27-Malaika: Idadi Ya Malaika

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

27:  Idadi Ya Malaika

 

Idadi ya Malaika ni kubwa mno na hakuna ajuaye idadi hiyo isipokuwa Allaah Ta’aalaa.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ ۚ وَمَا هِيَ إِلَّا ذِكْرَىٰ لِلْبَشَرِ"

 

“Na hakuna ajuaye majeshi ya Rabb wako isipokuwa Yeye Pekee.  Na haya si chochote isipokuwa ni ukumbusho kwa binaadamu”.  [Al-Muddath-thir: 31]

 

Kila aliyebaleghe anao Malaika wawili wa kusajili matendo yake mema na mabaya, mbali na wale wanaomlinda mtu asipatikane na dhara lolote ambalo Allaah Hakumwandikia.  Isitoshe, kuna wale wanaozunguka huku na kule kutafuta vikao vya kiilmu vya Waumini na kuvihudhuria, na wengineo wengi tu.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza Jibriyl (‘alayhis salaam) kuhusu Al-Bayt Al-Ma’amuwr.  Jibriyl akamwambia:

 

"هَذَا الْبَيْتُ الْمَعْمُورُ يَدْخُلُهُ كُلَّ يَوْمٍ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ إِذَا خَرَجُوا مِنْهُ لَمْ يَعُودُوا فِيهِ آخِرُ مَا عَلَيْهِمْ"

 

“Al-Bayt Al-Ma’amuwr hii, wanaswali ndani yake kila siku Malaika elfu 70, na wanapotoka hawarudi tena”.  [Al-Bukhaariy (3207) na Muslim (164)]

 

Ikiwa kila siku wanaingia kwa idadi hiyo na hawarudi tena baada ya kutoka, watakuwa ni kiasi gani toka wameanza kuingia hadi Qiyaamah!

 

Katika yanayoonyesha wingi wao, ni yale yaliyosimuliwa na ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu) toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"يُؤْتَى بجهَنَّمَ يَوْمَئذٍ لَهَا سَبْعُوْنَ ألفَ زِمامٍ، مَعَ كُلِّ زِمَامٍ سَبْعُوْنَ ألفَ مَلَكٍ  يجرُّونَها"  

 

“Italetwa Siku hiyo Jahannam ikiwa na hatamu elfu sabini, kila hatamu imekamatwa na Malaika elfu 70 wanaikokota”.  [Muslim (2842)]

 

Kwa hesabu ya haraka haraka, idadi ya Malaika hao itakuwa ni bilioni 4 milioni 900, yaani 70,000 X 70,000 = 4,900,000,000.  Hao pengine kazi yao ni hiyo tu kwa siku hiyo ya Qiyaamah.

 

Ibn Taymiyyah amesema:  “Hakuna awezaye kukokotoa idadi ya Malaika isipokuwa Allaah Pekee. Aayaat za Qur-aan na Hadiyth za Rasuli zinazozungumzia majukumu wanayoyasimamia Malaika kwa mwanadamu, zinaonyesha namna walivyo wengi.  Kuna Malaika mwenye jukumu la tone la uzazi, Malaika wawili wa kuandika matendo ya kila mwanadamu, Malaika wa kumlinda, Qarinu wa Kimalaika wa kumwongoza na kumwelekeza, na wengineo na wengineo.

 

 

Share