047-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Baadhi Ya Hukmu Za Msikiti

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

047-Baadhi Ya Hukmu Za Msikiti

 

Alhidaaya.com

 

 

Msikiti bora zaidi kuliko mingine:

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah moja ndani ya Msikiti wangu huu, ni bora zaidi kuliko Swalaah 1000 kwenye Msikiti mwingine, isipokuwa Al-Masjid Al-Haraam)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1190)].

 

· Misikiti Bora Zaidi

 

Ni Al-Masjidul Haraam, kisha Msikiti wa Rasuli, halafu Al-Masjidul Aqswaa kutokana na Hadiyth hii na zinazofuatia.

 

· Safari Haifungwi Isipokuwa Kuiendea Misikiti Mitatu

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Safari haifungwi isipokuwa kuiendea Misikiti Mitatu: Msikiti wangu huu, Masjidul Haraam na Masjidul Aqswaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1189) na Muslim (1397)].

 

· Ubora Wa Kujenga Misikiti

 

Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kujenga Msikiti kwa ajili ya Allaah, akitafuta kwa hilo Uso wa Allaah, basi Allaah Atamjengea nyumba peponi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (450) na Muslim (533)].

 

· Ukaraha Wa Kuipamba Misikiti Na Kurefusha Sana Majenzi Yake Zaidi Ya Inavyohitajia

 

Imepokelewa toka kwa Anas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Qiyaamah hakitosimama mpaka watu wajifakharishie kwa misikiti)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (449), An-Nasaaiy (689), Ibn Maajah (739) na Ahmad (11931)].

 

Na imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sikuamrishwa kujenga misikiti kama ngome)). Yaani: Kunyanyua majengo yake kupita kiasi ya inavyohitajia. [Ibn ‘Abbaas kasema: Hakika mtaipamba kama walivyopamba Mayahudi na Manasara]. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (448), Ibn Hibaan (1615), Al-Bayhaqiy (2/438) Abu Ya-’alaa (2454) na ‘Abdul Razzaaq (5127)].

 

Imepokelewa kwamba ‘Umar aliamrisha kujenga misikiti akisema: “Wahifadhi watu kutokana na mvua, na tahadhari usije kupaka rangi nyekundu au njano, watu wakaondokewa na khushuu kwa kushughulishwa na hilo”. [Al-Bukhaariy kaitolea maelezo katika mlango wa “Kujenga Msikiti” kwa kulitaja bayana jina la msimulizi wake (Swiyghat Al-Jazm)].

 

· Kuisafisha Misikiti Na Kuitia Vinukizo

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kujenga misikiti kwenye mitaa yenye watu, na akaamuru isafishwe na itiwe vinukizo. [Hadiyth Mursal: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (455), At-Tirmidhiy (594) na Ibn Maajah (759). Katika Sanad yake kuna mvutano kuhusiana na Hisham bin ‘Urwah. Lililo sawa -kama alivyosema Ad-daaraqutwniy katika Al’ilal- ni upokezi toka kwa Hisham toka kwa baba yake bila kumtaja ‘Aaishah. Angalia Al-Iswaabah (5/361)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba mtu mmoja mweusi –au mwanamke mweusi- alikuwa akisafisha Msikiti akafa, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuulizia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (458) na Muslim (956)].

 

Na katika tamko jingine toka kwa Abu Hurayrah: “Mwanamke alikuwa akiokota vijitaka na vijiti Msikitini”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (1300) na wengineo].

 

Na imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona kohozi kwenye Qiblah cha Msikiti, akaghadhibika mno mpaka uso wake ukawa mwekundu. Mwanamke mmoja wa Kiansari akasimama na kulikwangua, kisha akaweka mahala pake kinukizo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Uzuri ulioje wa kitendo hiki!!)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/25) na Ibn Maajah (762)].

 

· Kuihifadhi Na Taka Na Uchafu

 

Imepokelewa toka kwa Anas bin Maalik ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Misikiti hii haifai kwa jingine lolote kati ya mkojo huu wala uchafu, bali Misikiti ni kwa ajili ya kumdhukuru Allaah na kusoma Qur-aan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (537) kuhusiana na mtu aliyekojoa Msikitini].

