068-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kujichunga na Kuacha Mambo Yenye Shaka

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب الورع وترك الشبهات

068-Mlango Wa Kujichunga na Kuacha Mambo Yenye Shaka

 

Alhidaaya.com

 

 

قَالَ الله تَعَالَى

وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

Na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno. [An-Nuwr: 15]

إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ ﴿١٤﴾

Hakika Rabb wako bila shaka Yu tayari Awavizia. [Al-Fajr: 14]

 

 

 

Hadiyth – 1

وعن النعمان بن بشيرٍ رضي الله عنهما ، قَالَ : سَمِعْتُ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، يقول : ((  إنَّ الحَلاَلَ بَيِّنٌ ، وَإنَّ الحَرامَ بَيِّنٌ ، وَبَيْنَهُمَا مُشْتَبَهَاتٌ لاَ يَعْلَمُهُنَّ كَثيرٌ مِنَ النَّاسِ ، فَمَنِ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ ، اسْتَبْرَأَ لِدِينهِ وَعِرْضِهِ ، وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ وَقَعَ في الحَرَامِ ، كَالرَّاعِي يَرْعَى حَوْلَ الحِمَى يُوشِكُ أنْ يَرْتَعَ فِيهِ ، ألاَ وَإنَّ لكُلّ مَلِكٍ حِمَىً ، ألاَ وَإنَّ حِمَى اللهِ مَحَارِمُهُ ، ألاَ وَإنَّ فِي الجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَت صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ ، وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ ، ألاَ وَهِيَ القَلْبُ )) متفقٌ عَلَيْهِ ، وروياه مِنْ طرقٍ بِألفَاظٍ متقاربةٍ .

Imepokewa kutoka kwa An-Nu'maan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika halali iko wazi na haramu iko wazi; na baina ya vitu hivi viwili kuna mambo yenye shaka, watu wengi hawayajui. Basi mwenye kuepuka mambo yenye shaka, hakika amehifadhi Dini yake na heshima yake. Na mwenye kuingia kwenye mambo ya shaka ameingia kwenye haramu, kama mchunga anayechunga pambizoni mwa mpaka anachelea kulisha humo, jueni, hakika kila mfalme ana mpaka, na jueni kuwa hakika mwili kuna kinofu, kikitengemaa utatengemaa mwili wote, kikiharibika utaharibika mwili wote, jueni kuwa huo ni moyo." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 2

وعن أنسٍ رضي الله عنه : أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلم وَجَدَ تَمْرَةً فِي الطَّرِيقِ ، فَقَالَ : ((  لَوْلاَ أنِّي أخَافُ أنْ تَكُونَ مِنَ الصَّدَقَة لأَكَلْتُهَا )) متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwake Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliona tende njiani, akasema: "Lau kama mimi sikuhofia kuwa hii tende ni ya swadaqah ningeila." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 3

وعن النَّواسِ بن سمعان رضي الله عنه ، عن النبيِّ صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : ((  البِرُّ : حُسْنُ الخُلُقِ، وَالإِثْمُ : مَا حَاكَ فِي نَفْسِكَ ، وَكَرِهْتَ أنْ يَطَّلِعَ عَلَيْهِ النَّاسُ )) رواه مسلم.

Imepokewa kutoka kwa An-Nawwaas bin Sam'aan ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: "Kutenda wema ni tabia nzuri, na kitendo kiovu ni chenye kukukera katika nafsi yako na ukachukia watu wakuone nacho." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن وَابِصَةَ بن مَعبدٍ رضي الله عنه ، قَالَ: أتَيْتُ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، فَقَالَ: (( جئتَ تَسْألُ عَنِ البِرِّ ؟ )) قُلْتُ : نَعَمْ ، فَقَالَ : ((  اسْتَفْتِ قَلْبَكَ ، البرُّ : مَا اطْمَأنَّت إِلَيْهِ النَّفسُ ، وَاطْمأنَّ إِلَيْهِ القَلْبُ ، وَالإثْمُ : مَا حَاكَ في النَّفْسِ ، وَتَرَدَّدَ فِي الصَّدْرِ ، وَإنْ أفْتَاكَ النَّاسُ وَأفْتُوكَ )) حديث حسن ، رواه أحمد والدَّارمِيُّ في مُسْنَدَيْهِمَا .

Imepokewa kutoka kwake Waabiswah bin Ma'bad (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba nilikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye akaniuliza: "Je, umekuja kuuliza juu ya kutenda wema?" Nikamwambia: "Ndio." Akasema: "Ushauri moyo wako. Kutenda wema ni kufanya lenye kutuliza nafsi, na ukatulia moyo; na kitendo kiovu ni chenye kukera kwenye nafsi na kutaradadi kifuani hata kama wamekutolea fatwa watu (kuwa chafaa)." [Hadiyth Hasan, imepokewa katika Musnadi mbili: Ahmad bin Hambal na Ad-Daarimiyy]

 

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي سِرْوَعَةَ عُقبَةَ بنِ الحارِثِ رضي الله عنه : أنَّهُ تَزَوَّجَ ابنَةً لأبي إهَابِ بن عزيزٍ ، فَأتَتْهُ امْرَأةٌ ، فَقَالَتْ : إنّي قَدْ أرضَعْتُ عُقْبَةَ وَالَّتِي قَدْ تَزَوَّجَ بِهَا . فَقَالَ لَهَا عُقْبَةُ : مَا أعْلَمُ أنَّك أرضَعْتِنِي وَلاَ أخْبَرْتِني ، فَرَكِبَ إِلَى رسول الله صلى الله عليه وسلم بِالمَدِينَةِ ، فَسَأَلَهُ : فَقَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((  كَيْفَ ؟ وَقَد قِيلَ )) فَفَارَقَهَا عُقْبَةُ وَنَكَحَتْ زَوْجاً غَيْرَهُ . رواه البخاري .

