012-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kila Mnyama Mkali Mwenye Kucha
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا
Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi
012-Vyakula Vilivyoharamishwa Na Hadiyth Za Rasuli
Kila Mnyama Mkali Mwenye Kucha
2- Kila Mnyama Mkali Mwenye Kucha
Mnyama yeyote mwenye meno anayoulia kwayo kiwindwa, ni sawa akiwa mnyama mkali kama simba, mbwa mwitu, chui, chita na kadhalika, au mnyama wa kienyeji anayeishi na watu kama mbwa na paka, hawa wote si halali kuliwa kwa mujibu wa kauli ya Jumhuwr. Na hii ni kwa dalili zifuatazo:
1- Hadiyth ya Abu Hurayrah:
"كُلُّ ذِي نَابٍ مِنَ السِّباعِ فأَكْلُهُ حَرَامٌ"
“Kila mnyama mkali mwenye meno, kumla ni haramu. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1933)].
2- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ ُ َكُلِّ ذِيْ نَابٍ مِنَ السِّبَاعِ، وَعَنْ كُلِّ ذِيْ مِخْلَبٍ مِنَ الطَّيْرِ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila mwenye meno katika wanyama wakali, na kila mwenye kucha katika ndege”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1934), Abu Daawuwd (3785) na An Nasaaiy (7/206)].
3- Toka kwa Abu Az Zubayr:
"سَأَلْتُ جَابِرًا عَنْ ثَمَنِ الْكَلْبِ، وَالسِّنَّوْرِ. قَالَ: زَجَرَ النَّبِيُّ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ ذَلِكَ"
“Nilimuuliza Jaabir kuhusu bei ya mbwa na paka. Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuhusu hilo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1569)].
Imethibiti vile vile toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنً اللهَ إِذَا حَرًمَ عَلَى قَوْمٍ أَكْلَ شَيْءٍ حَرًمَ عَلَيْهِمْ ثَمَنَهُ"
“Hakika Allaah Anapowaharamishia watu kula kitu, Huwaharamishia pia thamani yake (kukiuza au kukinunua)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3488) na wengineo. Ina Hadiyth mwenza kwenye Swahiyh Mbili].
Faida:
Sungura Ni Halali Kuliwa
Ni halali kula sungura kwa mujibu wa rai ya Jumhuwr. Ni kwa Hadiyth ya Anas aliyesema:
"أَنْفَجْنَا أَرْنَبًا فَسَعَى الْقَوْمُ فَلَغَبُوا، فَأَخَذْتُهَا وجِئْتُ بِهَا إِلَى أَبِي طَلْحَةَ فَذَبَحَهَا، فَبَعَثَ بِوَرِكِهَا أَوْ قَالَ بِفَخِذِهَا إِلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَبِلَهُ"
“Mara moja tulimchokonoa sungura (toka ndani ya shimo lake akatoka), watu wakamfukuza na hatimaye wakachoka hoi. (Mimi nilimkimbiza mpaka nikamkamata), nikamchukua na kwenda naye kwa Abu Twalha, akamchinja, na akapeleka paja lake kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akalipokea”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al Bukhaariy (2572) na Muslim (1953)].
Na kwa vile sungura pia ni katika wanyama wanaopendeka, hawana meno ya kujeruhi, na hakuna matini yoyote inayogusia kuharamishwa kwake. [Al-Badaai’u (5/39), As Swaawiy (1/322), Nihaayatul Muhtaaj (8/143), Al-Mughniy (11/81) pamoja na Ash Sharhul Kabiyr, na Al Muhallaa (7/432)].