 

Na toka kwa Anas vile vile kwamba Rasuli wa Allaah amesema: ((Kutema mate Msikitini ni dhambi, na kafara yake ni kuyafukia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (552), Abu Daawuud (475), At-Tirmidhiy (572) na An-Nasaaiy (2/51)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Dharri toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Amali za Umma wangu zilionyeshwa kwangu; njema zake na mbaya zake, nikakuta katika amali zake njema adha inayoondoshwa njiani, na nikakuta katika amali zake mbaya kohozi lililopo Msikitini halifukiwi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (553)].

 

Katika sharhu yake, An-Nawawiy amesema: “Hadiyth hii inaonyesha kwamba ubaya huu na sifa hii hasi, hakuhusiani tu na aliyetema kohozi, bali anaingia yeye na kila aliyeliona akaliacha bila kulifukia, au kulikwangua au mfano wake”.

 

Na hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona mate kwenye ukuta wa Qiblah akayakwangua. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (406) na Muslim (547)].

 

· Faida

 

Afanye Nini Aliyelazimika Kutema Kohozi Akiwa Ndani ya Swalaah?

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona kohozi kwenye Qiblah cha Msikiti. Akawaelekea watu na kusema: ((Inakuwaje mmoja wenu asimame kumwelekea Mola wake halafu ateme kohozi mbele Yake? Je, anapenda mmoja wenu aelekewe kisha atemewe kohozi usoni? Basi ikiwa mmoja wenu atatema kohozi, ateme kushotoni mwake chini ya mguu wake, na kama hatoweza, basi afanye hivi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (550), An-Nasaaiy (1/163) na Ibn Maajah (1022)]. Akatemea kwenye nguo yake, kisha akaipangusia yenyewe kwa yenyewe.

 

· Marufuku Kunadia Kilichopotea Msikitini

 

Misikiti ni sehemu ya ‘’ibaadah, dhikri, na matendo ya utiifu. Haifai kunadiwa humo kitu alichopoteza mtu. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kumsikia mtu akinadia kitu alichopoteza Msikitini, basi aseme: “Kamwe Allaah Asikurejeshee”, kwani Misikiti haikujengwa kwa ajili ya hilo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (568), Abu Daawuud (4790) na Ibn Maajah (767)].

 

· Marufuku Kuuza Na Kununua Msikitini

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin ‘Amri ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kuuza na kununua Msikitini, kuimbwa humo mashairi, kunadiwa humo kilichopotea, na kunyoa ndevu siku ya Ijumaa kabla ya Swalaah. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1079), At-Tirmidhiy (322), An-Nasaaiy (2/47) na Ibn Maajah (766)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mkimwona mwenye kuuza au kununua Msikitini, basi semeni: Kamwe Allaah Asikutilie faida biashara yako)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1321)].

 

Jamhuri wamelichukulia katazo katika Hadiyth hizi kama katazo makruhu.

 

· Faida

 

Ama kuuza mbele ya mlango wa Msikiti (nje yake), huko kunajuzu bila ya ukaraha wowote. Dalili ya hili ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) aliliona guo zuri la mistari mistari linauzwa mbele ya mlango wa Msikiti akasema: “Ee Rasuli wa Allaah!! Ungelinunua hili ukalivaa siku ya Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (886) na Muslim (2068)].

 

· Marufuku Kuimba Mashairi Yasiyo Ya Kimaadili Msikitini

 

Tumeshaieleza Hadiyth Marfu’u ya ‘Abdullah bin ‘Amri isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kuuza na kununua Msikitini na kuimbwa humo mashairi”.

 

Katazo hili linahusiana na uimbaji wa mashairi yasiyo na maadili mema, na yenye kuvuka mpaka wa uwastani kiasi cha kuutoa Msikiti nje ya lengo la kujengwa kwake. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu Hassan bin Thaabit kuwaanikia mapagani maovu yao Msikitini. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “ ’Umar alimpitia Hassan akiwa anaimba Msikitini. Hassan akamwangalia kwa jicho la chaki kisha akasema: “Hakika nilikuwa naimba na yumo humu aliye mbora kuliko wewe”. Kisha akamgeukia Abu Hurayrah akamwambia: “Nakuapia Allaah. Je, umemsikia Rasuli wa Allaah akisema: ((Nijibie mimi (shutuma za makafiri). Ee Allaah! Mtilie nguvu kwa Roho Mtakatifu)). Akasema: “Na’am”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (453) na Muslim (2485)].

 

· Marufuku Kupaza Sauti Msikitini

 

Katika Hadiyth ya As-Saaib bin Zayd ni kwamba ‘Umar aliwaona watu wawili toka Taif wakizungumza kwa sauti akasema: “Mngelikuwa ni wenyeji ningewaadhibu vikali. Mnanyanyua sauti zenu kwenye Msikiti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)!!”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (470)].

