005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je Damu Ni Najsi?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
005-Je Damu Ni Najsi?
Damu ina vigawanyo:
1- Damu ya hedhi:
Damu hii ni najsi kwa makubaliano ya Maulamaa. Dalili ya unajsi wake imekwisha elezewa nyuma.
2- Damu ya mwanadamu
[Tafsiyr Al-Qurtubiy (2/221), Al-Majmuu (2/511), Al-Muhalla (1/102),Al-Kaafiy (1/110), As-Sayl Al-Jarraar na Bidaayat Al-Mujtahid (1/31), Ash Sharh Al-Mumtani-’i (1/376), As Silsilat As-Swahiyhah , na Tamaam Al-Minna (uk.50)].
Ni damu iliyosababisha mahitalifiano juu ya hukmu yake. Lililo mashuhuri kwa wafuasi wa madhehebu ya kifiqhi ni kwamba damu ni najsi, lakini hawana dalili. Isipokuwa damu imeharamishwa kwa matni ya Qur-aan katika neno Lake Aliyetukuka:
((قُل لاَّ أَجِدُ فِي مَا أُوْحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلاَّ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ ))
(( Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu)).[Al An-‘aam (6:145)].
Kwa hiyo, kutokana na kuharamishwa kwake, wao wameichukulia kwamba ni najsi - kama walivyofanya katika pombe - na yaliyomo ndani yake hayafichikani. Lakini amenukuu zaidi ya Mwanachuoni mmoja katika Maulamaa kuwa wanakubaliana wote kwamba damu ni najsi. Maelezo zaidi yatakuja katika hilo.
Ni wakati ambapo kundi la waliokuja baadaye akiwemo Ash-Shawkaany, Siddiyq Khaan, Al-Albaaniy, Ibn ‛Uthaymiyn (Allaah Awarehemu) wameelekea kusema kuwa damu ni twahara kwa kutothibiti Ijma’a kwa upande wao. Wao wametoa dalili vilevile kwa haya yafuatayo:
1- Asili ya vitu ni twahara mpaka iwepo dalili kuthibitisha unajsi wake. Na sisi hatujui kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuosha damu nyingine zaidi ya hedhi ingawa mtu hupatwa mara nyingi na majeraha na mfano wake. Na lau kama damu ni najsi, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha, kwa sababu hali ya mambo inahitajia hilo.
2- Ni kwamba Waislamu waliendelea kuswali na majeraha yao, na waliweza kuchuruzikwa na damu nyingi ambayo si ya kusameheka. Na wala haikupokelewa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliamuru kuiosha, au kupokelewa kuwa wao walikuwa wakijilinda kwa hadhari isiwapate.
Amesema Al-Hasan: "Waislamu bado wanaswali wakiwa na majeraha yao". [Isnadi yake ni Swahiyh. Ameisimulia Al-Bukhaariy ikiwa ni “Mu’allaq” (1/336). Ibn Abiy Shaybah ameiunga kwa Sanad Swahiyh kama ilivyo katika Al-Fat-h (1/337)].
Na katika kisa cha Swahaba Muanswaar aliyekuwa akiswali usiku, ni kuwa mpagani alimpiga mshale, naye akauchomoa. Akampiga mwingine hadi ikafika mitatu. Kisha alirukuu, akasujudu na akaendelea na Swalaah yake na huku akivuja damu. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy ameifanya ni “Mu’allaq” (1/336), na Ahmad na wengineo wameseama ni “Mawsuwl”iunga, nayo ni Hadiyth Swahiyh].
Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) amesema: [Tamaam Al-Minnah (51,52)].
"Nayo iko katika hukmu ya Hadiyth Marfu’u, kwa vile kwa kawaida haiyumkiniki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asilijue hilo. Na lau kama damu nyingi ingelikuwa inabatilisha Swalaah, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angebainisha hilo, kwani haifai kuchelewesha taarifa wakati ule inapohitajika kama inavyojulikana katika taaluma ya "usuul". Na kama tutachukulia kwamba hilo lilifichikana kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi halifichikani kwa Allaah Ambaye hakifichikani Kwake chochote kikiwa ardhini au mbinguni. Na lau kama (damu) ingelikuwa inabatilisha au ni najsi, basi Rasuli angeliteremshiwa wahyi kama inavyojulikana kwa kila mtu".
