02-Malaika: Hukmu Ya Kuamini Malaika
Malaika
02: Hukmu Ya Kuamini Malaika
Kuamini Malaika ni waajib kwa Muislamu, kwani kuamini uwepo wao ni nguzo kati ya nguzo za Iymaan. Iymaan ya Muislamu haiswihi bila kuamini uwepo wa Malaika. Nguzo za Iymaan kama tujuavyo ni sita: Kumwamini Allaah, kuamini Malaika Wake, kuamini Vitabu Vyake, kuamini Mitume Wake, kuamini Siku ya mwisho, na kuamini Qadar; kheri yake na shari yake. Haya yote ni lazima Muislamu ayaamini ili iymaan yake iwe ni sahihi.
Allaah Amesema:
"آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ"
“Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia). Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Rusuli Wake. (Nao husema): Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Rusuli Wake. Na wakasema: Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu, na Kwako ndio mahali pa kuishia”. [Al-Baqarah: (285)].
Na yeyote atakayekanusha uwepo wa Malaika, au akawatangazia uadui, au akawatukana, au akawacheza shere, basi huyo amekufuru. Allaah Anasema:
"مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّـهَ عَدُوٌّ لِّلْكَافِرِينَ"
“Yeyote aliyekuwa adui wa Allaah na Malaika Wake, na Rusuli Wake, na Jibriyl, na Miykaala, basi hakika Allaah Ni adui kwa makafiri”. [Al-Baqarah: (98)].
Kadhalika, anakuwa amepotea upotevu wa mbali kabisa. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا"
“Na atakayemkufuru Allaah na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Rusuli Wake na Siku ya Mwisho, basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali”. [An-Nisaa: (137)].
Hivyo ni lazima Muislamu aamini uwepo wa Malaika pamoja na nguzo zote za Iymaan, akiacha moja, basi Iymaan yake imebatilika.