232-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 232: وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
Al-Baqarah Aayah 232: Na mtakapowatalaki wanawake wakafikia muda wa...
وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ ۗ ذَٰلِكَ يُوعَظُ بِهِ مَن كَانَ مِنكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۗ ذَٰلِكُمْ أَزْكَىٰ لَكُمْ وَأَطْهَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢٣٢﴾
232. Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao; basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali) ikiwa wameridhiana baina yao kwa mujibu wa ada. Hayo anawaidhiwa kwayo yeyote miongoni mwenu mwenye kumwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo kwenu ni wema zaidi na safi kabisa. Na Allaah Anajua nanyi hamjui.
Sababun-Nuzuwl:
Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao; basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali)…”, imeteremka kuhusu Ma’aqil bin Yasaar (رضي الله عنه) ambaye alimuozesha dada yake kwa mwanaume kisha yule mwanaume akamtaliki, akakaa mpaka eda yake ikamalizika. Baada ya kumalizika eda, yule mwanaume akamchumbia tena huyo dada yake kwa Ma’aqil, lakini Ma’aqil alikataa. Ndipo hapo ikateremka Aayah hii. [Al-Bukhaariy kutoka kwa Ma’aqil (رضي الله عنه)]
Hadiyth kama ilivyothibiti:
عَنْ قَتَادَةَ، حَدَّثَنَا الْحَسَنُ، أَنَّ مَعْقِلَ بْنَ يَسَارٍ، كَانَتْ أُخْتُهُ تَحْتَ رَجُلٍ فَطَلَّقَهَا، ثُمَّ خَلَّى عَنْهَا حَتَّى انْقَضَتْ عِدَّتُهَا، ثُمَّ خَطَبَهَا فَحَمِيَ مَعْقِلٌ مِنَ ذَلِكَ أَنَفًا فَقَالَ: خَلَّى عَنْهَا وَهْوَ يَقْدِرُ عَلَيْهَا، ثُمَّ يَخْطُبُهَا فَحَالَ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا، فَأَنْزَلَ اللَّهُ: ((وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلاَ تَعْضُلُوهُنَّ)) إِلَى آخِرِ الآيَةِ، فَدَعَاهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَرَأَ عَلَيْهِ، فَتَرَكَ الْحَمِيَّةَ وَاسْتَقَادَ لأَمْرِ اللَّهِ.
Imepokelewa kutoka kwa Qataadah kwamba Al-Hasan ametuhadithia kuwa dada yake Ma’qil bin Yasaar aliolewa na mtu akamtaliki kisha akatengana naye mpaka muda wake wa eda ukamalizika. Kisha akarudi kutaka kumuoa lakini Ma’qil alikataa akasema kwa hamaki na kuringa: “Amemtenga hali angeliweza kukaa naye, sasa ndio anataka kumposa tena?” Basi Ma’qil akakataa kumuozesha tena hapo Allaah Akateremsha: “Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao; basi msiwazuie …” mpaka mwisho wa Aayah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuita akamsomea akaacha tena hamaki na maringo akaelemea amri ya Allaah. [Al-Bukhaariy – Kitaab Atw-Talaaq]