Imaam Ibn Baaz: Ramadhwaan: Kurefusha Qiyaamul-Layl, Tofauti Ya Taraawiyh Na Qiyaamul-Layl?

 

Kurefusha Qiyaamul-Layl Katika Siku Kumi Za Mwisho

Na Je Kuna Tofauti Ya Taraawiyh Na Qiyaamul-Layl?

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je, kuna tofauti baina ya Taraawiyh na Qiyaam? Na je kuna dalili za kufanya makhsusi (Swalaah) katika kumi la mwisho kwa kurefusha Qiyaam, na rukuu na sujuwd? 

 

 

JIBU:

 

Swalaah zote hizo katika Ramadhwaan zinaitwa “Qiyaam” kama alivyosema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

مَنْ قَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ

“Atakayesimama Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia.”

[Ahmad katika Musnad ndani ya ‘Baaqiy Musnad Al-Mukthiriyn’ (7729) na Al-Bukhaariy katika ‘Baab Al-Iymaan’ (37)]

 

Basi atakaposimama pamoja na Iymaan kiasi atakachowepesishiwa, inaitwa: “Qiyaam”.

 

Lakini katika (masiku) kumi ya mwisho, inapendekezwa kurefusha kwa sababu imewekwa katika shariy’ah kuhuisha usiku kwa Swalaah na Qiraa (cha Qur-aan) na du’aa kwa vile Rasuli (‘Alayhis-Swalaatu was-Salaam) alikuwa akihuisha usiku wote katika (masiku) kumi ya mwisho, na kwa hivyo ikawa ni shariy’ah kurefusha ndani yake (ndani ya masiku hayo) kama alivyorefusha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Hakika yey alikuwa akisoma katika baadhi ya usiku Al-Baqarah, na An-Nisaa na Aal-‘Imraan katika rakaa moja.

 

Kwa hiyo kusudio ni kwamba (‘Alayhis-Swalaatu was-Salaam) alikuwa akirefusha (Swalaah) katika kumi la mwisho na akikesha ndipo ikawekwa shariy’ah kwa watu kukesha na kurefusha humo ili kumuiga (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kinyume na (masiku) ishirini ya mwanzo, ambapo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akikesha, bali alikuwa akisimama Qiyaam na akilala (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyokuja katika Hadiyth.

 

Ama katika kumi za mwisho, alikuwa (‘Alayhis-Swalaatu was-Salaam) akikesha usiku wote na akiamsha ahli zake na akikaza izaar kikoi chake (akizidisha mkazo mkubwa) (‘Alayhis-Swalaatu was-Salaam) kwa sababu humo (katika masiku kumi hayo ya mwisho) kuna usiku uliobarikiwa, Laylatul-Qadr.

 

 

[Fataawa Ibn Baaz]

 

 

 

Share