaha illa-Allaah wa-Allaahu Akbar walaa hawla walaa quwwata illa biLlaah (Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Pekee Hana mshirika, Ufalme ni Wake na Himdi ni Zake Naye ni Mweza wa kila kitu. Ametakasika Allaah, na Himdi ni za Allaah, na hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ni Mkubwa kabisa, na hapana uwezo wala nguvu ila za Allaah), kisha akasema Rabbigh-fir-liy [ee Allaah, nighufurie] au akaomba, ataitikiwa. Na akiazimia kutawadha na kuswali atatakabaliwa Swalaah yake)) [Al-Bukhaariy na wengineo] 

 

 

 

2. Du’aa Inapoadhiniwa Swalaah:

 

Hii ni fursa adhimu kwa Muislamu kupata mara tano kwa siku kuwa ni nyakati za kukubaliwa du’aa. Hadiyth mbali mbali za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimethibiti baadhi yake zifuatazo:

 

عن أنس بن مالك (رضي الله عنه) عن النبي صلى الله عليه وسلم: ((إذا نودِي بالصلاةِ فُتحَتْ أبوابُ السماءِ، واستُجيبَ الدعاءُ))

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Inaponadiwa Swalaah, milango ya mbingu hufunguliwa na du’aa huitikiwa)) [Atw-Twayaalisiy, Abuu Ya’laa, Adhw-Dhwiyaa Al-Maqdasiy, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (818), na As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1413)]

 

 عَنْ أَبِي أُمَامَة الْبَاهِلِي (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) عَن النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّم) إِذَا نَادَى الْمُنَادِي فُتِحَتْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ، وَاسْتُجِيبَ الدَّعَاءِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Baahiliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ((Anaponadi muadhini, milango ya mbingu inafunguliwa na du’aa zinaitikiwa)) [Abu Ya’laa, Al-Haakim na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (803)]

 

 عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((ثِنْتَانِ لاَ تُرَدَّان أَوْ قَلَّمَا تُرَدَّانِ: الدُّعَاءُ عِنْدَ النِّدَاءِ, وَعِنْدَ الْبَأْسِ حِينَ يُلْحِمُ بَعْضُهُمْ بَعْضًا))

Imepokelewa kutoka kwa Sahl bin Sa’d (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Du’aa] Mbili hazirudishwi au nadra kurudishwa; du’aa inapoadhiniwa na wakati wa vita majeshi wanapotekana)) [Abu Daawuwd imepewa daraja ya Swahiyh na Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3079)]
 

 

 

3. Du’aa Baada Ya Kutawadha Kuomba Jannah:

 

Du’aa baada ya kutawadha iliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo ya kuomba Pepo:

 

 عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَتَوَضَّأُ فَيُحْسِنُ الْوُضُوءَ ثُمَّ يَقُولُ: أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إلاَّ اللَّهُ وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، إلاَّ فُتِحَتْ لَهُ ثَمَانِيَةُ أَبْوَابِ الْجَنَّةِ يَدْخُلُ مِنْ أَيِّهَا شَاءَ))

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna Muislamu yeyote anayetawadha akatia vizuri wudhuu wake, kisha akasema: “Ash-hadu anlaa ilaaha illa-Allaah wa ash-hadu anna Muhammadan ‘Abduhu wa Rasuwluhu [Nashuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na nashuhudia kwamba Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake] ila atafunguliwa milango minane ya Jannah ataingia wowote apendao)) [Ibn Maajah – Swahiyh Ibn Maajah (385)]

 

 

 

4. Du’aa Baina ya Adhaana Na Iqaamah:

 

Hii pia ni fursa nyingine kwa Muislamu kuwa katika mara tano kwa siku ana nyakati ya kuitikiwa du’aa zake:

 

 عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((الدُّعَاءُ لاَ يُرَدُّ بَيْنَ الأَذَانِ وَالإِقَامَةِ))  

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Du’aa hairudishwi baina ya adhana na iqaamah)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ahmad – Hadiyth Hasan Swahiyh, ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (212), Irwaa-u Al-Ghaliyl (244), Swahiyh Al-Jaami’ (3408)]

 

 

 

