Du'aa za Qunut Ziko Ngapi Na Je Lazima Zisomwe Katika Swalah Ya Alfajiri?

 

SWALI:

Salam alaikum,

Mie swali langu ni kwamba dua hii ya Qunut ni lazima iombwe usiku baa ya kusali rakaa mbili au unaweza ukaomba wakati wowote?

Pia naomba unipatie dua yenyewe kama iko tofauti na ile isomwayo katika swala ya alfajir.

Ahsante.

 JIBU: 

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad:

Kwanza tujue kwamba maana ya 'witr' (witiri) ni namba isiyoweza kugawanyika kama moja au tatu au tano na kadhalika. Na Swalah ya Witr ambayo ni Sunnah iliyosisitizwa sana, huswaliwa usiku baada ya Swalah ya 'Ishaa hadi asubuhi kabla ya Alfajiri. Hivyo hakuna Raka'ah mbili zinazoswaliwa usiku na kusomwa du'aa ya Qunuut kama ulivyosema, bali husomwa du'aa hiyo baada ya kuinuka kutoka kurukuu katika Raka'ah ya mwisho ya Swalah za Witr. Unaweza kuswali Raka'a tatu au tano au saba au tisa au kumi na moja. Utaswali Raka'a mbili mbili na kila baada ya Raka'a mbili utatoa salaam kisha utamalizia na Raka'ah moja ndio utasoma hiyo du'aa ya Qunuut baada ya kuinuka kutoka kurukuu. Na kama huna uwezo wa kuswali hivyo basi hata Raka'ah moja itakutosheleza kupata fadhila za Witr na kusoma du'aa ya Qunuut kutokana na dalili ya Hadiyth ifuatayo:   

((صلاة الليل مثنى مثنى فإذا خشيت الصبح أوتر بواحدة)) أخرجه البخاري

((Swalah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na ukiogopa kukukuta asubuhi  basi Swali Witr  [Raka'ah] moja)) [ Al-Bukhaariy]

Tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo marefu kuhusu Swalah ya Witr na Du'aa ya Qunuut:

Bonyeza hapa:

Je Ni Sunnah Kusoma Du'aa Ya Qunuut Katika Swalah Ya Alfajri

Surah Gani Kusoma Katika Swalah Ya Witr

 

Du'aa za Qunuut zilizothibiti katika Sunnah ni hizi zifuatazo unaweza kusoma moja wapo au zote.

اللّهُـمَّ اهْـدِنـي فـيمَنْ هَـدَيْـت، وَعـافِنـي فـيمَنْ عافَـيْت، وَتَوَلَّـني فيمَنْ تَوَلَّـيْت ، وَبارِكْ لـي فـيما أَعْطَـيْت، وَقِـني شَرَّ ما قَضَـيْت، فَإِنَّـكَ تَقْـضي وَلا يُقْـضى عَلَـيْك ، إِنَّـهُ لا يَـذِلُّ مَنْ والَـيْت، [ وَلا يَعِـزُّ مَن عـادَيْت ]، تَبـارَكْـتَ رَبَّـنا وَتَعـالَـيْت.

Allaahummah-diniy fiy man Hadayta, wa 'Aafiniy fiy man 'Aafayta, wa Tawallaniy fiy man Tawallayta, wa Baarik-liy fiy maa A'attawyta, wa Qiniy sharra maa Qadhwayta, Fainnaka Taqdhwiy  wa laa Yuqdhwa 'Alayka, innahu la yadhillu maw-Waalayta, wa laa ya'izzu man 'Aadayta, Tabaarakta Rabbanaa wa Ta'aalayta.

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na Uliowaongoza, na Unipe afya njema pamoja na Uliowapa afya njema, na Nifanye kuwa ni mpenzi Wako pamoja na Uliowafanya  wapenzi na Nibariki katika Ulichonipa na Nikinge na shari ya Ulilolihukumu kwani Wewe Unahukumu wala Huhukumiwi. Hakika hadhaliliki Uliyemfanya mpenzi (wala hatukuki Uliyemfanya adui) Umetakasika Ee Mola wetu na Umetukuka"

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِرِضـاكَ مِنْ  سَخَطِـك، وَبِمُعـافاتِـكَ مِنْ عُقوبَـتِك، وَأَعـوذُ بِكَ مِنْـك، لا أُحْصـي ثَنـاءً عَلَـيْك، أَنْـتَ كَمـا أَثْنَـيْتَ عَلـى نَفْسـِك

Allaahuuma inniy a'udhu Biridhwaaka min Swakhatwika, wa Bimu'aafaatika min 'Uquubatika, wa a'uudhu Bika Minka, laa ukhswiy Thanaan 'Alayka, Anta kamaa Athnayta 'Alaa Nafsika.

 “Ee Allaah! Hakika mimi najilinda kwa radhi Zako kutokana na hasira Zako na kwa msamaha Wako kutokana na adhabu Yako, na najilinda  Kwako kutokana na Wewe, mimi siwezi kuzidhibiti sifa Zako kwa kadiri ya idadi yake, Wewe ni kama Ulivyojisifu Mwenyewe”

اللّهُـمَّ إِيّـاكَ نعْـبُدْ، وَلَـكَ نُصَلّـي وَنَسْـجُد، وَإِلَـيْكَ نَسْـعى وَنَحْـفِد، نَـرْجو رَحْمَـتَك، وَنَخْشـى عَـذابَك، إِنَّ عَـذابَكَ بالكـافرين ملْحَـق. اللّهُـمَّ إِنّا نَسْتَعـينُكَ وَنَسْتَـغْفِرُك، وَنُثْـنـي عَلَـيْك الخَـيْرَ، وَلا نَكْـفُرُك، وَنُـؤْمِنُ بِك، وَنَخْـضَعُ لَكَ وَنَخْـلَعُ مَنْ يَكْـفرُك

Allaahumma Iyyaaka Na'budu, wa Laka nuswwaliy wa nasjudu, wa Ilayka nas'aa wa nahfidu, narjuu Rahmataka wa nakhshaa 'Adhaabak, Inna 'Adhaabaka bil-kaafiriyna mulhaqq. Allaahumma innaa Nasta'iynuka wa Nastaghfiruka, wa nuthniy 'Alaykal-khayra, wa laa Nakfuruka, wa nuuminu Bika, wa nakhdhwa'u Laka, wa Nakhla'u man Yakfuruka.

“Ee Allaah! Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na Kwako tunaswali na tunasujudu, na Kwako tunakimbilia na tunakutumikia, tunataraji rehma Yako na tunaogopa adhabu Yako, kwani adhabu Yako hakuna shaka kuwa makafiri itawafikia. Ee Allaah! Hakika sisi tunakutaka msaada na tunakutaka msamaha na tunakusifu kwa kheri na wala hatukukufurishi na tunakuamini Wewe, na tunakunyenyekea na tunamuepuka anayekukufuru”

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share