Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 3

 

Imeandikwa na www.alhidaaya.com

 

 

KUHAMA IRAQ

 

 

 

 

((وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ))

 

((Na Tukamwokoa yeye na Luutw Tukawapeleka kwenye nchi Tuliyoibariki kwa ajili ya walimwengu wote)) [Al-Anbiyaa:71]

 

Ibraahiym عليه السلام aliondoka Iraq pamoja na Luutw عليه السلام na wakaelekea kwanza katika mji unaoitwa 'Aur, kisha Haraan, kisha tena Falastina (Palestine).

 

 

 

ALIVYOMPATA HAAJAR

 

Akaelekea Misri   na wakati wote alipokuwa safarini  ilikuwa hima yake ni kuwaita watu katika Tawhiyd, kuwaongoza katika haki na katika mambo mema. Alipokuwa anaelekea Misri alipita mji wa dhalimu mmoja akapiga kambi hapo. Matukio yote hapo yameelezwa katika Hadiyth Sahiyh ifuatayo:

 

  عن أبي هريرة رضي الله عنه؛ أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم، عليه السلام، لم يكذب غير ثلاث: ثنتين في ذات الله ، قوله: ( بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَذَا ) وقوله (إِنِّي سَقِيمٌ ) قال: "وبينا هو يسير في أرض جبار من الجبابرة ومعه  سارة، إذ نـزل منـزلا فأتى الجبار رجل، فقال: إنه قد نـزل بأرضك رجل معه امرأة أحسن الناس، فأرسل إليه فجاء، فقال: ما هذه المرأة منك؟ قال: هي أختي. قال: فاذهب فأرسل بها إليّ، فانطلق إلى سارة فقال: إن هذا الجبار سألني عنك فأخبرته أنك أختي فلا تكذبيني عنده، فإنك أختي في كتاب الله، وأنه ليس في الأرض مسلم غيري وغيرك، فانطلق بها إبراهيم ثم قام يصلي. فلما أن دخلت عليه فرآها أهوى إليها، فتناولها، فأخذ أخذًا شديدًا، فقال: ادعي الله لي ولا أضرك، فدعت له فأرسل، فأهوى إليها، فتناولها فأخذ بمثلها أو أشد. ففعل ذلك الثالثة فأخذ، [فذكر] مثل المرتين الأوليين فقال ادعي الله فلا أضرك. فدعت، له فأرسل، ثم دعا أدنى حجابه، فقال: إنك لم تأتني بإنسان، وإنما أتيتني بشيطان، أخرجها وأعطها هاجر، فأخرجت وأعطيت هاجر، فأقبلت، فلما أحس إبراهيم بمجيئها انفتل من صلاته، قال: مَهْيَم؟ قالت: كفى الله كيد الكافر الفاجر، وأخدمني هاجر)

 

  قال محمد بن سيرين وكان: أبو هريرة إذا حدث بهذا الحديث قال: فتلك أمكم يا بني ماء السماء

 

