Skip navigation.
Home kabah

Umuhimu Wa Kuwa Na Rafiki Mwema

 

 

Ummu 'Ali

 

Bismillahi-Rrahmani-Rrahim. Alhamdulillahi Rabbil Aalamin, waswalatu wassalam alaa Rasulillahi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Amma baad. Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatu.

Ningependa kuwahusia enyi ndugu zangu kuhusu umuhimu wa kuwa na marafiki wema, kwa vile ni kawaida kwa  sisi binaadamu kuhitaji marafiki. Kuchagua rafiki mzuri ni lazima kwa ajili ya kuhifadhi deeni yetu .Waislamu wakiwa na tabia nzuri na wenye kufuata njia ya Allaah, basi uislamu utakuwa na nguvu, ni hivyo ndivyo inavyotakikana. Kufanya urafiki na watu wema wenye tabia nzuri, ni mojawapo ya njia ya kutufanya sisi  kuwa kwenye njia iliyonyooka.

Mtume Muhammad ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) amesema: "Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unaemfanya rafiki.( AbooDawood/Tirmidhi)

Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu  matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwasababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu. Kutangamana na marafiki ambao wanakwenda kinyume na njia ya Allaah Subhaanahu Wata'ala, inaweza ikatubadilisha tabia, fikra na mwenendo wetu. Lakini vile vile inatupasa kuwatendea wema.

Katika Hadith, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Mfano wa rafiki mwema na rafiki mbaya ni kama ule wa muuzaji wa misk na mhunzi (blacksmith). Basi kwa muuzaji wa misk, imma atakunusisha, au utanunua kwake ama angalau utafurahia harufu nzuri kwake. Na kwa yule mhunzi, imma atakuchomea nguo au utapata harufu mbaya kutoka kwake.”(Bukhari/Muslim)

Katika tafsiri ya Hadith hii, Imam An-Nawawy alisema; Mtume ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alilinganisha rafiki mzuri na muuzaji misk kwasababu, kwa rafiki mzuri mwenye tabia ya upole, na elimu, utapata faida kwake. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza kukaa na wale wenye kufanya maovu.

Mwanachuoni mmoja asema: “Kuweka uhusiano mzuri na watu wema waswalihina, matokeo yake ni kupata elimu iliyo na faida, tabia nzuri, na matendo mema, ambapo kuweka uhusiano na waliopotoka, huzuia hayo mema yote.”

Allaah Anasema katika Qur'an:  

27.   Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti   ningeli shika njia pamoja na Mtume!

28.    Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!

29.    Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na   kweli Shetani ni khaini kwa mwanaadamu

 (Al Furqan) [25:27-29]

Allaah, tena anasema:

67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachaMungu. (Azzukhruf43:67]

Ibn Katheer ameeleza kuhusu aya hii, kisa ambacho kimepokewa na Ali ibn Abi Talib(Radhiya Allaahu ‘anhu)kuwa, urafiki wowote ambao sio kwa ajili ya Allaah, hugeuzwa ukawa wa uadui ispokuwa chochote kilichokuwemo kwa ajili ya Allaah Subhaanahu wata’la 