5. Du’aa Kila Baada Ya Swalaah:

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قِيلَ يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَيُّ الدُّعَاءِ أَسْمَعُ؟ قَالَ: ((جَوْفَ اللَّيْلِ الآخِرِ وَدُبُرَ الصَّلَوَاتِ الْمَكْتُوبَاتِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:  Ilisemwa: Ee Rasuli wa Allaah, du’aa ipi inayosikilizwa zaidi (inayotakabaliwa zaidi)? Akasema: ((Sehemu ya mwisho ya usiku na baada ya kila Swalaah ya faradhi))  [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan, Swahiyh At-Tirmidhiy (3499) Swahiyh At-Targhiyb (1648)]

 

Ufafanuzi wa ‘Baada ya Swalaah”:  Je ni kabla ya tasliym au baada ya tasliym?

 

‘Ulamaa wamekubaliana kwamba ikiwa ni adhkaar (nyiradi) zilizothibiti katika Sunnah kama tasbiyh, tahmiyd, takbiyr, na Aayatul-Kursiy, Suwratul-Ikhlaasw na Al-Mu’awwidhatayn, basi ilokusudiwa ‘baada ya Swalaah’ ni baada ya kutoa salaam. Ama ikiwa ni du’aa basi ilokusudiwa ni kabla ya kutoa salaam. Kauli zao ni kama zifuatazo:

 

Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah):

“Kila baada ya Swalaah, inajumuisha kabla ya salaam na baada ya salaam. Na Shaykh wetu Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema (kuhusu du’aa) ni kabla ya salaam kwa dalili ya mfano wa: ‘kila baada ya nyuma ya kitu kama vile nyuma ya mnyama.” [Zaad Al-Ma’aad(1/294)]

 

 

Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah):

“Kila baada ya Swalaah inaainisha kabla ya tasliym, na ina maana baada ya tasliym moja kwa moja. Na Hadiyth Swahiyh zimetajwa ambazo zinaonesha ilokusudiwa kwamba kama ni du’aa basi ni kabla ya tasliym. Ama adhkaar zilotajwa kuhusiana na hili, basi Hadiyth Swahiyh zimeashiria kwamba hizo ni baada ya Swalaah, kwa maana baada ya tasliym.” [Majmuw’ Fataawa Ibn Baaz (11/194)]

 

 

Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah):

“Yaliyotajwa makhsusi (ya Sunnah) kila baada ya Swalaah ikiwa ni adhkaar (nyiradi) basi hizo ni baada yake, na ikiwa ni du’aa basi ni mwisho wake (kabla ya salaam)." [Majmuu’ Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn (13/268)]

 

 

 

6. Du’aa Katika Kusujudu:

 

Bin Aadam anapomsujudia Allaah (‘Azza wa Jalla) inadhihirisha unyenyekevu mbele Yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwani anaweka kipaji cha uso wake ardhini kujidhalilisha kwa Aliyemuumba. Na kipaji cha uso ni sehemu bora kabisa katika mwili wa bin Aadam, ndipo hapo anapokuwa mja karibu kabisa na Rabb wake:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّه عَنْهُ) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ فَأَكْثِرُوا الدُّعَاءَ))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja huwa karibu kabisa na Rabb   wake anapokuwa anasujudu, kwa hiyo zidisheni du'aa)) [Muslim (482), Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ahmad]

 

 

 

7. Du’aa Katika Thulutuhi Ya Mwisho Ya Usiku:

 

Neema na fadhila kubwa kwa binaadam kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla) Huteremka hadi mbingu ya dunia kututakabalia du’aa, kutukidhia haja na kutughufuria dhambi: 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْه)ُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ:  ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآَخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Rabb wetu Tabaaraka wa Ta’aalaa) Huteremka [kwa namna inavyolingana na utukufu Wake] kila siku katika mbingu ya dunia [ya kwanza] inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ananitaka jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad]

 

 

 

8. Du’aa Katika Saa Ya Usiku:

 

عَنْ جَابِرٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ)  قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ يَقُولُ: ((إِنَّ فِي اللَّيْلِ لَسَاعَةً لاَ يُوَافِقُهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ يَسْأَلُ اللَّهَ خَيْرًا مِنْ أَمْرِ الدُّنْيَا وَالآَخِرَةِ إِلاَّ أَعْطَاهُ إِيَّاهُ وَذَلِكَ كُلَّ لَيْلَةٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika katika usiku bila shaka kuna saa haimuwafikii mtu Muislamu anayemwomba Allaah khayr katika mambo ya dunia au Aakhirah ila Atampa, na hiyo ni kila usiku)) [Muslim (757), Swahiyh Al-Jaami’ (2130)]

