003-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Yanayoruhusiwa katika Kusengenya
Riyaadhw Asw-Swaalihiyn
باب مَا يباح من الغيبة
003-Mlango Wa Yanayoruhusiwa katika Kusengenya
Jua ya kwamba kuseng'enya kunakubalika kwa lengo sahihi linalo kubaliwa na sheria ambalo haliwezi kufikiwa ila kwa kufanya hivyo. Nazo ni sababu Sita:
1) Kudhulumiwa: Inafaa kwa aliyedhulumiwa kupeleka mashtaka yake kwa Sultani, Kadhi na watu wengineo wenye mamlaka au uwezo wa kumrudishia haki yake kutoka kwa dhalimu kwa kusema: "Fulani amenidhulumu kwa kitu kadha."
2) Kutaka usaidizi katika kubadilisha Munkar na kumrudisha aliye asi katika njia ya sawa, kwa kusema: "Na aseme kumwambia yule ambae anatarajiwa uwezo wake katika kuondoa Munkar fulani anafanya kadha, hivyo mzuilie na mfano wake huo." Na makusudio yake yanakuwa ni kufikia katika kuondosha Munkar, na ikiwa hatakuwa na lengo hilo basi itakuwa ni haramu.
3) Kutaka Fatwa: Hivyo kumwambia mufti: "Babangu au ndugu yangu au mume wangu au fulani amenidhulumu kwa kitu kadha. Je, ana haki nacho hicho? Na njia gani nitatumia kumalizana naye na kupata haki yangu na kuondosha dhulma? Na mfano wa hayo. Jambo hili linakubaliwa kwa haja. Lakini iliyo bora zaidi ni kusema: "Unasemaje kuhusu mtu, ambaye ana jambo fulani? Katika kufanya hivyo atapata lengo lake bila ya kumtaja yule mtu mwenyewe. Pamoja na hivyo, kutaja jina la mtu inakubaliwa kama tutakavyo taja mfano wa Hind in shaa Allaah Ta'aalaa.
4) Kuwatahadharisha Waislamu na shari na kuwanasihi, na hilo ni kwa njia zifuatazo:
i) Miongoni mwayo ni kuwakosoa wapokezi na mashahidi (wa Hadiyth za Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hilo ni jaizi kwa kukubaliwa na waaislamu wote. Bali jambo hilo ni wajibu kwa haja.
ii) Kutaka ushauri katika kutaka mahusiano ya kindoa na mwanadamu au kushirikiana naye au kuweka amana kwake au kuamiliana naye au mengineyo mbali na hayo au kutaka kuwa jirani yake. Na inapasa kwa mwenye kutoa ushauri asifiche hali yake bali ataje ubaya wake ikiwa upo ambao anao kwa njia ya nasiha.
iii) Anapomuona Fakihi anaingia katika Bid'ah (uzushi) au fasili ambaye anafundisha elimu na akahofu huenda akadhurika yule Fakihi kwa kufanya hivyo. Inatakiwa apatiwe nasaha ya kubainisha hali yake kwa sharti awe na nia nzuri. Na hili ni jambo ambalo hukosewa. Na hakika huenda mzungumzaji akabeba katika hilo chuki na hivyo shetani humvalisha yeye hilo. Na kumpatia yeye matumaini kuwa amemnasihi, hivyo kupata ufahamu juu ya jambo hilo.
iv) Kuwa na mlezi ambaye hatekelezi wajibu wake inavyotakiwa: Hii ni kutokana kuwa si mtu mwema kwake na ima ni fasiki au ameghafilika na wajibu wake na mfano wa hayo. Ni wajibu kukumbushwa hilo kwa yule mwenye jukumu la ulezi kwa ujumla kujivua na kazi hiyo na kumpatia mtu mwengine ambaye anafaa au kuambiwa aamiliane naye kwa ile hali aliyo nayo wala asimpoteze. Na afanye juhudi katika kumuhimiza juu ya kusimama imara (Istiqaamah) au kumbadilisha.
5) Kufanya ufasiki na ufisadi kwa dhahiri au kuzua kama mfano wa anaye kunywa pombe wazi wazi na kuwaonea watu na kuchukua ushuru na mkusanyaji wa mali kwa dhulma na kutawala katika mambo kwa batili. Hivyo, inafaa kumtaja kwa anayo yadhihirisha na ni haramu kumtaja kwa aibu asiyokuwa nayo isipokuwa kufaa kwake kuwe ni kwa sababu nyengine katika yale tuliyoyataja.
6) Kumtambua na kumtambulisha: Ikiwa mtu tayari anajulikana kwa lakabu kama ya kilema, au kiziwi, au kipofu, au kengeza na mengineyo. Kwa hayo inajuzu, lakini haifai (na ni haramu) kutumia jina hilo kumtweza na kumdhalilisha. Na lau inawezekana kumtambulisha kwa yasiyokuwa hayo basi itakuwa bora zaidi.
Hizi sababu sita, wamezitaja wanazuoni na nyingi kati ya hizo wamekubaliyana kwazo. Na dalili ya nukta hizi ni Hadiyth nyingi Swahiyh na mashuhuri. Na miongoni mwazo ni:
Hadiyth – 1
عن عائشة رَضِيَ اللهُ عنها : أنَّ رجلاً اسْتَأذَنَ عَلَى النبيّ صلى الله عليه وسلم ، فَقَالَ : (( ائْذَنُوا لَهُ ، بِئسَ أخُو العَشِيرَةِ ؟ )) . متفق عَلَيْهِ .