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  Ibraahiym عليه السلام hakuongopa ila mara tatu tu; mara mbili kwa ajili ya Allaah aliposema, ((Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao)) na aliposema, ((Hakika mimi ni mgonjwa!)). Na alipokuwa akisafiri katika mji wa dhalimu mmoja na Sarah alikuwa naye. Alipopiga kambi, mtu mmoja alikwenda kwa dhalimu na kumwambia, "Kuna mtu amepiga kambi katika ardhi yako na anaye mwanamke mzuri kupita wote". Dhalimu akamuita Ibraahiym عليه السلام kwake, na akamuuliza, "Nini uhusiano wa mwanamke huyu na wewe?". Akasema, "Yeye ni dada yangu". Dhalimu akasema, "Nenda kamlete kwangu". Ibraahiym عليه السلام akaenda kwa Sarah na akasema, "Dhalimu huyu ameniuliza kuhusu wewe, na nimemwambia kwamba wewe ni dada yangu, kwa hiyo usimfanye akajua kwamba nimeongopa, kwani hakika ni dada yangu kufuatana na kitabu cha Allaah, na hakuna Waislamu katika ardhi hii ila mimi na wewe". Ibraahiym عليه السلام akampeleka (Sarah) kwake, kisha akasimama na kuswali. Alipoingia kwa dhalimu na (dhalimu) alipomuona (Sarah), akataka kumshika kwa matamanio, lakini akagandishiwa (mkono) Akasema, "Niombee kwa Allaah na sitokudhuru". Sarah akamuombea, na akaachiliwa. Kisha akamfikia kwa matamanio,  lakini akapatwa tena (kuganda mkono) kama mwanzo au zaidi. Ikaendelea hivyo mara tatu, na kila mara alisema kama alivyosema mara ya mwanzo. Kisha akamwita mlinzi wake wa karibu naye kabisa na akasema, "Hukuniletea binaadamu bali umenilitea shaytwaan! Muondoshe na mpe Haajar". Akaondoshwa (Sarah) na kupewa Haajar, akarudi. Ibraahiym عليه السلام alipotambua kuwa (Sarah) amerudi, alimaliza kuswali na kugeuka akasema, "Imekuwaje?". Akasema, "Allaah Ametosheleza njama za kafiri dhalimu, na amenipa Haajar kama mtumwa")) [Al Bukhaariy na Muslim].

 

Muhammad bin Siriyn amesema, "Abu Huraryah amesimulia Hadiyth hii  na akasema: "Huyu ni mama yenu enyi wana wa maji ya mbinguni" (yaani Waarabu kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام, mwana wa Haajar ambaye ndiye aliyesababisha maji ya Zamzam). [Fat-h Al-Baariy 6:447, Muslim 4:1840]

 

Mke wa Ibraahiym عليه السلام Sarah, alikuwa tasa. Na Ibraahiym عليه السلام alikuwa anazeeka na nywele zake zikatawaliwa na mvi baada ya kuita watu miaka mingi katika dini ya Allaah. Sarah akafikiria kwamba yeye na Ibraahiym عليه السلام wako katika upweke kwa vile hawakupata mtoto. Kwa hiyo akampa mumewe mtumwa wake Haajar amuoe.  Haajar akamzaa Ismaa'iyl  عليه السلام ambaye ndiye mtoto wa mwanzo wa Ibraahiym عليه السلام.

 

Siku zikapita na Ibraahiym عليه السلام akawa na furaha ya kupata mtoto, lakini Sarah akawa na wivu sasa na Haajar, ingawa yeye mwenyewe ndiye aliyempa Ibraahiym عليه السلام Haajar amuoe. Wivu huo ukamfanya Haajar awe anajificha ili Sarah asimuone anapokwenda kwa mumewe. Akawa ni mwanamke wa kwanza kufunga mkanda kuficha alama zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ndefu kutoka kwa  Al-Bukhaariy iliyopokelewa na Ibn 'Abbaas kwamba "Haajar ni mwanamke wa mwanzo kutumia mkanda".

 

Makusudio hapo ni mkanda kiunoni kuzuia nguo yake ndefu inayoburuza ardhini isiache alama apitapo (ikaja ikajulikana na Sarah kuwa kapita). Inasemekana kuwa wakati huo wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu zinazoburuza. Na hii inaonyesha jinsi stara ilivyokuwa kwa wanawake tangu wakati huo.

 

Pia katika masimulizi kwenye Sahiyh Al Bukhaariy anasema, ''Wakati Nabii Ibraahiym عليه السلام alipomuoa Haajar na akamzalia Ismaa'iyl عليه السلام, mkewe wa mwanzo, Sarah, akapata wivu na akaapa kuwa atamkata mwili wake vipande vitatu, hivyo Haajar akajifunga mkanda kiunoni mwake na kukimbia huku akiburuza vazi lake nyuma yake ili kufuta alama za nyayo zake ili Sarah asiweze kujua alipoelekea. (Al Bukhaariy - Kitabu cha Visa Vya Mitume, hadiyth namba 3364)

 

Na Allaah Anajua zaidi. 

