Al-Lajnah Ad-Daaimah: Maulidi: Tarehe Aliyozaliwa Nabiy, Mashindano Ya Qur-aan, Kuchinja, Mihadhara
Tarehe Aliyozaliwa Nabiy Na Hukmu Ya Mashindano Ya Qur-aan
Na Kuchinja Na Mihadhara Kwa Ajili Ya Maulidi Yake
Al-Lajnah Ad-Daa'imah
SWALI:
Tunaomba mtujulishe tarehe sahihi ya Mawlid Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani tumepanga kufanya mashindano ya Qur-aan na kuchinja kondoo na kufanya mihadhara kwa ajili ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mnasaaba huu. Tunaomba mtuongoze kama programu hii inajuzu ki-Shariy’ah:
JIBU:
Kwanza: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezaliwa mwaka wa ‘Aam Al-Fiyl (mwaka wa tembo) kama alivyotaja Muhammad bin Is-haaq na ‘Ulamaa wa Siyrah katika vitabu vya Siyrah.
Pili: Miongoni mwa bid’ah zilokatazwa ni kusimamisha sherehe usiku wa mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kufanya mashindano ya Qur-aan na kuchinja na kutoa mihadhara kuhusu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mnaasaba huu, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliijua zaidi nafsi yake. (Angehitaji kujisherehekea au kusherehekewa angebainisha).
Na ni mjuzi zaidi wa Shariy’ah ya Allaah Ta’aalaa. Wala haipasi kumuadhimisha. Wala haikuthibiti kwamba yeye alisherehekea Mawlid yake wala Mawlid ya ndugu zake Manabiy waliotangulia ('Alayhimus-Salaam) wala Mawlid ya ndugu zake Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Na imethibiti kwamba amesema: “Atakayetenda katika jambo letu hili (Dini yetu) ambalo halikuweko basi itarudishwa.” na katika riwaayah: “Atakayetenda ‘amali isiyokuwa katika jambo letu hili basi itarudishwa.”
Wa biLLaahit-tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam
[Fatwa (5723 ) – Al-Lajnah Ad-Daaimah]