068-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Anayechelea Kudhurika Kwa Maji Baridi, Je Anaweza Kutayammamu Akiwa Na Janaba?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

068-Anayechelea Kudhurika Kwa Maji Baridi, Je Anaweza Kutayammamu Akiwa Na Janaba?

 

Alhidaaya.com

 

 

Anayejihofia kufa kutokana na maji baridi, inajuzu kwake kutayammamu kwa vile anakuwa katika ngazi ya mgonjwa. Huu ni mwelekeo wa Jamhuri ya Maulamaa. [Al-Mabswutw (1/122), Al-Majmu’u (2/330), Al-Istidhkaar (3/173), Al-Mughniy (1/163), Al-Muhalla (2/134) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/399)].

 

Hoja yao katika hili ni:

 

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم إن الله كان بكم رحيما))

((Wala msiziue nafsi zenu, hakika Allaah ni Mrehemevu mno kwenu)). [An-Nisaa (4:29)].

 

2- Ni yaliyopokelewa toka kwa ‘Amri bin Al-‘Aas kwamba wakati alipopelekwa katika vita vya Dhaatu As-Salaasil alisema: “Niliota katika usiku wa baridi kali, nikahofia kufa kama nitaoga. Nikatayammamu, kisha nikaswali na wenzangu Swalaah ya Alfajiri. Tulipowasili kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam), wao walimweleza hilo, akasema:

((Ee ‘Amri! Hivi umeswali na wenzako ukiwa na janaba?))

Nikamwambia: “Nililikumbuka Neno la Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم إن الله كان بكم رحيما))

nikatayammamu kisha nikaswali. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) akacheka, na hakusema neno)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (334), Ahmad (3/203), Ad-Daara Qutwniy (1/178), Al-Haakim (1/177) na Al-Bayhaqiy (1/225). Sanad na matni yake zimetiwa doa. Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (1/182) amesema ni Swahiyh].

 

Hadiyth hii ina mvutano, na lenye nguvu ni kuwa ni dhwa’iyf. Lakini pamoja na hivyo, kaida za kisharia zinaitolea ushahidi. Vile vile mwelekeo huu unaungwa mkono na Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ما يريد الله ليجعل عليكم من حرج))

((Hataki Allaah kuwafanyieni uzito)). [Al-Maaidah (5:6)].

 

Na hii ni baada ya kutaja tayammumi. Kana kwamba Ameashiria kuwa tayammumi inaruhusika panapokuwepo uzito wa kutumia maji. Na hakuna shaka kuwa ubaridi mkali wa maji ni katika uzito huo. Lakini inatakikana kutanabahisha kuwa kutayammumi hakuruhusiwi – katika hali hii – ila baada ya kushindwa kupasha maji moto. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share