 

 

 

SAFARI YA KWENDA MAKKAH

 

Siku moja Ibraahiym عليه السلام aliamka na kumwambia mke wake Haajar ajitayarishe kwa safari ndefu. Baada ya siku chache, Ibraahiym عليه السلام akaanza safari yake pamoja na mkewe na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام ambaye alikuwa bado ananyonya.

 

Ibraahiym عليه السلام akatembea na kupitia ardhi zilizolimwa, majangwa na milima hadi akafika katika jangwa la kisiwa cha Uarabu (Arabian Peninsula) na akafika katika bonde lisilolimwa ambalo halikuwa na miti wala matunda wala chakula wala maji. Bonde hilo halikuwa na athari yoyote ya maisha. Baada ya kumsaidia mkewe kuteremka kipando cha safari, akawaacha hapo wakiwa na chakula na maji kidogo tu ya kuwatosheleza kama siku mbili tu.

 

Aligeuka nyuma na kuondoka. Nyuma yake mkewe akamkimbilia na kumuuliza: "Unakwenda wapi Ibraahiym عليه السلام na kutuacha sisi katika bonde hili tupu?".Ibraahiym عليه السلام hakumjibu kitu bali aliendelea kuondoka. Haajar alirudia kumuuliza tena, lakini alinyamaza kimya bila ya kumjibu. Mwishowe alifahamu kuwa hafanyi hivyo kwa matamanio au amri yake, na akatambua kuwa Allaah سبحانه وتعالى Amemuamrisha kufanya hivyo. Akamuuliza: "Je, Allaah Amekuamrisha ufanye hivyo?". Akamjibu: "Ndio". Haajar akasema: "Basi hatutapotea ikiwa Allaah Aliyekuamrisha Atakuwa nasi". Ibraahiym عليه السلام akaondoka na alipokuwa mbali kiasi ya kutowaona akaomba:

 

((رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ)

 

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapate kushukuru)) [Ibraahiym :37]

 

 

 

KUPATIKANA ZAMZAM

 

Ibraahiym عليه السلام akamuacha mkewe na mwanawe katika jangwa na akarudi alikotoka kuendelea kufanya da'wah ya kuwaita watu katika katika Tawhiyd. Haajar akabakia kumlea mwanawe hapo alipoachwa. Chakula kiliwaishia, maziwa yakamkauka, jua lilikua kali mno, maji waliyokuwa nayo yalikwisha na kiu kikawashika, hali ikawa mbaya ya njaa ya kiu kikubwa.

 

Ismaa'iyl عليه السلام akaanza kulia kwa kiu, mama yake akamuacha kwenda kutafuta maji. Akatembea kwa haraka hadi akafikia kilima cha Swafaa. Akapanda kilima na kuangaza kama ataona kisima au aone kama kuna msafara au chochote ili apate maji, lakini hakuona lolote.  Akateremka kilima na akawa anahangaika kwenda baina ya kilima cha Swafaa na kilima cha Marwah akipanda vilima vyote kila anapofikia kuangaza kama ataona lolote, lakini hakufanikiwa, na huku mwanawe anagaragara na kulia kwa kiu. Akawa anatembea na huku akikimbia mara nyingine baina ya Swafaa na Marwah kwa mara saba. Na ndio maana Mahujaji huwa wanatekeleza kitendo hiki kitufu cha ibada wanapokwenda Hajj au 'Umrah.

 

Hakika hii taadhima kubwa Allaah سبحانه وتعالى Aliyomjaalia Haajar, na ni fakhari kwa wanawake wote wa Kiislamu kuwa kitendo hiki cha Haajar kimekuwa ni kitendo cha ibada tukufu na kinatekelezwa na milioni ya watu hadi siku ya Qiyaamah.

