036-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Usharia Wa Kupaka Juu Ya Khufu Mbili

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

036-Usharia Wa Kupaka Juu Ya Khufu Mbili

 

Alhidaaya.com

 

 

Wanachuoni wote wamekubaliana kwamba mwenye kutawadha kikamilifu, kisha akazivaa khufu zake mbili, halafu wudhuu ukamtenguka, basi anaruhusika kupukusa juu yake. [Al-Ijma’a cha Ibn Al-Mundhir (20) na Al-Awsatw (1/434)].

 

Ibn Mubaarak kasema: “Hakuna khitilafu yoyote kuwa  kupukusa juu ya khufu mbili, kunajuzu. Na hii ni kwa vile kila Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye imeripotiwa kuwa amekirihisha kupaka juu ya khufu mbili, imethibiti kinyume chake. [Al-Awsatw (1/434), Sunan Al-Bayhaqiy (1/272) na Al-Fat-h (1/305)].

 

Usharia wake umethibiti kwa Sunnah Swahiyh iliyo “Mutawaatir” toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na madhubuti zaidi linaloonyesha usharia huo ni Hadiyth ya Hammam aliyesema: “Jurayr alikojoa, kisha akatawadha, halafu akapaka juu ya khufu zake. Akaulizwa: Unafanya hivi? Akasema: Ndio. Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekojoa, kisha akatawadha na akapukusa juu ya khufu zake mbili”.

 

Al-A’amash anasema: “Ibrahim amesema: Walikuwa wakiipenda Hadiyth hii, kwani Jurayr alisilimu baada ya kuteremka Suwrat Al- Maaidah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (387) na Muslim (1568), na tamko ni lake].

 

Share