Imepokewa kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba mtu mmoja alitaka idhini kumuona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye alisema: "Mpatieni idhini aingie; ni mtu mbaya katika kabila lake." [Al-Bukhaariy na Muslim] Al-Bukhaariy ameitolea hoja katika kuruhusu kuwasengenya mafisadi na waenezaji fitina.
Hadiyth – 2
وعن عائشة رَضِيَ اللهُ عنها ، قالت : قَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( مَا أظُنُّ فُلاناً وفُلاناً يَعْرِفانِ مِنْ دِينِنَا شَيْئاً )) . رواه البخاري .
Imepokewa kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Sidhanii kuwa fulani na fulani wanajua chochote katika Dini yetu." [Al-Bukhaariy]. Amesema Al-Layth bin Sa'ad, mmoja wa wapokezi wa Hadiyth hii: "Watu hawa wawili walikuwa ni wanafiki."
Hadiyth – 3
وعن فاطمة بنتِ قيسٍ رَضِيَ اللهُ عنها ، قالت : أتيت النبيَّ صلى الله عليه وسلم ، فقلتُ : إنَّ أَبَا الجَهْم وَمُعَاوِيَةَ خَطَبَانِي ؟ فَقَالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( أمَّا مُعَاوِيَةُ ، فَصُعْلُوكٌ لاَ مَالَ لَهُ ، وأمَّا أَبُو الجَهْمِ ، فَلاَ يَضَعُ العَصَا عَنْ عَاتِقِهِ )) متفق عَلَيْهِ .
وفي رواية لمسلم : (( وَأمَّا أَبُو الجَهْمِ فَضَرَّابٌ لِلنِّساءِ )) وَهُوَ تفسير لرواية : (( لا يَضَعُ العَصَا عَنْ عَاتِقِهِ )) وقيل : معناه : كثيرُ الأسفارِ .
Amesema Faatwimah bint Qays (Radhwiya Allaahu 'anhaa): Nilikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikamwambia: "Hakika Abul Jahm na Mu'awiyah wameniposa?" Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ama Mu'awiyah ni masikini na hana mali yoyote na ama Abul Jahm fimbo yake haitoki kwenye mabega yake." [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na katika riwaayah ya Muslim: "Na ama Abul Jahm ni mtu anaye piga wanawake sana." Na hii ni tafsiri ya riwaayah yenyewe: "Haachi fimbo begani mwake." Na inasemekana: "Maana yake ni anasafiri sana."
Hadiyth – 4
وعن زيد بن أرقم رَضِيَ اللهُ عنه قَالَ : خرجنا مَعَ رسُولِ الله صلى الله عليه وسلم في سَفَرٍ أصَابَ النَّاسَ فِيهِ شِدَّةٌ ، فَقَالَ عبدُ اللهِ بن أُبَيّ : لاَ تُنْفِقُوا عَلَى مَنْ عِندَ رسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم حَتَّى يَنْفَضُّوا ، وقال : لَئِنْ رَجَعْنَا إِلَى المَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الأَعَزُّ مِنْهَا الأَذَلَّ ، فَأَتَيْتُ رسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم ، فَأخْبَرْتُهُ بذلِكَ ، فَأرْسَلَ إِلَى عبدِ الله بن أُبَيِّ ، فَاجْتَهَدَ يَمِينَهُ : مَا فَعلَ ، فقالوا : كَذَبَ زيدٌ رَسُولَ الله صلى الله عليه وسلم ، فَوَقَعَ في نَفْسِي مِمَّا قَالُوهُ شِدَّةٌ حَتَّى أنْزلَ اللهُ تَعَالَى تَصْدِيقِي : [ إِذَا جَاءكَ المُنَافِقُونَ ] ثُمَّ دعاهُمُ النبيّ صلى الله عليه وسلم لِيَسْتَغْفِرَ لَهُمْ فَلَوَّوْا رُؤُوسَهُمْ . متفق عَلَيْهِ .
Amesema Zayd bin Arqam (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari ambayo watu katika safari hiyo walipatwa na matatizo. 'Abdullaah bin Ubayy aliwaambia watu wake, walio kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) msiwape kitu mpaka wamuache. Na akasema: 'Kama tutarudi Madiynah, wenye nguvu watawatoa wanyonge humo'. Nikamwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza kuhusu suala hilo naye akaapa kuwa hakusema hayo. Wakasema: 'Zayd amemuogopea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)'. Walichokisema kikanipa matatizo nafsini mwangu mpaka Allaah Aliposhusha thibitisho la ukweli wangu katika, "Wanapokujia (ee Muhammad صلى الله عليه وسلم ) wanafiki." [Al-Munaafiquwn: 1]. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaita ili awaombee maghfira wakageuza vichwa vyao wakakataa." [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hadiyth – 5
وعن عائشة رَضِيَ اللهُ عنها ، قالت : قالت هِنْدُ امْرَأةُ أَبي سفْيَانَ للنَّبيِّ صلى الله عليه وسلم : إنَّ أَبَا سُفْيَانَ رَجُلٌ شَحِيحٌ وَلَيْسَ يُعْطِينِي مَا يَكْفيني وولَدِي إِلاَّ مَا أَخَذْتُ مِنْهُ، وَهُوَ لا يَعْلَمُ ؟ قَالَ : (( خُذِي مَا يَكْفِيكِ وَوَلدَكِ بِالمَعْرُوفِ )) . متفق عَلَيْهِ .
Amesema 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa): Hind, mke wa Abu Sufyaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Abu Sufyaan ni bakhili sana, hivyo hanipi hela zinazo nitosha mimi pamoja na mtoto wangu isipokuwa ninazochukua kwake bila ya yeye kujua?" Akasema: "Chukua hela zinazo kutosha wee na mtoto wako kwa wema." [Al-Bukhaariy na Muslim]