 

Alipofika Marwah kwa mara ya saba alisikia sauti, mara akamuona Malaika anachimba ardhini kwa mbawa zake na mara maji yakamwagika kwa nguvu kabisa, akawa anayateka na kuyazuia yasimwagike zaidi. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((يرحم الله أم إسماعيل لو تركت زمزم))  أو قال: ((لو لم تغرف من الماء لكانت زمزم عينًا معينًا)) البخاري

 

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  (Allaah Amrehemu mama yake Ismaa'iyl عليه السلام  angeliacha (maji ya zamzam)) (yamwagike bila ya kuyazuia) au kasema ((asingelichota kutoka katika maji hayo, zamzam ingelikuwa chemchemu inayoendelea kumwagika katika ardhi)) [Al-Bukhaariy]

 

Akanywa maji na kumnywesha mwanawe. Kulikuwa na misafara ya watu kutoka Yemen na walipoona kuna ndege wanazunguka wakatambua kuwa ni sehemu yenye maji.  Walikuwa watu wa kabila la Jurhum kutoka Yemen wakaja kuishi hapo. Wakamuuliza Haajar: "Je, unaturuhusu tuishi hapa?". Akajibu: "Ndio lakini hamtakua na haki kumiliki maji haya ya Zamzam". Wakakubali na Haajar akaridhika na akafurahi kupata watu kuishi nao. Wakaleta familia zao na wakazidi kuwa wengi hapo.

 

 

 

MTIHANI MKUBWA ALIOPEWA IBRAAHIYM عليه السلام  

 

WA KUMCHINJA  ISMAAI'YL عليه السلام

 

Ismaa'iyl عليه السلام akakua na baba yake Ibraahiym عليه السلام akawa anamtembelea mara kwa mara, kisha Allaah سبحانه وتعالى Akataka kumpa mtihani mkubwa mwingine Ibraahiym عليه السلام kutokana na mapenzi ya mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام.  Allaah سبحانه وتعالى Anatuelezea mtihani huu katika aya zifuatazo:

 

 وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَى رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿99﴾ رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿100﴾ فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿101﴾ فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاء اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿102﴾ فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿103﴾ وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿104﴾ قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿105﴾ إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ ﴿106﴾ وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿107﴾ وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿108﴾ سَلَامٌ عَلَى إِبْرَاهِيمَ ﴿109﴾ كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿110﴾ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿111﴾                   

 

((Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu ; Yeye Ataniongoa)) 

((Ewe Mola wangu ! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema))

((Basi Tukambashiria mwana aliye mpole)) 

((Basi alipofika makamo ya kwenda na kurudi pamoja   naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, In sha Allaah, katika wanaosubiri))

((Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya  kipaji)) 

((Tulimwita: Ewe Ibraahiym!)) 

((Umekwishaitimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo Tunavyowalipa wanaotenda mema)

((Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri)) 

((Basi Tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu)) 

((Na Tukamwachia (sifa njema) kwa watu waliokuja baadaye)) 

((Iwe salama kwa Ibraahiym!)) 

((Hivi ndivyo tunavyowalipa wanaofanya mema)) 

((Hakika yeye ni katika waja wetu walioamini)) 

[As-Swaaffaat: 99-111]

 

Hakika huu ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa Ibraahiym عليه السلام wa kuoteshwa amchinje mwanawe ambaye ndiye huyo huyo mmoja tu aliyempenda sana na ambaye amempata baada ya miaka mingi akiwa ameshakuwa mzee na baada ya kukata tamaa kabisa.  

 

Ibraahiym عليه السلام anatupa fundisho ya malezi mazuri baina ya baba na mtoto, kwani angelitaka maadamu ni amri ya kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى angelimchinja tu kama alivyoamrishwa katika ndoto, kwani ndoto za Manabii ni wahyi, lakini ametuonyesha adabu njema aliyomfanyia mwanawe kwa kutaka shauri aliposema:

 

 (( يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى))

 

((Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje?)) [As-Swaafaat: 102]

 

Na mtoto naye anatupa mafunzo kwa kuheshimu wito wa baba yake ambao anajua haukuja kwa matamanio yake bali ni kutimiza amri ya Allaah سبحانه وتعالى , amri ambayo baba yake alijua ni muhimu na ghali kuliko mapenzi, huruma kwa mwanawe. Naye Ismaa'iyl alimjibu:

 

   ((قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاء اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ))

 

((Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, In shaa Allaah, katika wanaosubiri. [As-Swaaffaat:102]

 

Ibraahiym عليه السلام alitambua kuwa mwanawe mwenyewe anashindana naye katika mapenzi ya Allaah سبحانه وتعالى  kwani hakujali kuchinjwa bali aliona kutekeleza amri ya Mola wake ni muhimu kuliko maisha yake.

