006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Matapishi Ya Mwanadamu Ni Najsi?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
006- Je, Matapishi Ya Mwanadamu Ni Najsi?
Tumetangulia kusema mara nyingi kwamba asili ya vitu vyote ni twahara, na kwamba havihamishwi toka kwenye asili yake ila kwa kinukuo sahihi cha kutolea hoja kisichopingana na kile chenye kutiliwa nguvu au kuwa sawa nacho. Na ikiwa tutalipata hilo, basi ni vizuri. Na kama hatukulipata, basi itatulazimu tusimame msimamo wa kumpinga anayedai kuwa ni najsi. Kwani kudai huku kunamaanisha kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewajibisha kwa Waja Wake kuviosha vitu hivyo vinavyodaiwa kuwa ni najsi, na kwamba kuwepo kwake kunazuia kuswali navyo. Basi ni ipi dalili ya hilo?!
Matapishi na mfano wake, hakuna kilichothibiti kwa njia sahihi chenye kuyahamisha toka kwenye utwahara wake wa asili.
Kuna kauli ya ‘Ammaar iliyopokelewa kuhusu matapishi akisema: "Wewe utaosha nguo yako iliyoingiwa na mkojo, kinyesi, matapishi, damu na manii".
Lakini kauli hii ni dhaifu haitolewi hoja. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
Na imethibiti toka kwa Abu Ad-Dardaai akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua na akatawadha. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2381), At-Tirmidhiy (87), Ahmad (6/443) na wengineo].
Katika Hadiyth hii, hakuna kiashirio chochote chenye kuonyesha kuwa matapishi ni najsi, na wala hakuna dalili juu ya ulazima wa kutawadha akitapika mtu, na wala haionyeshi kuwa wudhuu unatenguka kwayo, bali lengo lake ni kusunisha mtu atawadhe anapotapika. Kwani kwa kitendo tu cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuonyeshi kuwa ni wajibu.
Pamoja na hayo, si kila chenye kutengua wudhuu kinahesabiwa kuwa ni najsi. Ibnu Hazmi amelikhitari hili, na pia Shaykh wa Uislamu katika Al-Fataawaa.