28-Malaika: Je, Malaika Wanakufa?

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

28:  Je, Malaika Wanakufa?

 

‘Aqiydah ya Ahlus Sunnat wal Jama’a inaeleza kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Ameandika mauti kwa viumbe vyote hai, na Yeye Pekee Ndiye Atakayebakia.  Na juu ya msingi huu, wanaamini kwamba Malaika inajuzu kwao kupatwa na umauti, na Allaah Ana uwezo wa hilo.  Allaah Anasema:

 

"كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ"

 

Kila aliyekuwa juu yake ni mwenye kutoweka  ●  Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu”.   [Ar-Rahmaan: 26-27]

 

Ibn Kathiyr amesema:  “Allaah Anaeleza hapa kwamba wakazi wote wa ardhi wataondoka na watakufa wote, na pia vile vile wakazi wa mbinguni isipokuwa wale tu ambao Allaah Atataka wabakie.  Na hatobaki yeyote isipokuwa Wajihi Wake Mtukufu, kwa kuwa Rabbi Aliyetukuka Hafi, bali Yeye Ndiye Aliye Hai Ambaye Hafi milele.

Ibn Taymiyah aliulizwa:  Je viumbe vyote wakiwemo Malaika watakufa?  Akajibu: “Ambalo watu wengi wanaliamini ni kwamba viumbe wote wanakufa na hata Malaika.  Waislamu, Mayahudi na Manaswara wanakubaliana uwezekano wa hilo na uwezo wa Allaah wa kulitenda.  Allaah Ana uwezo wa kuwafisha kisha kuwahuisha kama Alivyo na uwezo wa kuwafisha wanadamu na majini kisha Akawahuisha tena.  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ"

 

“Naye Ndiye Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurudisha, nayo ni sahali mno Kwake”.  [Ar-Ruwm: 27]

 

As Suyuwtwiy amesema:  “Niliulizwa:  Je, Malaika watakufa kwa mpulizo wa kwanza wa baragumu, na watafufuka kwa mpulizo wa pili?  Nikajibu:  Ndio”.

 

 

Share