 

Hatujui ilikuwaje hisia ya Ibraahiym عليه السلام alipojisalimisha mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام achinjwe, bila ya shaka ilikuwa ni huruma ya hali ya juu hata akamlaza kifudifudi ili asimuone wakati anapomchinja. Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

 

((فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ))

 

((Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji ))

 

[As-Swaaffaat::103]

 

Maana kwamba wote wawili walipotamka Shahada na kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى kwani alikuwa Ibraahiym عليه السلام anakaribia kumchinja Ismaa'iyl عليه السلام, hivyo ingelikuwa ni mauti yake.  Au 'walipojisalimisha' ina maana kwamba walipofuata amri ya Allaah سبحانه وتعالى, Ibraahiym عليه السلام alimtii  Mola wake na Ismaa'iyl عليه السلام pia alimtii baba yake.  Hii ni rai ya Mujaahid, Ikrimah, Qataadah, As-Sudi na Ibn Is-haaq na wengineo.[At-Twabariy 21:77]

 

Maana ya:

 

((وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ))

 

 ((na akamlaza juu ya kipaji))

 

ni kwamba, alimuelekeza uso wake kifudifudi ili amchinje kutoka kwa nyuma ili iwe wepesi kwake kufanya hivyo (asipate kuuona uso wake akashikwa na huruma na kushindwa kutekeleza amri ya Mola wake).  Ibn 'Abbaas, Mujaahid, Sa'iyd bin Jubayr, Adhw-Dhwahaak na Qataadah wamesema ina maana kwamba, "Alimgeuza kifudifudi". [At-Twabariy 21:77,78]

 

 

 

SHAYTWAAN ANAMSHAWISHI IBRAAHIYM  ASIMCHINJE ISMAA'IYL, NA KUPATIKANA SUNNAH YA KURUSHA VIJIWE KWENYE HAJJ

 

Imaam Ahmad amerekodi kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Wakati alipokuwa anataka kutekeleza Ibraahiym عليه السلام amri ya kumchinja 'Ismaa'iyl عليه السلام, shaytwaan alimjia katika Mas'aa na akakimbia naye, lakini Ibraahiym عليه السلام alifika mwanzo. Kisha Jibriyl عليه السلام  akamchukua katika Jamratul-'Aqabah na shaytwaan akamjia tena huko, kwa hiyo akampiga vijiwe saba mpaka akatokomea. Kisha akamjia tena katika Jamratul-Wustwaa, akampiga vijiwe saba. Kisha akamlaza kifudifudi. Ismaa'iyl عليه السلام alikuwa amevaa shati jeupe na akasema: "Ewe baba yangu, sina nguo yoyote ambayo nitakafiniwa, kwa hiyo nivue ili iwe nikafiniwe nayo. Alianza kuivua ndipo alipoitwa nyuma:

 

((وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ))       ((قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا))

 

((Tulimwita: Ewe Ibraahiym!)) 

((Umekwisha itimiliza ndoto)) [As-Swaaffaat:104-105]

 

Ibraahiym عليه السلام aligeuka na akamuona kondoo mweupe mzuri mwenye pembe.

 

Ibn 'Abbaas kasema: "Tulikuwa tukitafuta aina kama ya huyo kondoo" (yaani wakati wa kuchinja katika 'Iydul-Adhwhaa)  [Ahmad:1:297]

 

As-Suddiy na wengineo wamesema kwamba alikipitisha kisu shingoni mwa Ismaa'iyl عليه السلام lakini hakikumkata kwa sababu aliwekewa bamba la shaba.

