048-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Ijumaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

048-Swalaah Ya Ijumaa 

 

Alhidaaya.com

 

 

[Mlango huu umechomolewa kwa muhtasari toka kitabu changu cha Allam-’atu Fiy Aadaab Wa Ahkaamil Jum-’at].

 

· Miongoni Mwa Fadhla Za Siku Ya Ijumaa

 

1- Siku ya Ijumaa ndiyo siku bora zaidi kwa Allaah Ta’aalaa:

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Halichomozi jua wala kuchwa juu ya siku iliyo bora zaidi kuliko siku ya Ijumaa)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/457), ‘Abdul Razzaaq (5563), Ibn Hibaan (2759) na Al-Baghawiy (1062). Ina Hadiyth wenza].

 

Na Allaah Mtukufu Ameiapia katika Kitabu Chake Akisema:

((وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ))

((Na Naapa kwa shahidi na kinachoshuhudiwa)). [Al-Buruwj (85:3)]

 

Abu  Hurayrah kasema: “Siku iliyoahidiwa ni siku ya Qiyaamah, na yenye kushuhudia ni Siku ya Ijumaa, na yenye kushuhudiwa ni siku ya Arafah”.  [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Jariyj (30/82), Al-Haakim (2/519) na Al-Bayhaqiy (3/170). Imesimuliwa ikiwa Marfu’u, lakini si Swahiyh].

 

2- Allaah Mtukufu Alifanya matukio makubwa katika siku hii

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Siku njema kabisa iliyochomokezewa na jua ni Siku ya Ijumaa. Katika siku hii, aliumbwa Aadam, aliingizwa peponi, alitolewa humo, alikubaliwa toba, alikufa na ndiyo siku ya kusimama Qiyaamah. Hakuna mnyama yoyote isipokuwa anakuwa ni mwenye kusikiliza katika Siku ya Ijumaa mpaka jua lichomoze kwa ajili ya kukiogopea Qiyaamah isipokuwa mwanadamu. Katika siku hii, kuna saa ambayo Muislamu haisadifu akiwa {amesimama} anaswali na akamwomba Allaah jambo lolote, isipokuwa Humpa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (584) kwa ufupi, Maalik (1/108) na kwa njia yake Abu Daawuud (1046) na At-Tirmidhiy (491)].

 

3- Ni siku ya sikukuu kwa Waislamu ambapo Allaah Aliwakamilishia Dini Yake na Akawatimizia Neema Yake

 

Imepokelewa toka kwa Twaariq bin Shihaab akisema: “Mtu mmoja katika Mayahudi alikuja kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akamwambia: Ee Amiri wa Waumini! Kuna Aayah katika Kitabu chenu mnaisoma. Lau ingeliteremshwa kwetu jamii ya Mayahudi, basi tungeliifanya siku hiyo sikukuu. Akasema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

 ‘Umar akasema: Hakika tumeijua siku hiyo, na mahala ambapo Aayah iliteremka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama Arafah Siku ya Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (45), Muslim (3017), At-Tirmidhiy (3043) na An-Nasaaiy (8/114)].

 

Imepokelewa toka kwa Anas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Alinijia Jibriyl na mithili ya kioo cheupe, kwenye kioo hicho kuna doa jeusi. Nikasema: Ee Jibriyl! Nini hii? Akasema: Hii ni Ijumaa, Allaah Ameifanya ni sikukuu kwako na kwa Umma wako)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Ya’alaa (4213) na wengineo kwa Sanad Hasan].

 

4- Kuna fadhla kubwa za kuiswali na kuihudhuria

 

Baadhi ya fadhila hizo tutazieleza katika mahala pake Insha-Allaah.

 

· Yanayofanywa Usiku Wa Kuamkia Ijumaa Na Katika Siku Yenyewe

 

1- Ni karaha kuuhusisha usiku wa Ijumaa kwa Swalaah au mchana wake kwa Swaum

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiuhusishe usiku wa Ijumaa kwa Swalaah kutofautisha na masiku mengine, wala msiihusishe siku ya Ijumaa kwa Swaum kutofautisha na siku nyingine isipokuwa iwe katika Swaum anayoifunga mmoja wenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1144), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (2751) na Ahmad (2/444). Na asili yake ni katika Al-Bukhaariy (1985) bila kutaja Swalaah].