 

 

 

9. Du’aa Katika Saa Ya Siku Ya Ijumaa:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ذَكَرَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ فَقَالَ:  ((فِيهِ سَاعَةٌ لاَ يُوَافِقُهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي يَسْأَلُ اللَّهَ تَعَالَى شَيْئًا إلاَّ أَعْطَاهُ إِيَّاهُ)) وَأَشَارَ بِيَدِهِ يُقَلِّلُهَا

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametaja Siku ya Ijumaa akasema: ((Humo mna saa haimwafikii mja Muislamu akiwa amesimama anaswali anamwomba Allaah Ta’aalaa kitu ila Anampa)). Akaashiria kuonyesha ukaribu wake [Al-Bukhaariy (935), Muslim (852) na wengineo]

 

‘Ulamaa wamekubaliana kuwa ni nyakati mbili kwa dalili zifuatazo:

 

Kwanza: Anapopanda Imaam katika minbari na kukaa kwake hadi anapomaliza Swalaah:

 

عَنْ أَبِي بُرْدَةَ بْنِ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ لِي عَبْدُ اللَّهِ بْنُ عُمَرَ: أَسَمِعْتَ أَبَاكَ يُحَدِّثُ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي شَأْنِ سَاعَةِ الْجُمُعَةِ؟ قَالَ: قُلْتُ: نَعَمْ سَمِعْتُهُ يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((هِيَ مَا بَيْنَ أَنْ يَجْلِسَ الإِمَامُ إِلَى أَنْ تُقْضَى الصّلاَةُ))

Kutoka kwa Abuu Burdah bin Abiy Muwsaa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: ‘Abdullaahi bin ‘Umar ameniuliza: Je umemsikia baba yako akihadithia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu saa ya [kutakabaliwa du’aa) Ijumaa? Akasema: Nikasema:  Ndio, nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hiyo ni baina ya anapokaa Imaam hadi inapomalizika Swalaah)) [Muslim (853)]

 

Pili: Baada ya Swalaah ya Alasiri hadi kuzama jua. Hii ni kauli inayokubalika zaidi miongoni mwa ‘Ulamaa kwa dalili:

 

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((يَوْمُ الْجُمُعَةِ اثْنَتَا عَشْرَةَ سَاعَةً ،لاَ يُوجَدُ فِيهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ يَسْأَلُ اللَّهَ شَيْئًا إلاَّ آتَاهُ إِيَّاهُ ، فَالْتَمِسُوهَا آخِرَ سَاعَةٍ بَعْدَ الْعَصْر))

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Siku ya Ijumaa kuna masaa kumi na mbili ambayo hapatikani mja Muislamu anayemwomba Allaah kitu ila Anampa, basi itafuteni baada ya Swalaah ya Alasiri))  [Swahiyh Abiy Daawuwd (1048), Swahiyh An-Nasaaiy(1388), Swahiyh Al-Jaami’ (8190)]

 

Kauli za Baadhi Ya ‘Ulamaa:

 

Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah):  

“Huu ndio wakati ambao ameupendekeza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya du’aa siku ya Ijumaa. Lakini hii haimaanishi kwamba Muislamu asimwombe Rabb wake siku ya Ijumaa ila wakati huu, bali ni Sunnah kuomba du’aa kila siku, na kila saa, na siku ya Ijumaa, isipokuwa tu saa iliyotajwa siku ya Ijumaa ni makhsusi.”

 

 

Al-Haafidhw Ibn Hajr (Rahimahu Allaah):

“Sa’iyd bin Manswuwr amesimulia katika Sunan yake kutoka kwa Abuu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan kwamba Maswahaba walijumuika wakataja kuhusu saa ya Ijumaa, kisha wakaachana, lakini hawakukhitilafiana kwamba ni saa ya mwisho ya siku ya Ijumaa.” [Fat-h Al-Baariy(2/421)]

 

 

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah):  

“Hadiyth nyingi kuhusu saa ambayo inatarajiwa kuitikiwa du’aa ni baada ya Swalaah ya Alasiri..." [At-Tirmidhiy (2/360)]

 

 

Hitimisho kuhusu rai hiyo ya pili ni kwamba, ‘Ulamaa wamekariri kutaja kwamba nyakati zote mbili hizo zihesabiwe kuwa ni saa iliyokusudiwa. Hata hivyo, anapaswa pia Muislamu ajitahidi kuomba du’aa siku nzima ya Ijumaa na haswa nyakati hizo zisikoswe kwa mwenye kutamani du’aa yake itakabliwe.

