Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?

 

Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalaam aleykum,

 

In shaa Allaah natuwai wote wazima na alhamdulilah kwa kuttuelimisha,mimi ni msichana wa miaka 23 naomba nasiha zenu In shaa Allaah mutaweza kunisaidia,mie siswali,na na[enda kuwa karibu na watu waovu,na najua kuwa nafaanya makosa nimejaribu kuacha lakini narudia tena, napenda kuangalia mambo yasio na maana, naomba munisaidie natamani kutubu kuwa kama wasichana walioshika dini, hijab, abaya yote navaa lakini matendo yangu yote kinyume na msichana wa kiislamu,naombeni munisaidie ndugu zangu wa kiislam, In shaa Allaah  Allaah atawalipa, shukran.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza tambua kuwa hiyo ni neema kwako kutoka kwa Rabb wako kwamba  Amekupa uongofu wa kutambua makosa yako kwa hiyo jambo la kwanza linalokupasa ni kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kukuzindua ukatambua kuwa uko makosani kabla ya adhabu Yake au mauti kukufika. Vile vile kupata uongofu katika umri kama huo pia ni jambo la kumshukuru Allaah kwani wengi huendelea na maasi na kuendelea kuchuma madhambi hadi wanafikia katika umri mkubwa. Yote hayo ni neema kutoka kwa Mola wako unapasa umshukuru sana kila wakati.

 

 

Pili jua kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawapenda sana waja Wake wanaofanya makosa kisha wakarudi Kwake kama Anavyosema:

اِنَّ اللّهَ یُحِبُّ التَّوَّابِینَ وَیُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِینَ

Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha.  [Al-Baqarah:222]

 

 

Kwa hiyo wewe ni miongoni mwa hao ambao (Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa)  Anawapenda, kwani wangapi wanafanya maovu lakini wamo tu na kuendelea na maovu hawashtuki wala hawajuti wala hawataki kurudisha nafsi zao katika Kumucha Allaah, lakini wewe ni kinyume.

 

 

Tafuta muda wa kusoma mada katika viungo vifuatavyo ambavyo viko katika tovuti hii ya Alhidaaya ili ujue jinsi ya kuomba Tawbah na pia utambue faida zake na uweze kurudisha nafsi na moyo wako katika hali ya kukuridhisha mwenyewe na kumridhisha Mola Wako ili uweze kufuzu duniani na Aakhirah In shaa Allaah.

 

 

Mahitajio Ya Nafsi

 

Tawbah

 

Nilipotoka Lakini Nimetubu Je Allaah Atapokea Du'aa Zangu? Vipi Kumkwepa Shaytwaan?

Nataka Kutubia...Lakini!!

 

Ana Tabia Za Maasi Anashindwa Kujizuia Nazo

 

 

Tatizo ulilonalo ni kwamba Shaytwaan amekuganda ili uendelee kufanya maovu na usibanduke. Na wewe inaonyesha umesalimu amri kwake na hutumii njia tulizofundishwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salaam) za kumfukuza na kumuepuka. Nazo ni kujikinga na Shaytwaan kama utakavyoona hapa chini. Kwa hiyo baada ya kuomba Tawbah kama utakavyojifunza katika mada hizo tulizokutajia, kisha fuata yafuatayo:

 

1.     Kaa na wudhuu kila mara.

2.   Jikinge na Shaytwaan kwa kusema ‘Audhu Billahi Minash-shaytwaanir-rajiym’ kila mara unapohisi kutaka kufanya jambo ovu.

3.    Tekeleza Swaalah Zako tano kwa wakati wake kwani Swaalah humuepusha mtu na maasi na maovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ 

Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. [Al-‘Ankabuut: 45]

4.   Mkumbuke sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kusoma Qur-aan kila siku japo ukurasa mmoja.

 

5.   Vile vile soma nyiradi za kila siku za asubuhi na jioni ambazo zimo humu katika site ya Alhidaaya katika kitabu cha Hiswnul-Muslim katika kiungo kifuatacho:

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

6.    Jitenge na marafiki waovu na ambatana na marafiki wema. Jaribu kuwakwepa marafiki zako waovu na anza kutafuta marafiki wacha Mungu wenye kupenda Dini yao. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesisitiza kuwa na marafiki wa Dini.

 

7.    Kumbuka mauti kila mara.

 

8.    Kumbuka pepo na kutarajia neema na raha zake.

 

9.   Wakati wako wa faragha soma vitabu vya dini upate elimu kwani utakapokuwa na elimu ya dini utajua maovu na utakuwa na khofu ya kujikinga nayo na utajua mema na kutarajia ujira mzuri.

 

10. Jitahidi sana kujiweka katika hali ya kuwa na kazi, usikae bure hata wakati mmoja, jishughulishe kila mara kwa kusoma, kusikiliza maiwadha, Qur-aan na hata kutazama video za mawaidha badala ya hizo chafu na utajikuta DAIMA huna muda wa kushawishika na upuuzi wowote na maovu.

 

11.    Kama kuna eneo linasomesha Darsa jaribu kujiungana kuhudhuria kila mara.

 

Umesema kwamba mavazi yako ni ya Kiislamu ila tu hufuati yanayompasa Muislamu kufanya, basi jitahidi kuendelea kujisitiri kwa mavazi ya hijaab ya kisheria na ujiepushe na maasi ili yalete maana na dhamiri khaswa yasije yakakukupeleka katika sifa ya unafiki. Allaah Akuepushe na sifa hiyo chafu.

 

 

Tunatumai kuwa In shaa Allaah baada ya kufuata maelezo na mafunzo yote hayo utaweza kujirekebisha na kujirudisha hali yako katika ucha wa Allaah ili upate kuiokoa nafsi yako na ghadhabu za Rabb wako upate Ridhaa Yake na uwe miongoni mwa waja Wake Alioridhika nao na upate kufuzu duniani na Aakhirah In shaa Allaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share