Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?

SWALI:

asalam alaykum,

mie nilikuwa naomba kuelimishwa kuhusu suali hili, ikiwa mwenzetu amefikwa na shida au maradhi tukakutana ndugu au jamaa lakini wanawake peke yao au wanaume peke yao tukamuombe dua jambo hili linafaa? na kama linafaa naomba utaratibu wake vipi iwe na kama haifai naomba tufahamishwe nini tunatakiwa tufanye kwa mujibu kwa sheria ya dini yetu na mafundisho ya Mtume wetu (s.a.w). nimesahau kwa kufahamisha zaidi nakusudia kwa mfano mgonjwa yupo mbali yaani nchi nyengine sie ndugu hatuwezi kuenda kumuona.

jazaka llahulkheir.

Mwenyezi mungu (s.w.t) awajaze kheri na afya njema na elimu bora zaid ili tuzidi kunufaika na sie amin.

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Ugonjwa unaomfika yeyote inakuwa ni mtihani kwake na jamaa zake na hivyo awali ya yote inafaa asisitiziwe mgonjwa awe na subira pamoja na jamaa zake pia wawe katika hali hiyo. Pia ifahamike kuwa mponeshaji mkubwa ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), ndipo Qur-aan ikatufahamisha yafuatayo: “Na ninapougua ni Yeye ndiye Anayeniponesha” (26: 80).

Zipo Du’aa nyingi ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha tunapomtembelea mgonjwa kwa mfano: “La ba-as twahuur inshaAllaah – Hakuna neno, ugonjwa ni kusafishwa dhambi akipenda Allaah” (al-Bukhaariy).

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana mja yeyote Muislamu anayemtembelea mgonjwa ambaye wakati wake wa kufa bado haujafika na akamuombea mara saba, hivi: “As-alu Llahal ‘Adhiym Rabbal ‘Arshil ‘Adhiym ay-yashfiyaka – Namuomba Allaah Mtukufu, Mola Mlezi wa Arshi tukufu akuponyeshe” Isipokuwa Allaah humponyesha mgonjwa huyo” (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

Hakujapatikana katika Siyrah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake kuwa wamekusanyikana ili wamuombee mgonjwa Du’aa. Hivyo, ni vyema nyinyi kama jamaa mulio mbali na mgonjwa wenu kumuombea katika kila nyakati hasa zile nyakati ambazo Du’aa hujibiwa kama mtu anapofungua akiwa amefunga, baina ya Adhaan na Iqaamah, baada ya Swalah, akiwa katika sijdah, akiwa safarini, kuinuka usiku watu wakiwa wamelala na wakati mwingine wowote.

Du'aa zifuatazo zimethibiti katika Sunnah kuwa ni za kumuombea mgonjwa:

 Duaa za Kumtembelea Mgonjwa 

Pia soma kitabu hichi muhimu cha Du’aa ujue Du’aa mbalimbali katika matukio tofauti:

HISWN AL MUSLIM

Na hapa pia tungependa kutoa nasaha kuwa mgonjwa huyo apatiwe matibabu kwa kupelekwa kwa madaktari waliobobea katika fani ya ugonjwa wake. Huko ni kufuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyotuagizia katika Hadiyth zake sahihi.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuafu na Ampatie shifaa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share