Na katika kisa cha kuuawa ‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Allaah Amridhie): "Umar aliswali, na huku jeraha lake linachuruzika damu". [Hadiyth Swahiyh. Maalik ameifanyia “ikhraaj”, na Al-Bayhaqiy kutoka kwake (1/357) na wengineo kwa Sanad Swahiyh].
3- Ni kwa Hadiyth ya 'Aaishah katika kisa cha kufa kwa Sa'ad bin Mu’aadh. Alisema: " Sa'ad bin Mu’aadh alipojeruhiwa siku ya Khandaq baada ya kupigwa mshale kwenye mshipa wa damu mkononi na mtu mmoja, Rasuli alimjengea hema Msikitini ili apate kumtizama kwa ukaribu. Na mara ghafla usiku, jeraha lake lilipasuka na damu ikachuruzika kwa wingi. Wakasema: Enyi wenyeji wa nyumba! Nini hiki kinatujia toka kwenu? Wakatazama. Wakashtuka kuona jeraha la Sa'ad limepasuka na damu inafoka, naye akafariki hapo hapo. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (3100) kwa ufupi, na Atw-Twabaraaniy katika kitabu cha Al-Kabiyr (6/7)].
Ninasema (Abuu Maalik): "Na wala haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru maji yamwagiwe juu yake na hasa pakizingatiwa kwamba yuko Msikitini kama alivyoamuru kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui.
4- Kwamba Ibn Rushdi wakati alipotaja hitilafu za Maulamaa kwa upande wa damu ya samaki, alieleza kwamba sababu ya kuhitalifiana kwao ni kuhitilafiana kwa upande wa maiti yake. Mwenye kuzingatia kwamba maiti yake inaingia ndani ya ujumuishi wa kuharamishwa, basi na damu yake ataizingatia hivyo hivyo. Na asiyezingatia hivyo, basi ataitoa damu yake kwa kipimo cha maiti yake.
Na tunasema: "Wao wanasema kuwa maiti ya mwanadamu ni twahara, na kwa hivyo damu yake iwe hivyo hivyo kwa mujibu wa kaida yao".
Na kwa ajili hiyo, Ibnu Rushdi alisema baada yake: "Na matni ya Hadiyth ishaonyesha kwamba damu ya hedhi ni najsi. Ama damu nyingine, basi hiyo iko katika uasili uliokubaliwa na wenye kuzozana ya kwamba ni twahara. Na haitoki kwenye utwahara, ila kwa matni ya kusimamishia hoja".
Na ikiwa mtu atauliza: "Kwa nini damu ya hedhi isifanywe kipimo, na damu hii ni najsi?”
Tunasema: "Hiki ni kipimo kisichoendana, kwani damu ya hedhi ni damu ya maumbile ya asili kwa wanawake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((ان هذا شيئ كتبه الله على بنات آدم))
((Hakika hiki ni kitu ambacho Allaah Amekiandika kwa mabinti wa Aadam (wanawake)).[Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (294) na Muslim (1211)].
Na akasema kuhusu istihaadhwah:
((انه دم عرق))
((Hakika hiyo ni damu ya mshipa (asili)). [Hadiyth Swahiyh, Al-Bukhaariy (327) na Muslim (333)].
Kisha damu ya hedhi ni damu nzito ya mvundo na harufu kali. Inafanana na mkojo na kinyesi, si damu yenye kutoka katika zisizo njia mbili.
3- Damu ya mnyama mwenye kuliwa
Mjadala kuhusu damu hii ni kama mjadala kuhusu damu ya mwanadamu kwa upande wa kutokuwepo dalili juu ya unajsi wake. Kwa hivyo inaambatana na utwahara wa asili.
Kusema kuwa ni twahara kunaungwa mkono vilevile na:
Yaliyoelezewa na Ibn Masu’ud, amesema: "Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali mbele ya Al-Ka’abah, na Abuu Jahli na marafiki zake wamekaa. Wakaambizana: “Ni nani kati yenu anaweza kwenda kwa ngamia wa akina fulani, kisha akusanye vinyesi, damu, na matumbo yao, halafu aje amsubiri mpaka atakaposujudu, amwagie mabegani mwake”? Mwovu wao akachomoka haraka, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposujudu, alim-mwagia kati ya mabega yake, na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) alitulia tuli katika sijdah, na wao wanacheka.[Hadiyth Swahiyh, Al-Bukhaariy (240) na Muslim (1794)].
