142-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 142: سَيَقُولُ السُّفَهَاءُ مِنَ النَّاسِ مَا وَلَّاهُمْ عَن قِبْلَتِهِمُ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
Al-Baqarah Aayah 142: Watasema wapumbavu miongoni mwa watu: “Nini kilichowageuza...
سَيَقُولُ السُّفَهَاءُ مِنَ النَّاسِ مَا وَلَّاهُمْ عَن قِبْلَتِهِمُ الَّتِي كَانُوا عَلَيْهَا ۚ قُل لِّلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿١٤٢﴾
142. Watasema wapumbavu miongoni mwa watu: “Nini kilichowageuza kutoka Qiblah chao ambacho walikuwa wakikielekea!” Sema: “Mashariki na Magharibi ni ya Allaah, Anamwongoza Amtakaye kuelekea njia iliyonyooka.”
Sababun-Nuzuwl:
Aayah hii na zinazofuatia zimeteremka kama alivyohadithia Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anaposwali, huelekeza uso wake Baytul- Maqdis. Lakini kila mara alikuwa anatazama mbinguni akingojea Amri ya Allaah. Kisha Allaah Akateremsha: “Kwa yakini Tumeona (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unavyogeuza geuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza Qiblah unachokiridhia. Basi elekeza uso wako upande wa Al-Masjidil-Haraam…” (2:144). Kisha tukatamani kujua kuhusu hukmu ya waliofariki kabla ya kugeuzwa Qiblah. Hapo Allaah Akateremsha: “Na Allaah Hakuwa Mwenye Kupoteza iymaan yenu (Swalaah), hakika Allaah kwa watu, bila shaka ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu.” (2:143) Kisha Mayahudi wakasema: Ni jambo lipi limewageuza na kuwatoa kwenye Qiblah chao? Hapo Allaah Akateremsha: “Watasema wapumbavu miongoni mwa watu: “Nini kilichowageuza kutoka Qiblah chao ambacho walikuwa wakikielekea…” mpaka mwisho wa Aayah (2:142). [Hadiyth ameipokea Imaam Ibn Is-haaq katika Siyrah]
Na katika riwaaya nyengine:
عَنِ الْبَرَاءِ بْنِ عَازِبٍ ـ رضى الله عنهما ـ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم صَلَّى نَحْوَ بَيْتِ الْمَقْدِسِ سِتَّةَ عَشَرَ أَوْ سَبْعَةَ عَشَرَ شَهْرًا، وَكَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُحِبُّ أَنْ يُوَجَّهَ إِلَى الْكَعْبَةِ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ :((قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ)) فَتَوَجَّهَ نَحْوَ الْكَعْبَةِ، وَقَالَ السُّفَهَاءُ مِنَ النَّاسِ ـ وَهُمُ الْيَهُودُ ـ ((مَا وَلاَّهُمْ عَنْ قِبْلَتِهِمُ الَّتِي كَانُوا عَلَيْهَا قُلْ لِلَّهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ)) فَصَلَّى مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم رَجُلٌ ثُمَّ خَرَجَ بَعْدَ مَا صَلَّى، فَمَرَّ عَلَى قَوْمٍ مِنَ الأَنْصَارِ فِي صَلاَةِ الْعَصْرِ نَحْوَ بَيْتِ الْمَقْدِسِ فَقَالَ هُوَ يَشْهَدُ أَنَّهُ صَلَّى مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم، وَأَنَّهُ تَوَجَّهَ نَحْوَ الْكَعْبَةِ. فَتَحَرَّفَ الْقَوْمُ حَتَّى تَوَجَّهُوا نَحْوَ الْكَعْبَةِ.
Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنهما) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiswali kuelekeza Baytul-Maqdis miezi kumi na sita au kumi na saba lakini alikuwa akipenda kuelekea Al-Ka’bah (Makkah). Basi Allaah Akateremsha: “Kwa yakini Tumeona (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unavyogeuza geuza uso wako mbinguni.” (2:144). Kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaelekea Al-Ka’bah na masafihi miongoni mwa watu nao ni Mayahudi wakasema: “Nini kilichowageuza kutoka Qiblah chao ambacho walikuwa wakikielekea!” Allaah Akasema: “Sema: “Mashariki na Magharibi ni ya Allaah, Anamwongoza Amtakaye kuelekea njia iliyonyooka”. Mtu mmoja akaswali na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kisha akatoka baada ya kuswali, akapita kwa watu miongoni mwa Answaariy waliokuwa wakiswali Swalaah ya Alasiri wakielekea Baytul-Maqdis. Akasema kuwa anashuhudia kwamba ameswali na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa ameelekea Al-Ka’bah, basi watu wote wakageuka kuelekea Al-Ka’bah. [Al-Bukhaariy Kitaab Asw-Swalaah- Baab At-Tawajjuh Nahwa Al-Qiblah Haythu Kaan]