 

 

 

10. Du’aa Baada Ya Jua Kufikia Upeo Kabla Ya Adhuhuri:

 

Ni wakati mwengine ambao mbingu huwa wazi na du’aa hupaa juu moja kwa moja bila ya kizuzi:

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ السَّائِبِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) كَانَ يُصَلِّي أَرْبَعًا بَعْدَ أَنْ تَزُولَ الشَّمْسُ قَبْلَ الظُّهْرِ وَقَالَ: ((إِنَّهَا سَاعَةٌ تُفْتَحُ فِيهَا أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَأُحِبُّ أَنْ يَصْعَدَ لِي فِيهَا عَمَلٌ صَالِحٌ))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin As-Saaib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaahh (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali [rakaa] nne baada ya jua kufikia upeo kabla ya Adhuhuri na akasema: ((Hakika hiyo ni saa inayofunguliwa milango ya mbingu na napenda zipande 'amali zangu njema)) [At-Tirmidhiy ameisahihisha Al-Albaaniy Swahiyh At-Tirmidhiy (478), Swahiyh At-Targhiyb (587)]

 

Swalaah hizo alizokuwa akiswali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa ni mbali na zile nne zinazoswaliwa kabla ya Adhuhuri zinazojulikana kuwa ni ‘rawaatib’ au ‘qabliyah’ Tofauti yake pia ni kwamba alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiziswali nne kwa pamoja badala ya mbili mbili kama kawaida.

 

 

 

11. Wakati Wa Kusubiri Swalaah:

 

Huu ni wakati wa baina ya Swalaah mbili pale mtu anaposwali kisha akabakia kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mpaka ufikie wakati wa Swalaah inayofuatia:

 

 عنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنه)  قَالَ: صَلَّيْنَا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) الْمَغْرِبَ فَرَجَعَ مَنْ رَجَعَ, وَعَقَّبَ مَنْ عَقَّبَ، فَجَاءَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) مُسْرِعًا قَدْ حَفَزَهُ النَّفَسُ وَقَدْ حَسَرَ عَنْ رُكْبَتَيْهِ فَقَالَ: ((أَبْشِرُوا هَذَا رَبُّكُمْ قَدْ فَتَحَ بَابًا مِنْ أَبْوَابِ السَّمَاءِ يُبَاهِي بِكُمْ الْمَلائِكَةَ يَقُولُ : انْظُرُوا إِلَى عِبَادِي قَدْ قَضَوْا فَرِيضَةً وَهُمْ يَنْتَظِرُونَ أُخْرَى))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Tuliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Magharibi, wakarudi walorudi, na wakabakia walobaki. Akaja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiharakiza kutokana na kuhamasishwa na nafsi na likiwa vazi lake limepanda hadi magoti yake kuwa wazi akasema: ((Bashirieni! Huyo ni Rabb wenu Amefungua mlango kati ya milango ya mbingu Anajigamba kwa Malaika Akisema: Tazameni waja Wangu wamemaliza fardhi kisha wanangojea nyingine))  [Ibn Maajah 'Baab Luzuwm al-Masaajid Wa Intidhwaar Asw-Swalaah' (793), Ahmad. Taz. Swahiyh Ibn Maajah (660), Swahiyh Al-Jaami’ (36), Swahiyh At-Targhiyb (445)]

 

 

 

12. Du’aa Inaponyesha Mvua:

 

Inaponyesha mvua au barafu katika nchi za baridi, ni wakati wa du’aa kutakabaliwa. Wanaoishi katika nchi ambazo zinapatikana majira ya mvua watakuwa na fursa kubwa kuomba du’aa zao kila inaponyesha mvua. Dalili ya kuitikiwa du’aa inaponyesha mvua:

 

