Suratul-An'aam Isomwe Siku 40 Kuondosha Mitihani Ya Dunia?

 

Suratul-An'aam Isomwe Siku 40 Kuondosha Mitihani Ya Dunia?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

nimewahi kusikia kuwa Suratul Al-An'aam ni sura nzuri sana unapofikwa na mitihani ya kidunia,nasikia unatakiwa uisome siku 40 mfululizo na zaidi usiiache maisha,kuna aya inasema allah mbili zinakutana so hapo unatakiwa usimame na uombe dua kila unalotaka,insh kila kitu kitakuwa sahal, Jee Kuna Ushahidi Ktk Hadiyth Za Nabiy Au Kuna Aayah Zinasema Watu Wasome Suwrah Al-an Am?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kuna mapokezi kuhusiana na Surah hii kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) yasemayo:

 

عَنْ اِبْن عَبَّاس قَالَ : ((نَزَلَتْ الْأَنْعَام بِمَكَّة لَيْلًا جُمْلَة وَاحِدَة حَوْلهَا سَبْعُونَ أَلْف مَلَك يَجْأَرُونَ حَوْلهَا بِالتَّسْبِيحِ)) رواه الطبراني  

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas: ((Imeteremshwa Al-An'aam Makkah usiku pamoja na Malaika sabini elfu wakimtukuza Allaah kwa sauti za juu))  [At-Twabaraaniy 12: 215]

 

 

Pamoja na baadhi ya Wanachuoni kusema maelezo hayo hapo juu ni Swahiyh au Hasan, lakini wengine wameeleza ni dhaifu kwa kuwepo mmoja wa wasimulizi aitwaye ‘Aliy bin Zayd bin Jad’aan kuwa ni dhaifu.

 

 

Kadhaalika, hatukupata mafunzo kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Suwrah hii isomwe siku kadha au mara kadha na kadha kwa ajili ya kuondosha mitihani ya dunia au kwa ajili ya jambo lolote jengine.

 

 

Ni kweli pia kwamba katika Aayah moja ya Suwrah hii limetajwa Jina la Allaah mara mbili kwa kufuatiliana, lakini vile vile hakuna uthibitisho kuwa ni sababu ya kuifanya Suwrah hii iwe ni yenye kukidhi haja au kuondosha matatizo au iwe ina fadhila fulani.  Kwa hiyo inapasa kuepukana na kauli zisizokuwa na dalili kwani kuamini na kufuata ni uzushi.

 

 

Juu ya hivyo ni kujikalifisha wakati wake Muislamu kufanya ibada isiyo na dalili kwa sababu:

 

1)    Suwrah hii ni ndefu, ni sawa na juzuu moja na robo takriban. Hivyo kuisoma siku arubaini mfululizo inahitaji kujiwekea wakati maalumu, nalo sio jambo lenye dalili katika mafunzo ya dini yetu. Je asipoweza mtu kuisoma mfululizo? Itamaanisha nini? Aanze tena kuhesabu upya?

 

2)   Kusema kuwa mtu asiache kuisoma maishani mwake pia sio kweli, kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni vigumu kwa Muislamu kupata muda wa kusoma Suwrah nyinginezo. Vile vile itamaanisha  kuzihama Suwrah nyingine na kung'ang'ania Suwrah moja pekee wakati tunapaswa iwe desturi yetu  kuisoma Qur-aan kwa kuindeleza kuanzia Suratul-Faatiha hadi mwisho Suwrah Al-Naas na kuendelea hivyo hivyo kukhitimisha Qur-aan mara kwa mara. Isiwe kama wanavyofanya baadhi ya watu kusoma Suwrah fulani makhsusi kila siku na kutozisoma nyinginezo, kwa kuamini hizo Suwrah zina fadhila fulani.    

 

 

Kwa ujumla, hayo ni mashaka wanayojibebesha Waislamu wengi wanaofuata kauli bila ya kuwa na dalili; mfano kuna wanaosoma Yaasiyn mara arubaini au mara nne, au utasikia watu wanaosma Qul-Huwa Allaahu Ahad mara elfu, au wanaosoma Suwrah Al-Waaqi’ah kila siku jioni n.k. Yote hayo ni mshaka tunayojitakia wenyewe katika ibada zetu ilhali mafunzo yake ni mepesi kabisa, na hata hayo mepesi tuliyoletewa hatuna wakati wa kutosha kuyatimiza kila siku.   

 

 

Du'aa za kusoma anapofikwa mtu na mitihani, balaa au jangwa ni zifuatazo katika kitabu cha Hiswnul-Muslim, kitabu ambacho kimekusanywa ndani yake kila aina ya du'aa tunazozihitaji katika kila harakaat za maisha yetu.

 

 

035-Hiswnul-Muslim: Du’aa Unapopatwa Janga Au Balaa

 

 

Vile vile ni kumkabili Allaah na kumuomba Akuondoshee matatizo na mitihani kwani Yeye yuko karibu na Mwenye kusikia na kupokea du'aa zetu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share