008-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Nyakati Zisizoruhusiwa Kuswali

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

008-Nyakati Zisizoruhusiwa Kuswali

 

Alhidaaya.com

 

 

1,2- Baada ya Swalaah ya Alfajiri mpaka kupanda jua kiasi cha mkuki, na baada ya Swalaah ya Alasiri mpaka kuchwa jua

 

Imethibiti kupigwa marufuku kuswali Swalaah za Sunnah katika nyakati hizi mbili, na asili katika hili ni:

 

(a) Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas akisema: “Walinieleza watu wasio na chembe ya shaka kuhusu ukweli na uaminifu wao – na pia kwa ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) - kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuswali baada ya Alfajiri mpaka jua lichomoze, na baada ya Swalaah ya Alasiri mpaka jua lichwe. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (581) na Muslim (826)].

 

(b) Hadiyth ya Abu Sa’iyd aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Hapana Swalaah baada ya Alfajiri mpaka jua lipande, na hapana Swalaah baada ya Alasiri mpaka jua lichwe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (586) na Muslim (827)].

 

3- Wakati jua linapopinduka Adhuhuri

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaahu Anhu) aliposema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitukataza kuswali au kuwazika maiti zetu katika nyakati tatu: Jua linapochomoza angavu mpaka lipande, jua linapokuwa katikati ya mbingu Adhuhuri mpaka lipinduke, na wakati jua linapokurubia kuchwa mpaka lichwe kabisa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (831)].

 

·       

Sababu Ya Katazo

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha sababu ya kukataza kuswali katika nyakati hizi alipomwambia ‘Amri bin ‘Absah: ((Swali Swalaah ya Alfajiri, kisha acha kuswali hadi jua lichomoze na mpaka linyanyuke, kwani jua huchomoza wakati linapochomoza kati ya pembe mbili za shaytwaan, na wakati huo makafiri hulisujudia. Halafu swali, kwani Swalaah huhudhuriwa na hushuhudiliwa mpaka kivuli kinapokuwa kando ya mkuki. Kisha acha kuswali, kwani wakati huo Jahannamu hukolezwa. Na kivuli kinapokuja, basi swali, kwani Swalaah huhudhuriwa na hushuhudiliwa mpaka utakaposwali Alasiri. Kisha acha kuswali mpaka jua lizame, kwani jua huzama kati ya pembe mbili za shaytwaan, na wakati huo makafiri hulisujudia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (832)].  

 

·       

Yasiyokuwemo Kwenye Katazo

 

1- Adhuhuri ya Siku ya Ijumaa

 

Wakati huu imesuniwa kuswali Sunnah yoyote kabla ya Swalaah ya Ijumaa mpaka khatibu apande mimbari. Anapopanda mimbari, basi hapo hairuhusiwi tena kuswali Sunnah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haogi mtu Siku ya Ijumaa, akajitwaharisha upeo wa kujitwaharisha, akajipaka mafuta au akajitia mafuta mazuri ya nyumba yake, kisha akatoka (mapema) asije kufarakanisha kati ya wawili, halafu akaswali kilichosuniwa kwake, kisha akanyamaza wakati khatibu anapozungumza, isipokuwa husamehewa yaliyo kati yake na ijumaa nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (883)].

 

Na kwa haya, Ash-Shaafi’iy (Rahimahul Laahu) anasema akitolea dalili kwa Hadiyth hii na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuswali nusu ya mchana mpaka jua lipinduke isipokuwa Siku ya Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (595), Abu Daawuud (439) na An-Nasaaiy (2/105)]

Ni Dhwa’iyf, na yaliyotajwa yanatosheleza, walil-Laahi Al-Hamdu.

 

Maulamaa wana kauli nyingine mbili:

 

Ya kwanza: Ni kuwa si karaha kuswali nusu ya mchana Swalaah yoyote sawasawa ikiwa ni Siku ya Ijumaa au siku nyingine. Hii ni kauli ya Maalik, na hoja yake ni kitendo cha watu wa Madiynah, lakini hoja yake hii inapingwa na Hadiyth zilizotangulia.

 

Ya pili: Ni karaha kuswali nusu ya mchana Swalaah yoyote sawasawa ikiwa ni Siku ya Ijumaa au siku nyingine. Ni kauli ya Abu Haniyfah na mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad.