 

2- Imesuniwa kusoma Suwrat As Sajdah na Suwrat Al-Insaan katika Swalaah ya Alfajiri yake

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Alfajiri ya Siku ya Ijumaa Alif Laam Miym Tanziyl (As Sajdah) katika rakaa ya kwanza, na katika rakaa ya pili

((هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا))"

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (891), Muslim (880) na wengineo].

 

· Maangalizo Mawili 

 

[Majmu’u Al-Fataawaa (24/205) na Zaad Al-Ma’ad (1/375)].

 

(a) Watu wengi ambao hawakuelimika, wanadhani kwamba makusudio ni kuihusisha Swalaah hii kwa sijdah ya ziada na huiita sijdah ya Ijumaa. Na kama mmoja wao hakuisoma Suwrah hii, basi husoma Suwrah nyingine yenye sijdah. Hili ni kosa, na lililo sawa ni kuwa sijdah imekuja kwa kufuata agizo na si makusudio yake kwamba mwenye kuswali akusudie kuisoma.

 

(b) Haikusuniwa kusoma kwenye Swalaah hiyo Suwrah nyingine ya sajdah kwa makubaliano ya Maulamaa wote.

 

3- Imesuniwa kukithirisha kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Imepokelewa toka kwa Aws akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika katika masiku yenu bora kabisa ni Siku ya Ijumaa. Siku hiyo aliumbwa Aadam, siku hiyo litapulizwa baragumu, na siku hiyo kuna mngurumo wa kutisha. Basi kithirisheni kuniombea rahma, kwani maombi yenu huonyeshwa kwangu)). Mtu mmoja akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Vipi sisi kukuombea wewe rahma kunaonyeshwa kwako nawe ushaoza? Akasema: ((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Ameiharamishia ardhi [kuila] miili ya Manabii)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1047), An-Nasaaiy (3/91), Ibn Maajah (1085) Ahmad (4/8) na wengineo].

 

4- Imesuniwa kusoma Suwrat Al-Kahf

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Sa’iyd ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kusoma Suwrat Al-Kahf Siku ya Ijumaa, basi itamwangazia nuru ya kati ya Ijumaa mbili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (2/368) na Al-Bayhaqiy (3/249)].

 

5- Kukithirisha du’aa kwa matarajio ya kusadifiana na saa ya kujibiwa

 

Tushaielezea Hadiyth Marfu’u ya Abu Hurayrah isemayo: ((Katika siku hii, kuna saa ambayo Muislamu haisadifu akiwa {amesimama} anaswali na akamwomba Allaah jambo lolote, isipokuwa Humpa)). [Hadiyth Swahiyh: Tushaielezea nyuma kidogo].

 

· Saa Ya Kujibiwa Ni Saa Ya Mwisho Baada Ya Alasiri ya Siku ya Ijumaa Kwa Kauli Yenye Nguvu

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Siku ya Ijumaa ni kumi na mbili (yaani saa). Hapatikani Muislamu anayemwomba Allaah Azza wa Jalla chochote isipokuwa Allaah Azza wa Jalla Humpa. Basi ipanieni kimakusudi saa ya mwisho baada ya Alasiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1047) na An-Nasaaiy (3/99), na tamko ni lake].

 

 Na imepokelewa toka kwa Anas akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Ipanieni kimakusudi saa ambayo hutarajiwa katika Siku ya Ijumaa baada ya Alasiri mpaka kuchwa jua)). [Hadiyth Hasan kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (489), na kwa njia ya Al-Baghawiy (1051). Angalia Swahiyh At-Targhiyb (793)].

