'Aqiyqah Ni Lazima Au Sunnah?

SWALI

 

Asalam alykum,

Swali langu ni, ningependa kujua hukmu ya kutofanya Aqiqa kwa mtoto wako.

Wabillahi tawfiq.

 


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako hilo kuhusu Sunnah miongoni mwa Sunnah nyingi za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tutayaeleza mas-ala haya kwa njia ambayo kila mmoja wetu ataelewa kwa uwazi zaidi.

 

Mtume katika Hadiyth zake nyingi ametueleza yafuatayo ili tusiwe na utata wa aina yoyote ule. Miongoni mwazo ni:

Salmaan bin ‘Ammaar adh-Dhibbiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mvulana ana ‘Aqiyqah, mtawanyieni damu na mumuondolee uchafu” [Al-Bukhaariy].

 

Samurah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila mvulana ameekwa rehani kwa ‘Aqiyqah yake achinjiwe siku yake ya saba, apewe jina siku hiyo na anyolewe kichwa chake” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mvulana achinjiwe mbuzi wawili walio sawa, msichana achinjiwe mbuzi mmoja” [Ahmad na at-Tirmidhiy]. 

 

Wanachuoni wamekuwa na rai tofauti kuhusu mas-ala haya ya ‘‘Aqiyqah. Wamegawanyika katika rai tatu kila mmoja akitoa ushahidi kwa rai yake. nazo ni:

 

 

Kwanza:

Ni Sunnah na mustahabu (kinachopendeza). Wenye rai hiyo ni Imaam Maalik, watu wa Madiynah, Ash-Shaafi‘iy na watu wake, Imaam Ahmad bin Hanbal, Ishaaq, Abu Thawr na kundi kubwa la watu wa Fiqhi, elimu na wenye ijtihadi. Hoja zao ni Hadiyth zilizotangulia hapo juu. Wenye rai hii wamewarudi wanaosema kuwa ni wajibu kwa kauli zifuatazo:

 

  • Lau ingalikuwa ni wajibu basi uwajibu wake ungalikuwa ni jambo lenye kujulikana katika Dini. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angewabainishia watu wake kwa bayana ya wazi kabisa.
  • Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelifunganisha jambo hili la ‘Aqiyqah pamoja na mapenzi ya mwenye kutaka kulifanya, akasema: “Anayejaaliwa mtoto na akataka kumchinjia basi afanye”.
  • Kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulifanya   jambo hili, halionyeshi kuwa ni wajibu, bali linaonyesha kuwa ni mustahabu.

 

 

Pili:

Ni lazima na ni wajibu. Wenye rai hii ni Imaam Hasan al-Baswriy, Katyth bin Sa‘d na wengineo. Hoja yao ni Hadiyth ya Buraydah na Ishaaq bin Raahawayhi: “Hakika watu siku ya Qiyaamah watachunguzwa ‘Aqiyqah zao, kama watakavyochunguzwa Swalah zao”. Vile vile wanatumia Hadiyth ya Samurah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kila mvulana ameekwa rehani kwa ‘Aqiyqah yake.” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Yaani amezuiliwa kuwaombea wazazi wake mpaka wamfanyie ‘Aqiyqah, hivyo linatilia nguvu uwajibu wake.

 

 

Tatu:

Kukana uhalali wake. Wenye kauli hii ni Wanachuoni wa Kihanafi. Wao wanatumia Hadiyth ifuatayo kama dalili yao. ‘Amr bin Shu‘ayb amempokea babake kutoka kwa babu yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu ‘‘Aqiyqah, akasema: “Sipendi ‘Aqiyqah.” [Al-Bukhaariy].

 

Vile vile Hadiyth nyengine ya Abi Rafi‘i (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa al-Hasan bin ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhuma), mama yake, ambaye ni Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha) alitaka kumfanyia ‘Aqiyqah ya kondoo wawili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Usifanye ‘Aqiyqah, lakini mnyoe nywele zake, halafu utoe sadaka ya fedha yenye uzito wa nywele hizo”. Kisha akazaliwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhuma), akafanya mithili ya hivyo” [Ahmad]. Hata hivyo haijathibiti hii riwaya ya kutolea sadaja nywele.

 

Ama Hadiyth walizotegemea Wanachuoni wa Kihanafi kupinga uhalali wa ‘Aqiyqah wamejibiwa hivi: Hadiyth zilizotolewa dalili hazifai kuwa ni dalili za kupinga uhalali wa ‘Aqiyqah. Ama ile Hadiyth isemayo: “Sipendi ‘Aqiyqah”, mwelekeo wa Hadiyth na sababu yake inaonyesha kuwa ‘Aqiyqah ni Sunnah na mustahabu. Hiyo ni kuwa lafdhi yake iko hivi: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu ‘Aqiyqah, akasema: “Sipendi ‘Aqiyqah”, kama kwamba alilichukia jina lenyewe, yaani alichukia dhabihu kuitwa ‘Aqiyqah. Maswahaba wakamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Tunakuuliza kuhusu mmoja kati yetu anayejaaliwa mtoto”. Akasema: “Anayependa mmoja wenu kumchinjia mwanawe basi afanye, mvulana ni mbuzi wawili na msichana ni mbuzi mmoja”.

 

Ama dalili ya Hadiyth ya Abu Rafi‘i: “Usifanye ‘Aqiyqah, lakini mnyoe nywele zake…” haionyeshi ukaraha wa ‘Aqiyqah kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) binafsi alipenda kumbebea bintiye Faatwimah jukumu la ‘Aqiyqah ndipo akamwambia: “Usifanye ‘Aqiyqah..” Ni maarufu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafanyia ‘Aqiyqah al-Hasan na al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwa wingi wa Hadiyth kuhusu hilo. Baadhi yake ni:

  

Imepokewa kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimfanyia ‘Aqiyqah Hasan na Husayn kondoo wawili. [Jaabir bin Hazm].

 

 

Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimfanyia ‘Aqiyqah Al-Hasan na Al-Husayn siku ya saba” (Yahya bin Sa‘iyd).

 

Baada ya yote hayo tunafupisha kwa kusema: Kumfanyia mtoto ‘Aqiyqah ni Sunnah mustahabu kwa Wanachuoni wengi, Maimamu na kwa wenye elimu. Basi ni juu ya baba ajaaliwapo mtoto na akawa na uwezo wa kuifufua Sunnah hii ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) afanye hivyo ili apate fadhila na ujira utokao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa), na pia ili azidishe utangamano, mapenzi na mafungamano katika jamii.

 

Zaidi kuhusu mas-alah haya unaweza kusoma makala hii:

 

Utaratibu Wa 'Aqiyqah Katika Sunnah

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share