 

Tumetangulia kusema nyuma kidogo kwamba ni marufuku kwa wenye kuswali kufanyiana tashwishi, na kunyanyua sauti hata kama ni kwa kusoma Qur-aan.

 

Ninasema: “Hili linachukuliwa ikiwa unyanyuaji wa sauti utakuwa ni wa kukera. Ikiwa haukeri, basi utaruhusiwa kwa ajili ya maslaha kama kudai haki na mfano wake. Ni kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Ka’ab bin Maalik ya kwamba alimdai Ibn Abiy Hadrad deni lake ndani ya Msikiti, sauti zao zikapanda mpaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawasikia akiwa nyumbani kwake. Kisha akawatokea. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (457)]. Hadiyth inaendelea kueleza kwamba hakuwakataza hilo. Pia inaruhusiwa kunyanyua sauti kwa ajili ya kutoa ‘ilmu au kuelezea jambo.

 

· Inajuzu Kuzungumzia Maneno Yenye Faida Msikitini

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samurah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hanyanyuki toka kwenye sehemu yake aliyoswalia Swalaah ya Alfajiri mpaka jua linapochomoza, na jua linapochomoza husimama”. Anasema: “Walikuwa wanazungumza, wakiyagusia masuala ya ujahilia, wakicheka na Rasuli akitabasamu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (670)].

 

· Inajuzu Kula, Kunywa na Kulala Msikitini

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Al-Haarith akisema: “Katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tulikuwa tunakula mkate na nyama Msikitini”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (3300)].

 

Na imethibiti kwamba mwanamke mmoja mweusi alikuwa akiishi Msikitini. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (439)].

 

Na pia Ahlus Swafah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6452) na At-Tirmidhiy (479)].

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema kwamba alikuwa akilala Msikitini naye ni kijana kapera. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7031), Muslim (2479) na wengineo kwa mfano wake].

 

· Inajuzu Kucheza Msikitini Kwa Maslaha

 

Imepokelewa na ‘Aaishah akisema: “Wahabeshi walikuja wakicheza siku ya ‘Iyd. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniita, nami nikaweka kichwa changu juu ya mabega yake, nikawa natizama wanavyocheza mpaka nikaondoka mwenyewe”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5190) na Muslim (892), na tamko ni lake].

 

· Ni Marufuku Kushikanisha Vidole Msikitini

 

Hili tushalielezea kirefu nyuma.

 

· Inajuzu Kumwingiza Mpagani Msikitini Kwa Ajili Ya Maslaha Isipokuwa Msikiti Mtakatifu Wa Makkah

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusiana na kisa cha kumfungia Thumaamah bin Athaal –wakati huo alikuwa ni mpagani- kwenye nguzo moja kati ya nguzo za Msikiti. Kisa kinaeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru aachiliwe katika siku ya tatu. “Akachomoka akaenda kwenye mtende ulioko karibu na Msikiti, akaoga, kisha akaingia Msikitini, akasilimu. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishaelezwa kwenye mlango wa kukoga].

 

Ama Msikiti Mtakatifu wa Makkah, mpagani haruhusiwi kuingia humo kwa Neno Lake Ta’alaa:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا ۚ وَإِنْ خِفْتُمْ عَيْلَةً فَسَوْفَ يُغْنِيكُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ إِن شَاءَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ))

((Enyi walioamini! Hakika washirikiana ni najisi, basi wasikaribie Al-Masjid Al-Haraam baada ya mwaka wao huu. Na mkikhofu umasikini basi Allaah Atakutajirisheni kutokana na fadhila Zake Akitaka. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote)). [At-Tawbah (9:28)]

Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm. [Al-Muhalla (4/243)].

 

· Ni haramu Kujenga Misikiti Juu Ya Makaburi

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Amewalaani Mayahudi na Manaswara. Wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1330) na Muslim (531)].

 

Imepokekewa toka kwa Jun-dub akisema: “Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema kabla hajafariki kwa siku tano: ((Jueni kwamba, hakika waliopita kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Manabii wao na watu wao wema kuwa Misikiti. Basi jueni, msije mkayafanya makaburi kuwa Misikiti. Hakika mimi nawakatazeni na hilo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (532), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (11123) na Ahmad (1/195)].

 

 

Share