 

· Hukmu ya Swalaah ya Ijumaa

 

Swalaah ya Ijumaa ni Fardhi ‘Ayn kwa kila Muislamu aliyebaleghe isipokuwa  yule ambaye dalili imemtoa kando. Asili ya ufaradhi wake ni kutoka kwenye Qur-aan, Sunnah na Ijma’a ya Umma:

 

1- Allaah Amesema:

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))

(( Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua)). [Al-Jum-‘ah (62:9)]

 

2- Imepokelewa toka kwa Hafswah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kwenda Ijumaa ni wajibu kwa kila aliye baleghe, na ni lazima kwa mwenye kwenda Ijumaa akoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An Nasaaiy (3/89), Abu Daawuud (342), Ibn Al-Jaaruwd (287) na Al-Bayhaqiy (3/172)].

 

3- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar na Abu Hurayrah ya kwamba wamemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa juu ya vigogo vya mimbari yake akisema: ((Watakoma watu kuacha Swalaah za Ijumaa, au Allaah Atawapiga muhuri kwenye nyoyo zao, kisha watakuwa ni miongoni mwa wenye kughafilika)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (865), An-Nasaaiy (3/88), Ibn Maajah (794) na Ad-daaramiy (1570)].

 

4- Imepokelewa toka kwa Abul Ja’ad Adw-Dwamariy akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuacha ijumaa tatu bila ya udhuru, basi atapigwa muhuri kwenye moyo wake)). [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1052), At-Tirmidhiy (500), An-Nasaaiy (3/88) na Ibn Maajah (1125)].

 

5- Imepokelewa toka kwa Ibn Mas-’oud ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia watu wasiokwenda Ijumaa: ((Nilikusudia nimwamuru mtu aswalishe watu, kisha mimi niende kuwachomea moto watu wasiohudhuria Ijumaa nyumba zao)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (4398), An-Nasaaiy (2/100), Ad-daaramiy (2/171), Ibn Maajah (2041) na Ahmad (6/100)].

 

6- Waislamu wote wamekubaliana juu ya wajibu wa Ijumaa. Lakini mvutano ulioko ni je, Ijumaa ni Fardhi ‘Ayn au Fardhi Kifaayah? [Al-Mughniy (2/111) chapa ya Al-Fikr na Badaai’u As-Swanaai’i (1/256)]..

 

Na kutokana na dalili zilizotangulia, inabainika kwamba ni Fardhi ‘Ayn. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Walio Nje Ya Wigo Wa Wajibu

 

Ni mtoto, mwanamke, mtumwa anayemilikiwa, mgonjwa, msafiri na wengineo wenye nyudhuru. Ikiwa yeyote katika hawa ataiswali, basi Swalaah yake ni sahihi na faradhi ya Adhuhuri itamwondokea.

 

Imepokelewa toka kwa Twaariq bin Shihaab kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ijumaa ni haki wajibu kwa kila aliye baleghe isipokuwa wanne: Mtumwa mmilikiwa, mwanamke, mtoto na mgonjwa)). [Hadiyth Hasan kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1067), Ad-daaraqutwniy (2/3) na Al-Bayhaqiy (3/183). Angalia Al-Irwaa (3/57)].

 

Imepokelewa na Jaabir kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi ni juu yake Ijumaa Siku ya Ijumaa isipokuwa mgonjwa, au msafiri, au mwanamke au mtoto au mtumwa)).

 

Nyudhuru nyingine zinazomruhusu Muislamu asiende kuswali Ijumaa ni baridi na mvua. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: “Ni kwamba yeye alimwambia mwadhini wake katika siku ya mvua kubwa: Utakaposema

أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن محمدا رسول الله , basi usiseme: حي على الصلاة , bali sema: صلوا في بيوتكم (swalini majumbani mwenu). Watu wakawa kana kwamba wameshangazwa na hilo naye akawauliza: Mnashangazwa na hili? Hakika alilifanya hili aliyekuwa mbora kuliko mimi. Hakika Ijumaa ni azma, na mimi nimeona tabu kuwatoeni, mkatembea kwenye tope na utelezi”. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishaelezwa].

 

 

Share