Mzigo Wa Mtu Hamjui Yuko Wapi Afanye Nini?

 

SWALI:

ASALAM ALYKUM SAMAHANI SANA MIMI NATAKA KUULIZA SUALI  MOJA MIMI NNA MZIGO WA MTU KANIWEKEA  NIKAKAA KWA MUDA MUDA MREFU HAJAJA KUCHUKUA MZIGO WAKE  NA  MIMI BAADAE YULE MTU NIMEMSAHAU NI NANI SASA ULE MZIGO NAWEZA KUUTUMIA,NIUTOE SADAKA ,NIUPELEKE MSIKITINI AU NIFANYE NINI? TAFADHALI NAOMBA JIBU.

 


JIBU:


Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuwa na mzigo wa mtu au pesa za mtu au chochote cha mtu ni haki yake huyo mtu, hivyo inapasa uirudishe haki hiyo kwa mwenyewe haraka iwezekanavyo kwa khofu ya kumfika mtu mauti akiwa bado anayo haki ya mtu.

Jambo la mwanzo ni kuwa ufanye kila jitihada ya kumtafuta mwenyewe kwa kujaribu kukumbuka sana na kuuliza huku na kule hadi umpate mwenyewe. Lakini pindi kama unvyosema kuwa umemsahau ni nani, au unamkumbuka lakini hujui yuko wapi, basi inakubidi ufanye mojawapo ya haya yafuatayo:

   1)     Kuuweka huo mzigo na lau atakuja mtu kuuudai mzigo huo umwamini na umpe ikiwa atataja aina ya huo mzigo. Na ni muhimu katika wasiya wako uandike na uwaachie warithi wako wajue kuwa unao mzigo wa mtu kadha na atakapotokea wakati ushafariki basi  apewe mwenyewe. Ikiwa hajapatikana kabisa Allaah سبحانه وتعالى Atakusamehe kwa kuwa umefanya juhudi zako zote za kumtafuta huyo mtu bila ya mafanikio. 

   2)     Ukipenda utoe huo mzigo kama sadaka, kwa nia ya thawabu zimfikie huyo mtu. Lakini ukubali sharti hii kwamba pindi atakapotokea mwenyewe umuelezee ulivyofanya, na ikiwa ataridhika sawa, na kama hakuridhika basi uwe tayari kumlipa wewe huo mzigo wake na kisha muombe Allaah Akutakabalie zile ulizotoa mwanzo kuwa ziwe ni sadaka yako.

 

                 Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share