عَنْ مَكْحُول (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَن النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَال: ((اطْلُبُوا إجَابَةَ الدُّعَاءِ عِنْدَ الْتِقَاءِ الْجُيُوشِ، وَإِقَامَةِ الصَّلَاةِ، وَنُزُولِ الْمَطَر)

Kutoka kwa Mak-huwl (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ombeni kuitikiwa du’aa wakati wa kukutana majeshi, na inapokimiwa Swalaah na inapoteremka mvua)) [As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1469)]

 

Pia:

ثنتان ما تردان الدعاء عند النداء وتحت المطر

(([Nyakati] mbili hazirudishwi du’aa; wakati inapoadhiniwa na wakati inaponyesha mvua)) [Al-Haakim katika Al-Mustadrak (2534) na Atw-Twabaraaniy katika Al-Mu’jam Al-Kabiyr (5756) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3078)]

 

Linalopasa ni kwamba pale inapoanza tu kunyesha mvua Muislamu asome du’aa iliyothibiti ya kunyesha mvua kisha aombe haja zake. Na inapomalizika kunyesha mvua pia kuna du’aa iliyothibiti katika Sunnah. [Rejea 

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

na Hiswnul-Muumin (kinapatikana madukani)]

 

 

 

13.  Du’aa Wakati Anapowika Jogoo:
 

Anapowika jogoo ni fursa ya mtu kuomba du’aa. Pia Hadiyth hii inatufunza pia kuomba du’aa ya kujikinga na shaytwaan na shari zake, jambo ambalo ni muhimu kwa Muislamu.

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((إِذَا سَمِعْتُمْ صِيَاحَ الدِّيَكَةِ فَاسْأَلُوا اللَّهَ مِنْ فَضْلِهِ فَإِنَّهَا رَأَتْ مَلَكًا، وَإِذَا سَمِعْتُمْ نَهِيقَ الْحِمَارِ فَتَعَوَّذُوا بِاللَّهِ مِنْ الشَّيْطَانِ فَإِنَّهُ رَأَى شَيْطَانًا))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnaposikia mlio wa jogoo basi mwombeni Allaah kutokana na fadhila Zake kwani ameona Malaika. Na mnaposikia mlio wa punda, basi jikingeni kwa Allaah kutokana na shaytwaan, kwani ameona shaytwaan)) [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy]

 

 

 

14. Du’aa Wakati Wa Kunywa Maji Ya Zamzam:

 

Ni fursa nyingine za wenye kutekeleza ‘Umrah na Hajj kuomba du’aa zao kila mara wanapokunywa maji ya zamzam. Pia fursa kwa wengineo wenye kuyapata maji hayo. Ni maji ya ajabu ambayo yana shifaa kwa magonjwa ya kila aina, hivyo inapendekezwa kwa Muislamu anapokunywa aombe siha na afya pamoja na haja zake nyinginezo. 

 

عن جَابِرَ بْنَ عَبْدِ اللَّهِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((مَاءُ زَمْزَمَ لِمَا شُرِبَ لَهُ))

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Maji ya zamzam kwa [niyyah] inayonywewa)) [Swahiyh Ibn Maajah (2502), Ahmad, Swahiyh Al-Jaami’(5502)]. Hata hivyo, japo Hadiyth hii Wanachuoni wenngine wamesema inatiliwa nguvu na zingine na kuwa ni Hasan, lakini pia kuna wengine walioidhoofisha].

 

 

 

15. Du’aa Anapotembelewa Mgonjwa:

 

Kumtembelea mgonjwa kuna fadhila nyingi tukufu kama zilivyothibiti katika Hadiyth kadhaa mojawapo ni kwamba mwenye kumtembelea mgonjwa huswaliwa na Malaika elfu sabini. Hadiyth ya ‘Aliy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

قَالَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِذَا عَادَ الرَّجُلُ أَخَاهُ المُسْلِمَ مَشَى فِي خِرَافَةِ الجَنَّةِ حَتَّى يَجْلِسَ فَإِذَا جَلَسَ غَمَرَتْهُ الرَّحْمَةُ، فَإِنْ كَانَ غُدْوَةً صَلَّى عَلَيْهِ سَبْعُوْنَ أَلْفَ مَلَكٍ حَتَّى يُمْسِيَ، وَإِنْ كَانَ مَسَاءً صَلَّى عَلَيْهِ سَبْعُوْنَ أَلْفَ مَلَكٍ حَتَّى يُصْبِحَ)).