Madhehebu ya Ash-Shaafi’iy ndiyo yenye nguvu zaidi, nayo ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Zaadul Ma’aad cha Ibn Al-Qayyim (1/378) chapa ya Ar-Risaalah]

 

2- Rakaa mbili za twawaaf katika Baytul Haraam

 

Haizuiliwi kuswali rakaa mbili za twawaaf katika nyakati za marufuku tulizozitaja kutokana na dalili zifuatazo:

 

(a) Hadiyth ya Jubayr bin Mutw’am (Radhwiya Alaahu Anhu) asemaye kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Enyi ukoo wa ‘Abdi Manaaf! Msimzuie yeyote aliyetufu Nyumba hii na akaswali saa yoyote aitakayo usiku au mchana)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (869), An-Nasaaiy (1/284) na Ibn Maajah (1254)].

 

(b) Ibn ‘Abbaas, Al-Hasan, Al-Husayn na baadhi ya Masalaf walilifanya hilo.

 

(c) Rakaa mbili za twawaaf zinaifuata twawaaf, na ikiwa chenye kufuatwa kinaruhusiwa, basi chenye kukifuata huruhusiwa pia.

 

Hii ndiyo kauli ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad, nayo imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar, Ibn Az-Zubayr, ’Atwaa, Twaawus na Abu Thawr. [Al-Ummu (1/150), Al-Majmu’u (4/72) na Al-Mughniy (2/81)]

 

3- Kulipa Swalaah za qadhwaa katika nyakati za marufuku

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya kulipa Swalaah iliyompita mtu katika nyakati za marufuku katika kauli mbili:

 

Ya kwanza: Haijuzu katika nyakati za marufuku. Ni kauli ya Abu Haniyfah na Asw-Haab Ar-Raay. [Al-Mabsuwtw (1/150)]

 

Hoja yao ni:

 

1- Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipolala ikampita Swalaah ya Alfajiri mpaka jua likachomoza, aliikawiza mpaka jua likawa angavu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (344) na Muslim (682) toka kwa ‘Imraan bin Haswiyn].

 

2- Hiyo ni Swalaah, hivyo haijuzu katika nyakati hizi kama Sunnah.

 

3- Yaliyosimuliwa toka kwa Abu Bakrah (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba yeye alilala huko Daaliyah, akaamka wakati jua linakuchwa, kisha akasubiri mpaka jua likazama, halafu akaswali. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/66) na ‘Abdul Razzaaq (2250)]

 

4- Yaliyosimuliwa toka kwa Ka’ab bin ‘Ajrah kwamba mwanaye alilala mpaka ilipotoka mboni ya jua, akamkalisha, na jua lilipopanda alimwambia: “Swali sasa”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: At-Tirmidhiy kaitaja ikiwa Mu’allaq (1/158) na Ibn Abu Shaybah kaifanya Mawswuul (2/66)]

 

Ya pili: Inajuzu kuzilipa qadhwaa katika nyakati za marufuku na nyakati nyinginezo. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Jamhuri ya Maswahaba na Taabi’iyna. [Al-Mudawwanah (1/130), Al-Umm (1/148), Al-Mughniy (2/80) na Al-Awsatw (2/411)]

 

Hoja yao ni:

 

1- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Aliyelala Swalaah ikampita au akaisahau, basi aiswali anapoikumbuka, hakuna kafara yake isipokuwa hilo)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshatajwa mara nyingi].

 

2- Hadiyth Marfu’u ya Abu Qataadah: ((Bali taksiri ni kwa yule ambaye hakuiswali Swalaah mpaka ukaingia wakati wa Swalaah nyingine. Mwenye kufanya hilo, basi aiswali anapozindukana)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (311) na wengineo, nayo ishaelezwa nyuma].

 

 Katika Hadiyth hizi mbili, kuna agizo la kuswali wakati mtu anapokumbuka au anapoamka bila ya kuzivua nyakati za marufuku.

 

Ninasema: “Hili ndilo lenye nguvu zaidi. Ama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuichelewesha Swalaah mpaka jua likawa angavu, ni kuwa kilichowaamsha hasa ni joto la jua. Na tushaeleza kwamba Rasuli alibainisha sababu ya kuwa mahala hapo walipolala, shaytwaan aliwahudhuria. Hivyo kizuizi cha kuswali kilikuwa ni mahala na si wakati. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

4- Kuzilipa Sunnah za rawaatib katika nyakati za marufuku

 

Inajuzu kuzilipa Sunnah za rawaatib ijapokuwa katika nyakati za marufuku kutokana na dalili zifuatazo:

 

(a) Hadiyth ya Ummu Salamah ya kwamba alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali rakaa mbili baada ya Alasiri. Akamuuliza sababu ya kufanya hivyo naye akajibu: ((Ee Binti Abu Umayyah! Umeuliza kuhusu rakaa mbili baada ya Alasiri. Hakika walinijia watu kutoka ukoo wa ‘Abdul Qays wakanishughulisha mpaka zikanipita rakaa mbili za baada ya Adhuhuri, nazo ndizo hizi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1233) na Muslim (297)].