 

Na ndipo Ibraahiym عليه السلام alipoitwa:

 

((قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا))

 

((Umekwisha itimiliza ndoto)) [As-Swaaffaat:105]

 

[At-Twabariy 21:74]

 

Ibn 'Abbaas amesema kuwa: "Kondoo huyo alikuzwa Peponi kwa muda wa miaka arubaini".[At-Twabariy 21:90]

 

Kitendo hiki cha kuchinja ndicho kinachofanyika katika taratibu za Hajj, kufuata Sunnah ya baba yetu Ibraahiym عليه السلام.

 

 

 

UTHIBITISHO KWAMBA ALIYETAKA KUCHINJWA NI IS'MAA'IYL NA SI IS-HAAQ KAMA WANAVYODAI MAYAHUDI NA MANASWARA

 

 

Imaam Ahmad amerekodi kwamba Swafiyyah bin Shaybah alisema: "Mwanamke kutoka Bani Sulaym ambaye alikuwa mkunga (midwife) wa wengi katika jamii yetu, kaniambia kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimtuma 'Uthmaan bin Talhah رضي الله عنه  akazifunike pembe katika Ka'abah ili zisiwashawishi watu wanaposwali: Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

 

))إني كنتُ رأيت قرني الكبش، حين دخلت البيت، فنسيت أن آمرك أن تخمرهما، فَخَمَّرْهما، فإنه لا ينبغي أن يكون في البيت شيء يشغل المصلي". قال سفيان: لم يزل قرنا الكبش معلقين في البيت حتى احترق البيت، فاحترقا)) أحمد.

 

((Niliziona pembe za kondoo nilipoingia katika Nyumba (yaani Kaabah) nikasahau kukuambia uzifunike, zifunike kwani kusiweko na kitu katika nyumba (Ka'abah) cha kuwashawishi watu wanaofanya ibada)). 

 

 [Ahmad 4:68]

 

 

 

Wasimulizi waliosimulia kuhusu pembe hizo za kondoo:.   

 

 -Sufyan kasema: "Pembe za kondoo zilibakia zikining'inia katika Nyumba (Ka'abah) hadi zilipoungua wakati Nyumba ilipoungua".

 

-Sa'iyd bin Jubayr, 'Aamir Ash-Sha'abiy, Yuusuf bin Mihraan, Mujaahid, 'Atwaa' na wengineo wameripoti kutoka Ibn 'Abbaas kwamba alikuwa ni 'Ismaa'iyl عليه السلام.

 

-Ibn Jariyr amesimulia kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Aliyefidiwa alikuwa ni Ismaa'iyl عليه السلام. Mayahudi wamedai kuwa ni Is-haaq, lakini Mayahudi wameongopa". [At-Twabariy 21:83]

 

-Ibn Is-haaq amesema, "Nimemsikia Muhammad bin Ka'ab Al-Quraazi anasema, "Ambaye Allaah سبحانه وتعالى Ameamuamrisha Ibraahiym عليه السلام kumchinja miongoni mwa wanawe wawili alikuwa ni Ismaa'iyl عليه السلام.  Tunapata dalili hii kutoka kitabu cha Allaah سبحانه وتعالى kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Anapomalizia kisa cha mmoja wa wana wawili wa Ibraahiym عليه السلام ambaye alitakiwa kuchinjwa Amesema:

 

((وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ))

 

((Na Tukambashiria kuzaliwa Is-haaq, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema)). [As-Swaaffaat:112]

 

Vile vile,

 

((فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَقَ وَمِن وَرَاء إِسْحَقَ يَعْقُوبَ))

 

((Basi Tukambashiria (kuzaliwa) Is-haaq, na baada ya Is-haaq Ya'aquwb)) [Huud:71]

 

Allaah سبحانه وتعالى Amemtaja mtoto na mwanawe, lakini Asingelimuamrisha kumchinja Is-haaq wakati Aliahidi kuwa mwanawe (Is-haaq) atazaa mtoto. Kwa hiyo  ni dhahiri kuwa yule aliyeamrishwa amchinje ni Ismaa'iyl عليه السلام". [At-Twabariy 21:84].

