055-Aayah Na Mafunzo: Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) Hakufa Na Atateremka Duniani Awe Katika Alama Kubwa Za Qiyaamah
Aayah Na Mafunzo
Aal-‘Imraan
Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) Hakufa
Na Atateremka Duniani Awe Katika Alama Kubwa Za Qiyaamah
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۖ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿٥٥﴾
55. Pale Allaah Aliposema: Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi Nitakuchukua na Nitakupandisha Kwangu na Nitakutakasa na wale waliokufuru na Nitawafanya wale waliokufuata (kujisalimisha kwa Allaah) kuwa juu ya wale waliokufuru mpaka Siku ya Qiyaamah, kisha Kwangu ndio marejeo yenu Nitahukumu baina yenu katika yale mliyokuwa mkikhitilafiana”[Aal-'Imraan: 55]
Mafunzo:
Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnyanyua Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) kuelekea mbinguni akiwa hai, na wala hakuuliwa kabla ya hapo. Na atakuja kuteremka duniani zama za mwisho, na atamuua Masiyh Ad-Dajjaal, na atawaua nguruwe wote, na atavunja misalaba yote na ataondosha kodi, na hatokubali isipokuwa Uislamu, na atahukumu kwa shariy’ah ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). [Dalili katika Suwrat An-Nisaa (4:157-159)]
Aayah hii tukufu ni dalili ya wazi kwa wanaodai kwamba neno la مُتَوَفِّيكَ lina maana “kukufisha kikamilifu.” Neno hilo hilo Amelitaja Allaah (سبحانه وتعالى) katika (Al-An’aam (6:60), Az-Zumar (39:42):
وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُم بِالنَّهَارِ ثُمَّ يَبْعَثُكُمْ فِيهِ لِيُقْضَىٰ أَجَلٌ مُّسَمًّى ۖ
Naye Ndiye Anayekufisheni usiku (mnapolala) na Anajua yale yote mnayoyafanya mchana, kisha Anakufufueni humo ili utimizwe muda maalumu uliokadiriwa. [Al-An'aam (6:60)]
Na pia:
اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ
Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake; na zile zisizokufa katika usingizi wake, kisha Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzirudisha nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Hakika katika hayo bila shaka kuna ishara kwa watu wanaotafakari. [Az-Zumar (39:42)]
Hapo tunafahamu kwamba, mtu anapolala anachukuliwa au anafishwa usingizini na kurudishwa katika uhai kwa kuwa roho yake inachukuliwa na ndio inayojulikana kuwa ni Al-Mawt As-Sughraa (mauti madogo). Kwa dalili pia kutoka katika mafunzo ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika nyiradi za kulala na kuamka tuwe tunasema:
بِاسْـمِكَ اللّهُـمَّ أَموتُ وَأَحْـيا
Kwa Jina Lako Ee Allaah ninakufa na ninakuwa hai.
الحَمْـدُ لِلّهِ الّذي أَحْـيانا بَعْـدَ ما أَماتَـنا وَإليه النُّـشور
Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ametupa uhai baada ya kutufisha na Ni Kwake tu kufufuliwa.
Na Hadiyth zimethibitisha mojawapo ni:
Abuu Huraryah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, anakaribia kukuteremkieni Ibn Maryam hali ya kuwa hakimu muadilifu. Atavunja misalaba, ataua nguruwe, na hatopokea kodi, na mali zitazidi mpaka haikubali yoyote. Na itakuwa sijdah moja ni bora zaidi kuliko dunia nzima na vilivyomo ndani yake. Kisha Abuu Hurayrah akasema: Mkipenda someni:
وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾
“Na hakuna yeyote katika Watu wa Kitabu ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao.” [Al-Bukhaariy (3448), Aayah; Suwratun-Nisaa (4:159)].