 

(b) Yaliyosimuliwa toka kwa Qays bin ‘Amri akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikiswali rakaa mbili za Alfajiri baada ya Swalaah ya Alfajiri akaniuliza: ((Rakaa hizi mbili ni za nini ee Qays?)) Nikasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Sikuwa nimeswali rakaa mbili za Alfajiri, naye akanyamaza”. [Hadiyth Hasan kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu  Daawuud (1267), At-Tirmidhiy (422) na Ahmad (5/447). Ni Hadiyth Mursal, nayo ina Sanad nyingine kwa Ibn Al-Mundhir katika Al-Awsatw (2/391), Al-Haakim (1/273), na Al-Bayhaqiy (2/483). Na kwa ujumuisho wa yote, ni Hadiyth Hasan]

 

Na katika riwaya nyingine: “Rasuli hakumkatalia hilo”.

 

(c) Kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuisahau Swalaah, basi aiswali anapoikumbuka)). Hii ni kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy. [Bidaayatul Mujtahid (1/137) na Al-Ummu (1/149)]

 

5- Swalaah ya maiti baada ya Alfajiri na Alasiri

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba inajuzu kumswalia maiti baada ya Swalaah ya Alfajiri na Alasiri. [Ibn Qudaamah ameinukuu katika Al-Mughniy (2/82)]

 

Kisha wakakhitalifiana kuhusiana na kuiswali Swalaah hii katika nyakati zilizotajwa katika Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir ambazo ni wakati jua linapochomoza mpaka lipande, wakati  linapolingamana sawa Adhuhuri mpaka lipinduke, na wakati linapokurubia kuchwa mpaka lichwe. Wamekhitalifiana kuhusu nyakati hizi tatu katika kauli mbili:

 

Ya kwanza: Haijuzu kuswalia maiti katika nyakati hizi tatu. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maalik, Ahmad na Maulamaa wengi. [Al-Mudawwanah (1/190), Al-Mabsuutw (1/152), Al-Mughniy (2/82) na Maalim As-Sunan (1/313)].

 

Na hii ni kwa Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitukataza kuswali katika nyakati tatu na kuwazika maiti wetu katika nyakati hizo…akazitaja”. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa karibuni hivi].

 

Ya pili: Inajuzu kuswalia maiti katika nyakati zote zilizokatazwa. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Ummu (1/150) na Al-Majmu’u (4/68)] Hoja ya Ash-Shaafi’iy ni kuwa Swalaah hii ina sababu, na hivyo inatolewa nje ya wigo wa umarufuku.

 

Ninasema: “Linaloonekana ni kuwa Swalaah hii haijuzu katika nyakati hizi tatu kwa ajili ya Hadiyth, kwa kuwa ndani ya Hadiyth, pamoja na kukatazwa Swalaah, pamekatazwa pia kuzika maiti katika nyakati hizo. Hivyo inazuilika kuivua Swalaah na katazo. Isitoshe, nyakati hizi tatu ni fupi na hakuna kinachochelewa ikiwa patasubiriwa mpaka zimalizike. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

6- Swalaah zenye sababu

 

Ni kama Swalaah ya maamkizi ya Msikiti, Sunnah ya wudhuu, Swalaah ya Kupatwa Jua na mfano wake. Kisha Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu suala hili juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza: Haijuzu kuziswali katika nyakati zilizokatazwa. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad. [Al-Mabsuutw (1/152), Sharhu Fat-hul Qadiyr (1/204) na Al-Mughniy (2/90)]

 

Ya pili: Inajuzu. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, na riwaya ya pili toka kwa Ahmad. Hoja yao ni:

1- Imethibiti kuwa inajuzu kuswali rakaa mbili za twawaaf wakati wowote. Hili lishaelezwa nyuma.

