028-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Niya Ni Sharti Ya Kuswihi Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

028-Niya Ni Sharti Ya Kuswihi Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

[Sharti ni jambo ambalo kutokuwepo kwake hulazimisha kutokuwepo, na kuwepo kwake hakulazimishi kuwepo au kukosekana kwa dhati yake. Sharti ni lazima iwepo kabla ya kitendo nje ya uhalisia wake].

 

Ili wudhuu uwe sahihi, ni lazima  pawepo niya. Niya ni kuazimia kwa moyo juu ya kufanya tendo la kutawadha kwa ajili ya kufuata Maagizo ya Allaah Mtukufu na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo kwenye ‘ibaadah nyinginezo za kisharia. Allaah Mtukufu Anasema:

(( وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ))

(( Na hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Allaah huku wakimtakasia Dini na kuwa mbali na shirki)). [Al Bayyinah (98:5)]

 

 

Na Rasuli ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( إنما الأعمال بالنيات، وإنما لكل امرء ما نوى...))

((Hakika matendo ni kwa niya, na kila mtu ni kwa lile alilolinuwiya..)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (1) na Muslim (1907)].

 

Huu ndio msimamo walioukhitari Maalik, Ash Shaafi’iy, Ahmad, Abuu Thawr na Daawuud. [“Bidaayatul Mujtahid” (1/6), “Al-Majmuu” (1/374), na “At-Tamhiyd” (22/100,101)].

 

Lakini Abuu Haniyfah msimamo wake ni kuwa niya si sharti kwa ajili ya wudhuu, kwa kuwa wudhuu ni ‘ibaadah ya kidhahania na wala haikusudiwi kwa dhati yake. [Badaai’u Asw Swanaai-’i” (1/19 – 20)].

 

Mfano wake ni kama kutwaharisha uchafu. Kauli ya Jamhuri ya Maulamaa ndio sahihi kwa kuwa matni inatutaarifu kuwa thawabu zinapatikana katika kila wudhuu, na kwamba thawabu hazipatikani kwa kisichonuwiliwa kwa Ijma’a, na kuwa wudhuu ni ‘ibaadah ambayo haijulikani ila kwa sharia. Na kwa ajili hiyo, niya imekuwa ni sharti.  [Al-Furu’u” cha Muflih (1/111)].

 

Mahala Pa Niya Ni Moyoni

 

Shaykh wa Uislamu (Allaah Amrehemu) anasema: [Majmuuat Ar-Rasaail Al-Kubraa (1/234)].

“Mahala pa niya ni moyoni na si katika ulimi kwa makubaliano ya Maimamu wa Kiislamu katika ‘ibaadah zote; twahara, Swalaah, Zakaat, Swaum, Hajji, kuacha huru mtumwa, Jihaad na kadhalika”.

 

Hakuna usharia ya kuitamka kwa sauti au kuikariri. Aliyezoea kufanya hivyo na hususan kama anawaudhi watu, inatakikana atiwe adabu au afanyiwe izari lakini baada ya kueleweshwa. Mwenye kuitamka niya, ni mkosa, na lau kama ataitakidi kwamba kuitamka ndio dini na ‘ibaadah kwa Allaah, basi huyo amezua. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba Zake hawakuwa wakiitamka niya kabisa, na hilo halikurekodiwa kutoka kwao. Na lau kama lingekuwa ni jambo la kisharia, basi Allaah Angelibainisha kupitia kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mbali ya hivyo, hakuna haja ya kuitamka niya, kwa kuwa Allaah Anaijua. [Angalia Zaadul Ma’aad (1/196), Ighaathat Al-Lahafaan (1/134), Badaai’ul Fawaaid (3/186), Al-Furu’u (1/111) na Sharhul Mumti-’i (1/159)].

 

Faida

 

1- Shaykh wa Uislamu anasema:

“Lau kama atatamka kwa ulimi wake kinyume na alichonuwia moyoni, kinachozingatiwa ni kile alichokinuwia na si alichokitamka. Na lau kama atatamka kwa ulimi bila kunuwia moyoni, basi hilo halitosihi kwa makubaliano ya Maimamu wa Kiislamu, kwa kuwa niya ndio makusudio na azima yenyewe”.

 

 

2- Hadathi zinazowajibisha kutawadha zikikusanyika pamoja kama mtu kwenda haja ndogo, kisha kubwa, halafu akalala, ikiwa atanuwia kuondosha moja tu kati ya hizo, basi zote zitaondoka – kwa kauli sahihi – kwa kuwa hadathi wasifu wake ni mmoja ingawa sababu zake ni tofauti. [Angalia Al-Majmu’u (1/385) na Ash Sharhul Mumti’i (1/165)].

 

 

3- Ni vyema kwa mwenye kutawadha anuwie kuondosha hadathi tu ili kuepukana na mahitilafiano ya Maulamaa katika kujuzisha baadhi ya picha za niya pasina nyinginezo. Picha hizi ni kunuwia kuondosha hadathi, au kunuwia twahara kwa lililo wajibu kwake, au kunuwia twahara kwa lililo sunna kwake, au kunuwia kujadidisha wudhuu kulikosuniwa. [Angalia namna Maulamaa walivyokhitilafiana katika masuala haya katika kitabu cha Al-Majmu’u (1/385)].

 

 

 

Share