Na lau kama damu ya ngamia ingelikuwa ni najsi, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliitenga kando nguo yake, au angeikatisha Swalaah yake.
Aidha, imethibiti kwa njia sahihi kwamba Ibnu Mas-’oud aliswali na tumboni mwake kuna kinyesi na damu ya ngamia aliowachinja, lakini hakutawadha. [Isnadi yake ni Swahiyh. Muswannaf ‘Abdul Razzaaq (1/25), na Ibn Abiy Shaybah (1/392)].
Athar hii inaweza kuleta mvutano katika kutolea ushahidi juu ya utwahara wa damu ya mnyama, kwa vile Ibnu Mas-’oud hakuwa akiona kwamba utwahara wa mwili na nguo ni sharti ya kusihi Swalaah, bali anaona kuwa ni jambo linalopendeza (mustahab).
Ninasema (Abuu Maalik): “Lau kama imethibiti kwa Ijma’a kwamba damu ni najsi, basi hatutaziangalia dalili za waliofuatia baadaye. Na kama haikuthibiti, basi asili ni utwahara, na sisi hatuhitajii dalili hizo. Na lililodhihiri kwangu - baada ya kuchagua kauli (isemayo kuwa) damu ni twahara kwa kipindi cha miaka kumi - ni kwamba Ijma’a katika suala imethibiti. Ijma’a hii imenukuliwa na Maulamaa wengi na hakikuthibiti chenye kuitengua. Na nukuu ya juu zaidi kati ya hizo ni yale yaliyonukuliwa toka kwa Imaam Ahmad, kisha yale aliyoyanukuu Ibn Hazm, kinyume na yule aliyedhani kwamba madhehebu yake yanasema kwamba damu ni twahara!! Na kati ya niliyoyafahamu katika hilo ni:
Ibnu Al-Qayyim katika Ighaathat Al Lahafaan (1/420) amesema:
“Ahmad aliulizwa: Je, damu na usaha kwako ni sawa"? Akasema: "Hapana, watu hawakuhitilafiana kuhusu damu".
Na alisema mara moja: "Usaha kwangu ni afadhali kuliko damu".
Na imenukuliwa toka kwa Ibnu Hazm katika Maraatib Al Ijma’a: "Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni najsi ".
Vile vile Al-Haafidh katika Al Fat-h (1/420) amekunukuu kukubaliana huko.
Na Ibnu ‘Abdul-Barri katika At-Tamhiyd (22/230) anasema:
"Na hukmu ya kila damu ni kama damu ya hedhi, isipokuwa damu kidogo husamehewa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameweka sharti ya unajsi wa damu kuwa iwe ni yenye kuchuruzika, na hapo inakuwa ni uchafu, na uchafu ni najsi. Na hii ni Ijma’a ya Waislamu kwamba damu yenye kuchuruzika ni uchafu na najsi..".
Na Ibnu Al-Araby katika Ahkaam Al-Qur-aan (1/79) anasema:
"Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni haramu na ni najsi kwa kinacholiwa na haitumiwi kwa manufaa yoyote. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameiainisha hapa kwa kuifanya ni damu ya aina yoyote ile (mutwlaq), na katika Suwrat Al-An 'Aam Ameiainisha kwa kuiwekea mpaka (muqayyad) ile tu ya kuchuruzika. Na Maulamaa kwa Ijma’a hapa, wameichukulia damu yoyote wakaiacha iliyoainishwa".
Na An-Nawawy katika Al-Majmu’u (2/576) amesema:
"Na dalili juu ya unajsi wa damu zinatiliana nguvu zenyewe kwa zenyewe, na mimi sijui kama kuna hitilafu yoyote toka kwa Muislamu yeyote ila tu yale aliyoyaelezea mtunzi wa Al-Haawiy toka kwa baadhi ya Maulamaa wa tawhiyd. Amesema kuwa ni twahara, lakini maneno ya Maulamaa wa tawhidi hayachukuliwi katika Ijma’a au mahitalifiano…".
Ninasema (Abuu Maalik): “Ninalolipa nguvu na uzito ni kuwa damu ni najsi kwa kuthibiti Ijma’a mpaka inukuliwe toka kwa Imaam mwingine atakayempiku Imaam Ahmad – (Allaah Amrehemu) – kwa kusema kuwa damu ni twahara. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.