 

2- Imethibiti kuwa inajuzu kuswali baada ya kutawadha wakati wowote ule kama ilivyo katika Hadiyth ya Bilaal wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia: ((Nielezee amali yenye matarajio zaidi uliyoifanya katika Uislamu)). Bilaal akasema: “Sikufanya amali yoyote yenye matarajio makubwa kwangu zaidi ya kuwa sikupata kujitwaharisha wakati wowote wa usiku au mchana, ila huswali kwa twahara hiyo kile nilichoandikiwa kukiswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa katika mlango wa wudhuu].

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kupatwa jua: ((Mnapoliona limepatwa, basi kimbilieni kwenda kuswali. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Swalaah ya kupatwa jua na mwezi].

 

4- Ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapoingia mmoja wenu Msikitini, asiketi mpaka aswali rakaa mbili. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Swalaah za Sunnah].

 

5- Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Sunnah ya Adhuhuri baada ya Alasiri kama tulivyoeleza kabla.

 

6- Ijma’a ya Maulamaa wanaosema kwamba inajuzu kumswalia maiti baada ya Alfajiri na Alasiri.

 

Wanasema: “Swalaah zote hizi ni Swalaah zenye sababu na imejuzu kuziswali wakati wowote, nazo haziko ndani ya wigo wa katazo”.

 

Ninasema: “Madhehebu haya yanatolewa dalili vile vile na haya yafuatayo:

 

7- Hadiyth ya Abu Dharr wakati Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam alipomwambia: ((Ee Abu Dharr! Utafanyaje ikiwa viongozi wako wanaiua Swalaah (au alisema) wanaichelewesha Swalaah na wakati wake?)) Nikamjibu: “Unaniamuru nini?” Akasema: ((Swali Swalaah katika wakati wake, na ikiwa utaiwahi pamoja nao basi swali, kwani hiyo itakuwa ni ziada kwako)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (648) na Abu Daawuud (431). Angalia Taadhiymu Qadris Swalaat (1008) nilichokifanyia uhakiki].

 

Na katika Hadiyth Mawquuf ya Ibn Mas-’oud: (( Watakuja viongozi watakaoitendea Swalaah ubaya, wataisonga mpaka mwisho wa mchana)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (534) na wengineo. Angalia Qadrus Swalaat (1015) nilichokifanyia uhakiki].

Na ametaja mfano wa Hadiyth ya Abu Dharr, akajuzisha Swalaah ya Sunnah katika wakati wa karaha kwa sababu iliyotajwa.

 

8- Hadiyth ya Yaziyd bin Al-Aswad aliyesema: “Nilikuwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hijjah yake. Nikaswali pamoja naye Swalaah ya Alfajiri katika Msikiti wa Al-Khayf. Alipomaliza Swalaah yake na kuondoka, mara walikuja watu wawili katika watu waliochelewa ambao hawakuwahi kuswali pamoja naye. Akasema: ((Nitawafuatia)). Wakaletwa huku vifua vyao vikitetema. Akawauliza: ((Kitu gani kimewazuia msiswali nasi?)) Wakasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tumeswali safarini. Akawaambia: ((Msifanye! Mkiswali safarini, kisha mkaja Msikiti wa Jamaa, basi swalini pamoja nao, kwani hiyo ni ziada kwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (219), An-Nasaaiy (2/112) na wengineo].

 

Al-Khattwaabiy kasema: “Katika neno lake: ((kwani hiyo ni ziada kwenu)), ni dalili kwamba Swalaah ya Sunnah inajuzu baada ya Alfajiri kabla ya kuchomoza jua ikiwa Swalaah ina sababu”. [Maalimus Sunan (1/165)]

 

Ninasema: “Juu ya msingi wa tuliyoyazungumzia, katazo la kuswali katika nyakati zilizotajwa katika Hadiyth, linahusiana hasa na Sunnah zisizo na sababu yoyote, na kwa mtu aliyekusudia kwa ari kuziswali katika nyakati hizo. Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Asipanie mmoja wenu akaswali wakati wa kuchomoza jua wala wakati wa kuchwa kwake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (585) na Muslim (828)].

 

·       

Faida

 

Nyakati zilizokatazwa kuswali tulizozielezea, ni zile ambazo katazo linafungamana na nyakati za asili. Kuna nyakati nyinginezo ambazo Swalaah imekatazwa kutokana na kufungamana kwake na jambo ambalo liko nje ya asili ya wakati. Litakuja kuelezewa kichambuzi katika sehemu zake katika mlango wa Swalaah za Sunnah Insha-Allaah.

 

 

Share