027-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Sifa Ya Wudhuu Uliokamilika (Kiujumla)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

027-Sifa Ya Wudhuu Uliokamilika (Kiujumla)

 

Alhidaaya.com

 

 

Imepokelewa toka kwa Humraan mwachwa huru wa ‘Uthmaan kwamba alimwona ‘Uthmaan bin ‘Affaan akiagiza chombo, kisha akamimina juu ya viganja vyake mara tatu na kuviosha. Kisha akauingiza mkono wake wa kuume kwenye chombo, akasukutua na kupaliza maji puani. Kisha akaosha uso wake mara tatu, na mikono yake hadi kwenye viwiko mara tatu. Halafu akapukusa kichwa chake, kisha akaosha miguu yake mara tatu hadi kwenye vifundo, kisha akasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( من توضأ نحو وضوئي هذا، ثم صلى ركعتين لا يحدث فيهما نفسه، غفر له ما تقدم من ذنبه))

((Mwenye kutawadha mfano wa wudhuu wangu huu, kisha akaswali rakaa mbili, haizungumzishi nafsi yake ndani yake, hughufiriwa madhambi yake yaliyopita)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (158) na Muslim (226)].

 

 

Na kutokana na Hadiyth hii na nyinginezo zitakazokuja kuzungumziwa kwa ufafanuzi, tunaweza kuiweka sifa ya wudhuu katika haya yafuatayo:

 

 

1-Atanuwia wudhuu kwa ajili ya kuondosha hadathi.

 

2-Atalidhukuru Jina la Allaah Mtukufu.

 

3-Ataviosha viganja vyake mara tatu.

 

4-Atateka maji kwa mkono wake wa kuume, kisha atayaweka mdomoni na puani kwa teko moja, atasukutua na kupaliza.

 

5-Atapenga kwa kutumia mkono wake wa kushoto. Atafanya hivi mara tatu.

 

6-Ataosha uso wake wote mara tatu pamoja na kupachanyisha ndevu.

 

7-Ataiosha mikono yake miwili – wa kulia kisha wa kushoto – mpaka juu ya viwiko viwili pamoja na kupachanyisha vidole vya mikono miwili.

 

8-Atapukusa kichwa chake chote kwenda nyuma na mbele mara moja.

 

9-Atapukusa masikio yake mawili nje na ndani.

 

10-Ataosha miguu yake miwili pamoja na vifundo vyake viwili - wa kulia kisha wa kushoto - pamoja na kupachanyisha vidole vya miguu miwili.

 

 

 

 

Share