Amesema (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) ((Mtu anapomtembelea ndugu yake Muislamu mgonjwa basi hutembelea katika bustani ya Jannah mpaka atakapoketi, na anapoketi hufunikwa na Rahmah ikiwa ni asubuhi wanamtakia Rahmah Malaika sabini elfu mpaka jioni. Na ikiwa ni jioni wanamtakia Rahmah Malaika sabini elfu mpaka asubuhi)) [Swahiyh Ibn Maajah (1/244), Swahiyh At-Tirmidhiy (1/286)]

 

Juu ya hivyo ni fursa kwa Muislamu kuomba du’aa yake itakabaliwe. Aanze kwanza kumwombea mgonjwa du’aa zilizothibiti katika Sunnah kisha ajiombee nafsi yake:

 

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رضي الله عنها)  قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِذَا حَضَرْتُمْ الْمَرِيضَ أَوْ الْمَيِّتَ فَقُولُوا خَيْرًا فَإِنَّ الْملآئِكَةَ يُؤَمِّنُونَ عَلَى مَا تَقُولُونَ)) قَالَتْ: فَلَمَّا مَاتَ أَبُو سَلَمَةَ أَتَيْتُ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَقُلْتُ:  يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ أَبَا سَلَمَةَ قَدْ مَاتَ قَالَ:  ((قُولِي: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي وَلَهُ وَأَعْقِبْنِي مِنْهُ عُقْبَى حَسَنَةً)) قَالَتْ: فَقُلْتُ فَأَعْقَبَنِي اللَّهُ مَنْ هُوَ خَيْرٌ لِي مِنْهُ مُحَمَّدًا (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)

Imepokelewa kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnapohudhuria mgonjwa au maiti basi semeni yaliyo mema kwani Malaika wanaitikia ‘Aamiyn’ msemayo)). Akasema: Alipofariki Abu Salamah nilimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah! Abu Salamah amefariki. Akasema: ((Sema: ‘Allaahumma-ghfir-liy wa lahu wa a-’qibniy minhu ‘uqba hasanah’ [Ee Allaah, nighufurie pamoja naye na nilipie baada yake badali iliyo njema])). Akasema:  Akanilipa Allaah ambaye ni mbora zaidi kuliko yeye; (ambaye ni) Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  [Muslim, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah]

 

 

 

16. Du’aa Za Watu Baada Ya Mja Kutolewa Roho:

 

Lilothibiti pale mtu anapotolewa roho ni kumuombea maiti du’aa na kujiombea kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

  عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: دَخَلَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) عَلَى أَبِي سَلَمَةَ وَقَدْ شَقَّ بَصَرُهُ فَأَغْمَضَهُ ثُمَّ قَالَ: ((إِنَّ الرُّوحَ إِذَا قُبِضَ تَبِعَهُ الْبَصَرُ)) فَضَجَّ نَاسٌ مِنْ أَهْلِهِ فَقَالَ: ((لاَ تَدْعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ إلاَّ بِخَيْرٍ فَإِنَّ الْمَلآئِكَةَ يُؤَمِّنُونَ عَلَى مَا تَقُولُونَ)) ثُمَّ قَالَ: ((اللَّهُمَّ اغْفِرْ  لإَبِي سَلَمَةَ وَارْفَعْ دَرَجَتَهُ فِي الْمَهْدِيِّينَ، وَاخْلُفْهُ فِي عَقِبِهِ فِي الْغَابِرِينَ، وَاغْفِرْ لَنَا وَلَهُ يَا رَبَّ الْعَالَمِينَ، وَافْسَحْ لَهُ فِي قَبْرِهِ وَنَوِّرْ لَهُ فِيهِ)) 