Watu wawili ambao ni marafiki kwa ajili ya Allaah Subhaanahu wata’la ; mmoja wao akifariki, hupewa bishara nzuri kuwa amejaaliwa pepo, basi humkumbuka rafiki yake na kumuombea dua akisema: “ Ewe Mola wangu, rafiki yangu alikuwa akiniamrisha Kukutii na kumtii Mtume Wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akiniamrisha kufanya mema na alikuwa akinikataza kufanya maovu. Na aliniambia kuwa nitakutana na Wewe. Ewe Mola wangu, basi usimuache kupotea baada ya mimi kuondoka, na muoneshe haya ulionionesha mimi, Na Uwe Radhi nae kama Ulivyoridhika na mimi.” Basi ataambiwa: “Laiti ungelijua aliyoandaliwa rafiki yako, basi ungefurahi sana na ungelia kidogo.” Kisha rafiki yake akifariki, roho zao zinakusanywa, na wote wana ambiwa watoe maoni kuhusu killa mmoja. Basi killa mmoja anamwambia mwenzake: “Ulikuwa ndugu mzuri kabisa, mwenzangu mzuri kabisa, na rafiki mzuri kabisa.” Na mmoja wa wale marafiki wawili wasioamini anapokufa na kupewa bishara za moto wa Jahannam, humkumbuka rafiki yake na kusema: “ Ewe Mola wangu, rafiki yangu alikuwa akiniamrisha nikuasi na nimuasi Mtume Wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na likuwa akiniamrisha kufanya maovu na kunikataza kufanya mema, na akaniambia sitokutana na wewe. Ewe Mola wangu, usimuongoze baada ya mimi kufa, na Muoneshe haya ulonionesha mimi, na Usiwe Radhi nae kama ambavyo Huko Radhi na mimi.” Alafu yule rafiki mwengine akifa na nyoyo zao zikikusanywa, wote wawili wana ambiwa watoe maoni kuhusu killa mmoja. Basi killa mmoja anamwambia mwenzake: “Ulikuwa ndugu mbaya kabisa, mwenzngu mbaya kabisa, na rafiki mbaya kabisa.” 

Kwahivyo ni katika urafiki mwema ndio Allaah SUBHAANAHU WATA’ALA Humuokoa aliyepotea  na kumuongoza aliyekosa . Faida ya kutangamana na marafiki wema ni kubwa kupita kiasi na inshaAllaah itakuwa wazi zaidi kwetu siku ya kiama, kama tulivyoona kwenye aya na visa vilivyopita.

Na katika hadith nyengine pia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamrisha  kutangamana na mu'min peke yake. (Aboo Dawood/Tirmidhi) Na pia kuwa mtu atakuwa na wale awapendao   (Bukhari/Muslim).

Kwa hivyo tukiwapenda na kuwaandama waliopotoka, lazima tujiogopee mwisho wetu.

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu)alisema: "Tangamana na watu wema wapole, utakuwa mmoja wao; na epukana na watu waovu usalimike na maovu yao."

Mu’min ni kioo cha ndugu yake, akiona makosa ya mu’min mwenzake inampasa, amueleze kwa uzuri na kumsaidia kurekebisha kosa hilo.

Ibn Hazm amesema: “Yeyote anaekukosoa, anajali urafiki wako. Na yeyote ambae anachukulia wepesi makosa yako, basi hajali urafiki wako.”

Kwa hivyo ikiwa tunafikiria kuhusu mwisho wetu, lazima tutambue kuwa,wale ambao wanatuepusha na Kumkumbuka Allaah Subhaanahu Wata'ala na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wale ambao hawatukumbushi swala zetu na wala hawatupi mawaidha mazuri kuhusu dini yetu, basi wao kweli ni maadui sio marafiki zetu. 

Allaah Subhanaahu Wata’ala Anasema katika.

Na atakayefanya urafiki na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na walio amini, basi Hakika kundi la Allaah ndilo lenya kushinda.”

 Al Maida: 56

 

Hitimisho

 

Namuomba Allaah Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja Wake wema na atupe katika marafiki ambao watatuepusha na ghadhabu Yake, na watakaotuelekeza kwenye njia ya Allaah na Radhi Zake. Namuomba Allaah Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja Wake wema ambao watakutana kwa furaha na kusifiana kama kile kisa tulichokisikia. Na atujaaliye tuingie katika  pepo Yake ya Firdaus kwa Rehma Zake..  Aamiyn

 

Alhamdulilah kuna website

Alhamdulilah kuna website nzuri kama hii inayotuelimisha mengi. Mashallah tabarakallah wa la haula wala quata illa billah. Jazakillah kher mwandishi.
Inshallah Mungu atuongoze daiman Ameen.