 

 Hadiyth nyingi zimenukuliwa kuhusu mas-ala haya [Tafiiyr Ibn Kathiyr 8:277-279]

 

 

 

ZIARA YA IBRAHIYM عليه السلام  KWA WAKE ZAKE ISMAA'IYL

 

[Maelezo haya yamenukuliwa kutoka Hadiyth ndefu ya Ibn 'Abbaas iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy]

 

 Baada ya kufa mama yake Ismaa'iyl عليه السلام, Ibraahiym alikuja kumtembelea Ismaa'iyl عليه السلام nyumbani kwake (ambaye alikuwa amekwishaoa). Alipofika hakumkuta Ismaa'iyl عليه السلام bali alimkuta mkewe peke yake. Akamuuliza: "Yuko wapi Ismaa'iyl?". Akajibu: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym عليه السلام akamuuliza kuhusu hali ya maisha yao, akajibu: "Tunaishi katika shida, dhiki na karaha". Akamwambia: "Atakaporudi mumeo mpe salam zangu na mwambie abadilishe kizingiti chake".

 

Aliporudi Ismaa'iyl عليه السلام alihisi hali sio ya kawaida yaani kama kumetokea kitu, akamuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote kukutembelea?" Akajibu: "Ndio, bwana mmoja mtu mzima mwenye sifa kadha na kadha amekuja na ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akaniuliza kuhusu hali ya maisha, nikamuambia kuwa tunaishi katika shida, dhiki na umasikini". Ismaa'iyl عليه السلام hapo akamuuliza: "Je, amekupa maagizo yangu yoyote?".  Akajibu: "Ndio, amenipa salam zako, kisha amesema nikuambie kuwa ubadilishe kizingiti chako". Ismaa'iyl عليه السلام akasema: "Huyo ni baba yangu, na ameniamrisha nikupe talaka, basi rudi kwenu". Ismaa'iyl عليه السلام akampa talaka, kisha akaoa mwanamke mwingine miongoni mwao (yaani kutoka kabila la Jurhumu).

 

Mara ya pili alipokuja Ibraahiym عليه السلام kumtembelea Ismaa'iyl عليه السلام alimkuta mke wake Ismaa'iyl عليه السلام wa pili, alipoumuuliza kuhusu Ismaa'iyl عليه السلام alisema: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym عليه السلام akamuuliza kuhusu maisha yao, akajibu: "Tuko katika neema na tumebahatika (yaani tuna kila kitu cha kututosheleza)". Akamshukuru Allaah سبحانه وتعالى. Ibraahiym عليه السلام akamuuliza: "Aina gani ya chakula mnakula?". Akasema: "Nyama". Akasema: "Mnakunywa nini?", Akasema: "Maji". Akasema: "Ya Allaah Wabarikie nyama yao na maji yao".  (Mkewe amesema hivyo ingawa hali yao ilikuwa ni ya shida).

 

Ibraahiym عليه السلام akamwambia mke wa Ismaa'iyl عليه السلام: "Atakaporudi mumeo mpe salam zangu na mwambie ashikilie kizingiti chake". Aliporudi Ismaa'iyl عليه السلام alimuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote?". Akajibu: "Ndio, amekuja bwana mmoja mtu mzima mwenye sura nzuri". Akamsifia kisha akaendelea: "Ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akauliza kuhusu hali ya maisha yetu, nikamuambia kuwa tunaishi katika hali nzuri". Ismaa'iyl عليه السلام akamuuliza: "Je, alikupa nasiha yoyote?". Akajibu: "Ndio, amekupa salaam zake kisha anakuamrisha ushikilie kizingiti chako".

 

Kwa maneno haya, Ismaa'iyl عليه السلام akasema: "Huyo alikuwa ni baba yangu na  wewe ndio kizingiti, na ameniamrisha nibakie na wewe".

 

  

 

Kisa kinaendelea ...../4

 

 

Share