Imaam Ibn Baaz: Rajab: Kuhusisha Mwezi Wa Rajab Kwa ‘Ibaadah

Kuhusisha Mwezi Wa Rajab Kwa ‘Ibaadah

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Baadhi ya watu wanaufanya mwezi wa Rajab makhsusi kwa ‘ibaadah kama Swalaatur-Raghaaib na kukesha usiku wa tarehe 27; je, kuna asili yoyote katika Shariy’ah? Jazaakumu Allaahu khayraa.

 

 

JIBU:

 

Kuufanya mwezi wa Rajab kuwa ni makhSusi kwa Swalaatur-Raghaaib au kusherehekea usiku wa tarehe 27 wakidai kuwa ni usiku wa Israa na Mi’raaj yote hayo hayajuzu kwani ni bid’ah, hayana asili katika Shariy’ah.

 

Na wamehakiki hayo miongoni mwa Ahlul-‘Ilm ('Ulamaa) na tumeshaandika hayo mara kadhaa na tumebainisha wazi kwa watu kwamba Swalaatur-Raghaaib ni bid’ah!

 

Na hayo wanayofanya baadhi ya watu usiku wa Ijumaa katika Rajab na kadhaalika kusherehekea usiku wa tarehe 27 wakiitakidi  kuwa ni usiku wa Israa Wal-Mi’raaj yote hayo ni bid’ah hayana asili katika Shariy’ah.

 

Na usiku wa Israa na Mi’raaj haujulikani, na ingekuwa unajulikana pia isingejuzu kusherehekea kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusherehekea siku hiyo wala pia hawakusherehekea Makhalifa waongofu na Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Na ingekuwa ni Sunnah basi wangetutangulia kuitekeleza. Na khayr yote imo katika kuwafuata na kwenda katika Manhaj yao kama Anavyosema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah: 100]

 

Na imesihi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ

((Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini yetu) basi litarudishwa.)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

Na akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

مَنْ عَمِلَ عَمَلاً ليسَ عليه أمرُنا هذا فهو رَدٌ

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa katika jambo letu hili (Dini yetu) basi kitarudishwa.)) [Al-Bukhaariy] 

 

Na maana ya “kitarudishwa” ni: kitarudishwa kwa mwenyewe aliyekizusha. Na pia (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema katika khutbah zake:

 

أَمَّا بَعْدُ فَإِنَّ خَيْرَ الْحَدِيثِ كِتَابُ اللَّهِ وَخَيْرُ الْهُدَى هُدَى مُحَمَّدٍ وَشَرُّ الأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا وَكُلُّ بِدْعَةٍ ضَلاَلَةٌ

Ammaa ba’d: Hakika usimulizi bora kabisa ni Kitaab cha Allaah, na mwongozo mbora kabisa ni mwongozo wa Muhammad, na mambo maovu kabisa ni yenye kuzushwa, na kila bid’ah ni upotofu)) [Ameihadithia Muslim pia]

 

Basi, ni ni wajibu kwa Waislamu wote kufuata Sunnah na kuthibitika nayo na kuusiana nayo na kutahadharisha na bid’ah zote kwa matendo kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ  

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah: 2]

 

Na kauli Yake (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَالْعَصْرِ ﴿١﴾

Naapa kwa Al-‘Aswr (zama).

 

إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢﴾

Hakika mwana wa Aadam bila shaka yumo katika khasara.

 

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana haki na wakausiana subira.  [Al-‘Aswr 103]

 

 

Na kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

(الدِّينُ النَّصِيحَةُ)). قُلْنَا: لِمَنْ؟ قالَ: ((للهِ، ولِكِتَابِهِ، ولِرَسُولِهِ، ولِلأَئِمةِ المُسْلِمِينَ، وعامَّتِهِمْ)) رَوَاهُ مُسْلِمٌ    

((Dini ni nasiha))  Tukauliza: Kwa nani? Akasema: ((Kwa Allaah na Kitabu Chake, na Rasuli Wake, na kwa viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida)) [Muslim]

 

Ama kuhusu ‘Umrah, hakuna ubaya kuitekeleza katika mwezi wa Rajab kutokana na ilivyothibiti katika Swahiyhayn kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametekeleza ‘Umrah katika Rajab na Salaf walikuwa wakitekeleza ‘Umrah katika Rajab kama alivyotaja hivyo Al-Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) katika Kitabu chake: “Al-Latwaaif” kutoka kwa ‘Umar na mwanawe na ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhum)  na imepokelewa kutoka kwa Ibn Siriyn kwamba Salaf walikuwa wakifanya hivyo.

 

Na Allaah ni Mlinzi wa tawfiyq.

 

 

[Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Al-Imaam Ibn Baaz]

 

Share