Imepokelewa kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwa Abuu Salamah akiwa macho yake ya wazi kabisa. Akayafunga na akasema: ((Hakika roho inapotolewa, macho yanafuatia [kupoteza uoni)). Baadhi ya watu katika familia yake wakalia na kuomboleza [kwa sauti]. Akasema: ((Msijiombee nafsi zenu ila ya khayr kwani Malaika huitikia ‘Aamiyn’ kwa myasemayo)). Kisha akasema: ((Allaahumma-Ghfir-li abiy Salamah, warfa’ darajaatahu fil-Mahdiyyiyn, wakhluf-hu fiy ‘aqibihi fil-ghaabiriyn, wa Ghfir-lanaa walahu yaa Rabbal ‘Aalamiyn, wafsah lahu fiy qabrihi, wa Nawwir lahu fiyhi  [Ee Allaah, Mghufurie Abuu Salamah, mpandishe daraja yake pamoja na walioongoka, na mfuatilishie katika kizazi chake wanaobakia, na Tughufurie pamoja naye ee Rabb wa walimwengu, na mpanulie kaburi lake na mtilie mwanga humo]))  [Muslim]

 

 

 

17. Du’aa Mwezi Wa Ramadhwaan:

 

Mwezi wa Ramadhwaan unatambulikana pia kuwa ni mwezi wa du’aa kwa vile Aayah kuhusu kuomba du’aa imetanguliwa na Aayah za Swawm [Al-Baqarah: 183-186]. Vilevile ni mwezi ambao milango ya Jannah hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo:

 

عن أبي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِذَا دَخَلَ رَمَضَانُ فُتِّحَتْ أَبْوَابُ الْجَنَّةِ وَغُلِّقَتْ أَبْوَابُ جَهَنَّمَ وَسُلْسِلَتْ الشَّيَاطِينُ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Inapoingia Ramadhwaan, milango ya Jannah hufunguliwa, milango ya Moto wa Jahannam hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo)) [Al-Bukhaariy, An-Nasaaiy]

 

Kwa hivyo, nyoyo za Waislamu hubakia katika taqwa na twaa’ah (utiifu), hali ambayo ina matumaini makubwa ya kutakabaliwa du’aa. Kwa hiyo Muislamu ajitahidi kuomba du’aa kwa wingi nyakati zote za Siku za Ramadhwaan khaswa kuomba aghufuriwe dhambi zake:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)) مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutarajia malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

18. Du’aa Laylatul-Qadr:

 

Masiku kumi ya mwisho katika mwezi wa Ramadhwaan kunapatika usiku mtukufu, wenye baraka wa Laylatul-Qadr ambao umejaa fadhila kama zilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Ni fursa ya Muislamu awe macho usiku wake kuomba aghufuriwe madhambi yake:

 

عن أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ)) 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy (1910) na Muslim (760)]  

 

Na du’aa muhimu usiku huo mtukufu ni kuomba msamaha:

 

  عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّهَا قَالَتْ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَرَأَيْتَ إِنْ وَافَقْتُ لَيْلَةَ الْقَدْرِ مَا أَدْعُو؟ قَالَ: ((تَقُولِينَ: اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, nitakapojaaliwa kuupata usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?   Akasema: ((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'afwa fa'-fu 'anniy. [Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye kusamehe Unapenda kusamehe basi nisamehe))  [Swahiyh Ibn Maajah (3119)]

 

 

 

19. Du’aa Wakati Wa Kusoma Qur-aan:

 

Muislamu anaposoma Qur-aan, anapopitia Aayah zenye kubashiriwa Jannah, basi aiombe Jannah, na anapopitia Aayah za Moto, aombe kujikinga nao. Na anapopitia Aayah zenye maonyo ya adhabu za Allaah aombe kujikinga na adhabu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) duniani na Aakhirah na aombe Rahmah za Allaah. Hivyo ni kufuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن ‏حُذَيْفَةَ بِنْ اليمان (رضي الله عنه): أنَّ النَّبِيَّ‏ ‏(صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ‏) كَانَ ‏إِذَا مَرَّ بِآيَةِ رَحْمَةٍ سَألَ، وَإِذَا مَرَّ بِآيَةِ عَذَابٍاسْتَجَارَ، وَإِذَا مَـرَّ بِآيَةٍ فِيهَـا تنزيهٌ للَّهِ سبَّحَ

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah bin Al-Yamaani (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapopitia Aayah ya Rahmah aliomba (Rahmah), na alipopitia Aayah ya adhabu aliomba kujikinga, na alipopitia Aayah zenye kumtakasa Allaah alimsabbih)) [Swahiyh Ibn Maajah (1119)]

 

Na katika riwaayah nyingine:

 

