30-Malaika: Aina Za Ibada Ambazo Malaika Wanazifanya: (1)- Kumsabbih Allaah
Malaika
30: Aina Za Ibada Ambazo Malaika Wanazifanya
(1)- Kumsabbih Allaah
Allaah Ta’alaa Amesema:
"وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً ۖ قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ ۖ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لَا تَعْلَمُونَ"
“Na pale Rabb wako Alipowaambia Malaika: Hakika Mimi Nitaweka katika ardhi khalifa. Wakasema: Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu, na hali sisi tunakusabihi kwa Himidi Zako na tunakutukuza kwa Utakatifu Wako? (Allaah) Akasema: Hakika Mimi Nayajua zaidi msiyoyajua". [Al-Baqarah: 30]
Na Anasema tena Akiwazungumzia Malaika wabebao ‘Arshi Yake:
"الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ"
“(Malaika) ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih na kumhimidi Rabbi wao”. [Ghaafir: 07]
Malaika wote kiujumla wanamsabbih. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِن فَوْقِهِنَّ ۚ وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"
“Zinakaribia mbingu kuraruka moja juu ya nyingine, na ilhali Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini. Tanabahi! Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Ash-Shuwraa: 05]
Kumsabbih kwao Allaah ni jambo la kudumu, halisimami. Allaah ‘Azza wa Jalla Anasema:
"يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ"
“Wanasabihi usiku na mchana, hawaishiwi nguvu”. [Al-Anbiyaa: 20]
As-Sa’adiy amesema: “Malaika wamezamia katika kumwabudu Allaah na kumsabbih katika wakati wao wote, hawana wakati wa faragha wala wa kupita bure, wako katika sifa hii pamoja na wingi wao. Na hii inabainisha Uadhwama wa Allaah, Utukufu wa Mamlaka Yake, ukamilifu wa Elimu Yake na Hikma Yake, na haya yanawajibisha asiabudiwe mwingine yoyote zaidi Yake”.
Abu Dharri (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: Ni maneno yepi yaliyo bora zaidi? Akasema:
"مَا اصْطَفَى اللَّهُ لِمَلاَئِكَتِهِ أَوْ لِعِبَادِهِ سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ " .
“Ni yale ambayo Allaah Amewachagulia Malaika Wake au Waja Wake, nayo ni: Subhaana Allaah wa bihamdihi. [Muslim (2731)]
Hadiyth hii inatukumbusha kwamba dhikri ya tasbiyh ndiyo iliyochaguliwa na Allaah kwa Malaika na sisi pamoja na vitu vyote Alivyoviumba Allaah ambavyo vyote hivyo vinamsabbih. Usije wewe ukawa nje ya duara hili. Allaah Anasema:
"تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا"
“Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na waliomo humo. Na hakuna kitu chochote isipokuwa kinasabihi na kumhimidi Yeye, lakini hamzifahamu tasbiyh zao. Hakika Yeye Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria”. [Al-Israa: 44]