Ukumbusho Wa Takbiyr Katika Masiku Kumi Na Tatu Ya Dhul-Hijjah: Tarehe 1–13 Dhul-Hijjah
Ukumbusho Wa Takbiyr Katika Masiku Kumi Na Tatu Ya Dhul-Hijjah:
Tarehe 1 – 13 Dhul-Hijjah
Ndugu Waumini! Tukumbushane kuifufua Sunnah ya kuleta Takbiyr kuanzia unapoandama mwezi wa Dhul-Hijjah mpaka mwisho wa Ayyaamut-Tashriyq (Yaani kuanzia tarehe 1 Dhul-Hijjah mpaka 13 Dhul-Hijjah) baada ya Swalaatul-'Asr ndio kumalizika kwake kutokana na dalili zifuatazo:
Allaah ('Azza wa Jalla) Anaamrisha:
لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ
((Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. [Al-Hajj 28]
Na pia:
كَانَ إبْن عَمَر وَأبُو هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّه عَنْهُما يَخْرُجَانِ إِلَى السُّوقِ فِي أَيَّامِ العَشْرِ يُكَبِّرَانِ، وَيُكَبِّرُ النَّاسُ بِتَكْبِيرِهِمَا .
Ibn 'Umar na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) walikuwa wakienda sokoni katika siku kumi (za Dhul-Hijjah) na kutamka Takbiyr kwa sauti na watu wakiwaigiza. [Al-Bukhaariy]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚ
Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika. [Al-Baqarah: 203]
Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Siku za kuhesabika ni siku za tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na siku maalumu ni siku za kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah. [Al-Qurtwubiy: 3.3]
Takbiyr katika masiku haya matukufu ni aina mbili:[1]
Takbiyr Al-Mutwlaq: Za Nyakati Zote:
Takbiyr wakati wote mchana na usiku, mahali popote ulipo, tokea unapoingia mwezi wa Dhul-Hijjah na inaendelea mpaka siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah) na kumalizika baada ya kuingia Magharibi.
Takbiyr Al-Muqayyad: Za Kuthibitika Mahali Maalumu Na Nyakati Maalumu, Za Kukadirika:
Takbiyr baada ya kila Swalaah za fardhi na huanza baada ya Swalaah ya Alfajiri Siku ya 'Arafah mpaka mpaka baada ya Swalaah ya Alasiri siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah).
Inavyopasa kufanya Takbiyr:
اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، وَلِلَّهِ الْحَمْد
Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, laa Ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar Allaahu Akbar WaliLLaahil-Hamd
Bonyeza bango upate takbiyrah kwa sauti:
[1] Takbiyr hizo za masiku haya matukufu zimetekelezwa na baadhi ya Maswahaba watukufu na ni Mustahabb (imependekezwa) na wengi katika Salaf wa madhehebu ya Hanbaliy, Ash-Shaafi’iyy, Hanafiy na wengineo kama ifuatavyo:
Imaam An-Nawawiy - Al-Majmuw’ (5/32).
Ibn Rajab - Fat-hul-Baariy (6/125, 130).
Ibn Taymiyyah - Majmuw’ Al-Fataawaa (24/220. 222).
Imaam Ibn Baaz - Fataawaa Nuwr ‘Alad-Darb (13/355).
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn - Ash-Sharh Al-Mumti’ (5/166), Majmuw’ Fataawaa wa Rasaail Al-‘Uthyamiyn (16/262, 265).