011-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Nyama Ya Punda Wa Mjini

 

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

Alhidaaya.com

 

 

011-Vyakula Vilivyoharamishwa Na Hadiyth Za Rasuli

Nyama Ya Punda Wa Mjini  

 

 

Vilivyoharamishwa Na Hadiyth Za Rasuli

 

 

1-  Nyama Ya Punda Wa Mjini

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wote wameharamisha kula nyama ya punda wa mjini kutokana na Asaaniyd zilizothibiti kwa uwazi kabisa ya kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha nyama ya punda wa mjini.  Kati ya Asaaniyd hizo ni:

 

1-  Hadiyth ya Anas:

 

"أَنً رَسُوْلَ اللهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ أَمَرَ مُنَادِيًا فَنَادَى : إِنَّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ يَنْهَيَانِكُمْ عَنْ لُحُومِ الْحُمُرِ الأَهْلِيَّةِ، فَإِنَّهَا رِجْسٌ‏.‏ فَأُكْفِئَتِ الْقُدُورُ وَإِنَّهَا لَتَفُورُ بِاللَّحْمِ‏"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru mwenye kunadi akatangaza:  Hakika Allaah na Rasuli Wake wanawakatazeni nyama ya punda wa mjini, kwani nyama yake ni mbaya, si salama.  Vyungu vikamwagwa vikiwa vinachemka nyama”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5528) na Muslim (1940)].

 

2-  Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah:

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى يَوْمَ خَيْبَرَ عَنْ لُحُومِ الْحُمُرِ الْأَهْلِيَّةِ وَأَذِنَ فِي لُحُومِ الْخَيْلِ"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza Siku ya Khaybar nyama ya punda wa mjini, na akaruhusu nyama ya farasi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4219) na Muslim (1941)].

 

Baadhi ya wafuasi wa dhehebu la Maalik –na hii ni kauli yenye nguvu zaidi kwao- wanasema nyama ya punda wa mjini huliwa pamoja na ukaraha wa “tanziyh”, yaani ukaraha au katazo hafifu lisilo na dhambi!!

 

Na imesimuliwa kuhusiana na Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah kwamba wao walikuwa wakiichukulia kama ilivyo Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَن يَكُونَ مَيْتَةً"

 

“Sema: Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahyi kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu”.  [Al-An’aam: 145].

 

Na lililopokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Abbaas ni kuwa yeye alisita kuhusiana na Aayah hii na kusema:  “Sijui kama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikataza kwa sababu punda walikuwa wanawabebea watu  mizigo, na hivyo akachukia wabebaji wao kumalizika, au aliharamisha Siku ya Khaybar nyama ya punda wa mjini”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4227) na Muslim (1939)].

 

Tukiachilia yote hayo,  Ibnu ‘Abdul Barr amesema:  “Hakuna makhitalifiano baina ya ‘Ulamaa wa Kiislamu leo kuhusiana na kuharamishwa nyama ya punda”.

 

Ninasema: “Kuharamishwa kwake kumethibiti uthibitisho usioweza kupingika kutokana na wingi wa upokezi juu ya hili (tawaatur).  Uthibitisho huu ni hoja kwa kila mtu, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Faida Mbili:

 

Ya Kwanza:  Nyama Ya Punda Milia Ni Halali

 

‘Ulamaa wote wamekubaliana hili.  Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikula yeye pamoja na Maswahaba Wake.

 

Katika Hadiyth ya Abuu Qataadah:

 

"أنَّهُ كانَ مَعَ قَوْمٍ مُحْرِمِيْنَ – وَهُوَ حَلَّالٌ- فَسَنَحَ لَهُمْ حُمُرٌ وَحْشٌ ، فَحَمَلَ عَلَيْهَا أَبُوْ قَتَادَةِ فَعَقَرَ مِنْهَا أَتَانًا فَأَكَلُوْا مِنْهَا وَقَالُوْا : نَأْكُلُ مِنْ لَحْمِ صَيْدٍ وَنَحْنُ مُحْرِمُوْنَ؟ فَحَمَلُوْا مَا بَقِيَ مِنْ لَحْمِهَا ، فَقَالَ رَسُوْلُ اللهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ : "كُلُوا مَا بَقِيَ مِنْ لَحْمِهَا"

 

“Ni kwamba yeye alikuwa pamoja na watu waliokuwa wamehirimia (Hijja) hali ya kuwa yeye hakuhirimia.  Punda milia wakawajia karibu yao, na Abu Qataadah akawawinda na kuwapata, akamchinja jike kati yao kisha wakala sehemu ya nyama yake.  Halafu wakajiuliza:  Hivi tunakula nyama ya kuwinda na sisi tumehirimia?!  Wakabeba nyama iliyobaki, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: “Kuleni nyama yake iliyobakia”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1824) na Muslim (1196)].