كان إذا مرَّ بآيةِ خوفٍ تعوَّذَ، و إذا مرَّ بآيةِ رَحمةٍ سألَ، و إذا مرَّ بآيةٍ فيها تَنزيهُ اللهِ سبَّحَ

Alikuwa anapopitia Aayah ya khofu, alijikinga, na alipopitia Aayah ya Rahmah aliomba (Rahmah), na alipopitia Aayah ya kumtakasa Allaah, alimsabbih)) [Swahiyh Al-Jaami’ (4782)]

 

Pia:

 

أَنَّهُ ‏صَلَّى إِلَى جَنْبِ النَّبِيِّ (‏صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ‏) ‏لَيْلَةً فَقَرَأ فَكَانَ إذَا مَرَّ بِآيَةِ عَذَابٍ وَقَفَ وَتَعَوَّذَ وَإذَا مَرَّ بِآيَةِ رَحْمَةٍ وَقَفَفَدَعَا

Kwamba ameswali pembeni na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku mmoja, akasoma akawa kila anapopitia Aayah ya adhabu alisita na akajikinga, na alipopitia Aayah ya Rahmah alisita akaomba. [Swahiyh An-Nasaaiy (1007)]

 

 

 

20. Du’aa Katika Masiku Kumi Ya Dhul-Hijjah:

 

Masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah ni matukufu mno kwa sababu ‘amali yoyote ile inayotendwa humo ni kipenzi kabisa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم): ((مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهِنَّ أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الأَيَّامِ الْعَشْرِ)) فَقَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ: ولاَ الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((ولاَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إلاَّ رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْءٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi)) [siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah] Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo)) [Al-Bukhaariy].

 

Na kwa vile kuomba du’aa ni ‘amali tukufu kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama ilivyothibiti:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنْ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لَيْسَ شَيْءٌ أَكْرَمَ عَلَى اللَّهِ تَعَالَى مِنْ الدُّعَاءِ))  

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitu kitukufu mbele ya Allaah Ta’aalaa kama du’aa)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, na amesema At-Tirmidhiy: Hasan Ghariyb na Ibn Hibbaan na Al-Haakim wameipa daraja ya Swahiyh, na ameiwafiki Adh-Dhahaabiy na Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh Al-Adaab Al-Mufrad, na pia Swahiyh At-Tirmidhiy (3370), Swahiyh Al-Jaami’ (5392)]

 

Basi bila shaka kuomba du’aa itazidi kuwa ni kipenzi Kwake Allaah Ta'aalaa.

 

Zifuatazo ni nyakati nyiginezo na sehemu mbalimbali za kuomba du’aa kwa mukhtasari. Lakini Muislamu anaweza kuomba du’aa zake wakati wowote pale anapotaka, ila katika au sehemu, au hali hizi huwa ni makhsusi kutokana na dalili kuwa kuna uzito wa du’aa kutakabaliwa: [Taz. Ad-Du’aa wa yaliyhi Al-‘Ilaaj Bir-Ruqyaa Minal-Kitaabi was-Sunnah – Sa’iyd bin ‘Aliy Al-Qahtwaaniy]

 

 

21. Du’aa katika kusoma Suwratul-Faatihah.

 

22. Du’aa baada ya kusema ‘Laa ilaaha illa Anta Subhaanaka inniy kuntu minadhw-dhwaalimyn’.

 

23. Du’aa baada ya kutaja Jina Tukufu la Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

24. Du’aa ya mwenye kutekeleza Hajj.

 

25. Du’aa ya mwenye kutekeleza ‘Umrah.

 

26. Du’aa katika Twawaaf.

 

27. Du’aa katika jabali la Swafaa.

 

27. Du’aa katika jabali la Marwah.

 

28. Du’aa baina ya majabali ya Swafaa na Marwah.

 

29-Du’aa katika Mash-‘aril-Haraam  (Muzdalifah).

 

30. Du’aa siku ya ‘Arafah.

 

31. Du’aa katika kurusha vijiwe katika Jamarah ndogo.

 

32. Du’aa katika kurusha vijiwe Jamarah la wastani (katikati).

 

33. Du’aa katika kurusha vijiwe Jamarah kubwa.

 

34. Du’aa wanapojumuika Waislamu katika vikao vya kumdhukuru Allaah.

 

 

 

 

 

Share