Imepokewa kutoka kwa Abu Sirwa'ah 'Uqbah bin Al-Haarith (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba alimuoa bint wa Abu Wahaab bin 'Aziyz, akaja kwake mwanamke alliyemwambia: "Hakika mimi nimemnyesha 'Uqbah na mkewe." 'Uqbah akamwambia: "Sijui kama wewe umeninyonyesha wala hujanijulisha hilo." Akafunga safari kuelekea Madiyah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na alipofika alimuuliza (kuhusu jambo hilo). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: "Vipi, na tayari ushaelezwa?" 'Uqbah alimuacha mkewe huyo na kuoa mwanamke mwengine." [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 6

وعن الحسن بن علي رضي الله عنهما ، قَالَ : حَفِظتُ من رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((  دَعْ مَا يريبُكَ إِلَى ما لاَ  يَرِيبُكَ )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Imepokewa kutoka kwa Al-Hasan bin 'Ali (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kuwa alisema: "Nimehifadhi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka." [At-Tirmidhiy, na akasema kuwa ni Hadiyth Hasan]

 

 

Hadiyth – 7

وعن عائشة رضي الله عنها ، قالت : كَانَ لأبي بَكر الصديق رضي الله عنه غُلاَمٌ يُخْرِجُ لَهُ الخَرَاجَ ، وَكَانَ أَبُو بَكْرٍ يَأكُلُ مِنْ خَرَاجِهِ ، فَجَاءَ يَوْماً بِشَيءٍ ، فَأكَلَ مِنْهُ أَبُو بَكْرٍ ، فَقَالَ لَهُ الغُلامُ : تَدْرِي مَا هَذَا ؟ فَقَالَ أَبُو بكر : وَمَا هُوَ ؟ قَالَ : كُنْتُ تَكَهَّنْتُ لإنْسَانٍ في الجَاهِلِيَّةِ وَمَا أُحْسِنُ الكَهَانَةَ ، إِلاَّ أنّي خَدَعْتُهُ ، فَلَقِيَنِي ، فَأعْطَانِي لِذلِكَ ، هَذَا الَّذِي أكَلْتَ مِنْهُ ، فَأدْخَلَ أَبُو بَكْرٍ يَدَهُ فَقَاءَ كُلَّ شَيْءٍ فِي   بَطْنِهِ . رواه البخاري .

Imepokewa kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amesema: Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu)alikuwa na kijana aliyekuwa akimtolea mapato. Abu Bakr alikuwa akila humo. Akaja siku moja na kitu na  Abu Bakr akala. Kijana Akamwambia: "Unajua nini hiki?" Akasema Abu Bakr: "Ni nini hicho?" Akasema: "Nilimfanyia uchawi mtu katika jahiliyyah (ujinga) na sikujua uchawi ila nilimhadaa. Alikutana nami na kunipa kitu hicho ambacho umekula." Abu Bakr alitia mkono wake kwenye mdomo na kutapika chote kilichokuwa ndani ya tumbo lake." [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 8

وعن نافِع : أن عُمَرَ بن الخَطّاب رضي الله عنه كَانَ فَرَضَ لِلمُهَاجِرينَ الأَوَّلِينَ أرْبَعَةَ الآفٍ وَفَرَضَ لابْنِهِ ثَلاَثَة آلافٍ وَخَمْسَمئَةٍ ، فَقيلَ لَهُ : هُوَ مِنَ المُهَاجِرينَ فَلِمَ نَقَصْتَهُ ؟ فَقَالَ : إنَّمَا هَاجَرَ بِهِ أبُوهُ . يقول : لَيْسَ هُوَ كَمَنْ هَاجَرَ بِنَفْسِهِ . رواه البخاري .

Imepokewa kutoka kwa Naafi' kwamba 'Umar bin Al-Khattaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa anawapatia Muhaajiriyn wa mwanzo elfu arobaini na akawa anampatia mtoto wake elfu tatu na mia tano. Akaambiwa: "Yeye pia ni miongoni mwa Muhaajiriyn kwa nini unampunguzia kiwango chake?" Akawaambia: "Hakika yeye alihama na babake, hivyo hawi sawa na yule aliyehama pake yake." [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 9

وعن عَطِيَّةَ بن عُروة السَّعْدِيِّ الصحابيِّ رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم : ((  لاَ يَبْلُغُ الْعَبدُ أنْ يَكُونَ منَ المُتَّقِينَ حَتَّى يَدَعَ مَا لاَ بَأسَ بِهِ ، حَذَراً مِمَّا بِهِ بَأسٌ )) رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن )) .

Imepokewa kutoka kwa 'Atiyyah bin 'Urwah As-Sa'adiy amabaye ni Swahaaba (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakuna mja atakayefika daraja ya uchamngu mpaka aache yale mambo yasiyo na tatizo lolote kama tahadhari kwa yale yenye madhara." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan]

 

 
Share