 

Na katika riwaayah, ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza:

 

"هَلْ مَعَكُمْ مِنْهُ شَيْءٌ؟  قَالُوْا: مَعَنَا رِجْلُهُ، قَالَ: فَأَخَذَهَا رَسُوْلُ اللهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ فَأَكَلَهَا"

 

“Je, mna chochote chake kilichosalia?  Wakasema:  Tuna mguu wake.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauchukua akaula”.

 

 

Ya Pili:  Ni Halali Kula Nyama Ya Farasi

 

[Al-Badaai’u (5/38), Ad-Dusuwqiy (2/117), Al-Majmuw’u (9/5), Al-Mughniy (11/66 pamoja na sharhu), Subulus salaam (4/87) na Naylul Awtwaar (8/125)].

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa; Mashaafi’iy na Mahanbali, nayo ni kauli ya Maalik pia, pamoja na Jumhuwr ya Maswahaba na Taabi’iyna, hawa msimamo wao ni kuwa ni halali kula nyama ya farasi, ni sawa akiwa farasi wa asili ya Kiarabu au asili nyingine.  Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth ya Jaabir:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ يَوْمَ خَيْبَرَ عَنْ لُحُومِ الْحُمُرِ الأَهْلِيَّةِ وَأَذِنَ فِي لُحُوْمِ الخَيْلِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza Siku ya Khaybar nyama ya punda wa mjini, lakini aliruhusu nyama ya farasi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4219) na Muslim (1941)].

 

2-  Hadiyth ya Asmaa bint Abiy Bakr:

 

"نَحَرْنَا عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اَللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ فَرَساً فَأَكَلْنَاهُ وَنَحْنُ  بِالمدِيْنَةِ"

 

“Tulichinja farasi enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tukamla, nasi tuko Madiynah”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5510) na Muslim (1196)].

 

Lakini Mahanafiy, ikiwa pia ni kauli ya pili ya Wamaalik, nayo pia ni kauli ya Ibn ‘Abbaas, wao wanaona kwamba kuna ukaraha au uharamisho wa kula nyama ya farasi.  Hoja yao ni:

 

1-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً"

 

“Na farasi, na baghala, na punda, ili muwapande na wawe mapambo”.  [An-Nahl: 08].

 

Wanasema:  Kufupisha manufaa yake katika kupandwa na kuwa mapambo tu, kunadulisha kwamba wanyama hawa si wa kuliwa, kwani lau kama wangelikuwa ni wa kuliwa, basi Allaah Angelisema:

 

"وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ"

 

“Na miongoni mwao mnawala”.

 

Hoja hii inajibiwa hivi:  Kwamba Aayah hii ilishuka Makkah kwa makubaliano ya Mufassiruna wote, na ruksa ya kula ilikuja baada ya Hijrah.  Isitoshe, Aayah haigusii katazo la kula huku zikiwepo Ahaadiyth zilizo wazi kabisa katika kuhalalisha.

 

2-  Yanayohadithiwa toka kwa Khaalid bin Al Waliyd (Radhwiya Allaah ‘anhu):

 

"أَنَّ النَّبِيَ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنْ أَكْلِ لُحُومِ الْخَيْلِ وَالبِغَالِ وَالحَمِيرِ ، وَكُلِّ ذِيْ نَابٍ مِنَ السِبَاعِ ، وَكُلِّ  ذِيْ مِخْلَبٍ مِنَ الطَّيْر"ِ

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kula nyama ya farasi, baghala na punda, na kila mnyama mwenye meno katika wanyama wakali, na kila mwenye kucha katika ndege”.  [Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haitolewi hoja kwayo, nayo imekharijiwa na An Nasaaiy (4332), Abu Daawuwd (3790), Ibn Maajah (3198) na Ahmad (16214)].

 

Lililo sahihi ni kauli ya Jumhuwr isemayo kuwa kula farasi ni halali.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

 

 

Share